SHETANI RUDISHA AKILI ZETU.
MTUNZI: SINGANOJR
SEHEMU YA 93.
Haikuwa rahisi kwa Regina kuondoka ndani ya eneo hilo amuache Shangazi yake , Familia yake yote ilikuwa imekwisha kutangulia mbele za haki na mtu pekee ambae alikuwa ni mwanafamilia alikuwa ni Shangazi na kama atauliwa na huyo mtu ingekuwa ngumu mno kwake kukubaliana na swala hilo.
“Naomba uache , Mzee Suwi sikujui wewe ni nani , lakni naomba uache unachokifanya tafadhali”Aliongea Regna lakini bwana alieitwa Mzee Suwi hakuwa na nia ya kuacha.
Muda huo Shangazi alikuwa ashasukumizwa kwa shambulizi na kwenda kugonga mlima na kufanya mawe kuanza kuporomoka wakati huo huo akiachia shambulizi la wimbi la upepo kumshambulia Mzee Suwi lakini bwana yule alionekana kuwa mtaalamu kwa kile alichokifanya kwani alichezesha vidole na wimbi la upepo lilimrudia Shangazi kwa nguvu.
“Bam!!”
Nguvu halisi ya nishati za mbingu na ardhi ililiripuka na kumfanya Shangazi kutoa yowe la maumivu huku kila kiungo cha mwili wake kikiwa kimekufa ganzi kutokana na maumivu makali.
“Ndio kwanza upo kwenye levo ya Wito na mimi mwishoni mwa levo ya Wito , nimekuacha hatua nne mbele , huwezi kunishinda hata kidogo”Aliongea Suwi huku akitoa tabasamu la ujivuni na kupiga hatua mbele kutaka kumkamata Shangazi.
Shangazi alichokifanya ni kusogea upande wa kushoto kwake na kisha alifyatua jiwe kwa nguvu kubwa na lilienda moja kwa moja kutua kwenye kifua cha Suwi.
“Boom!!!”
Haikueleweka kilichotokea lakini jiwe lile kabla halijamdhuru lilipasuka vipande vipande kana kwamba limepasuliwa na bomu.
“Una uwezo wa kuita Kinga ya nishati za mbingu na ardhi!?”Aliuliza Shangazi kwa mshangao.
“Kama unaijua Kinga ya nishati ya mbingu na ardhi basi jua huniwezi hata kidogo hivyo jisalimishe”Aliongea Mzee Suwi.
“Siwezi kujisalimisha kirahisi , hata kama nikiishiwa uwezo wangu wote siwezi kukuacha ufanikiwe”Aliongea Shangazi kwa ujasiri mkubwa huku akimgeukia Regina na Hamza ambao bado walikuwa wamesimama wakimwangalia.
“Hamza mbona bado umesmama hapo , ondoka na Regina haraka”
Licha ya kuongea hivyo Hamza hakuongea wala kufanya chochote,alionekana tu akifikiria kitu huku sura ikiwa imejikunja
Hata Regina hakutaka kuondoka na alimshika Hamza shati akimuomba amsaidie shangazi yake na Hamza licha ya kuombwa hivyo alisita kidogo na alimgeukia Regina na kumuuliza kama yupo tayari kuitoa pete kwenda kwa Suwi ili vita hio iishe.
Swali hilo la Hamza lilimfanya Regina kukosa jibu la moja kwa moja maana ni kama hakutegemea Hamza angemuuliza swali la namna hio.
“Kuna mawili hapa, kumsaidia Shangazi au kuondoka na wewe , lakini hata kama tukiondoka lazima watakuja tena kututafuta maana pete tunayo, labda tu uwe tayari kuwapa”Aliongea Hamza.
“Hio pete ni kitu ambacho babu yangu na bibi wamekitunza kwa hali na mahali kwa muda mrefu , haiwezekani kuikabidhi kirahisi hivyo”aliiongea Regina.
“Lakini ujue ndio mwanzo wa matatizo”
“Matatizo hayajawahi kuisha , mshindi pekee ndio anakuwa huru , simjui huyu mzee ni nani lakini ni bora nife kuliko kumpigia magoti”aliongea Regina kwa kiburi cha hali ya juu.
Hamza mara baada ya kusikia kauli hio kutoka kwa Regina macho yake yalisinyaa huku akitoa tabasamu hafifu na alinyoosha mkono wake na kumshika Regina kidevu.
“Kama nilivyotarajia , nimeoa mwanamke jasiri”Aliongea
“Wewe unanifanyia nini?”Alongea Regina mara baada ya kuona anashikwa kidevu kwa namna ambayo hapendi.
“Usiwe na wasiwasi kwasasa ninachojua mimi Shangazi hawezi kufa kirahisi”Aliongea Hamza lakini kauli yake ilimfanya Regina kuchanganyikwa, lakini dakika ileile macho yake ni kama yameshkwa na ukungu kwani Hamza alipotea mbele yake.
Upande wa Suwi alikuwa amekusanya wimbi kubwa la nishati ya mbingu na ardhi kwenye mkono wake kwa ajili ya kumshambulia nalo Shangazi.
Kutokana na Shangazi kuwa upande wa mlima ilimfanya kukosa namna ya kukwepa shambulizi hilo na kitu pekee alichofanya ni kuitutumua nguvu yake ya ndani ili kupokea pigo hilo, lakini wakati shambulizi lile linamsogelea ghafla tu kivuli cha mtu kilitokea mbele yake kama mzimu.
“Bam!”
Haikueleweka Hamza alifanya nini lakini mara baada ya kuinua mkono wake wa kulia kama anapunga upepo shambulizi la Suwi lilishindwa kumfikia yeye na Shangazi huku Suwi akikosa balansi na kudondoka chin kutokana na upepo uliotokea, mara baada ya kusimama na kuangalia upande wa Hamza alijikuta akishangazwa na jambo lile.
“Ni wewe?”
Mzee Suwi hakuweka umakini wake juu ya Hamza tokea mwanzo, kwasabbau Hamza hakuwa na msisimko wowote wa nishati ya mbingu na ardhi.
Lakini sasa sekunde hio mara baada ya Hamza kuzuia shambulizi lake na kumsukuma kiasi cha kudondoka ilimfanya kushikwa na mshituko mkubwa.
Hata Shangazi mwenyewe alijikuta akishangazwa na jambo lile , alikuwa akijua Hamza sio mwepesi tokea mwanzo lakini hakuwahi kuushuhudia uwezo wake.
“Shangaz vipi upo sawa?”Aliuliza Hamza na Shangazi alitingisha kichwa akikubali huku akihema kama mbwa.
“Wewe ondoka na Regina , niache hili swala nitadili nalo”Aliongea
Ktendo cha Shangazi kusikia kauli hio kutoka kwa Hamza alijihisi kifua kumpanda na kumshuka kutokana na presha kubwa.
Shangazi alikuwa na uzoefu mkubwa mno na alihisi kabisa uwezo wa Hamza sio wa kawaida na hauwezi kueleweka , ukweli ni kwamba tokea aanze kukaa nae alikuwa akimfuatilia mienendo yake hata kule kucheza mdundiko asubuhi asubuhi kwake hakuchukulia kama Hamza anacheza mdundiko bali aliona kitu ambachho sio cha kawaida.
Shangazi aliishia kuitikia tu huku sauti yake ikionekana ya heshima na baada ya hapo alimsogelea Regina.
“Wewe lazima utakuwa ndio mume wa Regina , kama sikosei jina lako unaitwa Hamza , si ndio?”Aliongea Mzee Suwi na Hamza aliishia kutoa tabasamu tu na muda uleule alingiza mkono wake kwenye mfuko na kutoka na ile pete.
“Unachotafuta ni hii pete sio?”Aliuliza.
Yule mzee mara baada ya kuona hio pete macho yake yalichanua huku akinyoosha mkono kuelekea kwa Hamza.
“Nipatie hio pete haraka maana sio ya kwako”
“Hii Pete ni ya kwangu na alieniachia ni Bibi Mirium”
“Acha kuongea ujinga na nipatie haraka”Aliongea yule bwana huku akiwa amekunja sura.
Upande wa Hamza hakubadili muonekano na palepale aliivaa kidoleni huku akiongea kwa kumwemwesha maneno ya kingereza.
“See-the -Truth”
Maneno yale yalimfanya Mzee Suwi kutetemeka kidogo huku uso wake ukikakamaa lakini hakuonekana kukata tamaa juu ya kupata pete ile.
“Wewe sio mwanachama wa Binamu wala huna hadhi ya damu ya watu wa Kondeni, hata uvae hio pete huwezi kuniamrisha”Aliongea.
“Kulingana na sheria za jicho la anga , haimzuii mtu ambae asie wa urithi wa damu wala asie mwanachama wa Binamu kutokuwa Mkuu wa miliki ya watu wa Kondeni, isitoshe pia umekuja peke yako hapa ikionyesha sio makubaliano ya umoja unaotokea , lakini bado nimevaa hii pete unashindwa kupiga magoti na kuonyesha heshma, kama wakuu wako wakijua hiki unachokifanya , unadhani ni kipi kitakachokutokea?”Aliongea Hamza.
“Wewe ni nani na kwanini unazijua sheria hizi za jicho la Anga kutoka Kondeni?”Aliuliza huku akiwa na mshituko na wasiwasi.
“Haha.. kama nilivyootea unaonekana umetokea Binamu bila idhini ya wakuu wako”
“Itategemea kama utakuwa hai na kusambaza taarifa zangu la sivyo sina cha kuogopa”Aliongea na palepale ulitokea mkandamizo mkubwa wa nishati ya mbingu na ardhi na ghafla tu kwenye mikono yake kulitokea tufe la hewa la rangi nyeupe na alilirusha kuelekea aliposimama Hamza na mpira ule wa nishati uligeuka na kuwa kama mshale wa moto mweupe ukitaka kumshambulia Hamza kila pande.
Hamza upande wake hakuonyesha kushitushwa na shambulizi lile na alisimama sehemu moja kama mtu ambae hakuwa na nia ya kukwepa.
Upande wa mbali , Regina na Shangazi walijikuta wakishikwa na kiwewe mara baada ya kuona Hamza amesmama tu bila ya kufanya chochote wakati anashambuliwa.
“Hamza kimbia, kimbia!”Regina alishindwa kujizuia na kumpigia Hamza makelele.
Upande wa Mzee yule mara baada ya kuona Hamza anakaribia kumezwa na moto wa nishati ya mbingu alijikuta akitoa tabasamu la ushindi.
“Bang , Bang , Bang!!!”
Ulikuwa ni mlipuko mkubwa ambao haukuwa na moto uliosikika na kusababisha upepo mkubwa kiasi cha baadhi ya miti ambayo haikuwa na mashina imara kudondoka huku sehemu aliosimama Hamza ikiwa mefunikwa na wingu kubwa kama la mvuke na kumfanya asionekane.
Sasa mara baada ya kiwingu kile kuisha wote walijikuta wakishangaa mara baada ya kutokumuona Hamza , hata kama ameyeyushwa na shambulizi hilo jambo ambalo haliwezekani mifupa ingebakia lakini haikuonekana kitu kilichomfanya Mzee Suwi kuona kuna kitu hakipo sawa na kuanza kugeuza uso wake kulia na kushoto akimtafuta Hamza.
“Unanitafuta?”Aliongea sauti ya kichokozi ilisikika nyuma yake na kumfanya Mzee huyo kutetemeka.
Kitendo cha kugeuka na kumuona Hamza akiwa nyuma yake bila kuonyesha ishara yoyote ya kuumia alijikuta macho yakimtoka.
“Nishati za mbingu na ardhi siku zote zina nguvu kubwa , hakuna ubishi wa wewe kutokea Kondeni, lakini kwa bahati mbaya hata kama shambulizi lako lina nguvu kiasi gani litaweza kumuua mtu ambae sio mjuzi pekee”Aliongea Hamza huku akicheka.
“Wewe.. umewezaje..”Mzee Huyo hakuweza kuelewa Hamza amepotea poteaje katika eneo la shabaha yake , kilichomchanganya Hamza hakuwa na ishara yoyote ya kutumia nguvu mbingu na ardhi , sasa alijiuliza ina maana Hamza ametegemea pekee uwezo wake wa kuruka ndio maana ameweza kukwepa shambulizi lake.
“Mimi sio levo yako acha kujihangaisha , hivyo kabla sijawa siriasi ni bora ukaondoka”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Suwi kushikwa na hasira mno kwani aliona ni kama kudharauliwa uwezo wake na kwa ukaribu aliokuwepo kati yake na Hamza alijiambia hawezi kumwacha aondoke hata kidogo hivyo alipanga kumshambulia , lakini Hamza alikuwa na spidi mno kwani palepale alimsogelea kwa spidi na kumshka mkono kwa nguvu.
“Narudia tena, mimi sio levo yako hivyo ondoka hapa?”Alongea Hamza kwa msisitzo na baada ya hapo alimvuta kwa nguvu kupitia ule mkono wake na kumrusha.
Mzee Suwi alijikuta akizunguka zaidi ya mara nane hewani kutokana na namna alivyorushwa na kwenda kudondokea kwenye makaburi..
Baada ya kujigonga chini alihisi maumivu makali mno , huku mkono ambao Hamza aliutumia kumrushia uliumia mno na alihisi ni kama umejitegua kutoka kwenye viungio vya bega.
Tukio lile lilimfanya Shangazi aliekuwa akiangalia kushikwa na mshituko wa hali ya juu mno , Regina ambae alikuwa na uwezo wa kibinadamu wa kawaida hakuweza kuona kilichotokea lakini Shangazi aliona kila kitu.
Kilichompagawisha zaidi ni Hamza kutotumia nishati za mbingu na ardhi maana kwa uwezo wa binadamu wa kawaida ni ngumu kumrusha mtu umbali ule bila ya nguvu za ziada.
Makisio pekee ambayo alikuja nayo ni labda Hamza anajifunza mbinu ambayo inaenda kinyume kabisa na kanuni ya nishati za mbingu na ardhi, lakini alijiuliza kam ni hivyo inawezekana vipi maana hakuwahi kusikia kitu cha namna hio.
Mzee Suwi ambae alikuwa amechafuka matope kwenye mlima kutokana na mvua aliishia kukaa chini huku akiwa haelewi , hakujua hata ni kwa namna gani alirushwa na alijishitukia tu yupo hewani.
Alijikuta akiangalia Hamza alipo na aliona kuna umbali wa mita nyingi mno na kwa mantiki hio mtu yoyote anaweza kuamini ili kumrusha mtu kwa umbali huo Hamza ametumia nguvu nyingi sana.
“Pumbavu, wewe mwanaharamu ni nani wa kunitesa kiasi hiki?”Aliongea kwa sauti kubwa na Hamza aliishia kumwangalia Suwi akiwa upande wa chini wa makabuli na alipiga hatua mbili tu alikuwa ameshafika alipo.
Mzee Suwi mara baada ya kuona Hamza anamsogelea , haraka haraka alirudi nyuma akionekana kumhofia kwani hakuwa akimjua Hamza vizuri.
“Huna haja ya kuogopa maana sina mpango wa kukupiga, nadhani unachopaswa ni kufikiria namna ya kudili na kitakacho kutokea”Aliongea Hamza na palepale alinyoosha mkono kuelekea nyuma yake.
Mzee Suwi mara baada ya kugeuza sura alijikuta mwili wake ukimtemeka.
Kulikuwa na mwanaume mtanashati mno alievalia suti , Mzungu ambae ana nywele nyeusi ndefu zilizofungwa na kibanio nyuma , hakuwa peke yake bali ametangulizana na watu waliovalia sare za majoho ya rangi kama vile ni wachungaji , sawa kabisa na namna ambavyo Mzee Suwi alikuwa amevalia.
“Suwi umeamua kukiuka sheria za jicho la Anga na kuja hapa kwa ajili ya kuipoka pete, hili swala limekwisha kuripotiwa kwa mkuu wetu na tumekuja hapa kukukamata na kukurudisha Kondeni ukapate adhabu yako inayokustahlili”Aliongea yule bwana Mzungu kwa lugha ya kingereza.
"Huge unaongea ujinga gani , nipo hapa kwa maagizo ya baba kwa ajili ya kutoa heshima zangu za mwisho kwa marehemu na sijaja kukwapua pete”Aliongea Mzee Suwi na muda ule alimgeukia Hamza.
“Pete unayozungumzia ipo kwenye mikono ya mtu wa nje ya umoja wetu ambae hana urithi wa damu”Aliongea huku akimnyooshea kidole.
Yule bwana aliefahamika kwa jina la Huge mara baada ya macho yake kutua kwa Hamza hasa kwenye kidole chake muonekano wake ulibadlika.
“Wewe ni nani?”Aliulza yule bwana Huge , lakini Hamza tofauti kujibu aliishia kutoa tabasamu.
“Mkuu kwahio kumbe unaitwa Huge?”Aliuliza.
“Vipi kama nikiitwa Huge?”
“Kwasababu Huge ni jina la ukoo , nikuulize je unamjua Mathiasi Huge?”Aliongea Hamza na swali lake lilibadilisha muonekano wa yule bwana mara moja.
“Unamfahamu vipi Master wangu?”Aliuliza kwa kingereza.
“Oh, kumbe ni mwalimu wako?” Aliongea Hamza huku akionekana kutaka kuongea kitu lakini alisita na kubadili mada.
“Nadhani mnapaswa kuondoka ndani ya hili eneo , ijapokuwa sijui ni kipi kinaendelea huko Kondeni na ndani ya kitengo chenu cha Binamu, lakini hii pete ni ya mke wangu , kama hataki kuwapatia basi hamuwezi kuichukua”Aliongea Hamza.
“Wewe ndio mume wa Regina?, kama ndio hivyo basi utakuwa unajua hio ni pete ambayo sio kila mtu anaweza kuivaa”Aliongea.
“Kwanza kabisa mim na Regina ni wanandoa hivyo huwezi kuniita mtu yoyote , pili hata kama nitake kuivaa huna cha kunifanya”Aliongea Hamza.
“Huge unamsikia , yaani anasema anaweza kufanya atakalo na hatuna la kumfanya , unadhani hii ni sawa?”Aliuliza Suwi.
“Kuhusu hili sina mamlaka nalo , nitaenda kuripoti kwa wakuu na ndio watakaofanya maamuzi , kuhusu wewe huna haki ya kuuliza chochote”Aliongea Huge na kumfanya Suwi kuishia kukunja sura kwa chuki, lakini bwana alefahamika kwa jina la Huge hakuwa na muda nae na alimwangalia Hamza kwa shauku.
“Sijawahi kumsikia Master akikuzungumzia , unafahamu vipi jina lake?”
“Simjui Master wako mimi , kwanini unauliza au unataka kushindana na mimi?”Aliuliza Hamza.
“Hio pete haiwezi kuvaliwa na mtu ambae hafahamiki”Aliongea Huge akiwa siriasi.
“Inaonekana watu wa Kondeni siku hizi mmechuja , yaani pete ipo kidoleni lakini hamuonyeshi heshima yoyote?”
“Kama sio heshima yetu , tungekuwa tushakushambulia sekunde tuliofka hapa”Aliongea na muda ule Hamza alinyamaza kimya akionekana kuwaza.
“Vipi kuhusu Selaph..”Aliongea Hamza na kauli ile ilivyomtoka Huge palepale muoenekano wake ulibadilika mara moja na wote walirudi nyuma kana kwamba wamekutana na adui mkubwa zaidi yao.
Wote walionekana kuwa na wasiwasi na mara baada ya kumwangalia Hamza na kuona hakukuwa na ishara za ukali alionyesha heshima yake.
“Since that’s the case , we’ll leave first and report this to my master”Aliongea akimaanisha kwamba kwasababau ipo hivyo basi wataondoka na kutoa ripoti kwa Master wao.
Muda ule Suwi na yeye alionyesha shara ya woga , alijua sasa kwanini Hamza alikuwa akmwambia sio levo yake , alijikuta akishukuru bado alikuwa hai.
“Mwambieni mkuu wenu kwamba , pete niliokuwa nayo ni ya mke wangu na itabakia kwangu kwa usalama kwanzia sasa na kwasababu ya amani iliokuwepo kati yetu na yeye haina haja ya kufanya mambo kuwa magumu”Aliongea Hamza
“Nitampatia taarifa hio kama ulivyoongea , Farewell”Aliongea na palepale aliawapa ishara wasaidizi wake wawli pamoja na Suwi na kisha walitoweka ndani ya hilo eneo.
Baada ya watu wale kuondoka hatmae hali ya utulivu ilirudi kwa mara nyingne na Hamza alivua ile pete na kisha alimkabidhi Regina.
“Regina unaonaje ukikaa nayo?”Aliuliza Hamza.
Regina aliishia kumwangalia Hamza na muonekano usiokuwa ukielezeka , ijapokuwa alkuwa ameshikiliwa na Shangazi kwa sababu za ki usalqama lakini aliweza kujua mambo mengi bila hata ya kuambiwa.
“Ulijua tokea mwanzo itakuletea matatizo sio?”Aliuliza Regina akikumbuka wakati ule alionekana kukataa na ni kama sasa anajua sababu iliokuwa nyuma yake.
“Ndio nilijua”Aliongea.
“Kama ni hivyo kwanini bado ukaipokea?”
“Siku zote anaekubali kupata lazima akubali kupoteza , kukubali kumuoa mwanamke mrembo kama wewe haiwezi kuwa bure”Alongea Hamza huku akicheka.
“Kwahio kwa kutaka kunioa ndio ukaamua kuhatarisha maisha yako kwa kupokea kitu cha hatari?”
“Regina babe , haina haja ya kuwa siriasi namna hio , nipo sawa”
“Lakini vpi kama ukifa?”Aliuiza Regina.
“Kama ni hivyo sitojutia kukuoa?”
“Wewe.,, wewe ni mjinga. Kichaa kabisa”Aliongea Regina huku sura ikimshuka.
“Regina tunapaswa kumshukuru Madam kwa kuona mbali , sikukosea nilivyomfikiria Hamza “Aliongea Shangazi na Regina macho yake yalianza kuwa mekundu.
“Tokea mwanzo mpaka sasa ni mimi pekee ambae sikuwa nikijua kinachoendeleam, najiona mjinga kweli”
“Kwanini unafikiria hivyo , tulifanya hivyo kwa ajili ya kukulinda , kuna vitu vngi sana kama ungejua mapema ungekuwa kwenye hatari kubwa”Aliongea Shangazi.
“Vipi kuhusu sasa , je sipaswi kujua ni kipi babu na bibi walikuwa wakinificha tokea mwanzo , kwanini hawa watu wamekuja na kuanza kuulizia hii pete , nataka kujua kila kitu”Aliongea Regina.
“Kuhusu hili..”Shangazi alionekana kusita.
“Shangazi sioni kuna haja ya kuendelea kumficha, mimi pia kuna vitu vngi sijaelewa na natarajia kuvijua kutoka kwako , ni kheri ukatuambia kila kitu ili tujue tunajilinda vipi baadae”Aliongea Hamza.
“Basi hakuna shida , nitawaeleza kila kitu maana sikutarajia kama watajitokeza mapema hivi , tukirudi nyumbani tutakaa chini na tutaongea”Aliongea Shangazi
Hamza na Regina hawakuwa na haraka , baada ya kuweka kaburi la bibi yake vizuri waliondoka na kurudi kwenye jumba lao la kifamilia na giza lilikuwa lishaingia tayari.
Kwasababu kulikuwa na baridi waliandaliwa chai ya moto na wahudumu na kisha wote walikaa kwenye masofa ili kumsikiliza Shangazi anachokwenda kusema.
Shangazi mara baada ya kuvuta pumzi kwa sekunde kadhaa , alionekana kukosa namna ya kuanza na alimwangalia Hamza kwanza.
“Hamza wewe unajua nini kwanza , hebu ongea na nitaongezea”Aliongea na Regina muda ule alimgeukia Hamza na kumwangalia kwa macho yake mazuri.
Hamza alitingisha kichwa chake kukubaliana nae na kisha alimwangalia Regina.
“Regina unakumbuka ile juzi nilivyokuwa nikikuelezea kuhusu madaraja ya taasisi na makundi ya ulimwengu wa Giza na nikaelezea kwa ufupi kuhusu taasisi ya daraja S?”Aliuliza Hamza.
“Ndio ulisema Daraja S ndiio la juu kabisa na wamefikia katika hatua hio kwa kupata maksi sawa na Ratio ya moja kwa Elfu kumi na kuendelea”Aliongea Regina na Hamza alitingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kama ulivyosema , mpaka sasa dunia nzima kuna makundi au taasisi kuu tatu za siri ambazo zipo daraja S na kati ya taasisi hio moja wapo ni taasisi ya siri inayofahamika kwa jina la SkyEye au unaweza kuita watu wa Kondeni na wana tawi lao maarufu la kijasusi dunani lenye makao makuu yake katika ukanda wa Africa walilolipatia jina la B-I-N-A-M-U, kirefu chake ni Bureau of interdimensional Nexus and Multiversal understanding”
“Inasemakana kwamba hakuna kitu ambacho dunia iwe inafanya na kisifahamike kwao , ki ufupi ni kwamba hakua siri ambayo inaweza kufichwa mbele ya watu hawa wa Kondeni, ikitokea wakitaka kujua kitu chochote basi uwezo huo wa kujua wanao na si vnginevyo, wanajua siri nyingi sana , siri ambazo zinaweza kuiweka dunia hatarini kama wakizitoa na hata kuwafanya viongozi wakubwa kujisalimisha kwao, hakuna nchi wala kiongozi ambae anaweza kwenda kinyume zidi yao , hata kama uwezo wao wa kupigana ni mdogo lakini mfumo wa intellijensia ambao wameutengeneza miaka na miaka umeshikilia dunia nzima , hivyo ndio maana wakaamua kuitwa mfumo wao wa intellijensia Jicho la Anga , maana yake wanaona kutoka angani, moja ya lugha yao ya kutambuana ni kupitia kutamka neno la See-the- truth, maana yake ikiwa ni kwamba ukweli wa mambo yote hauwezi kuonekana isipokuwa kwa neno la pete ya Kondeni”Aliongea Hamza na maneno yale yalimshangaza mno Regina.
“Kwahio unasema kwamba babu na bibi walikuwa wanachama wa huu umoja wa siri?”Aliuliza.
“Hawawezi kumiliki pete na wasiwe wanachama , kwa kile ninachojua mwanacama ambae anamiliki pete basi cheo chake ni kikubwa mno, lakini hata hivyo ni mara yangu ya kwanza kusikia Mwafrika kumiliki pete yenye nguvu namna hii ya huu umoja na kisha akaonekana kama sio mwanachama , hiki ndio kitu ambacho kinanifanya kuwa na shauku ya kutaka kujua zaidi”Aliongea Hamza.
“Hamza mpaka hapo upo sahihi na inaonekana kweli unajua mambo mengi, ngoja niendelee sasa kwanzia hapo..”Alionea Shangazi na kuvuta pumzi.
“Nadhani Regina hujawahi kusikia ila babu yako Mzee Dosam hakuwahi kuifahamu famiilia yake kwasababu mama yake alibeba ujauzito baada ya kubakwa”Aliongea Shangazi na kauli ile ilimfanya Regina kushangaa.
“Shangazi unamaanisha Babu hakujua familia yake?”
“Sijasema hakuijua familia yake , mama yake ndio ilikuwa familia yake pekee, wakati mama yake anapitia kitendo hicho cha kusikitisha ndio alipoweza kuipata hio pete”Aliongea na kauli hio hata Hamza alimshangaza.
“Unamaanisha aliokota ama ilikuwaje?”Aluliza Hamza.
“Hapana sio kwa kuikotota , kwa maelezo yake mama yake Dosam alisema wakati akitokewa na kitendo hicho kulikuwa na mwanaume ambae alikuwa akiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea na alijitahidi kuomba msaada kwa mtu huyo amsaidie asifanyiwe kitendo hiko , lakini yule mwanaume hakufanya chochote zaidi ya kuangalia tukio zima linafanyka mwanzo hadi mwisho na wale wabakaji kutoweka , anasema alichogundua juu ya yule mwanaume aliekuwa akiangala tukio lile, wale wabakaji hawakuwa wakimuona kama yeye alivyokuwa akimuona ndio maana hata baada ya kuomba msaada yule mtu hakuweza kusaidia , baada ya kupoteza fahamu alipokuja kushituka yupo eneo lilelile lakini yule mtu aliekuwa akimwangalia hakuwepo tena lakini aligundua kidoleni alikuwa amevishwa pete ambayo ndio hii sasa”Aliongea Shangazi na stori hio fupi ilimshangaza mno Hamza na Regina.
“Kwamba huyo mtu alikuwa ni kama kivuli tu na Mama yake Babu ndio mtu pekee aliekuwa akimuona?”
“Ndio hvyo kwa maelezo ya babu yako , alivyosimuliwa na mama yake”
“Baada ya hapo nini kilitoke?”
“Alibeba ujauzito ambao ndio ulimleta Dosam duniani , baada ya Dosam kufikisha umri wa miaka kumi na mbili mama yake alifariki na kabla ya mama yake kufariki alimuagiza Dosam kutafuta maana ya hio pete ni nini na kwanini mtu yule hakuonekana na wale watu , Dosam alimwamini mama yake juu ya stori yake kutokana na ushahidi wa hio pete, baada ya mwaka mmoja wa kifo cha mama yake ndipo alipokuja kukutana na Madam yaani bibi yako”
“Bibi!?”
“Ndio bibi yako na ndio kipindi ambacho Dosam alizama penzini na bibi yako na ndio huyo huyo ambae alimwambia maana ya hio pete”
“Unamaanisha Bibi Mirium alikuwa akijua maana ya hio pete?”AliulizaHamza.
“Kwasababu bibi yako asili yake ni ya watu wa Kondeni na baba yake alikuwa mwanachama mwenye cheo kikubwa ndani ya umoja huo na kwa muda mrefu umoja huo ulikuwa ukiitafuta hio pete”Aliongea.
“Kwahio baada ya hapo kipi kilimtokea Babu?”
“Kulingana na imani ya kimaandiko , Dosam alikuwa akisubiriwa na sio kutafutwa , kwani mara baada ya kuelezea namna alivyozaliwa ni kama ambavyo maandiko yalivyokuwa yametabiri , mtoto atakaezaliwa kutokana na mama yake kubakwa na kumiliki hio pete na ndio mwanzo wa damu mpya , hivyo Dosam mara baada ya kuelezea historia ya mama yake mara moja alitambulika kama mmiliki halali wa hio pete na kiongozi kulingana na sheria za umoja lakini Dosam alikataa kuwa kiongozi na kitu pekee alichohitaji ni Madam kuwa mke wake na kwasababu yeye na Mirium walikwisha kupendana tokea wakutane hakukuwa na pingamizi. Mara baada ya Ndoa Dosam alijiondoa kwenye Umoja na kutokana na Mirium kutokuwa na ndugu zake wengine , uongozi ukahama kutoka kwa baba yake ambae alifarki na kwenda kwa familia nyingne ambayo ni ya kizungu ambayo ni ya Huge, lakini licha ya kujitoa Dosam aliendelea kubakia kuwa mmiliki wa Pete na mtu mwenye ushawishi Kondeni, hivyo kujibu swali lako babu yako alikataa kujihusisha na maswala ya umoja , ila bibi yako alikuwa ni mzaliwa wa huko Kondeni”Aliongea Shangazi na maneno yote yalimshangaza mno Regina.
“Lakini kulingana na imani ya umoja na maandiko waliokuwa wakifundisha , kitendo cha Dosam kujitokeza ilikuwa ni kitu kilichosubiriwa kwa muda mrefu kwa maana iliaminika uzao wake utakuwa ni watoto wenye akili sana waliojaariwa vipaji , ambao wataweza kujifunza kuvuna nishati za mbingu na ardhi na kufikia levo ambazo hazijawah kufikiwa, hivyo hata baada ya baba yako Wilsoni kuzaliwa babu yako alifuatwa na watu wa Kondeni wakitaka kumchukua kwenda kumfunza mbinu za mapigano pamoja na nshati za mbingu na ardhi , lakini baada ya kumchunguza Wilsoni ilikuwa nje ya mategemeo kwani hakuonekana kuwa na akili nyingi.
Mzee Dosam licha ya kutokujihussha na umoja huo alihofia usalama wa familia nzima kwasababu watu ambao walikuwa na nguvu ndani ya umoja ambao alikuwa akiwategemea walianza kufariki , hata kama angesema familia yake ijilinde kwa kurudisha hio pete bado tu usalama usingekuwepo kwasababu historia ilikuwa ikimbeba’”
“Unamaanisha kwasababu alizaliwa kulingana na kile kilichotabiriwa?”Aliuliza Hamza.
“Hakika , ndio maana alichukua jukumu la kumrudisha Regina kwenye familia na mpango wake ilikuwa ni kumuingiza Regina kwenye mafunzo ya mapigano na sio kumrithisha kampuni , lakini familia ya Huge ndani ya umoja huo ilikuwa tishio na ilikuwa ikimfuatilia babu yako kwa kila hatua, hivyo kitu pekee walichofanya ili kuhakikisha amani inaendelea waliamua kuingia katika makubaliano ya kutoingilia maswala yote yanayoendelea ndani ya Umoja na pia kuishi kimya kimya”Aliongea
“Mimi nnachoona hapo Mzee Dosam na Bibi Mirium walikuwa wakijidanganya tu , kwa ninachojua huu umoja unajali sana kitu kinachoitwa urithi wa damu kuliko kitu chochote na ni muda tu haujawadia ila muda wowote watamtaka Regina kama mwanafamilia pekee aliebakia ambae ana damu ya urithi au kumuua kabisa asije kuhatarisha nafasi yao ya kimamlaka”Aliongea Hamza.
“Kwa ufupi ni kwamba licha ya kwamba upo sahihi , lakini wanachokiwinda sio urithi wa damu pekee?”
“Unamaanisha nini Shangazi?”Aliuliza Hamza kwa mshangao.
SEHEMU YA 94.
Hata Regina alishangaa mara baada ya Shangazi yake kuongea kauli hio na alitaka kujua.
Upande wa shangazi alionekana kusita kuongea na aliishia kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha.
“Ni kuhusiana na upande wa pili wa Regina”Aliongea Shangazi na kauli hio ilimfanya Edna kushituka.
“Shangazi!!”Aliongea Regina huku akionyesha shara asiendelee kuongea kwani ni kama alishajua Shangazi anataka kuongea nini.
“Unamaanisha juu ya Regina kuwa na split personality?”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Regina kushituka na hata shangazi alishangaa.
“Ulikuwa ukijua?”Aliuliza Shangazi.
“Ndio nilikuwa nikijua”Aliongea Hamza lakini upande wa Regina aliishia kumwangalia kwa muonekano ambao haukuwa ukielezeka amekasirika Hamza kufahamu siri yake ya kuugua akili au alikuwa na hisia za kutaka kujua amefahamu vipi.
“Regina wewe ni mke wangu tayari , huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu hili , nilikuwa nikikusubiria uniambie mwenyewe lakini kwasababu hili ni sawala linalohusu usalama wako sina haja ya kuficha kama najua”Aliongea Hamza na Shangazi alimuunga mkono Hamza.
“Alichoongea Hamza ni sahihi , unapaswa kumwambia kila kitu ili kujua namna ya kukulinda”Aliongea Shangazi lakini Regina bado hakuwa ameridhika bado , lakini kwa muda huo alilifanya swala hilo kiporo.
“Shangazi kwahio kuna uhusiano gani wa Regina kuwa na utu wa aina mbili?”Aliuliza Hamza.
“Sina uhakika wa maelezo yote , kitu pekee ambacho Madam aliniambia ni kwamba Regina sio mgonjwa wa akili na hali yake ya kubadilika ni kutokana na kuamka kwa nafsi nyingine ndani yake”
“Kuamka kwa nafsi nyingine ndani yake, unamaanisha kitu kama reincarnation au?”Aliuliza Hamza kwa mshangao.
Reincarnation ni hali ya mtu kuzaliwa upya katika mwili wa mtu mwingine.
“Shangazi huna haja ya kuupamba ugonjwa wangu , ipo hivi nikipatwa na shida ya akili nabadilika na kuwa mtu mwingine kabisa na najiita kwa jina tofauti na Regina”
“Jina gani?”
“Princess Natasha!”
“Unajiita Princess Natasha?”Aliuliza Hamza kwa mshangao huku akijiambia ni kipi kinaendelea.
“Shida yake haijawahi kujitokeza mara nyingi , lakini katika kipindi hicho anajita hivyo”Aliongea Shangazi.
“Sasa kwanini hawa watu wa Kondeni kupitia kitengo chao cha Binamu kuutaka upande wake wa pili?”
“Hilo ndio swali ambalo mpaka sasa halina majibu na pengine huko mbeleni tunaweza kujua zaidi”Aliongea Shangazi huku moyoni akijiambia sio muda wa kuongea kila kitu ambacho hana uhakika nacho.
Upande wa Hamza kuna kitu pia alihisi lakini hakuwa na uhakika nacho, ila alijiambia kadri siku zitakavyosogea ataweza kujua kila kitu.
“Shangazi tukiachana na upande wangu usio na majibu , je hii pete na maana gani kwao mpaka kuonyesha ni kitu cha thamani sana na vipi kuhusu wewe ni moja ya watu kutoka Kondeni?”Aliuliza Regina.
“Mimi sio mwanachama wa Binamu , ukizungumziia Binamu kama alivyosema Hamza ni shirika la kiitelijensia la watu wa Kondeni kupitia umoja wao wao wa SkyEye(jcho la Anga), sio kila mshirika wa Binamu ni mzaliwa wa Kondeni, mimi ni mzaliwa wa Kondeni na familia yangu ilikuwa ya daraja la chini hivyo niliangukia katika nafasi ya ukijakazi, licha ya kujua pete hio ni ya thamani kwa watu wa Kondeni lakini sina taarifa kazi yake kubwa nini ni ipi, lakini kitu nilichoweza kusikia ni kwamba pete hio ilimilikiwa na mwanzlishi wa eneo lote la Kondeni na ndio huyo huyo aliemvisha mama yake Dosam kidoleni”
Kwa namna ambavyo Regina alielewa Shangazi yake ni mtu wa Kondeni na watu wa Kondeni wana umoja wao wa siri unaitwa Jicho la Anga(Skyeye’s) na kitengo cha kiitelijensia kiitwacho Binamu.
“Kwahio Regina tulijitahidi kutokukuambia haya yote kwa muda wote kwasababu ya kukuweka salama , lakini kwAsababu sasa hivi familia ya Suwi imejitokeza inamaanisha Kiongozi mkuu anashindwa kudhibit kile kinachoendelea ndani ya Umoja, hivyo Hamza unatakiwa kuilinda hio pete kwa namna yoyote ile”Aliongea Shangazi.
Upande wa Hamza hakujua acheke ama alie maana tokea mwanzo anapokea hio pete lilikuwa wazo la Bibi Mirium kuilinda hio pete.
“Shangazi kwahio huko Kondeni ni nchi gani au ni wapi?”Aliuliza Regina
“Kondeni ni sehemu ambayo ipo ndani ya dunia lakini haionekani kwa macho ya kawaida , kuna namna ya kuingia na kutoka Kondeni , asilimia tisini ya watu wa Kondeni wanaishi kwa kuvuna nishati za mbingu na ardhi”Aliongea.
“Nakumbuka nishawahi kusikia uvumi kipindi juu ya sehemu ya siri kama hio ndani ya dunia , inasemekana mwanzilishi wa eneo hilo aliweza kufanikisha kugundua uwepo wa hilo eneo kwa kutumia kitabu kisichokuwa na maandishi”Aliongea Hamza.
“Kitabu kisichokuwa na maandishi , ni katabu cha aina gani?”Aliuliza Regina.
“Master wangu ndio alienisimulia juu ya uwepo wa hiki kitabu , ni kitabu ambacho kina kurasa hazina maandishi na inasemekana kilitupwa duniani pamoja na malaika ,sababu ya mataifa kutambua hili eneo ni kutokana na kwamba kitabu hiko baadhi yao walikiona na mara baada ya mwanzilishi huyo kufanikiwa kukisoma alipotea katika macho ya kawaida , licha ya kitabu hicho kuwa katika mikono ya bindamu mara moja lakini mpaka leo hii tofauti na mwanzilishi hakuna ambae ashawahi kujua maana yake , wanachofahamu tu ni kitabu cha malaika kisichokuwa na maandishi basi, lakini licha ya uwepo wa hii simulizi hakuna ambae aliamini na tafiti ziliishia kusema ni kitu ambacho hakiwezekani na ni hadithi tu”Aliongea Hamza.
Regina aliishia kushangaa, siku zote alikuwa ni mwanamke ambae kila alichofanya kiliendana na ushahidi wa kimantiki na hakuwahi kuamini vitu vya kufikirika hata mara moja.
Lakini Hamza aliongea kwa kujiamini mno na hakuweza kujizuia kuhisi pengne ni kweli
“Shangazi huna cha kuongezea?”
“Mimi ni kijakazi pekee , wakati Madam anakuja kuishi huku baba yake aliniambia nijifunze mbinu za mapigano na kuvuna nishati ili niwe mlinzi wake , lakini baadae Mzee Dosam aliniambia nikulinde wewe, hivyo sijui chochote , Hamza ndio mtu anaeonekana kujua vitu vngi kuliko mimi”Aliongea Shangazi na Hamza alishia kcheka.
“Regina unajua katika dunia hii kuna vitu ukiambiwa utahisi ni ngano tu za kutunga kwasababu hakuna ushahidi wa kisayansi , lakini hebu fikiria hujawahi kumuona Farao , hujawahi kumuona Yesu, wala mtume lakini maandiko na ushahidi unakufanya uamini ni watu waliowahi kuwepo , hivyo baadhi ya mambo ni hivyo hivyo , hakuna aliewahi kuona madragoni, majini wala malaika lakini kwasababu hakuna ushahidi haimaanishi kwamba hawakuwahi kuonekana au ni uongo, mpaka sasa tafiti za kisayans zinaonyesha kwamba ulimwengu ambao binadamu tunaona kwa macho ni asilimia mbili tu ya ulimwengu wote na asilimia tiisini na nane ya ulimwengu wote hatuujui na hauonekani kwetu.
“Kama Binadamu akitegemea tu ushahidi wa kisayansi na akili kwa ajili ya kufikiria uwepo ambao unapita akili zetu za kibinadamu haitokuwa tofauti na kipofu anaejaribu kugundua kitu kipya bila kuona”Aliongea Hamza.
“Kwanini unaongea hivyo , hata hivyo sitaki kufikiria chochote mlichoniambia maana kichwa kinaniuma tu , ni bora nifikirie nitakachofanya baadae na sio hili”Aliongea Regina na kisha alisimama na kupandisha ngazi kwenda floor ya juu na kujifungiia chumbani.
Hata Hamza hakumlaumu , aliona kwa mtu yoyote asingeweza kuelewa kila kitu kinachoendelea , maana vitu vingine havikuhitaji tu uelewa , vilihitaji pia uwezo wa kuhimili ukubwa wa ukweli hata kama unaonekana kuwa uongo.
Shangazi mara baada ya kuona maongezi yameisha alisimama na kisha alipiga magoti kwenye kapeti mbele ya Hamza na jambo lile lilimshitua Hamza.
“Shangazi unafanya nini?”
“Hamza kama sio wewe leo , mimi na Regina tungemalizwa na yule Wisu, kwanzia sasa Regina yupo mikononi mwako naomba usije kumkatia tamaa..”Aliongea Shangazi na Hamza hakujua acheke ama alie lakini haraka sana alimsimamisha Shangazi juu
“Shangazi usiwe na wasiwas , sijutii maamuzi yangu ya kuipokea hii pete na ili mradi nipo hai hawawezi kuichukua na kumgusa Regina”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Shangazi machozi kumtoka.
“”Nimefurahi kusikia hivyo , ngoja nikamwandalie Regina supu”Aliongea.
*****
Kutokana na tukio lililitokea siku iliofuata Regina alighaiirisha safari ya kurudi Dar na kutokana na mazngira kuwa tulivu na ya msitu Hamza aliona ni vizuri kwa Regina kupumzisha akili.
Mwanzoni Hamza alitaka kumchukua Regina na kwenda kutembea nae , lakini Regina alimwambia hajisikii vizuri , hivyo Hamza alighairisha na kubakia nyumbani kwa muda akiendelea kuangalia runinga mpaka alivyochoka na kutoka nje.
Mji huo ulikuwa ni wa kitalii na ulikuwa na maeneo mengi ya kutembelea
Wakati Hamza akiendelea kutalii kwenye mitaa mbalimbali akishangaa shangaa mazingira , simu yake ilianza kuita na mara baada ya kuangalia jina la anaepiga alikuwa ni Amiri rafikki yake na palepale alikumbuka swala la Mellisa.
*****
Saa moja kumi za jioni alionekana Kanali na Jasusi Mstaafu Amosi wakingia katika mgahawa wa kuuza chai unaomilikiwa na mrembo Dina.
Kwa Amosi hakuwa mgeni wa eneo hilo , lakini kwa Kanali ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kufika hapo na alishangaa mara baada ya kuona kuna watu wengi tu waliokuwa wakijipatia chai na vitafunwa.
“Hujawahi kuingia ndani ya hili eneo nini?”Aliuliza Amosi.
“Nalijua hili eneo sana , lakini sikuwahi kuelewa kile kinachouzwa hapa”Aliongea.
“Hapa kunauzwa chai za kila namna ila za viwango , kwa wale ambao hawanywi pombe lakini pia wapenzi wa chai zenye faida kwa mwili hii ndio sehemu yao ya kujidai, ndio maana unaona kuna waatabu wengi hapa”Aliongea Amosi na Dastani alionekana kuelewa.
Muda huo huo mhudumu aliwasogelea na kuwakaribisha kwa ajili ya kupata huduma.
“Hatupo hapa kwa ajili ya huduma ya chai bali tumekuja kuonana na bosi wa hili eneo”Aliongea Kanali.
“Mna miadi nae?”Aliuliza yule mhudumu wa kike maana kidogo alionekana kushangazwa kauli ya watu hao.
“Hatuna miadi lakini lazima tuonane nae , ni jambo muhimu”Aliongea Amosi.
“Nadhani mnapaswa kukaa kwanza ili niongee na meneja”Aliongea yule mhudumu na Kanali alitingisha kichwa na kisha walionyeshwa sehemu ya kukaa huku yule mhudumu akiwaacha.
Ndani ya dakika chache tu , alionekana Lawrence akifika eneo walipo na alijitambulisha kama Meneja wa mgahawa huo.
“Amosi, jasusi mstaafu , unafanya nini hapa mpaka kutaka kuonana na bosi wangu”Aliongea Lawrence, alikuwa akimfahamu vyema Amosi kama mtukutu aliekuwa juu ya sheria kwa kufanya alivyokuwa akitaka kwa wadeni wake na serikali haikumchukulia hatua.
“Leo sijaja kwa shari , licha ya tofaut zetu zilizotokea wakati ule , niliweza kutii masharti yenu yote na sikumsumbua tena yule mwanamke”Aliongea Amosi akimlenga Eliza.
“Hata kama umekuja kwa shari hili ni eneo la biashara”Aliongea huku akitoa tabasamu.
“Bosi wangu hapa anatokea serikalini na ana mazungumzo na bosi wako, ni swala muhimu hivyo ni vyema kama ukitoa taarifa juu ya ujio wetu”Aliongea Amosi akiwa siriasi na Lawrence alifikiria kidogo na kisha aitingisha kichwa na kupiga simu.
“Mnaweza kunifuata madam yupo tayari kuongea na nyie”Aliongea na Amosi na Kanali waliangaliana na kisha walimfuata Lawrence mpaka ndani ya ofisi ya Dina.
Mwanamke huyo licha ya kubarikiwa uzuri , lakini vlevile alijua kukaa kimaponzi mno na kama humjui vizuri utadhani anakutega lakini ni hulka yake tu kama mwanamke.
Sio kwamba Kanali hakuwa akimjua Dina , alimfahamu sana lakini hakuwahi kukaa nae meza moja na alijikuta akijisemea ndani kwa ndani Dina alikuwa ni mzuri mno, pengine wanafikiana uzuri na hawala wake Tresha.
Dina hakuwa peke yake ndani ya ofisi hio , alionekana kuwa na mwanaume mwingine alievalia suti ambae aliwapa mgongo.
“Amosi na Dastani karibuni?”Aliongea Dina kwa sauti ya mapozi na muda uleule yule mwanaume aliewapa mgongo aligeuka na kuwaangalia huku akiwa na tabasamu usoni.
Kitendo cha Amosi na Dastani macho yao kutua kwa huyo mwanaume walijikuta wakishikwa na mshituko kama kwamba hawakutarajia kumuona ndani ya eneo hilo.
ITAENDELEA
Mnaotaka kujiunganasi watsapp nitafutnikwanamba 0687151346