SHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI: SINGANOJR
SEASON 2.
Regina alienda mbali na kukumbuka aligombana na Hamza kwa kutotaka kutupa mavazi yake , alishindwa kuzuia hisia mbaya zilizoanza kumvaa na kujiambia kama kweli anachosema Fellini ni kweli basi mavazi hayo ya thamani si yatamfanya aonekane mjinga na mshamba.
“Mr Fellini macho yako yatakuwa yanakudanganya , haya mavazi aliovaa unaweza kuyakuta kila mkoa ndani ya Tanzania yanauzwa”Aliongea Regina kuepusha kuabika.
“Msiniambie hakuna ambae anaona uzuri wa mavazi aliovaa Mr Hamza pamoja na pensi yake?”Aliongea huku akiwaangalia mmoja mmoja kana kwamba anaomba kuungwa mkono.
Lakini wote walitingisha vichwa vyao kukataa , hakuna cha maana kwenye hayo mavazi zaidi ya uchakavu tu”
“Nyie watu hamjui kabisa , nadhani kwasababu sio mafundi, katika ulimwengu wa kifundi utaalamu wa juu zaidi ni kutengeneza vazi ambalo unao uwezo wa kulirudisha upya kwa mchakato mwepesi sana na ukauza sokoni kwa bei ileile”Aliongea mzungu huyo lakini hakuna hata mmoja ambae alielewa anachomaanisha, hata Salma aliesomea Person chuo namba moja cha mitindo kutoka Marekani hakuelewa.
SEHEMU YA 31.
Regina mara baada ya kuona haelewi alichomaanisha Fellini aliomba aeleze kwa lugha nyepesi, bado hakuwa amekubali nguo alizovaa Hamza ni za bei ya juu.
“Mr Fellini unaonaje ukituelezea kwa urahisi tupate kuelewa?”Aliongea na Fellini alimwangalia Hamza.
“Mr Hamza naomba ruhusa yako kushika nguo zako”
“Hakuna shida , ungeniambia vizuri ningekuelewa tokea mwanzo”Aliongea Hamza huku akicheka.
“Salma nadhani utakuwa unajua ni malighafi za nguo za namna gani zimetumika”Aliongea akimpa ishara Salma kusogea karibu na yeye pia alishika lakini dakika ileile muonekano wake ulibadiika.
“Noble family material!!?”Aliongea Salma huku akishangaa.
“Correct, hii ni aina ya kitambaa cha SCUBA ambacho kiliongezewa ubora kwa mara ya kwanza nchini Ubelgiji na baadae kikawa kitambaa namba mmoja kinachotumiwa ndani ya Savile , ni aina ya kitambaa ambacho mchakato wa kukitengeza kuwa mgumu na ndio maana sio swala la hela tu kununua kitambaa hiki, sasa unadhani nguo yoyote ambayo imetengenezwa na aina hii ya kitambaa inaweza kuwa ya kawaida?”
Regina mara baada ya kusikia kauli hio alishindwa kujizuia na kusogea na yeye ili kugusa kitambaa hicho kwa umakini , ijapokuwa alishawahi kugusa nguo za Hamza mwanzo lakini ile kejeli juu ya nguo hizo hakuweza kuona kitu special.
Lakini muda huo alivyogusa nguo hio ki uchunguzi ndio sasa anagundua ni kweli kitambaa chake hakikuwa cha kawaida kabisa.
“Mnajua nini kimeongezewa upande wa hio michirizi ya pensi kushoto na kulia?, angalia kwa pembeni utaona ni kama inabadilika rangi kutokana na mwanga?”Aliuliza Fellini na wanawake wote waliangalia kwa kutumia angle ya macho na kuona ni kweli rangi ya nguo inabadilika, lakini hakuna ambae alikuwa na majibu.
“Ngoja niwaambie , ni nyuzi nyuzi za madini ya Platinum kutoka Afrika ya kusini, hii inafanya kitambaa chake kuwa cha thamani ya juu mno na adimu dunia nzima, gharama ya uzalishaji wa kutengeneza suruali ni Euro laki moja”Aliongea
Euro laki moja inamaana Hamza amevaa nguo ya thamani ya milioni mia tatu za kitanzania , Regina , Linda na Salma mara baada ya kusikia kauli hio walishindwa hata kupumua vizuri.
“Hey usiongee kwa nguvu , unataka watu wasikie na kuniwinda wanivue nguo nitembee uchi”Aliongea Hamza akimwambia Fellini.
Fellini alijikuta akigundua alikuwa na mzuka kiasi kwamba alikuwa akiongea kwa sauti na aliinamisha kichwa kuonyesha ishara ya kuomba radhi.
“Hilo ni la kwanza , kinachofuata na kutofautisha hizi nguo ni aina yake ya ushonaji”Aliongea na kisha alishika kola ya tisheti ya Hamza na kuinyanyua kwa juu.
“Nadhani mshawahi kusikia teknolojia ya Hermes ya ushonaji wa nguo za leather wanatuia SDD- stilt method , hii njia ya ushonaji mara nyingi inatumia sindano mbili kwa wakati mmoja na kufanya bidhaa yoyote ya kampuni ya Hermes ya Leather kuwa imara sana na kupendeza kwa wakati mmoja
Ukweli ni kwamba kati ya washonaji wengi , kuna mbinu ya kale ambayyo ipo karibu kupotea , inaitwa Concealment Saddle needle techinique, hii ndio mbinu ambayo Master George anatumia , lakini mpaka leo hii hata yeye mwenyewe hajabobea kuitumia kwa asilimia mia moja , mbinu hii inakupa nafasi ya kutumia nyuzi tatu katika uzi mmoja, hivyo kufanya nguo kuwa imara na kudumu kwa muda mrefu”Aliongea na Regina na Salma walisogea karibu kuangalia namna ya ushonaji ulivyokaa na kwa kuangalia tu waligundua mashine ya cherehani ni ngumu sana kufanikisha ushonaji huo.
“Hakuna ushonaji wa aina yoyote duniani unaoifikia hii mbinu , cha kufurahisha zaidi ukitaka kuifumua nguo yote kwa urahisi unagusa sehemu moja na unatoa nyuzi zote na nguo inarudi katika kitambaa na baada ya hapo inaweza kufanyiwa maboresho na kisha kurudishwa katika muonekano wake mpya”
Regina aliishia kukosa hiari na kuamini kabisa maamuzi yake ya wakati ule hayakuwa sahihi , lakini aliona pia Hamza alikuwa ni mshenzi sana , yaani mtu anavaa nguo ya thamani kubwa namna hio lakini anajifanyisha ni masikini tena mbaya zaidi anajifanyisha mtu anaependa sana hela.
“Hamza kwahio ni kweli unafahamiana na huyo Master Alec , kwanini hukusema?”Aliuliza Regina.
“Umesahau nilikuambia nguo hizi nilipewa na rafiki yangu , halafu sio kama uliniuliza ni rafiki gani?”Aliongea na kumfanya Regina kumwemwesa midomo , ilikuwa ni kweli hakuuliza ni rafiki gani.
“Wewe ni dereva tu , kwanini nguo zako zitengenezwe na mafundi wanaoshonea nguo wafalme , au umeziiba ndio maana umeshindwa kujua thamani yake?”Aliongea Salma.
Fellini mara baada ya kusikia kauli hio ni kama hata yeye wazo hilo lilimwingia , kwani ni ngumu mtanzania kama Hamza kuwa na nguo ambayo imetengenezwa na Alec , hata kama Hamza alionekana kuchanganya damu ya kizungu lakini bado ilikuwa ni ngumu kuamini, isitoshe swala la kuchanganya damu halikuwa la kushangaza sana , Waafrika wengi walikuwa wanaanza kupoteza rangi yao halisi kutokana na kuzaa na watu weupe, hivyo kumuona mtu mwenye muonekano wa Hamza sio swaa la kushangaza.
Leo hii unaweza kukuta watoto wa mtaani wenye muonekano wa kizungu na kiafrika au waarabu na waafrika.
“Sidhani ni sahihi kusema hivyo , maana ninazo nguo nyingine nyingi tu ambazo ametengeneza Alec?”
“Nani anajua , pengine uliiba furushi la nguo , kama una urafiki na mtu mkubwa kama huyo inakuwaje leo hii upo hapa Tanzanina , tena Dereva , si ulitakiwa uwe Ulaya huko?”Aliuliza Salma , hakutaka kukubali kabisa.
“Kwahio vipi msaidizi wangu kuwa dereva , kwahio siku hizi tunabaguana kwasababu ya mavazi?”Aliongea Regina , hakutaka kuona Salma anapandisha mdomo mbele ya Hamza.
“Regina haijalishi unachoongea , tena nimezidi kuwa na mashaka , kuna namna mmepanga bada ya kuhisi hamuwezi kushidana na kampuni yetu , hivyo mnacheza kamchezo ka kumfanya Fellini kukubaliana na nyie”
“Unaumiza kichwa chako bure kwa kufikiria sana , kama nilivyosema , sina mpango wa kushirikiana tena na Zara, tuondokeni”Aliongea Regina lakini muda ambao Regina alianza kupiga hatua kuondoka hapo alizuiwa na Hamza.
“Hamza , unafanya nini?”
“Msaidizi wako nimeitwa mwizi , unadhani tunaweza kuondoka hivi hivi?”Aliongea.
“Kwahio wewe sio mwizi?”Aliuliza Salma.
“Mr Hamza , je una ushahidi wowote wa kutuonyesha hizi nguo ni za kwako au unafahamiana na Master Goerge?”Aliuliza Fellini.
“Sasa hivi ni saa saba kasoro hivyo itakuwa ni Asubuhi London , nadhani Mzee Roboti muda huu atakuwa macho , ninaweza kumpigia simu”Aliongea
“Nini , unasema una namba ya Master?, wakati hata mimi sina”Aliongea Fellini kwa mshituko.
“Unaongea ujinga , kama hakutengenezei nguo , kwanini uwe na namba yake”Aliongea na kumfanya Fellini kukakamaa mwili , alikuwa akijisikia vibaya kana kwamba ameona mende.
Regina na Linda wote walikuwa na hali ya shauku na matarajio kwa wakati mmoja , upande wa Salma alikuwa na wasiwasi mno.
Hamza alitaka kutumia simu yake kupiga lakini alisahau kwamba ni kimeo hivyo alimwangalia Regina.
“Mkurugenzi niazime simu yako , siwezi kupiga kimataifa kupitia simu yangu”Aliongea na Regina alitoa Iphone yake na kumkabidhi Hamza na palepale aliingiza namba alizokariri na kupiga na ndani ya dakika chache tu simu ilipokelewa baada ya kuita.
“Who is it …”Sauti ya kingereza ya kizee upande wa pili ilisikika , ilikuwa nzito mno na lafudhi ya London na Hamza alitoa tabasamu mara baada ya kutambua sauti hio ambayo hajaisikia muda mrefu.
“Elmo , its me..”Aliongea Hamza upande wa pili kulikuwa na kimya kama cha sekude arobaini hivi.
“Do you finally rembember this lowly person!?”Sauti upande wa pili ilijibu na ndio dakika ileile Hamza aliweka simu aweze kusikia yeye tu ili wasije kusikia jina ambalo Alec anaweza kumuita.
Hamza asingejua namna ya kujieleza kama wangesikia Alec anamwita kwa cheo chake cha heshima.
“Mzee Roboti sio kama nimekusahau , mpaka sasa kila nilipokuwa ikivaa mavazi ulionipa kama zawadi nakukumbuka , ni miaka mingi lakini nguo zako bado nazivaa”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu.
“Niheshima kwangu kufanya kazi na wewe na nilikuwa nikitegemea tuendelee kufanya kazi pamoja ila umepotea , nakumbuka wakati nakutengenezea hizo nguo ilikuwa ni miaka mitatu iliopita”Aliongea mzee huyo akionekana kama vile analalamika.
“Okey , Okey mzee nilikupa likizo kwanza ili ujali afya yako , lakini kwasababu unaonekana kuwa tayari kunitengenezea tena nguo basi nakupa ruhusa , nitakutumia anuani ya ninapoishi kwasasa , nadhani unajua ninachopendelea”
“Kweli !, nipo tayari kufahamu sehemu unayoishi kwasasa , najua umeondoka bila kuaga hivyo itakuwa siri yetu kama tunawasiliana”
“Mzee japo umezeeka lakini akili yako inafanya kazi vizuri , ninakuamini ndio maana nimeamua kukupigia”Aliongea Hamza huku akicheka, alikuwa akiongea kingereza na lafudhi yake ni kama vile amekulia jijini London.
“Mimi kama kijakazi wako lazima niwe na akili japo kidogo , vinginevyo nitaweza vipi kutimiza wajibu wangu wa kukuhudumia?”Aliongea.
“Sawa sawa , tuachane na hayo kwanza , nimekupigia leo kwasababu kuna baadhi ya mambo nataka unisaidie kuyaweka sawa”Aliongea Hamza.
“Usisite kabisa kuniambia , nipo tayari kufanya chochote , hata kama nikuhatarisha maisha yangu”
“Sio swala kubwa sana , usiwe na wasiwasi , je kuna mwanaume anaefahaika kwa jina la Fellini kati ya wanafunzi wako ?"Aliuliza Hamza na wakati huo alikuwa akimwangalia Fellini.
Muda huo Fellini uso wake wa kizungu ulikuwa umepauka na kulikuwa na viashiria vya jasho katika paji la uso wake , alikuwa akijiuliza kama kweli Hamza aliekuwa akiongea nae ni Master Alec , Hamza mwenyewe atakuwa ni nani
Salma na yeye alikuwa aking’ata lipsi zake huku akiwa amekunja ngumi , alionekana kuwa na wasiwasi mno.
“Mkurugenzi ni kweli anafahamiana na huyo mtu mzito , mbona naona kama anatufanyia magizo?”Aliuliza Linda.
Upande wa Regina yeye alikuwa katika kuwaza na aliishia kutingisha kichwa ,huku akishindwa kuongea neno, alijiambia atajua baada ya matokeo.
Lakini muda huo mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda kasi mno , alijiambia kama ni kweli basi koneksheni ya Hamza ni kubwa mno kama vile yupo ndotoni.
“Felini!?, Oh nimemkumbuka sasa , Fellini ni mwanafunzi aliekuja akiwa mdogo katika duka langu kwa ajili ya kujifunza kushona, lakini hakuweza kudumu sana maana moyo wake ulikuwa haujatulia sehemu moja , ijapokuwa alikuwa na kipaji lakini hakuwa na Ari ya kuja kuwa mshonaji mkubwa hivyo aliondoka , kwanini unamuulizia , Mshonaji kama Fellini ni wa daraja la pili na hana hadhi ya kuandaa nguo zako”Aliongea.
“Hamna mzee, sijakutana nae kwa ajili ya kunitegneenea nguo , nimekutana nae kwa bahati mbaya na ameweza kugundua maazi yangu wewe ndio umeyatengeneza, ila haamini amesema mimi mwizi”
“Nini!!, anakitafuta kifo , tafadhari bwana wangu naomba usiwe na hasira juu ya tabia ya Fellini , nitamwambia Eric amfukuze , mtu kama yeye hawezi kutuingiza kwenye mgogoro na wewe , kama bado hutoridhika unaweza kumfanya chochote nitaandaa maelezo”Aliongea na kumfanya Hamza kutamani kucheka kutokana na namna Alec alivyopaniki.
“Ndio maana nakuita Mzee Roboti unaishi kikanuni sana , haina haja ya kupaniki , sina mpango wa kumfanya chochote , nitampatia simu uongee nae , ninachotaka ni wewe kumthibitishia tunafahamiana , usiongee zaidi kuhusu mimi , nadhani umenielewa”Upande wa pili kimya kilitawala.
“Sawa sawa , najua nini chakufanya”Alijibu na Hamza alimpatia Fellini simu.
Upande wa Fellini mikono ilikuwa ikimtetemeka , ilimchukua sekunde kadhaa mpaka kupokea simu hio kutoka kwenye mikono ya Hamza.
Hakuwahi kuongea na mwalimu wake huyo kwa zaidi ya muongo mmoja,sasa wazo la kuona kwamba anakwenda kuongea na mwalimu wake huyo mtu mzito sana ndio maana alikuwa na hofu.
“Nice to talk to you , Master Alec”Aliongea Fellini kwa kitetemeshi lakini upande wa pili hakukuwa na jibu.
“I heard from Eric that you’re now quite famous outside ?”Sauti upande wa pili iliongea na palepale Fellini ni kama vigoti vinamlainika
“Hapana Master ,Mimi ni kivuli cha Sir Eric tu , nimekosea Master naomba radhi”Aliongea na upande wa pili ilionyesha ni kiasi gani Alec alikuwa amekasirika.
Muonekano aliokuwa nao Fellini ulimfanya Salma ambae alikuwa pembeni kushangaa mo , Mbobezi maarufu wa ulimwengu wa fasheni amebadilika na kuwa kama piritoni hivyo kwa kuongea na mtu kwenye simu
Regina na Linda na wao walikuwa sasa washaamini mtu ambae anaongea na Fellini ni kweli ni huyo Alec mweye hadhi ya juu.
“Sikiliza wewe mtoto , mtu uliekutaa nae huwezi kumwita mwizi , ukimfaya akasirike basi hutonilaumu tukikutoa kwenye circle yetu na umaarufu wako kupotea , nadhani unajua ninachomaanisha”
Fellini alikuwa na hofu mno , alikuwa akijua maneno ya Alec sio ya kumuogopesha tu , ukweli ni kwamba kauli yake moja tu hawezi kuwa na umaarufu aliokuwa nao , alijua nguvu iliokuwa nyuma katika fasheni ya mavazi ilitawaliwa na watu kama Alec.
“Master usiwe na wasiwasi , najua nini napaswa kufanya”Aliongea.
“Mrudishie simu”
Fellini alimwangalia Hamza kama vile ni kiongozi wa heshima na jambo hilo liliwashangaza zaidi Regina , Linda na msaidizi wa Alec, upande wa Salma muonekano wake ulikuwa mbaya mno , maana kile kinachoendelea ni kama matusi kwake .
Hamza aliongea na Alec kwa dakika kama mbili hivi na kisha alikata simu na kumrudishia Regina.
“Sasa nadhani kila mtu amethibitisha nguo hizi ni zangu , Mkurugenzi , tunaweza kuondoka sasa”Aliongea Hamza.
Regina alijihisi ni kama yupo ndotoni na aliishia kutingisha kichwa huku akimwangalia Hamza kwa wasiwasi.
Upande wa Fellini aliona haiwezi kuwa nzuri kama atamuacha Hamza aondoke akiwa na kinyongo.
“Mr Hamza nakiri ilikuwa ni ujinga wangu , hivyo naomba msamaha wako , kama ningejua na wewe ni mmoja ya watu wa kampuni ya Dosam nisingesita kufanya nao ushirikiano, naomba unipe nafasi ya kurekebisha makosa , nipo tayari kampuni ya Zara kushirikiana na Dosam Group”
“Mr Fellini huwezi kufanya hivi , tushakubaliana kampiuni zetu zinaenda kushirikiana”Aliongea Salma kwa hasira.
“Miss Salma, hakuna mkataba wowote tuliosaini kati yetu , hivyo siwezi kusema kuna makubaliano ya kufanya kazi pamoja , baada ya kufikiria kwa kina nimeona kampuni ya Dosam inaweza kukuza hadhi yetu”
“Kwanini unaenda kinyume na maneno yako?” Aliongea Salma huku akiona swala hilo ni kama udhalilishaji, lakini Fellini alimpotezea kabisa.
“Kama nilivyokwisha kujitambulisha, mimi ni msaidizi tu , unapaswa kuongea na Mkurugenzi akikubali sina neno”Aliongea Hamza.
“Miss Regina naomba mazungumzo yetu yaanze upya , naomba kuona mipango yenu”Aliongea mara baada ya kupata ruhusa.
Upande wa Regina alikuwa asharudi katika hali ya kawaida akiuzima mshangao wake na alimwangalia Salma kwa macho ya uchokozi na palepale alichukua mkataba ambao ulikuwa umeshikiliwa na Linda na kuuchana mbele yake.
“Cooperation is fine , but we need to redesign the cooperation proposal”Aliongea akimaanisha ushirikiano hakuna shida lakini wataenda kuandaa upya vipengele.
Fellini aliishia kuangalia chini , kwa wakati huo Regina alikuwa na Upperhand , hivyo ni kama yeye ndio anaomba ushirikiano na kampuni ya Dosam na sio Regina kumuomba yeye ushirikiano., Regina alishaliona hilo hivyo alitaka kubadilisha vipengele ili kuinufaisha kampuni yake.
“Hakuna shida, nipo tayari kusubiri kwa siku kadhaa”Aliongea Fellini , hakuwa yule mwenye ratiba iliobanana tena.
Hamza alimwangalia Regina kwa macho ya kuridhika , alimuona Regina kama mwanamke ambae akili yake inafanya kazi kuendana na hali kwa haraka , hali ya mazungumzo ya kibiashara imebadilika hivyo hakutaka kwenda na mkataba uleule.alitaka kubadilisha mbinu ili kujinufaisha.kitaalamu alimuona Regina kama mwanamke ambae sio mzembe kabisa likija swala la fursa.
Kwa vyovyote vile Kampuni ya Zara lazima ishirikiane na Dosam kama Fellini anataka kulinda hadhi yake katika ulimwengu wa fasheni.
Fellinni aliwasindikiza kabisa Hamza na Regina mpaka kwenye gari yao na kuwafungulia mlango huku akiwa na heshima kubwa .
Upande wa Salma alimwangalia Hamza kwa macho yenye ukali mno na kisha aliondoka bila hata ya kuaga.
“Mr Fellini huna haja ya kuwa hivi , ijapokuwa leo sijafurahishwa na namna tulivyoanza lakini nimeridhika na matokeo”Aliongea Regina.
“Ili Mradi Mkurugenzi umeridhika , hakuna tatizo kabisa , natarajia kufanya kazi na Dosam kwa miaka mingi”
“Kama hakuna lingine tunaondoka”Aliongea Hamza.
“Mr Hamza tafadhari subiri kidogo , najua nimekukosea leo , naomba uniwie radhi , kama kuna mahali ambapo hujaridhika tafadhari naomba uniambie nitarekebisha”
“Usiwe na wasiwasi , ili mradi kila kitu kitaenda sawa mimi sina shida , nitakusaidia pia kukupigia chepuo kwa Alec “
“Thank you so much, you are so magnanimous”Aliongea na muda huo Hamza alikumbuka aliachaga nguo kwenye hilo gari.
“Mkurugenzi , hivi zile nguo zangu bado zipo humu?”
Regina muonekano wake ulikuwa na hali ya kukosa utulivu na alinyoosha mkono nyuma na kutoa ule mfuko , mwanzoni alitumia nguo hizo kumdharau Hamza lakini dakika chache zilizopita zimegeuka kuwa hazina.
Hamza alichomoa shati kutoka kwenye mfuko huo na alivyolinusa lilinuka jasho kali mpaka akakunja sura, lakini katika macho ya Fellini alionekana kuwa katika mchangao.
“Unaweza kuchukua hizi nguo , chukulia kama zawadi kutoka kwangu kwa kuingia makubaliano ya kibiashara”Aliongea Hamza na kumkabidhi mfuko wote Fellini aliepokea kwa mikono miwili.
Hamza hakuwa na wasiwasi na nguo tena , alishaahidiana na Alec angeletewa nguo nyingine mpya
Mtu yoyote angeona shati ambalo Hamza amemkabidhi Mzungu Fellini wangesema huyo mzungu ni kichaa.
“Mr Hamza asante sana kwa ukarimu wako, nitaweka nguo hizi sehemu salama kabisa nikirudi” Aliongea Fellini, alipanga kuzifanya nguo hizo kama sehemu ya maonyesho ofisini kwake , ili kutukuza uwezo wa Master Alec katika swala zima la ushonaji.
Isitoshe Master Alec alikuwa ametengeneza kwenye maisha yake nguo nyingi sana lakini sio watu wengi ambao washawahi kuona nguo yenye muonekano wa kawaida kama hio lakini ya thamani , Rare things are priceless.Aliwaza Alec.
Kwa furaha mazungumzo yao yaliisha hivyo na Hamza aliendesha gari kurudi nyumbani.
Linda ambae alifika na gari yake aliweza kuangalia gari ya Regina ikitokomea huku akiwa na muonekano usioelezeka , katika macho yake kulikuwa na hali flani hivi ya kukata tamaa.
******
Upande mwingine ndani ya jiji la London ilikuwa ni asubuhi karibia maeneo yote , Uingereza haikuwa kama nchi ya Marekani ambayo ina Time Zone zaidi ya nne, pengine ni kutokana na udogo wa kijiografia wa nchi hii yenye maendeleo makubwa sana katika nyanja zote.
Katika mtaa wa Savile Row mwanaume mzungu mzee hivi mwenye nywele nyeupe pamoja na miwani alionekana akishuka katika ngazi katika moja ya jengo kwa kukimbia, alikuwa amevalia shati jeupe na Vest nyeusi.
“Erice, John”Mwanaume yule aliita kwa nguvu.
Dakika hio hio mwanaume bonge mzungu alijitokeza akiwa ameambatana na mwanaume mwingine kimbau mbau ,wote walionekana katika umri wa iaka hamsini hivi na walikuwa wameshikilia vitambaa.
“Mwalimu , una maagizo yoyote”Yule bonge ndio aliitwa Erice na ndio alieuliza.
“Wote nyie acheni kazi zenu zote kwa sasa na mnifuate , nahitaji kutengeneza nguo nyingi suti na suruali”
“Mwalimu , bado hatujamaliza kutengeneza nguo za Mfalme wa Hispania na Prince wa Wales, sidhani kama tunaweza kukusaidia”Aliongea John.
“King or Prince let them all wait, For the past week, we have served one lord” Aliongea akimaanisha Mfalme au mwana mfalme wote wasubiri. kwani kwa wiki za nyuma walikuwa wakihudumia bwana mmoja tu.
“Mwalimu unamzungumzia bwana gani?”Erice aliuliza.
“Seraph”Aliongea Alec huku akigusa gusa kifua chake.
Erice na John mara baada ya kusikia jina hilo moja kwa moja walielewa ni mtu gani anaelengwa na wote kwa pamoja walikakamaa huku wakitamka kwa juu “Divine Wrath”
SEHEMU YA 32.
Kwa zaidi ya dakika ishirini au therathini hivi hakuna aliemuongelesha mwenzake , Regina alidhania Hamza angempa sababu japo kidogo tu ya kutuliza shauku yake , alitamani kusikia hata kisingizio tu pengine angeelewa lakini licha ya hivyo Hamza alikuwa akiendesha huku akipiga ukimya.
“Huna kitu chochote cha kuniambia?”Aliuliza Regina baada ya kukosa uvumilivu na kumfanya Hamza kuangalia kioo cha nyuma.
“Ni kweli asubuhi nilikuwa na dharula muhimu , ningechelewa kidogo kungekuwa na tatizo , alikuwa ni mteja wangu alienipigia , sikutaka kumpotezea”Aliongea Hamza lakini Regina hakuwa hata na haja ya kusikiliza hizo porojo.
“Sitaki kusikia kuhusu hilo , kwanini hukuniambia unafahamiana na huyo Master Alec?”
“Ah.. Unamzungumzia mzee Roboti , kwanini nimzungumzie sasa bila sababu?”
“Wakati ule nilikuambia ukatupe mavazi yako lakini ukang’anania kubaki nayo , kwahio ulikuwa ukinikejeli kisirisiri kwa kuwa mshamba sio , unaonekana kabisa umeisubiria kwa hamu hii siku kwa ajili ya kuniumbua mbele za watu, sasa hiivi nadhani unajichekea mwenyewe moyoni kwa raha zako”Aliongea huku akionyesha kinyongo.
“Regina unaongea nini , sikufikiria sana wakati ule ni kwamba tu nimezoea haya mavazi ndio maana, ni zawadi kutoka kwa mzee , isingekuwa vizuri kuyatupa ilihali aliweka moyo wake wote kwenye kuyatengeneza”
“Basi niambie wewe na huyo Master Alec mnafahamina vipi?”
“Nilikutana nae Shardland Bar huko Uingereza kipindi flani hivi cha mwaka mpya na ndio tulianza kuongea kwa kubishana na urafiki wetu ukaanzia hapo”
“Unaniona mjinga , unadhani naweza kuamini huo uongo , mbona unapenda kuniona kama kichekesho?”
“Ananiona mjinga huyu sijui yukoje , yaani mtu amemtisha Fellini vile lakini sasa hivi anasema amekutana nae bar “Aliwaza Regina huku akiwa na hasira kali.
Muda uleule wakati washafika Kigamboni Hamza alisimamisha gari pembeni na kumshitua Regina aliekuwa kwenye mawazo.
“Wewe .. unafanya nini?”Aliuliza lakini Hamza hakujibu zaidi ya kufungua mlango na kutoka nje na kutembea upande wa madukani, Regina na yeye hakutaka kukaa ndani ya gari , alishuka na kumfuata huko huko na kufanya watu kumkodolea macho kutokana na urembo wake.
Baada ya kumfikia Hamza alimuona akiwa amesimama mbele ya Freezer akichagua Ice Cream za Bakhresa na alichukua yenye Strawberry na kumpa Regina ambae aliipokea bila kupenda.
“Unafanya nini sasa?”
“Mrembo maswali mengi ya nini , huoni hio ni Ice Cream”Aliongea na muda huo Hamza alichukua na ya kwake ya ukwaju na kisha akaenda kulipa na sasa hapo ndio Regina alijua kumbe huyu mwehu kaja kununua Ice Cream.
“Acha kusimama hapo twende , tumeegesha gari sehemu mbaya , hata kama una hela huwezi vunja sheria za barabarani”Aliongea Hamza na kumshitua Regina ambae alikuwa kwenye mshangao.
“Nani kakuambia nina shida ya Ice Cream , jali mambo yako”
“Kama hutaki ilete basi ninao uwezo wa kula zote mbili kwa pamoja”Aliongea Hamza akijaribu kumpokonya lakini Regina alipindisha mkono mbali.
“Unasema huitaki , nataka kuichukua unaktaa , nyie wanawake ni viumbe wa ajabu sana”
“Unasemaje wewe…”Aliuliza Regina lakini Hamza alijifanyisha mjinga na kumuacha Regina akiwa amesimama
Wateja baadhi na watu wauza maduka waliishia kutabasamu , kwani walionekana kama wapenzi.
Hamza mara baada ya kuingia garini aliliwasha na kupiga honi na kumfanya Regina kwa hasira kukimbilia na kuingia.
Baada ya wote kuingia kwenye gari na Hamza kulirudisha kwenye barabara aliendesha kwa mkono mmoja huku mwingine ukishikilia Ice Cream , Regina hakuuliza tena swali , aliona hata akiuliza kusingekuwa na majibu hivyo alijikaliza zake kimya , huku akila Ice Cream kwa kutumia kijiko
Kama alivyosema Hamza wanawake hawaeleweki , Kwa Regina ilikuwa hivyo hivyo kulikuwa na wanaume kibao ambao washawahi kumtongoza kwa kumpatia zawadi kama vile magari , vito vya thamani na ahadi kibao , lakini kitendo cha Kununuliwa Ice Cream ndio zawadi ya thamani ya juu iligusa moyo wake.
Wakati wanafika nyumbani Shangazi alikuwa sebuleni akiangalia TV, na hata walivyoingia hakuweza kuwaona.
“Shangazi unaangalia nini , mpaka kuwa siriasi hivyo?”Aliuliza Regina.
“Taarifa ya habari , wanasema kumekuwa na mauaji mfululizo ya wanawake ndani ya jiji la Dar es saalam na muuaji hafahamiki hivyo wanaasa raia kuwa makini, Regina uwe makini , ukitoka kazini hakikisha uwe na Hamza pembeni yako , wakati wa mchana usitoke peke yako pia”
Hamza aliangalia taarifa hio ya habari na alishangaa na kuona namna muuaji alichokuwa akifanya , tofauti na kuua tu alikuwa pia akikata maeneo nyeti ya wanawake kama vile manyonyo na ngozi, yalikuwa mauaji ya kikatili mno.
“Muuaji wa namna hii muda si mrefu atakamatwa , shangazi huna haja ya kuwa na wasiwasi sana”
“Natamani wakimuona wampige risasi wamuue kabisa , jamani mtu anaua watu wasio na hatia kikatili namna hio , tena wasichana wadogo”Aliongea Shangazi na muda huo huo kengele iligonga ikionyesha kuna mgeni.
Shangazi alienda kufungua mlango wa geti na alishangaa baada ya kuona ni Polisi.
“Ndugu polisi kwanini…”
Walikuwa ni Polisi wanne wote wakiwa katika sare zao za kipolisi , aliekuwa mbele alikuwa na uso ulichongoka na mweusi Tii.
“Mama hapa ni nyumbani kwa Regina Wilson?”
“Ndio , upo sahihi , mnamtafuta?”
“Naitwa Afande Mlonga kutoka kituo cha polisi mjini kati idara ya uchunguzi , kuna kesi inayomhusu Regina Wilsoni na tupo hapa kwa uchunguzi”
Muda uleule Regina alikuwa ashatoka nje baada ya kuona Shangazi harudi na mara baada ya kuona ni polisi alimwambia shangazi awaruhusu.
Polisi wale walikaribishwa mpaka ndani sebuleni huku wakiangaza angaza kulia na kushoto kwa namna ya kuchunguza uzuri wa jumba hilo kabla ya kukaa kwenye sofa.
Shangazi kwa haraka hraka alikimbilia friji na kuwaletea maji kama walivyoomba , lakini alikuwa na wasiwasi mno kiasi cha mikono yake kutetemeka.
Afande Mlonga macho yake yalikuwa kwa Hamza tu , ni kama alikuwa akimchhunguza , upande wa Hamza alikuwa zake bize akitafuna ma’apple’.
“Miss Regina naomba kuuliza huyu Mr hapo ni nani kwako?”Aliongea Mlonga na swali lile lilimfanya Regina kusita lakini kutokana na uwepo wa Shangazi aliamua kuongea.
“Ni mpenzi wangu”
Baada ya kujibu hivyo Afande Mlonga na wenzake ni kama hawajatarajia jambo hilo.
“Tulisikia habari nyingi unaenda kuolewa na mtoto wa Mzee Benjamini , hatukutarajia kuona tayari una Boyfriend”
“Naona taarifa zangu zinazagaa sana lakini hili linanihusu mimi na yeye , sikuona haja ya kuliweka wazi, sidhani kama ni kosa?”
“Hakuna mgongano wowote baada ya hili na familia ya Mzee Benjamini?”Aliuliza Mlonga huku wakionyesha kunakiri majibu.
“Nyie wote ni polisi , sidhani ni vizuri kuuliza maisha yangu binafsi”
“Usituelewe vibaya Madam , ni kwasababu kilichotuleta hapa kina uhusiano na maisha yako binafsi”Aliongea na muda uleule Afande Mlonga aliweka picha chini , zilikuwa ni za gari ya Regina.
“Hili gari limesajiliwa kwa majina ya Regina Wilsoni ambapo tunaamini wewe ndio mmiliki halali , juzi limeonekana katika kijini cha Wavuvi Zinga bagamoyo na Dereva aliekuwa akiendesha gari hio ni moja ya mhangwa wa mauaji.. wakati wa kurudi gari ilikuwa ikiendeshwa na huyu mwanaume ambae umesema ni Boyfriend wako”Aliongea huku akiweka picha ya Hamza akiendesha gari hio hio na gari ikiendeshwa na mwanamke, alikuwa ni Corresa.
Regina mikono yake ilicheza na bila hata kujijua alihikilia sketi yake , akiwa na wasiwasi, mwanamke aliekuwa kwenye picha alimfahamu ni moja ya watekaji.
“Kwahio amekufa?”
“Kwanini unauliza , inamaana hujui kama amekufa, tunaamini watu wote waliokufa walikuwa ndani ya gari lako”
Regina aliishia kugeuza kichwa chake na kumwangalia Hamza lakini upande wa Hamza hakuonyesha wasiwasi kabisa , lakini kwake aliona hio kesi sio nyepesi, baada ya kufikiria kwa muda Regina aliona aeleze moja kwa moja kilichotokea.
“Nilitekwa siku hio , lakini sikujua watu wale walikuwa ni wakina nani maana walikuwa ni raia wa kigeni , nilikuwa sina fahamu na pale niliposhituka nilikuwa nishaokolewa tayari na Hamza , kuhusu watu hao kufa sikuwa nikijua chochote”
“Kwahio unamaanisha huyu Mr Hamza ndio aliekuokoa na baada ya hapo akawaua hawa wahalifu?”
“Ma afande mnakosea , sijaua mtu , mimi nilienda nikawapa kichapo tu , sidhani kama mnaweza kunilaumu kwa hilo”Aliongea Hamza lakini Regina aliona hali inazidi kuwa mbaya na alitaka kutumia nguvu yake hivyo alisimama.
“Afisa mna ushahidi wowote wa kuonyesha Hamza ndio aliewaua?”
“Usipaniki Madam , hata kama Mr Hamza ndio aliehusika sio kosa , kwasababu hawa wahalifu ni kama Mr Hamza tu , lakini tunahitaji kuchunguza hili swala, tunataka kujua imekuwaje Mr Hamza akawa na uwezo wa kuua hawa wahalifu wa daraja la juu , wanaosakwa dunia nzima”
“Mimi ni mwanafunzi wa chuo na fundi , nina nguvu nyingi hivyo mapigano yalikuwa makali sana , lakini sijua mtu”Aliongea Hamza.
“Mr Hamza tunakuahidi hatutokutia hatiani kwa kuuwa hawa watu , tunachotaka kujua ni kilichotokea katika mazingira ya kirafiki tu”AliongeaMlonga huku akiwa na tabasamu bandia.
“Kama mnao ushahidi wa kutthibitisha niliwaua basi nitawaelezea kilichotokea , lakini ushahidi hamna na mpo hapa mnanijaribu siwezi kuwaambia chochote”
Polisi hao walijikuta wakiwa kimya , alichoongea Hamza kilikuwa na ukweli ,hata hivyo kesi haikuwa chini yao , baada ya kesi hio kutolewa ktuoka kitengo cha MALIBU na kuhamishiwa idara ya polisi Afande Mlonga ndio alipewa kazi ya kuongoza uchunguzi , lakini licha ya kupata picha hakukuwa na alama za vidole zinazomlenga moja kwa moja Hamza ndio alifanya mauaji.
“Afande Mlonga kama hakuna ushahidi siwezi kukubali mpenzi wangu kusingiziwa , kama kuna ambacho nitaweza kufanya kwasasa ni kumshirikisha mwanasheria wangu ili muongee nae yeye , hivyo naomba muondoke nyumbani kwangu na mkatafute Warantt kwanza”
“Madam , mpaka sasa nadhani umeona taarifa ya habari inayohusisha muuaji anaeua wasichana wadogo kwa kuwakata viungo vya siri , unadhani ni salama kwako kukaa na mtu ambae humjui vizuri”
“Chunga maneno yako afande , chochote utakachoongea bila ushahidi nitakushtaki nacho”Polisi wengine walitaka kuongea lakini Afande Mlonga aliwazuia.
“Kama ni hivyo basi hatuna haja ya kukaa zaidi na tutaondoka , ila kama kuna ushahidi tutarudi”Aliongea na kisha wote kwa pamoja walitoka nje.
“Regina nini hiki kinaendelea , ulitekwa?”Shangazi ndio aliekuwa akiuliza huku akionekana kuwa na maumivu ya moyo.
“Shangazi sikufanya makusuti kutokukuambia , sikutaka kukufanya kuwa na wasiwasi , lakini lishaisha”Aliongea na Shangazi aliishia kuvuta pumzi huku akijikalia kwenye sofa.
“Asante Mungu angalau amekukutanisha na Hamza angalau anaweza kukulinda, ningefanya nini mimi kama ningekuwa peke yangu”Aliongea Shangazi akijituliza lakini wakati huo Regina alimwangalia Hamza kwa macho ya kuchukia.
“Sijui kama umeua au hujaua , lakini hili swala linapaswa kuisha ukiwa hujaua”Aliongea.
“Haha.. Regina asante sana kwa kunijali”
“Eti kukujali , sitaki kuhusika katika hili ndio maana , nina kazi nyingi za kufanya”Mara baada ya kuongea hivyo kwa hasira alipandisha juu huku akifunga mlango kwa nguvu.
Upande wa Shangazi alimwangalia Hamza kwa macho yenye umakini mkali , ni kama kuna kitu anakitafuta.
“Hamza hukupata tatizo?”Aliuliza.
“Shangazi usiwe na wasiwasi ni swala dogo na lishaisha”Aliongea na Shangazi alitingisha kichwa kuelewa.
“Naona unatafuna sana matunda , kama hamjala mchana niwaandalie chochote”
“Hakuna shida shangazi”
*****
Upande mwignine mara baada ya mafande wale kutoka walisogelea gari ya Land Cruiser na kuingia ndani , kulikuwa na watu wawili ndani ya gari hio tayari , mmoja akiwa dereva na mwingine akiwa ni mwanaume mnene hivi mwenye kitambi aliekaaa nyuma.
“Kanali , tumemaliza mahojiano nae , lakini mambo yamekuwa magumu kuliko tulivyotarajia”Aliongea Mlonga akimwambia yule mzee aliekuwa kwenye gari.
“Nini kimetokea?”
“Amekataa yeye kutohusika kabisa , cha kushangaza sio dereva wala mlinzi tu ni Mpenzi wa bosi Regina”
“Nini , mpenzi!!, Sio James tena”
“Hata sisi tumeshangaa , inaonekana kuna kinachoendelea , lakini sidhani kama kinahusiana na hii kesi”Aliongea Mlonga na kumfanya mwanaume alieitwa Kanali kufikiria kidogo.
“Mlonga nakuamini uwezo wako wa kumjua mtu kwa kumwangalia tu , wewe unamuonaje , unadhani ndio aliehusika kuua watu hatari kama wale?”
“Dastani sijui hata namna ya kumuelezea , ukiachana na ushombeshombe wake nimemuona kama mtu wa kawaida sana… lakini kuna kitu sio cha kawaida nimekiona”Aliongea.
“Kitu gani mmekiona?”
“Hakupaniki kabisa , ni kama vile alitarajia ujio wetu na wala hakuonyesha kukasirika hata tulivyomwambia ameuwa watu wale , ki ufupi hakuonyesha kuwa na wasiwasi wakati tunamuuliza maswali, lakini ukiachana na hilo sioni kama ni mtaalamu , anaonekana kama vile ni mfanyakazi wa kawaida tu wa kwenda kazini na kurudi nyumbanni kuangalia TV”Aliongea na Kanali Dastani alionekana kuwaza.
“Kanali hii kazi haiwezi kuwa rahisi kama ikiendelea kuwa chini ya Idara ya polisi , Kitengo cha MALIBU kina kila rasilimali ya kufanikisha hili”Aliongea Mlonga.
“Unadhani hatujui kuhusu hilo , unadhani kwanini sikutaka kuambatana na nyie moja kwa moja kwenda kufanya mahojiano nae , hizi ni taratibu za kitengo pia katika hatua za ki uchunguzi”
“Mkuu unamaanisha na nyie mnaendelea na uchunguzi kimya kimya?”
“Mlonga licha ya kwamba upo vizuri kwenye mahojiano lakini kuna baadhi ya sehemu haupo vizuri , Ni lini ushawahi kuona MALIBU wakimhoji raia moja kwa moja , tunatumia idara ya polisi kufanya kazi hii , hivyo mlichofanya ni kutimiza wajibu wenu na sisi tutatimiza wajibu wetu”Aliongea na Mlonga alitingisha kichwa kukubali
“Ila Kanali kama kweli ndio amehusika na mauaji ya maninja kutoka Ufilipino basi ni mtaaamu wa hali ya juu na atakuwa ameficha ushahidi wa sisi kumfikia , hivyo uchunguzi chini ya idara yetu utakuwa mgumu kweli”
“Kama unahisi hivyo , basi atakuwa haogopi hata tukiwa na ushahidi kuna kinachoniambia sio wa kawaida”Aliongea moja ya polisi akitoa mchango wake.
“Kama ulivyosema ni sahihi , unadhani kwanini hakukuwa na alama yoyote hata ya vidole tu kuonyesha yeye ndio muuaji , alionekana kuwa makini , hata kama ameonekana kwenye gari ashajiandaa namna ya kujitetea”
“Kanali kwanini tusimkamate moja kwa moja , kuna uwezekano akawa na uhusiano na mauaji ya wanawake yanayoendelea”
“Hatuwezi kwenda moja kwa moja kwenye hitimisho , iwe yeye ndio muuaji au sie kama polisi mnapaswa kuendeleza uchunguzi wetu na kuwe na ushahidi , muuaji lazima akamatwe na haya ni maagizo kutoka juu , mkitimiza wajibu wenu na sisi wa kwetu kazi itakuwa rahisi , Mlonga hili lipo juu yako na timu yako, Ondoa gari napaswa kwenda kuripoti makao makuu”Aliongea Kanali na gari iliendeshwa muda uleule.
Nusu saa tu Kanali Dastani alikuwa akiingia katika kitengo cha MALIBU makao makuu , na alipiga hatua zake kana kwamba hataki kufanya watu wajue amefika.
Hakuelekea moja kwa moja katika ofisi ya mkuu wake bali alienda moja kwa moja katika ofisi yake , alitaka kukusanya ripoti kamili kabla ya kuiwasilisha.
Siku kadhaa nyuma alipewa kazi ya kuhakikisha anajua ni nani aliehusika katika kuuwa wale raia wa kigeni na kazi hio alikuwa ameifanya kwa uadilifu mkubwa mpaka kumpatia majibu aliokuwa akitaka.
Mara baada ya kufika katika ofisi yake aliingiza nywira katika tarakishi yake na palepale ilionekana Vidio ambayo ilionekana ilikuwa ikicheza lakini ikasitishwa kwa muda.
Kanali mara baada ya kukaa kwenye kiti aligusa batani na palepale Vidio ile ilianza kuonyesha Kapteni Yonesi akipigana na Master Konki na kudhibitiwa na ghafla tu Hamza anaingilia na kumuadhibu Master Konk.
Aliichezesha kwa kuirudisha mbele na nyuma kwa zaidi ya mara tano na alionekana kufikiria kitu.
Baada ya kukaa kwa muda katika ofisi yake , ujumbe wa meseji uliingia kupitia watsapp na alipoona jina lililomtumia ujumbe huo alifungua haraharaka na alikuta kuna kiambatanisho cha nyaraka iliokuwa katika mfumo wa PDF.
Kwa haraka haraka aliihamishia kwenye tarakishi yake na kisha akaigeuza nyaraka ile kwa kuiprint, kadri alivyokuwa akiisoma ndio jinsi uso wake ulivyojikunja.
“Hamza ndio muhusika , nina uhakika asilimia mia moja , kabla ya ripoti ngoja nikutane na Yonesi kwa siri kwanza”Aliongea na kisha palepale alizima tarakishi yake na kuchukua karatasi alioprinti na kujiandaa kutoka lakini muda uleule simu yake iliiita na alipoangalia jina lilisomeka Dokta Bensoni.
“Bensoni’Aliongea mara baada ya kupokea.
“Amosi amerudiwa na fahamu nusu saa iliopita” sauti ilisikika na kufanya moyo wa Kanali Dastani kudunda.
“Nakuja sasa hivi Dokta , mdunge kwanza sindano ya usingizi?”
“Kuna tatizo Dastani”
“Tatizo gani?”
“Nimefanya kupigiwa simu baada ya kurudiwa na fahamu , lakini nafika hospitalini Amosi hayupo”Aliongea na Kanali Dastani palepale uso wake ulikunjamana.
“Unamaanisha nini Bensoni”
“Ametolewa hospitalini na haieleweki amepelekwa wapi , ki ufupi Amosi ametoweka”
“Fu**ck , unanitania Bensoni , Amosi anatoweka vipi ndani ya hospitali ya jeshi”
Kanali Dastani hakuwa hata na muda wa kumfikiria tena Yonesi , aliona analo swala muhimu zaidi la kushughulika , hofu ilimvaa , kama Amosi ametoweka bila ya kupata maelekezo yake kuna hatihati familia yake inaweza ikawa mashakani , lazima Amosi atakuwa anafikiria kulipa kisasi kwa kumsaliti.
****
Hamza hakuwa hata na wasiwasi juu ya polisi waliofika hapo , mawazo yake yalikuwa siku ya kesho wapi anamtoa out mpenzi wake Eliza, ki ufupi hata swala la Frida hakulitilia maanani kabisa.
Sio kama hakuwa na uzoefu , ukweli ni kwamba pengine Eliza anaenda kuwa mwanamke wake wa kwanza kuwa nae katika mahusiano yenye usiriasi.
Hamza aliona kabisa amekuwa mzembe , kitendo cha mrembo Anitha wa chuo kumkataa ilithibitisha kabisa alikuwa mzembe na mvuto wake umeshuka , hivyo alitaka kujua namna ya kumpagawisha Eliza.
Baada ya kuwaza kwa muda alienda mpaka chumba cha kujisomea cha Regina na aligonga mlango na kuambiwa aingie na mara baada ya kuingia Hamza alianza kuangalia vitabu vilivyokuwa kwenye Shelf bila ya kuongea.
“Wewe unafanya nini?”Aliuliza Regina , wakati huo aliwaza Hamza alifika kwa ajili ya kuelezea kwanini wale watekaji walikuwa wamekufa lakini anaanza kuchunguza vitabu vyake.
“Naangalia kama nitaona kitabu cha kunifaa hapa”
“Naona umekumbuka kuwa ni mwanachuo , kitabu gani unataka?”
“Hehe.. kinachohusiana na mapenzi”Aliongea na kauli ile ilimshangaza Regina.
“Yaani hakuna kitabu cha maana unachotafuta zaidi ya vitabu vya kipuuzi namna hio?”Aliongea kwa hasira.
“Nataka kujifunza namna mapenzi yanavyoendeshwa , jinsi vitu vya kumfanyia mpenzi wako akolee bila ya kumhonga , kuna haja gani ya kukasirika hivyo bosi?”
Mapenzi!, Regina hakujizuia na kuwaza au Hamza anataka wawe wapenzi kweli , baada ya wazo hilo aliona aibu za kike na kugeuka.
“Sina hivyo vitabu , unaweza kuondoka”Aliongea akiwa siriasi.
“Kama huna ngoja nikatafute mtandaoni, nilijua pengine na wewe una shauku ya mapenzi yalivyo”Aliongea Hamza na kisha alitoka nje.
Regina mara baada ya Hamza kutoka alijikuta akivuta pumzi nyingi , mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda kasi mno kana kwamba amekutana na Simba mkali , alijikuta akishika uso wake na kuona umepatwa na joto.
“Mjinga huyu , kuna haja hata ya kusoma kwenye kitabu..”Aliwaza.
Baada ya kukaa akifikiria kwa muda alishika tarakishi yake na alisita kwa muda lakini alijikuta akiingia mtandao wa Google na kuandika , How to fall in love.
*****
Asubuhi kama kawaida Hamza aliamka mapema na kucheza mdundiko nje katika mpangilio maalumu , na baada ya kunywa chai alibadili katika mavazi mapya kabisa alionunuliwa na Regina.
Wakati akishuka kutoka chini Regina alikuwa sebuleni akiangalia taarifa ya habari kupitia CNN.
“Regina nadhani leo hakuna kazi yoyote , si ndio?”
“Ndio huna kazi ya kufanya leo , vipi unatoka?”Aliuliza na kumwangalia Hamza namna alivyopendeza.
“Ndio , nitatoka leo siku nzima , msinihesabu chakula cha mchana wala usiku”
“Unaenda wapi , kwenye kazi zako za ufundi kama kawaida , kama ni kazi ninazo nyingi tu unaweza kunisaidia”Aliongea Regina huku maneno yake akiwa hana uhakika nayo , alijua Hamza alikuwa na koneksheni kubwa hivyo hata hela lazima alikuwa nazo sasa alijiuliza kwanini anasoma chuo , kwanini aliishi maisha ya kimasikini kama vile hana hela.
“Wewe usinipe kazi ,nimepndeza vyote hivi niende kufanya kazi tena za nini, nina mtoko na mtoto mzuri leo , hivyo bosi leo ni siku yangu usinipigie simu”
Regina mara baada ya kusikia kauli hio , alijikuta akinywea lakini alibadilika dakika hio hio.
“Haina haja ya kuripoti una mtoko na mtoto mzuri”
“Haja ipo , tunaishi ndani ya nyumba moja na mimi ni mfanyakazi wako , sitaki itokee dharula nikiwa nakula bata uniambie nirudi nitamkera mpenzi wangu , lakini hata hivyo usiwaze sana , mpango wangu ndani ya miezi mitatu ikiisha sitotaka kuchelewa kuondoka hapa hata kwa sekunde, ila kwasasa nitahakikisha jambo letu linaendelea kuwa siri “
“Sina haja ya kujua kama una mpenzi hayo ni maisha yako ungeondoka zako tu bila kuniaga , kuna haja gani ya kuniambia”Aliongea Regina kihasira na kutupa Rimoti kwenye sofa na kupandisha zake juu.
Hamza aliishia kukuna kichwa chake na kujiambia kwani kosa lake ni lipi hapo , yeye kaomba ruhusa kwa bosi ni kufuata itifaki, hakutaka itokee anakula maisha na mrembo Eliza mara Regina anapiga wakutane.