SEHTANI RUDISHA AKILI ZETU.
MTUNZI: SINGANOJR
SEHEMU YA 85.
Mzee Tui aliona kabisa kuna kitu ambacho hakipo sawa , kwasababu aliagiza vijana wake walete gari ambayo haijatumika ndani ya ardhi ya Tanzania , sasa kitendo cha gari kuonekana kuharibika pasipo chanzo alijikuta akishangaa.
“Nyie, mliangalia hii gari kabla ya kuichukua?”Aliuliza.
“Bosi haiwezekani , hii gari tumeitoa karakana kabisa na hata namba tumebandika wenyewe”Aliongea Dereva akitingisha kichwa na palepale akili yake ilimwambia au ni Hamza ila bado hakutaka kuamini.
Baada ya kupata wazo hilo kwa haraka haraka alikimbilia nyuma ya gari kuangalia na alijikuta akishituka mara baada ya kukuta vijana wake wawili ambao hakuingia nao ndani ya gari wakiwa wamedondoka chini huku eneo la vichwani mwao kukiwa na alama ya kupigwa na mawe kiasi cha kuvuja damu.
Alijikuta akianza kupaniki na kugeuka geuka kutafuta nani kafanya tukio hilo maana vijana wake ni kama walishambuliwa na bunduki.
“Mkuu unanitafuta?”
Sauti ilisikika nyuma yake na alijikuta akishituka mno maana upande sauti ilikotokea alikuwa amekukagua tayari.
“Wewe… imekuwaje , inamaana hujafa?”Aliuliza Mzee Tui kana kwamba alikuwa akiangaliana na Mzimu wa Hamza.
Hamza alikuwa na vumbi kama vile ni kichaa , muonekano wake haukuwa mzuri hata kidogo na mavazi aliokuwa amevaa yalichanika baadhi ya sehemu, lakini hakuonekana kuwa na alama ya kuvuja damu ama kuungua.
Muda huo Regina ambae alikuwa ashatolewa kwenye gari na James alijikuta akibung’aa kana kwamba alichokuwa akiona ni udanganyifu wa macho.
Alimshuhudia Hamza kwa macho yake kupitia Kamera mpaka sekunde ya mwisho jengo lilivyolipuka , lakini dakika hii yupo mbele yake akiwa hai hakujua kabisa nini kilitokea.
Lamla , James na Mzee Benjamini walimwangalia Hamza kwa hofu kama wameona mzimu.
Hamza hakujali mshangao wao , kitendo cha kumsogelea Regina James alimwachia na kurudi nyuma kwa hofu na kumfanya Hamza atabasamu.
“Wife hawajakuumiza sana , ngoja nikufungulie kwanza”Aliongea Hamza na kwa wepesi sana mara baada ya kushika kamba zilizomfunga Regina alizifungua kwa kuzikata na mikono.
Regina alijikuta akivuta pumzi nyingi kana kwamba anajaribu kujirudisha hai na kisha alimshikaHamza mkono huku akitetemeka.
“Hamza … hujakufa kweli au nakuona ndotoni”Aliongea Regina na kauli ile ilimfanya Hamza kufurahi kuona mrembo huyo alikuwa akiwa na wasiwasi juu yake.
“Kwahio hata kwa kunigusa bado hujaamini tu , haya sikiliza mapigo ya moyo wangu?”aliongea Hamza huku akichukua mkono wa Regina na kuuweka kwenye kifua chake karibu na eneo la moyo na Regina alijikuta ahueni kubwa ikimvaa.
“Ila niliona kabisa ukilipuka ..”
“Usiwe na waswasi , nilifanya vile makusudi , nilikuwa nishajua nimewekewa mtego , hivyo nilijiandaa namna ya kujiokoa”Aliongea Hamza huku akimkonyeza Regina.
Ukweli ni kwamba Hamza hata hakuwa amejiandaa kukwepa mtego huo , yeye aliamini katika uwezo wake pekee na kujiambia kama ni mtego kwa spidi yake basi anaweza kujiokoa , hivyo mara baada ya kutokea ule mlipuko aliweza kuruka kwa spidi kubwa na kwenda kutua pembeni na kilichomfikia pekee ni vumbi na vipande vya zege na mbao.
“Kwahio ulijua?”
“Ndio nilijua , mtego wao ulikuwa unaonekana sana , kwa wataalamu wa kuteka nyara kama hawa isingekuwa rahisi kuacha viashiria vya uelekeo wao , wamekuteka jana usiku lakini nimekuja maeneo haya nimekuta damu wameisambaza. Hata kama ni kweli ni damu ambayo hawakuacha makusudi eneo lile linamchanga na kutokea jana mpaka sasa hivi viashiria vingekuwa vimeshapotea , hivyo niliona kabisa wanajaribu kunivutia sehemu ili waniue aidha kwa bomu au gesi ya sumu , maana ndio njjia nyepesi kwao, nimeamua kujifanyisha kufa kwa sekunde kadhaa ili tu wapoteze umakini na iwe rahisi kukuokoa bila kupata shida”Hamza alielezea kana kwamba kilichomtokea ni tukio la kawaida sana , yaani ki ufupi hakuwa na wasiwasi.
Ilikuwa kweli kwa mtu mwingine wa kawaida hilo tukio linaweza kuwa kubwa maisha yake yote lakini yeye alishapitia kwenye hali za hatari mara kumi zaidi ya hilo.
“Huyu kweli ni mwiba, Hamza ni kama nilivyosikia sifa zako , hakika una bahati”Aliongea Mzee Tui baada ya kusikia maelezo yake.
“Maisha yangu hayajawahi kuwa ya kawaida , lakini kwa upande wenu sina uhakika kama mtaendelea kuishi kwa muda mrefu”Aliongea Hamza huku kwa macho ya ukauzu akimwangalia Mzee Bemjamini , James na Lamla.
“Kitendo chenu cha kushiriki katika hili , hata ile bahati kidogo mliobarikiwa mnakwenda kuipoteza”Aliongea Hamza huku akimkazia macho Lamla.
Upande wamwanamke huyo alijikuta akiwa na hofu mno na alienda kujificha nyuma ya hawala wake.
“Lamla ndio mhusika mkuu , aliniwekea mtego kwa kunipigia simu nifungue mlango , ndio maana ikawa rahisi kwao kuniteka”Aliongea Regina akimnyooshea Mkono Lamla kana kwamba anamsemea kwa Hamza.
“Kama ni hivyo unaonaje nikimuua hapa hapa?”Aliongea Hamza maana hakutaka kuchukua maamuzi kwani kwa nje bado alikuwa ni mama wa kambo kwa Regina.
“Wewe… unamaanisha nini , unataka kuua na sio sheria kuchukua mkondo wake?”Aliongea Regina huku sauti yake ikikataa kabisa ambacho Hamza anataka kufanya.
“Babe unadhani nisipowaua muda huu watakuacha uwe na amani?”Aliongea Hamza na Regina alijikuta akikosa neno la kuongea , ukweli hakutaka Hamza kuua mtu yoyote na hata alivyosikia aliua alichukia sana , lakini muda huo alikuwa kwenye dilema , alijifikiria pia kama kweli wasipokufa si watamsumbua tu , alifikiria pia kama atajaribu kutumia njia za kisheria si watatoka tu polisi maana alikuwa akijua kuna watu wazito nyuma yao, mwisho wa dakika alijikuta akikosa cha kuamua.
“Wewe amua tu unachotaka”Aliongea Regina kwa sauti hafifu.
Hamza alijua maneno hayo yalikuwa na maana gani kutoka kwa Regina , lakini aliona angalau Regina anajua kumuacha Lamla kuendelea kuwa hai ni tatizo ambalo litachipukia muda wowote.
Baada ya Mzee Benjamini kusikia kauli ya Regina wasiwasi ulimvaa palepale na alimgeukia Mzee Tui na watu wake.
“Mzee Tui umesema wewe ni mwanajeshi wa jeshi la watu elfu moja , fanya haraka muue kabla hajamfikia Lamla?”
“Usiwe na haraka , moja ya mbinu yetu kama nafsi zinazotangatanga hatujawahi kuwa na mpango mmoja”Aliongea Mzee Tui na muda ule ni kama Lamla ameshituka na kuanza kucheka.
“Upo sahihi , Wilsoni, baba yako yupo kwenye mikono yetu , Hamza kama unataka amuone baba yake anaendelea kuishi , unatakiwa usikilize kila tunachokuambia kwa utii”Aliongea na Regina mara baada ya kusikia hivyo alishituka.
“Mlimteka na baba yangu pia , hata kama sijawahi kuwa mtoto wako , yule ni mume wako wa ndoa”
“Nani mume wangu , yule ni furushi tu la takataka kwangu”Aliongea na muda uleule alimsogelea Mzee Benjamini na kujiinamiza.
“Kama unataka baba yako kuendelea kuishi , saini mkataba wa makubaliano ya kuhamisha hisa zako zote za kampuni kuja kwangu”
“Wewe…”Regina alijikuta akisaga meno kwa hasira.
“Niambie baba yangu yupo wapi ,najuaje yupo salama?”Aliongea.
Ijapokuwa uhusiano wake na baba yake haukuwahi kuwa mzuri sana lakini alikuwa ni baba yake mzazi , hivyo isingekuwa rahisi kwa Regina kuona baba yake anakufa.
Muda huo huo waliweza kusikikia ngurumo ya gari ikisogelea eneo hilo.
“Kama unataka kumuona baba yako hakuna shida , ila tunapaswa kwanza kuondoka ndani ya hili eneo , Hamza unaonaje tukihama kwanza hapa?”Aliongea Mzee Tui
Hamza alijikuta akifikiria , ukweli hakuwaza kama kundi hilo lingeenda mbali na kumkamata na baba yake Regina kwa wakati mmoja , ilionekana walichukua kila tahadhari ya kujiokoa mambo yakienda ndivvyo sivyo.
“Tunaelekea wapi , kama mnataka twende wote ,tutapanda gari tofauti?”Aliongea Hamza.
Ukweli isingekuwa tatizo kupanda nao kwenye gari moja , lakini kwa sababau alikuwa akimzingatia na Regina kwa wakati huo aliona achukue uamuzi huo.
“Naona unajaribu kuwa makini , lakini usiwe na wasiwasi , sehemu tunayoenda ni karibu mno , tukutane chumba namba 230 floor ya ishirini ndani ya Dar Lux Hotel”
Baada ya kuongea hivyo alitoa kadi ya chumba mfukoni na kisha alimrushia Hamza.
“Hakuna shida mkuu tutaonana basi”Aliongea Hamza kivivu huku akipokea ile kadi.
Dakika hio hio Mzee Tui na watu wake waliingia kwenye Gari ndogo ya abiria na kisha walitoweka ndani ya eneo hilo .
“Kwanini una uwezo mkubwa sana , ushawahi kuwa mwanajeshi?”Aliuliza Regina.
“Sio lazima kuwa mwanajeshi ili uwe na uwezo , nimejifunza namna ya kuishi katika aina zote za changamoto”Aliongea Hamza huku akiwa na tabasamu.
Lakini upande wa Regina hakumwamini kirahisi , aliona sio kawaida kwa mtu kama huyo kuwa na uwezo kama huo , alijiambia Hamza anamficha vitu vingi sana.
Hamza hakujali kuridhika ama kutoridhika kwa Regina ,muda huo alifikira namna ya kumsaidia baba yake na bila ya kuchelewa alitoa simu na kupiga namba ya Afande Himidu ambae alipokea haraka kana kwamba alikuwa akiisubiria na swali la kwanza kutoka kwa Afande huyo ilikuwa ni kumuliza kama amefanikiwa kumpata mke wake na Hamza alimwambia alimpata .
“Afande wewe ndio mshauri na mtaalamu wa mmbinu jeshini lakini mmeshindwa kujua Kundi la Wandering Souls limeingia Dar es salaam na kumteka mke wangu”Aliongea Hamza lakini akitumia lugha ambayo haikueeweka ili kumfanya Regina asijue.
“Bosi unamaanisha hawa wachawi wapo Dar , vijana watakuwa wamefanya makosa makubwa kutokana na akili zao kuwekeza mipakani”Aliongea.
“Najua una teknolojiakubwa ya kuweza kuwapata ndani ya muda mfupi , wameondoka nilipo na gari aina ya Hiece yenye namba T385BGN, najua ni namba feki ila unajua cha kufanya”Aliuongea Hamza.
“Usiwe na wasiwasi bosi , tulikuwa tukiwafatilia kwa muda mrefu sana,awau hii lazima tulizime hili kundi”Aliongea kwa kujiaini.
“Kuhusu hio kazi nitawasaidia , wewe tafuta uelekeo wao mkiupata niambie niwafanyie ziara”
“Hapana bosi , huko ni kujisumbua hawa hawajawahi kutushinda ni mbinu zao tu za hila ndio maana wanatuponyoka , vijana wa kitengo chetu cha Malibu wataweza kuwadhibiti awamu hii”Aliongea Afande Himidu na Hamza mara baada ya kufikiria aliona ni sahihi kabisa na amuamini , hivyo hakutaka kuingilia sana na maswala ya ulinzi wa taifa na kuishia kukata simu.
“Ulikuwa unaongea na nani?”Aliuliza Edna.
“Ni rafiki yangu jeshini ili atusaidie”Aliongea Hamza.
“Una rafiki jeshini?”
“Ndio , siswezi kukuelezea sana , lakini kama tukikutana nae nitakubatambulisha , ngoja tumpigie Shangazi kwanza nimwambie upo salama maana ana wasiwasi”Aliongea Hamza.
Regina bado alikuwa hana taarifa juu ya bibi yake kufariki na hakutaka kumwambia katika hayo mazingira
Licha ya Hamza kumpa kazi rafiki yake Himidu , lakini bado safari ya kwenda hoteli ya Dar Lux aliendelea nayo, alichokuwa akilenga Hamza mpaka kumwambia mjeda kuweka kitengo chake katika kufuatilia ni kutokana na kwamba aliamini watu wa The Loner lazima watakuwa wengi na kuna sehemu wameweka kambi ya muda.
Mara baada ya kuchukua taksi hatimae walikuja kusimamishwa ndani ya hoteli ya Dar Lux na kwasababu walikuwa na kadi tayari walipita moja kwa moja na kuingia kwenye lift ambayo iliwapeleka Floor husika na kwenda kusimama katika mlango wa chumba namba 230.
Hamza mara baada ya kupitisha kadi mlango ulifunguka na mara baada ya kuingia ndani waliweza kuona Laptop ikiwa juu ya kimeza huku ikiwa imegeuziwa upande wa mlangoni na kuna vidio ambayo ilikuwa ikionekana mubashara.
Regina mara baada ya kuangalia kinachoonekana kwenye hio laptop alijikuta akiziba mdomo na kiganja cha mkono wake asiamini anaeonekana ni baba yake kwenye laptop hio.
“Baba..!!”
Mzee Wilsoni alionekana kufungwa akiwa amekalishwa kwenye kiti , na nyuma yake kulikuwa na mtu ambae alionekana ndio watu walewale wa kundi la nafsi zinazotangatanga , muonekano wa mtu huyo ulikuwa wa kikauzu na alioekana kuwa tayari kwa maagizo yoyote.
Baba yake alionekana kuitaji kuongea kitu lakini midomo yake ilikuwa imefungwa na plasta.
“Hii ndio sababu wametuleta hapa hotelini kwasababu hawataki tujue wanaelekwa wapi”Aliongea Hamza akionekana hana mshangao kabisa , ukweli alijua kundi hilo lisingekaa hotelini tokea mwanzo na wanakuja kukutana na kitu kama hiko.
Upande wa Regina alichojua ni kufanya biashara na alijua kuja ndani ya hoteli hio anakuja kukutana na baba yake.
“Hamza tunapaswa kufanya nini kumsaidia baba?”
“Hili kundi ni la ulimwengu wa giza la daraja B na kwa kiongozi wao kuchukua jukumu kuja kwa ajili ya hii misheni maana yake ni kwamba ameongozana na wataalamu wa hali ya juu anao waamini , hebu fikiria namna ulivyotekwa na wakati huo baba yako akiwa ameshtakewa tayari , lakini pia mpaka kukodi hiki chumba kuweka hii laptop, hii maana yake ni misheni ambayo wameichukulia siriasi kuliko misheni zote , malengo yao ni kwa ajili ya wewe kuachia hisa za kampuni kwenda kwa kampuni ya Zena na kama ikitokea mpango wao kufeli washatangeneza njia ya kukimbilia”
“Kama wanachotaka ni hela , mimi nipo tayari kuwapa hata mara tatu ya walioahidiwa”Aliongea Regina.
“Haiwezekani , ni kweli makundi kama haya yanajali misheni zenye hela na wao pia wanapenda hela lakini ili waendelee kupata misheni lazima wajali taswira yao , wamekwisha kupokea misheni tayari hivyo hawawezi kuvunja mkataba hata kama waahidiwe kiasi kikubwa zaidi , labda wakamilishe kazi na baada ya hapo mkataba uishe na ndio wewe uwatafute wafanye kinyume chake , hio ndio sheria”Aliongea Hamza.
Regina alijikuta akishindwa hata kujua cha kufanya , katika mambo hayo alijiona mjinga kabisa.
Muda huo wakati wakiendelea kuangalia kinachoendelea kwenye laptp, Lamla na wenzake walijitokeza kwenye Kamera mmoja baada ya mwingine.
“Mr Hamza , Regina tunaomba tadhi kwa kuchelewa”Aliongea Mzee Tui au The Loner.
“Unataka nini kutoka kwetu?”Aliongea Regina kwa haraka haraka, ile laptop haikuwa ikionyesha tu kinachoendelea lakini pia ilikuwa ni njia ya mawasiliano , ki ufupi ilikuwa ni Vidio call.
Mzee Tui aliishia kugeza kichwa chake pembeni na alionekana kujadiliana kitu na watu waliokuwa ndani ya eneo hilo na kisha alimgeukia Regina.
“Angalia pembeni ya laptop kuna nyaraka , kama ukikubali na kuzisaini na sisi kuthibitisha hazina makosa na kampuni ya usafirishaji kuja kuzichukuwa , tutamuachia baba yako. Kumbuka huwezi kufanya hila yoyote maana tukigundua kosa kidogo tu ndio utakuwa mwisho wa uhai wa Mzee Wilsoni”
Regina aliishia kuangalia nyaraka zilizokuwa pembeni na zilionekana kuwa ni kama zilezile waliokuwa wakimlazimisha azisaini.
“Nitawaamini vipi kama nikisaini mtamwachia baba yangu , kama mnataka nisaini muachieni baba yangu kwanza na nikihakikisha yupo salama , nitasaini huu mkataba na mnaweza kuomba guarantee juu ya nilichokisema”Aliongea Regina na kumfanya Mzee Tui kuanza kucheka.
“Regina huna vigezo vya kuweka masharti kwetu, kama bado unajiona ni ngumu kutimiza unaonaje ukimuuliza baba yako kwanza tuonne anaongea nini?”Aliongea huku akicheka na palepale aliondoa plasta aliomfunga Mzee Wilsoni.
“Regina usije kusaini ,tafadhari usisaini na usijali kuhusu mimi”
“Wewe takataka unaongea nini , kaa kimya”Aliongea Lamla kwa kufoka huku akimpiga kibao cha uso.
“Lamla kwaninni unafanya haya yote , ni kipi nimekukosea mpaka unaenda mbali hivi , kuna ambacho nimefanya hakijakuridhisha mpaka unisaliti?”Aliongea kwa hasira na masikitiko.
“Nadhani una shida kwenye ubongo wako , kama sijawahi kukupenda kabisa kwanini uone nimekusaliti , hebu fanya haraka na umwamrishe binti yako asaini haraka”Aliongea Lamla kwa ukali.
“Lamla wewe ni mke wangu na sisi ni familia..”
“Nani ni familia yako , unadhani ilikuwa hiari yangu kuolewa na wewe , kama sio wazazi wangu kunilazimisha kuolewa na wewe nisingekusogelea mwanaume kilaza kama wewe”Aliongea kwa kejeli na muda huo Mzee Benjamini alimsogelea Mzee Wilsoni.
“Wilsoni , nimesikia kutoka kwa Lamla wewe ni mjinga mpaka kwenye sita kwa sita , kwa miaka ishirini yote kama sio mimi Lamla angekuwa mpweke sana”Aliongea kwa jeuri na kauli hio ilimfanya Mzee Wilsoni macho kuwa mekundu kama yanavuja damu.
“Kwahio wewe ulikuwa ukilala na mke wangu?”Aliuliza lakini aliambulia kibao kutoka kwa Lamla.
“Mpuuzi wewe usie na thamani , mwanaume nilietokea kumpenda kwenye maisha yangu ni Benja na wewe uliingilia , tena kwa muda mrefu sana nilitaka kukuambia hili , mwanangu Frank sio damu yako sa kwa taarifa yako ulikuwa ukinitunza kwa ajili ya mwanaume mwenzio hahaha…”
Yalikuwa maneno makali sana kuyasikia , isitoshe alikuwa akimpenda Lamla licha ya madhaifu yake , aliishia kutoa macho kama vile amepigwa na radi
Regina ambae alisikia kila kitu na kuona alijikuta akiweka mikono yake juu ya meza kwa kutoamini.
“Lamla acha ukichaa… Frank ni mtoto wangu , unaongea ujinga gani?”Alijikuta akianza kubweka kwa hasira lakini Lamla aliishia kuinua mguu wake na kisha kumpiga teke la tumboni na viatu vyake vya skuna.
“Unabweka nini sasa wewe mjinga , unadhani sijui baba wa mtoto wangu, yaani wewe ni mjinga sijapata ona , miaka yote ishirini unashindwa hata kufikiria kupima DNA licha ya mtoto kutofanana ne kwa kiasi kikubwa?”Aliongea huku akisonya kwa nguvu.
“Lamla huna haja ya kuendelea kuwa na hasira kwa huyu mjinga, tuache kupoteza muda wetu hapa kuongea na mjinga ambae hawezi kukuelewa, MzeeTui mpe kitu chochote akili imkae sawa”Aliongea Mzee Benjamini.
Mkuu yule wa kundi bila ya kuchelewa aliwapa ishara vijana wake kuanza kazi na waliibuka na kisu na kumsogelea kisha wakamkata kwenye pingili ya kiganja cha mkono
“Arghhhhhh…!!!”
Mzee Wilsoni alijikuta akitoa ukulele usio kuwa na mfano baada ya kuhisi kisu kimeingia mpaka kugusana na mfupa , jasho jingi lilimtoka.
Kitendo kile cha baba yake kupitia maumivu makali yalimshinda Regina kuendelea kuangalia.
“Msiendelee kumuumiza , acheni kumtesa baba”Regina alijikuta akipiga makelele.
Hamza aliishia kukunja ngumi kwa hasira , kama sio kwa ajili ya kumlinda Regina angekuwa ashatoka hapo na kwenda kuua mmoja baada ya mwingine kwa namna yoyote ile.
Lakini kwa muda huo kitu pekee ambacho aliwekea tumaini ni kitengo cha Malibu kuwahi eneo la tukio na kutoa msaada.
“Wewe mtoto wa kahaba umeona eh , mimi na Frank hatuna mahusiano yoyote na familia yenu , hivyo usije kudhani siwezi kumuua baba yako ukiendelea kunipotezea muda, bibi yako hakuwahi kunichukulia kama mwanafamilia na nilichokifanya ni kuishi kwa kuivumilia kuifikia hii siku, hatimae baba yako yupo kwenye mikono yangu , kama unataka aendelee kuwa hai fanya haraka na saini hizo nyaraka”Aliongea Lamla.
Mzee Wilsoni matumaini yote yalikuwa yamemtoka , aliishia kutoa kilio kama mtoto.
“Unalia nini wewe mpuuzi, mwanaume unashindwa kujikaza hata kwa maumivu kidogo?” Lamla aliendeleza kejeli zake.
“Mzee Tui hebu muongezee kidogo maumivu kumpa motisha binti yake asaini haraka , akiendelea kuleta ubishi kata nyama kidogo kidogo”
Mzee Tui aliishia kuchezesha vidole kwa mbwembwe na vijana wake walisogelea mkono wa pili wa Mzee Wilsoni na kuupitishia kisu.
Damu zilifyatuka pande zote na ndani ya dakika chache tu eneo lote lilinuka na kutapakaa damu.
Hamza kwa namna ambavyo alimuona Regina alipatwa na wasiwasi kwani ni kama vile amebadilika.
“Regina nadhani uharakishe kufanya maamuzi la sivyo watamfanya kuwa kilema”Alishauri Hamza.
Regina aliishia kuchukua karamu kwa mikono yenye kutetemeka, kana kwamba alikuwa akijitahidi sana kufanya maamuzi.
“Hata kama ukisaini haimaanishi ndio mwisho , tuna muda mwingi wa kutosha kufikiria namna ya kumuokoa baba yako na hizi nyaraka zisiwafikie kwenye mikono yao”Aliongea Hamza kwa sauti ya chini mno.
“Nitasaini , msiendelee kumuumiza baba yangu”Aliongea Regina na kauli hio iliwafanya Lamla na James kushikwa na msisimko wa furaha.
“Fanya haraka acha mapepe “
Waliamini ili mradi Regina kukubali kuachia kampuni kwenda kwao , watahakikisha Mzee Wilsoni anaendelea kubakia kama mtumwa katika mikono yao na kuhakikisha kampuni ya Zena haifirisiki na kipindi hicho watakodi mtaalamu wa hali ya juu ambae ana uwezo wa kumuua Hamza.
Lakini sasa sekunde ambayo Regina anataka kusaini , ghafla tu Wilsoni alibweka kama vile ni mnyama wa mwituni.
“Nitakuuuuaaa… wewe kahaba”
Haikueleweka Mzee huyo alikuwa amerudiwa na nguvu zake lakini ilionekana majonzi yamefikia ukomo na kaamua kutumia nguvu zake zote na kusababisha hata kamba ambazo amefungwa miguuni kukatika
Kiti kikiwa bado kipo mgongoni kama vile amerukwa na akili alimsogelea Lamla kwa nguvu akidhamiria kumgonga nacho.
SEHEMU YA 86.
Lamla alijikuta akipiga ukulele kwa woga , lakini hata hivyo Mzee Wilsoni alikuwa mwanaume wa kawaida na watu wa kundi la Nafsi zinazotangatanga walimuwahi na kumkalisha chini huku wakimuwekewa kisu shingoni.
“Ukisogea kidogo tu , nitakukata kata”Muuaji aliongea kwa msisitizo na kumfanya mzee huyo kutulia.
“Wewe mpuuzi bado tu unajjiona una nguvu , mshenzi wewe kufa”Aliongea Lamla kwa hasira huku akimpiga aliekuwa mume wake mateke.
“Lamla hebu punguza jazba , hebu muangalie vizuri damu zinavyomtoka,unadhani ni kipi anaweza kufanya zaidi , ukiendelea hivyo utamuua halafu kipi kitafuata , unadhani tutaweza kuipata vipi kampuni ya Dosam?”Aliongea Mzee Benjamini kwa hasira kidogo na kumfanya Lamla kutulia.
“Upo sahihi , hatupaswi kumuua maana baadae familia yetu itamtegemea”Aliongea na kisha alimsogelea Mzee Benjamii na kumkisi kwenye shavu kumtuliza.
Mzee Wilsoni aliishia kutoa macho kama kabanwa na mlango kwa hasira hasa wakati huo ambapo aliona wanabusiana.
“Lamla huwezi kunifanyia hivi….. nilimtelekeza mama yake Regina kwa ajili yako .. haya ndio matokeo?”Aliongea huku akikumbwa na majonzi makubwa pamoja na majuto.
Regina alijikuta akitoa mshangao mara baada ya kusikia kauli hio , sekunde ileile alijikuta machozi yakimtoka na kudondokea karatasi anazokwenda kusaini.
“Kwasababu wewe ni mjinga , unamlaumu nani kwa makosa yako , kama ulimuacha ungemucha moja kwa moja kwanini baba yako akaenda kumleta Regina, jibu ni moja tu ,kwasababu ulikuwa mjinga ndio maana”Aliongea Lamla huku akisonya.
Mzee Wilsoni aliishia kutetemeka kwa hasira na palepale aligeuza kichwa chake na kuangalia Kamera.
Na kupitia Kamera zile upande wa pili kwenye chumba cha hoteli Regina na Hamza waliweza kushuhudia tabasamu hafifu.
“My Daughter kwa miaka ishirini yote sijawahi kuwa baba mzuri kwako … naomba unisamehe, mambo yamefikia mpaka hatua hi lakini bado upo tayari kutoa umiliki wako wa kampuni kwasababu yangu , nimemkosea sana babu yako , nimemkosea sana mama yako … nimefeli kabisa kimaisha .. haya yote ni kutokana na kugeli kwangu..”Aliongea huku akitoa machozi na kutingisha kichwa akijilaumu.
“Baba usiongee tena…”Regina alishindwa kujizuia kwa upande wake na yeye lakini upande wa Mzee Wilsoni macho yake yalionyesha kudhamiria kitu..
“Naomba nitumie nafasi hii kuwa baba yako hata kwa siku moja…”
Kabla hata hawajaelewa mzee huyo anamaanisha nini , Mzee Wilsoni aligeuka na kwa nguvu aligeukia kile kisu kilichowekwa shingoni mwake.
“Ondoa kisu!!?”
Mzee Tui alipiga kelele lakini kijana wake alikuwa amezubaa na kilichotokea ni kile kisu kuzama katika shingo ya mzee huyo na damu kama bomba lililopasuka zilifyatuka na akadondoka chini palepale akitapatapa.
“Nooo!!!”
Regina mara baada ya kuona tukio lile alipiga ukulele wa juu mno huku akianza kulia kwa kwikwi kiasi cha kuanza kukosa pumzi na nguvu kiasi cha kuishia kupiga magoti chini kwenye sakafu akiwa si mwenye kuamini baba yake amejimaliza.
Hata Hamza hakuwa ametegemea jambo lile kabisa , hakudhania Mzee Wilsoni angechukua maamuzi ya kujiua kwa ajili ya kumlinda Regina na mali za familia.
Alikuwa ni baba kwa zaidi ya miaka ishirini , lakini katika kipindi hicho alionekana kama baba ambae hakuwa akijali na maisha yake yalikosa maana mbele ya macho ya waliompenda , lakini katika dakika za mwisho anaamua kutokubali kuwa sababu ya familia yake kuyumba , hakutaka nguvu ambazo baba yake na mama yake walizotumia kupotea katika mikono ya watu kama hao.
“Pumbavu kabisa , umesababisha haya wewe mwanamke , kama usingeongea maneno mengi asingeamua kujiua”Aliongea Mzee Benjamini kwa hasira akimlaumu Lamla.
“Sikutegemea pia… sikujua angejiua, nilichotaka ni kumuogopesha Regina …”Lamla alijikuta akijitetea huku akiwa haamini kama Wilsoni angechukua maamuzi ya namna hio.
“Sasa amekwisha kufa nini tunafanya tena?”
“Kwanini unanifokea?”Wawili hao walijikuta wakianza kufokeana na Mzee Tui hakutaka kuendelea kuwangaangalia
“Kaeni kimya , tuliemteka amekufa huu ni muda wa kuondoka hapa”
“Ndio , tuondokeni hapa mapema kabla hajafikiwa”Aliongea James ambae pia alikuwa kwenye mshituko.
Katika chumba cha hoteli Hamza aliishia kumkumbatia Regina katika kifua chake huku akiendelea kulia , kitendo cha kuona uchungu na machozi ya Regina moyo wake ulimuuma mno.
Kila kitu kilitokea haraka sana na hakuwa na namna ya kuzuia kisitokee.
“Regina nyamaza , tunachopaswa sasa hivi ni kuwakamata mapema la sivyo kifo cha baba yako kitapotea bure”Aliongea Hamza.
Na Regina kama binadamu aliekosa hisia aliishia kumwangalia Hamza bila ya kuongea chochote.
Upande wa wale watekaji ripoti ilifika ndani ya chumba kile.
“Bosi , watu wetu wa doria wamegundua kitengo cha jeshi cha Malibu wamekamata gari tuliosafiria kuja hapa , tunatakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo ndani ya Dar es salaam”
“Malibu!!, Hamza unaonekana wewe sio mtu wa kawaida lakini usidhanie nitaendelea kukaa hapa mpaka nije nikamatwe”Aliongea Mzee Tui na palepale alikata mawasiliano ya Kamera.
Ijapokuwa ni maneno machache ambayo aliweza kusikia lakini alipata taarifa muhimu sana , Hamza alijiuliza kama Mzee Tui na wenzake wamekwisha kushuka kwenye gari , kwanini kitengo cha Malibu walikuwa wakiendelea kufuatilia gari ambayo ni tupu, jibu pekee aliloweza kupata ni kwamba inaonekana walichezewa akili kuaminishwa watu hao walikuwa ndani ya gari kumbe walishatoka muda mrefu.
Kitu kingine Hamza alichonasa ni kuhusu kundi hilo kutaka kuondoka ndani ya Dar es salaam mapema iwezekanavyo na njia pekee ya kuweza kuondoka hapa Dar na kutokamatwa ni njia ya baharini na kuna uwezekano eneo walipo lipo karibu na bahari na wameshaa andaa boti.
Hamza mara baada ya kuifikiria ramani ya jiji la Dar ilivyokaa , palepale aliweza kupata uelekeo ambao wanaweza kujificha kwa ajili ya kutoroka na boti.
“Regina nitakupeleka sehemu salama kwanza”Aliongea Hamza , hakutaka kumuacha Regina ndani ya hilo eneo , alijua kundi kama hilo lazima ndani ya hii hoteli watakuwa wamejaza maninja kwa ajili ya kumaliza kazi.
“Hapana, wewe nenda tu ukawatafute ,ni bora pia ukipigia huyo rafiki yako iwe rahisi “Aliongea Regina.
“Kuwakamata nitawakamata tu hata wakimbie mpaka wapi , lakini kwasasa sidhani watakuwa wamemalizana na wewe , nikikuacha na wakikushambulia kila kitu kitakuwa hakina maana tena”Aliongea Hamza kwa msisitizo na kisha alimchukua Regina kumtoa ndani ya chumba hiko.
Dakika ambayo wanatoka nnje ya chumba waliweza kumuona mhudumu wa kiume akisogea upande wao kwenye Korido akiwa anaendesha kitoroli cha chakula
Hamza alimwangalia yule mhudumu kwa macho ya uchunguzi na palepale alijikuta akikunja sura mara baada ya kuona kuna kitu hakipo sawa , ilikuwa ni kwasababu ni ngumu sana kwa mhudumu kuwa na sugu za mikono kama alivyokuwa huyo mhudumu , maana yake ni kwamba mtu huyo alikuwa ametumia siraha kwa muda mrefu.
Mhudumu yule ni kama vile alijua Hamza amekwisha kumgundua na ghafla tu alifyatua kitambaa cheupe kilichokuwa kimefunika kile kitorori na aliibuka na bastora ya rangi ya silver na kufyatua risasi tatu kumlenga Regina.
Lakini hata hivyo Hamza alikuwa ashamuotea tayari kwani alimsukuma Regina pembeni huku akiruka sarakasi ya mtelezo na kupiga teke lile tolori na yule ninja kitendo cha kutaka kumkwepa, Hamza alifyatuka sarakasi nyingine na ilikuwa ni kufumba na kufumba alishafikiwa na shingo yake kuzungushwa na kilichosikika ni mifupa ya shingo kupishana na ukawa mwisho wake.
Sekunde ambayo Regina anashituka kutoka kwenye mlio wa bunduki aliweza kukutana na maiti iliolala chini na hakuamini kidogo tu angepoteza maisha.
“Nadhani ushaniamini sasa nilichokuwa nikimaanisha , unadhani hawa watu watakuacha tu hivi hivi na wasifanye chochote baada ya kusaini mkataba , tena ndani ya hoteli ambayo wameiandaa wao?”Aliongea lakini Regina aliishia kutoa macho huku akitetemeka.
Hamza hakuwa na muda wa kupoteza alimsogelea Regina na kumnyanyua na kisha waliendelea kutembea kuzisogelea lift
Kitendo cha kuzifikia Hamza alimrudisha Regina nyuma kwa kuhofia kunaweza kuwa na maninja wengine waliojitega ndani ya lift , lakini sasa kitendo cha lift ile kufunguka Regina na Hamza walijikuta wakishikwa na mshangao.
Sio kwasababu wamemuona adui , hapana , ni kwasababu kitendo cha kufungua wanaume wawili waliokuwa wameshikilia bastora walidondoka mbele yao kama mafurushi wakionekana hawana fahamu huku nyuma akiwa amesimama Shangazi.
Shangazi Mariposa alikuwa amesimama akiwa na macho mekundu na wasiwasi kibao, mara baada ya kumuona Regina akiwa salama alivuta pumzi nyingi na kumsogelea.
“Regina uko sawa?”Aliongea huku akimchunguza Regina kwanzia kichwani mpaka miguuni huku akipatwa na ahueni lakini muda huo Regina alikuwa akiangalia watu waliokuwa wamepoteza fahamu chini bila hata ya kumjibu shangazi yake.
Ni kama ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuona Shangazi kuwa na uwezo wa kudhibiti wanaume wenye siraha tena wawili.
********
Upande mwingine siku hio hio walionekana Kanali Dastani na Amosi wakiwa katika gari ya Toyota Camry ya rangi nyeupe, gari hio haikuwa ikitembea bali ilikuwa imesimama nje ya lango la shule ya St Antonny maeneo ya Mbagala rangi tatu.
“Una uhakika dogo amekwisha kurudi shule?, mbona kama mapema sana kwa mtu aliefiwa?”Aliuliza jasusi mstaafu Amosi.
“Wakati nilipokuwa msibani kuna mtu nilimwachia kazi ya kunitaarifu, nina uhakika amerudi , msiba wa kiislamu hauchukui muda mrefu baada ya kuzika , atakuwa anasubiria arobaini kwasasa akiwa shuleni”Aliongea na Amosi alitingisha kichwa kukubaliana nae.
“Bado nashindwa kuamini kama Afande Mchuku aliacha hio rekodi hapa shuleni tena kwa mtoto wake ,si itakuwa ni kumuingiza kwenye hatari?”Aliongea.
“Upo sahihi ,Mchuku ana akili yule ,hawezi kuhatarisha maisha ya mwanae kwa ajili ya hela”
“Kama ni hivyo tunafanya nini hapa?”Aliuliza Amosi huku akionyesha hali ya kukosa utulivu.
“Kuna sababu mbili zimetuleta hapa , mosi Mchuku hawezi kuacha kitu cha hatari kwa mtoto wake , pili sehemu salama zaidi ni ile isio salama , kauli uliosema wewe inatufanya tuamini kuna kitu mchuku aliacha, ndio kilichotuleta”Aliongea Dastani na dakika ileile mlango mdogo wa geti la kuingilia shuleni hapo lilifunguliwa na alitoka mwalimu wa Kike alievalia gauni la kitenge.
“Madam niliewasiliana nae huyo hapo , wana visheria vikali hapa na bila sababu ya msingi tusingeweza kuingia”Aliongea Kanali.
“Kwahio unamaanisha hatuingii ndani?”
“Inategemea , tutoke nje ya gari kwanza”Aliongea na kisha alifungua mlango na kutoka nje na alifuatia Amosi vilevile.
“Neema naona Braza angu ashasababisha?”Aliongea Kanali huku akiweka tabasamu na kauli ile ilimfanya yule madam kujishitukia na kisha akacheka.
“Wewe umejuaje wakati hata kitumbo bado hakijatokea”
“Nina watoto watatu , maana yake nina uzoefu wa kutosha kutoa kwa mke wangu”Aliongea na kumfanya Neema kucheka.
“Halafu wifi akaondoka kimya kimya kwenda nje ya nchi bila kutuambia , Dastani una roho mbaya , unanifanya nione ni kama unanitenga , Jesca ni rafiki yangu ujue”Aliongea akilalamika na Kanali alimwangalia Amosi.
Ukweli aliwatoa nje ya nchi watoto wake kwa kumhofia Amosi na siku hio alishangaa kufanya kazi pamoja na Amosi licha wanachukuliana kama maadui.
“Safari ilikuwa ya haraka ile, unajua mfadhili wako akitoa maagizo unajikuta unatii tu, halafu wakati wanaondoka nilisikia sijui mpo Tour na wanafunzi wako Ngorongoro”Aliongea na Mwalimu Neema alionekana kumwelewa na kukubali kwa wakati mmoja.
“Haya umsema kuna maswali unataka kuniuliza na nimeshangaa?”
“Ndio , si unajua maswala ya ki upelelezi , huyu ni mfanyakazi wangu anaitwa Amosi nipo nae kwenye kesi inayohusiana na kifo cha Mkuu wa Magereza , Afande Mchuku”Aliongea Amosi.
“Unamaanisha baba yake Mchuku?”Aliuliza huku akionyesha mshangao.
“Ndio huyo , kumbe na huku wanamwita Mchuku?”
“Ndio alivyozoeleka”
Sasa tunataka kujua kabla ya kifo chake je alitembelea hapa shuleni?”
“Ndio habari iliohuzunusha walimu wengi na watoto wanaosoma na Mchuku , kila mtu anasema alikuja kumuaga mwanae kwa kukiona kifo chake mapema ndio maana mpaka ada alilipa ya miaka yote miwili aliobakisha”Aliongea.
“Unasema alikuja pia na kulipa ada?”Aliuliza Dastani mara baada ya kuangaliana na Amosi.
“Ndio wanavyosema , mimi sikuwepo ila kulingana na maneno ya Mhasibu alikuja akamuona Hassani na kisha akalipa ada ya mihula minne”Jibu lile ni kama lilitosha kuwajulisha ni kwanini Marehemu alitembelea shuleni hapo.
“Yaani imekuwa habari ya kuhuzunisha mno , lakini Dastani kwanini mnaonekana kushangaa , kuna zaidi juu ya Marehemu?”Aliuliza.
“Kuna taarifa hazijakaa sawa eneo alilokuwa anafanyia kazi ndio maana tunajaribu kuhoji watu walionana nae , kifo chake kilikuwa cha kawaida kabisa , kansa ya mapafu ni hatari mno”Aliongea Dastani kupotezea.
“Ndiio hivyo , ila ikishaamuliwa haijalishi una ugonjwa au huna , ili mradi zimefika ndio basi”Aliongea na wote waliunga mkono.
“Hivi Shemeji hapa ada kwa mwaka ni shilingi ngapi?”Aliuliza Amosi
“Hapa kila muhula ni milioni moja kwa mwaka ni milioni mbili ,hio ni ada tu nje ya michango mingine, sio kiasi kikubwa cha pesa kutokana na ubora wa elimu inayotolewa”Aliongea.
Neema alijua Amosi pengine anaulizia kwa ajili ya kuleta mtoto wake.
“Amosi hapa mtoto wako anapata elimu ya daraja A , Mwalimu Neema ni mfano wa walimu bora wanaopatikana ndani ya hii shule”Aliongea Dastani kumsifia na kumfanya Madam kucheka.
Baada ya kuongea kidogo waliishia kuagana na Amosi na Dastani walirudi ndani ya gari.
“Hatuonani na mtoto?”Aliuliza Amosi.
“Haina haja”
“Kwanini?”
“Kwasababu tulichotaka kujua ni kwanini Amosi amefika hapa , na tumejua amekuja kulipa zaidi ya milioni nne za hela kama ada , unadhani hela katoa wapi?”Aliuliza Dastani na Amosi alijikuta akitingisha kichwa.
“Unataka kusema amemuuzia mtu mwingine hio rekodi?”Aliuliza huku akionyesha kushangaa kidogo.
“Sina uhakika , lakini kwa ninavyomjua Mchuku uwezekano huo upo , kama sivyo basi kuna kitu alifanya , tunapaswa kwanza kufuatilia wapi katoa hela, tukijua hilo tutapata uelekeo mwingine”Aliongea Dastani.
“Huyu Mchuku anaonekana kuwa na akili mno”Aliongea Amosi.
“Unadhani asingekuwa na akili angeomba kupewa ukuu wa gereza la Silo?, pale ndio kuna wafungwa wa kila aina kuanzia wahujumu uchumi mpaka wauza madawa maarufu , mchuku alipaswa kuwa kitengo cha TISA kwa muda mrefu sana lakini aliangalia wapi atapiga hela”Aliongea Kanali na kumfanya Amosi kutigisha kichwa kukubaliana nae.
“Naomba isiwe tunapoteza muda tu ,halafu kwanza alifanikisha fanikisha vipi kurekodi mazungumzo ya siri namna hio?”Aliuliza Amosi na swali lile lilimfanya Kanali kumwangalia kwa mshangao.
“Swali zuri sana kijana , kafanikiwa vipi bila kugundulika? , sidhani waliokuwa wakiongea na mfungwa ni wajinga, tena wazungu kabisa wamuache afanye atakacho?”Aliongea na Amosi alitingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kuna uwezekano Mchuku alikuwa na mtaalamu anaemsaidia kazi, hili tunafanya kulifanyia kazi kwa wakati mmoja sasa hivi , wewe unaonaje ukienda gerezani kujua kama kuna mtu alikuwa akishirikiana nae na mimi nishughulikie wapi katoa hela?”Aliongea Kanali na Amosi alikubaliana nae.
Dakika chache baadae waliachana Amosi akielekea uelekeo wa Gereza la Silo, huku Amosi akielekea makao makuu kwa ajili ya kupata kibali cha kuangalia akaunti za benki zote zonazohusiana na Mchuku.
Ukweli ni kwamba alijiambia kama sio rekodi hio kutakiwa na wakuu wake angetumia hata njia ya kumtafuta mfungwa aliehusika katika hayo maongezi na kumtesa mpaka aongee.
“Amosi nitakutumia mpaka ufanikishe hili na baada ya hapo utanisamehe”Aliwaza Kanali Dastani.
Wakati akiwa njiani simu yake ilianza kuita na jina lilijitokeza Tresha , aliishia kutoa tusi la chini chini huku akipokea simu.
ITAENDELEA JUMANNE SAA 5 USIKUWATSAPP 0687151346