SEHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI:SINGANOJR
SEHEMU YA 28.
Hamza ilibidi amuelezee Regina kwanini anataka aachane nae , alimwambia kwamba kama wataendeea kuwa pamoja kuna watu lazima wataendelea kufika kumtafuta na kusababisha matatizo , hivyo watu wa karibu yake watakuwa hatarini , hivyo hakutaka kumuingiza yeye katika matatizo yake.
“Usiwe na wasiwasi kabisa, nitalipa malipo ya kuvunja mkataba , pia haina haja ya kunilipa kupitia kampuni , nitaondoka bila kuchukua hela”Aliongea Hamza.
Regina macho yake yalichanua , hakujua kwanini lakini licha ya uhusiano wao kuwa wa kimkataba ila baada ya Hamza kusema anataka waachane kila mtu ajue mambo yake , alijihisi kukosewa , kutokubali na kujisikia vibaya.
“Kama ukiondoka sasa hivi , nitadili vipi na familia ya Mzee Benjamini , nitaenda kuwaambia nini wazazi wangu , unataka kuondoka halafu uniachie matatizo, huo ni ubinafsi usingekubali tokea mwanzo kama ungeondoka unapojisikia”Aliongea Regina huku akiwa amebadilika kabisa.
“Regina nilijua tu utakasirika , lakini jua ukiwa na mimi utajiingiza kwenye matatizo , hivyo ni kheri mimi kuondoka kuliko kuhatarisha usalama wako”
“Nimekasirika ndio lakini siogopi hatari yoyote itakayonijia kwanini unanisemea?”
“Lakini hizi ni hatari za kujitakia hazikuhusu kabisa , wewe ni wa nje tu , hivyo haina haja ya kujiingiza kwenye matatizo yangu”
“Wa nje? , wewe si ndio wa nje?”
“Unamaanisha nini?”
“Sikukuambia chochote kuhusu James wakati ule unasaini mkataba lakini pia wazazi wangu , sasa kwasababu yangu unachukiwa na James na familia yake na wazazi wangu hawakupendi pia, katika hili hata wewe ni wa nje tu na halikuhusu lakini mimi ndio nimekuingiza , kwanini hukuondoka wakati ule na kuamua kuondoka sasa baada ya matatizo yako?”Aliuliza Regina na kumfanya Hamza kushangaa , ni kweli hakuwahi fikiria juu ya hilo.
“Ngoja nikuambie sababu , hukuondoka kwasababu huwaogopi, wewe ni muongo, wasifu wako ni feki , kila kitu ni feki , pengine hata jina lako sio Hamza lakini kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho , hukuwahi kuwahofia James na familia yake kama wangeamua kukushambulia , si ndio”Aliongea Regina na Hamza alishindwa kujibu chochote.
“Sasa hivi ndio umeniingiza kwenye matatizo ndio unataka tuvunje mkataba , unanichukuliaje? , unaniona dhaifu sio??, unadhani mimi sio mvumilivu?”
Hamza na Regina waliishia kuangaliana tu kama mambwa wanaobwekeana, lakini kwa upande wake baada ya kuona namna mwanamke huyo alivyokasirika na muonekano wa kukosewa Hamza alishindwa kujizuia na kutabasamu.
“Sio kwamba nakuona dhaifu , niwe tu mkweli mimi sio mtu wa kufikiria mbali kama wewe , ninachotaka ni kutokukuingiza kwenye matatizo tu”
“Kwahio unadhani ukiondoka na matatizo yangu ndio yataisha?,unadhani tokea niwe CEO nishawahi kuwa salama , hivi unadhani kwanini nimeweka bajeti kubwa kwa ajili ya kitengo cha ulinzi wa kampuni na hata kumuajili Yonesi kutoka jeshini kwa ajili ya kuwafundisha wenzake?,wewe ni mwanaume lakini matatizo yakitokea unataka kukimbia, Uoga tu ndio unakusumbua?”
Hamza hakudhania Regina angelichukulia hilo swala kwa namna hio , alichokuwa akijaribu kufanya ni kuhakiksiha anabakia kuwa salama.
“Regina nimesema muda gani nakimbia matatizo , umenielewa vibaya , kama kweli unaniona mimi muoga unadhani ningekuja kukuokoa?”
“Kama wewe sio muoga na mimi kama mwanamke siogopi kitu , kinachokugopesha nini mpaka unataka kunikimbia?”Aliuliza Regina huku akimwangalia Hamza machoni.
“Ungejua ninachojaribu kukuepushia ni kheri usingejibishana na mimi na kukubali mara moja”Aliwaza Hamza katika kichwa chake lakini hakutaka kuongea waziwazi na aliishia kutoa tabasamu kwa namna Regina alivyoonyesha ujasiri mbele yake.
“Kwasababu wewe ndio umesema hivyo basi sitofanya kama nilivyosema”Mara baada ya mrembo huyo kusikia hivyo alivuta pumzi.
“Unadhani unaweza kuja kwenye maisha yangu na kuondoka , unadhani unaweza kuwa msaidizi wangu na Boyfriend feki unavyojisikia , hata kama unataka kuvunja mkataba mimi ndio mhusika mkuu lazima nikubali maana nimekuajiri”
“Ni kweli wewe ndio mwenye kauli ya mwisho , lakini tuishie hapa , sitotaka kukuelezea zaidi kuhusu mimi , isitoshe uhusiano wetu ni wa kikazi zaidi hivyo sio wajibu wangu”Aliongea Hamza.
“Okey , nitakuacha kwa leo , lakini nitajua tu iwe ni mapema au kwa kuchelewa”
Mpaka hatua hio Regina ashaona kabisa Hamza alikuwa akificha vitu vingi sana kuhusu yeye , kitu ambacho kilimfanya yeye mwenyewe kuvutiwa kujua zaidi.
Asichokijua Regina ni kwamba baada ya hapo hatokuwa wa kawaida tena, hisia zake mbele ya Hamza ndio zilianza kubadilika mara moja kuanzia siku hio.
Hamza na yeye aliishia kumwangalia mwanamke huyo , alikuwa mzuri mnno wa kuvutia kwa macho , licha ya madhaifu machache lakini upande wake mzuri ulikuwa umeyafunika.
Ghafla tu Hamza alijiktua akiangua kicheko , jambo ambalo lilimshangaza Regina.
“Unacheka nini?”
“Nimekumbuka ulivyosema hata jina langu linaweza kuwa feki , Mimi naitwa Hamza Mzee ndio jina langu halisi”Mara baada ya kusikia hivyo alijikuta akiona aibu za kike.
“Wewe ni mjinga , nani kasema anataka kujua jina lako halisi , hata kama umedanganya tutaenda na hili hili la Hamza”
“Vizuri , kwasababu mimi ni mfanyakazi tu huna haja ya kuwa na wasiwasi na mimi sana haha…”
“Hebu harakisha uko , chakula kinapoa kwa kuongea muda wote pumba”
“Sawa sawa , nitamaliza , ni bahati tu nimebakisha miezi mitatu pekee , vinginevyo nani anaweza kukuvumilia..”
“Unasemaje?”
“Ah .. sijasema kitu”
“Wewe, tutaona , mshahara wako lazima ni ukate”
“Haiwezekani Boss , nimefanya kosa gani”
******
Swala la Regina kutekwa liliisha kimya kimya , huku likijulikana kati ya Hamza na Regina mwenyewe , upande wa Regina hakuwa mdhaifu dhaifu hivyo halikumuathiri , ilikuwa ni kama kitu cha kawaida tu kumtokea.
Kils siku kama kawaida Regina alikuwa na utaratibu wa kutumia Makeup kwa mbaali na kufanya uso wake ambao tayari ni wa kirembo kuzidi kuvutia .
Kila nguo Regina aliovaa ilikuwa ikimpendeza , iwe ni rangi nyeusi , ya kijani au nyekundu, nguo nyingi za kike ambazo zilimfiti ni kama ametengenezewa yeye tu.
Hamza alijiuliza inakuwaje mwanamke akawa mrembo hivi , siku za nyuma wanawake aliowaona kama kipozeo tu kwa mwanaume , hakuwahi kupenda hapo kabla wala kumhusudu mwanamke , alijua kila mwanamke mzuri ni mali ya wenye nazo kwa ajili ya kutuliza akili zao.
Hamza alitamani Regina awe anakaa siti ya mbele lakini alipendelea kukaa nyuma na kushindwa kuuthaminisha vizuri urembo wake , kitu ambacho kilimshangaza zaidi jana walikuwa wakiongea na kucheka wakati wakurudi , lakini asubuhi hio Regina alikuwa kauzu isivyokuwa kawaida.
Hali hio ilimfanya Hamza kuona labda kuna kosa amefanya asubuhi na kumsababishia mwanamke huyo kukasirika..
“Hakikisha kesho hukai mbali na mimi?”Aliongea Regina aliekuwa siti ya nyuma ya gari.
“Kesho si jumamosi wikiendi , unakuja kazini pia?”
“Kuna mgeni wa muhimu tutakutana nae kesho muda wowote , ni Mfaransa na wewe unakijua vizuri kifaransa , hivyo itakuwa vizuri ukiwa na mimi kama msaidizi”
“Okey Boss”
Tokea asubuhi itimie ndio mara ya kwanza Regina ananyanyua mdomo na kumuongelesha.
“Hivi Regina , kuna kitu chochote ambacho nimefanya kimekukasirisha?”Aliuliza Hamza.
“Kwanini?”
“Kwasababu umekuwa kauzu sana”
“Wasiwasi wako tu , au unataka nikuchekee chekee muda wote”
“Sio hivyo , nakosa tu amani ulivyo mkimya”Aliongea na Regina aliishia kuonyesha muonekano wa kimapozi bila kubadili muonekano.
“Otea..”Aliongea
“Naoteaje sasa?”
“Basi tafuta majibu”Mara baada ya kuongea hivyo hakuonekana kujisumbua tena na Hamza.
Hamza aliona bora hata asingeuliza maana amejitia mawazo tu , hajafannya chochote lakini anaambiwa atafute majibu.
Mara baada ya kufika kazini Hamza alifanya kazi kama kawaida , hakuwa akizembea , ijapokuwa kila akifanya kazi alitafuta muda wakupumzisha akili yake kwa kufanya vitu anavyopenda mtandoani lakini kazi alizopatiwa alizifanya vizuri tu.
Muda wa mchana kama kawaida alishuka mpaka mgahawani na kuchukua chakula chake na kisha mara baada ya kumuona Yonesi akiwa peke yake kwenye meza alienda kukaa.
Hamza hakuwa muongeaji mara baada ya kukaa katika maeza ya Yonesi aliendelea kujiweka bize na chakula hata kwa Yonesi ni kama vile alikuwa ashazoea tu na hakumfukuza Hamza , lakini alikuwa na wasiwasi kutokana na utulivu wa Hamza , alimzoea kuwa roporopo.
“Unafikiria nini?”.
“Unaniuliza mimi?”
“Kuna mtu mwingine hapa?”
“Umeanza lini kunijali?”
“Nani kasema anakujali , nimekuuliza swali tu kama hutaki kujibu acha, wasiwasi wangu muhuni kama wewe kuna kitu lazima unakipnga kichwani”
“Kapteni wewe na Regina mmefahamiana kwa muda gani?”
“Muda mrefu tu , kwanini unauliza?”
“Regina ni mtu wa kubadilika badilika kuna muda unaweza kuongea nae vizuri lakini dakika chache zijazo anakuwa mtu mwingine kabisa , nimejairbu kuwaza labda nimemkosea mahali lakini nimeshindwa kukumbuka kabisa”Yonesi baada ya kusikia kauli ya Hamza alijikuta akishangaa lakini muonekano wake ulibadilika na kuwa ule wa kejeli.
“Unafikiria sana vitu visivyo na maana , Mkurugenzi akuongeleshe wewe ni nani , hayo ni mawazo yako tu ndio yanakusumbua”
“Kama ni hivyo basi nyie wanawake hamueleweki”
Hamza licha ya kwamba amepitia maisha flani ambayo mtu wa kawaida hawezi kupitia na hata kuwa na uzoefu wa hali ya juu lakini likija swala la kumuelewa mwanamke ilikuwa ngumu mmno kwake.
Baada ya lunch, Hamza alichukua matunda kama kawaida na kwenda nayo juu, wakati anatoka kwenye lift aliweza kukutana na Eliza ambae alionekana alikuwa akitoka ofisini kwa Regina.
“Eliza umerudi!?”Aliuliza Hamza huku wakionyesha furaha ya kumuona mrembo huyo.
“Huruhusiwi kuonyesha unanijua sana tukiwa kazini”Aliongea Eliza kikauzu.
“Oh , hakuna shida , halafu vipi mbona upo hivyo , hujafurahi kuniona?”Aliuliza Hamza mara baada ya Eliza kuonekana hataki kuongea nae.
“Nina kazi kibao, tutaonana”Aliongea Eliza na kisha aliingia kwenye lift akimuacha Hamza akimwangalia mpaka mlango ulipojifunga.
Hamza alijikuta akihema kwa nguvu na kujiuliza kwanini leo ni kama vile kila mwanamke hakuwa akitaka kumuongelesha.
Aliamua kuingia zake kwa Mkurugenzi ili kukabidhi yale matunda , Regina alikuwa bize kama kawaida yake akiwa na furushi la makatarasi juu ya meza yake.
“Mkurugenzi , kula matunda kidogo usifanye kazi na njaa”
“Sawa , unaweza kuyaweka hapo”Aliongea Regina bila hata ya kuinua macho.
Kwa namna Regina alivyokuwa makini Hamza alikuwa na shauku ya kutaka kujua mwanamke huyo ni kitu gani anafanyia kazi , hivyo alisogea karibu na upande wa meza yake kuchungulia.
“Hey , usichungulie, toka ofisini kwangu”Aliongea kikauzu na kumfanya Hamza kulazimisha tabasamu na kimya kimya akatoka huku akimwemwesa midomo na kujiambia wanawake wa aina hii ni ngumu sana kuendana nao vizuri hata kama una nia nzuri kwao.
Hamza mara baada ya kuingia ofisini kwake alianza kumfikiria Eliza na muonnekano wake wa dakika kadhaa zilizopita , baada ya kufikiria alihisi pengine Eliza na Regina waliongea kuhusu yeye ndio maana alionekana kana kwamba alikuwa akimkwepa.
Hamza mara baada ya kushikwa na wazo hilo palepale , hakutaka kusubiri alinyanyuka na kuelekea katika ofisi ya Eliza ili kujua kwanini mrembo huyo ni kama hana furaha kumuona.
Dakika chche tu alikuwa ameshafika katika idara ya mauzo(Sales department) , Eliza alikuwa akiongoza idara hio kama meneja mara baada ya kupandishwa cheo kutoka kuwa msaidizi wa Regina.
Baada ya kufika katika idara hio alikaribishwa , alijulikana tayari kama msadizi wa Regina hivyo mara baada ya kutaja shida yake ni kuonana na Eliza alielekezwa katika ofisi yake.
“Come in” Sauti kutoka ndani iiliitikia baada ya Hamza kugonga mlango na kumfanya aingie.
Eliza ambae alikuwa akiangalia tarakishi alishangaa mara baada ya kuona ni Hamza.
“Kwanini upo hapa?”Aliuliza na Hamza alitembea na kwenda kuweka mikono yake yote juu ya meza huku akimwangalia mrembo huyo kwenye macho.
“Eliza je kuna kitu chochote unahisi kunishuku?”
“Kukushuku , unamaanisha nini?”Aliuliza Eliza huku akiwa na muonekano wa kushangaa na kuchanganyikiwa kwa wakati mmoja.
“Unaonekana kutokuwa furaha hata pale uliponiona , au kuna mtu alisema chochote kunihusu mimi?”
Eliza mara baada ya kujua kile kilichomleta Hamza hapo aliishia kuweka mikono yake juu ya meza na kupitisha vidole vyake na kuishia kutoa tabasamu.
“Hakuna”
“Kama ni hivyo kwanini unaonyesha kutokuwa furaha baada ya kuniona?”
“Otea”
Hamza mara baada ya kusikia kauli hio hakujua alie au acheke , maana hata Regina alimwambia hivyo hivyo.
“Eliza hebu acha kunitesa na kujitesa , naoteaje sasa kitu nisichokijua , hatujaongea zaidi ya wiki sasa , mimi nitajua ni wapi nimekukosea?”
“Kwahio unakiri kabisa hatujaongea wiki nzima , tuseme hukuwa na salio kunipigia , vipi hata meseji umeshindwa kunitumia?”Hamza sasa alijua wapi kosa lake lilipo.
“Eliza nisamahe , mimi sio mzoefu sana likija swala la mahusiano ndio maana sikupiga simu”
“Nani aamini maneno yako , sipo kichwani mwako ndio maana, usingenikiss kabisa kama unashindwa kujua namna ya kuwajibika”Eliza alitaka kusema umenikisi kitaalamu vile halafu unasema huna uzoefu ila hakutaka kuongea hivyo na kubadilisha maneno.
“Eliza kukukiss na kukupigia simu ni vitu viwili tofauti , nilikosa tu sababu ya kukupigia ndio maana , ila nilikuwa nikikuwazia”
“Kwahio unapiga ukiwa na sababu ya kunipigia , hebu toka ofisini kwangu acha kunipotezea muda nina vitu vya kufanya”Aliongea huku akionyesha kukasirika akiwa amesimama.
Hamza aliona kuendelea kuongea nae akiwa amekasirika hivyo haina maana tena , alimsogelea Eliza kwa haraka na kushika kiuno chake na kisha akamkiss na kumfanya Eliza kutoa macho maana hakutegemea kile kitendo , Eliza aliishia kushika mbavu za Hamza na kuziminya , alikuwa hataki lakini kujiondoa alishindwa.
Baada ya dakika moja Hamza alimuachia , alijua akiendelea wanaweza kuingia katika hatua isiofaa katika mazingira hayo ya kazini.
“Nakuahidi kuanzia sasa nitakuwa nakupigia bila hata ya sababu”Aliongea Hamza huku akimwangalia Eliza ambae ameshikwa na aibu lakini kwa namna moja alijisikia vizuri mno na furaha.
“Nimekusikia ,ushamaliza kazi zako , niache nimaliza na zangu”
“Jumapili utakuwa na muda , unaonaje tukitoka out hata kwenda kupunga upepo baharini na kula mihogo?”
Eliza alifikiria kwa muda na kweli aliona hana ratiba yoyote Wikiend hivyo aliishia kutingisha kichwa kukubali.
Muda huo huo mlango wa ofisi ya Eliza uligongwa na sauti ya Mirium ilisikika.
“Meneja , hali sio nzuri huku , kuna tukio kubwa limetokea”.Eliza alijiweka sawa huku akiondoa hali ya aibu usoni na kurudia ile ya kazini na kisha alisogelea mlango na kuufungua.
“Nini tatizo?”
Mirium mara baada ya kuona na Hamza yupo ndani ya ofisi aliishia kutingisha kichwa kumpa ishara ya salamu.
“Dakika chache zilizopita kupitia taarifa ya habari Afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Omega ametangaza kukubali kutia saini kwa niaba ya kampuni yake kuuzwa kwenda Zena Corporation”
Eliza macho yake yalisinyaa na alitoka moja kwa moja na kwenda katika ofisi kubwa pana iliokuwa na Tarakishi nyingi za wafanyakazi wa idara ya mauzo.
Muda huo wafanyakazi wa kampiuni nzima walikuwa wakiangalia taarifa hio ya bahari.
Zena Corporation ilikuwa chini ya familia ya mzee Benjamini baba yake na James.
Kila mtu alionekana kuwalaani Zena kwa kukosa aibu na kuingilia dili lao la kuiunua kampuni ya Omega.
Eliza aliongoza wafanyakazi wenzake katika idara ya mauzo kujadili kile kilichokuwa kimetokea.
Upande wa Hamza alikuwa akijua dili hilo la kampuni ya Dosam kutaka kuinunua Omega hivo kuona taarifa hio alijua na Regina atakuwa katika hali mbaya, ukweli hakujua kama Regina atakuwa katika hali gani.
“Kama sio pingamizi kutoka kwa wakurugenzi wasaidizi , Zena wasingeweza kufanikiwa”
“Ndio , Mkurugenzi alikuwa sahihi pia , kama sio hivyo mnadhani Zena wangefikiria kuinunua Omega?”
“Mimi nashindwa kuelewa , hawa wakurugenzi ni wazee lakini bado wanashindwa kuelewa soko linakoelekea , kwanini wanapinga ustawi wa kampuni”
Wafanyakazi walikuwa wakiongea wao kwa wao huku wakimuonea huruma bosi wao kwa namna ambavyo wakurugenzi wenzake wamemsaliti mpaka kufanikisha Zena kuinunua Omega.
Mipango ya Regina katika kupanua kampuni ilikuwa wazi kwa kila mmoja , alitaka kununua kampuni ya maswala ya Tehama ya Omega kwa ajili ya kuingia katika biashara ya Akili Mnemba(Artificial intelligence), alijua ili kampuni yake iweze kupanuka zaidi alihitaji kitu ambacho kinaendana na wakati uliopo na ujao , kwa Regina aliona mfumo wa akili bandia utakuwa ndio kesho ijayo.
“Meneja ni nini tunapaswa kufanya , Omega ndio hio tushaikosa , unadhani mauzo yetu yataendelea kupanda”’Aliuliza Asha na wengine wote.
“Tupo kwenye idara ya mauzo, tunachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wetu , hili swala lipo chini ya idara ya Trustees , Mikakati na masoko , tunamuamini Mkurugenzi wetu Regina, najua atapata ufumbuzi ,nimeongea vya kutosha sasa , tungieni kazini”Aliongea huku akipiga makofi akitawanya wafanyakazi wote kurudi katika nafasi zao za kazi.
Hamza mara baada ya kuona hilo alijua lazima Regina atakuwa anajisikia vibaya , ilionekana dhahiri kuna mtu ndani ya kampuni alivujisha taarifa.
Muda wote wa mchana wafanyaazi wa juu wa kampuni waliingia ndani ya ofisi ya Afisa mtendaji mkuu wa kampuni mmoja baada ya mwingine , ilikuwa ni kama kampuni yote ilikuwa katika hatari , Hamza aliweza kuona namna ambavyo Regina amechoka wakati wa kuondoka.
Mara baada ya kuingia kwenye lift aliishia kuegamia lift na hakuongea neno , Hamza na yeye hakutaka kumsumbua , ilikuwa ni mara ya kwanza kuona mwanamke huyo akionyesha hali ya kukosa utulivu na kwa namna flani Hamza alimuonea huruma.
Kwa mfanyabiashara kama Regina kwake hela inakuwa sio kipaumbele tena , bali kipaumbele ni malengo ya kampuni kutimia.
Kitendo cha kufika katika maegesho ili kuingia kwenye gari waliweza kuona gali nyeusi aina ya Caddilac ikiwa imeegeshwa.
Mabodigadi wawili wenye miili ya kibaunsa walikuwa wamesimama pande zote za gari wakiwa na miwani za jua huku mlango wa kuingilia katika gari hio ukiwa umefunguliwa na alionekana James ambae alikuwa amevalia shati la mikono mirefu na suruali ya kitambaa pamoja na saa ya dhahabu.
Ukiachana na mabodigadi hao pamoja na James kulikuwa na mtu mwingine mzee hivi , alikuwa amevalia shati refu mfano wa kaunda rangi ya bluu bahari , kitu kimoja ambacho hakikuwa cha kawaida kutoka kwa mzee huyo ni macho yake , yalikuwa yamejaa uovu sio wa kawaida.
Dakika ile le Kaptenni Yonesi pamoja na walinzi walitokea mbio mbio
“Mkurugenzi , samahani tumeshindwa kuwazuia ndani ya muda”Aliongea Yonesi.
Regina macho yake yalikuwa yamejaa ukauzu na alionyesha kila ishara ya kuwa na hasira , mara baada ya kumwangalia James kwa sekunde alitembea kulisogelea gari lake.
Lakini James alitabasamu kikejeli na alimkinga Regina kwa mbele na kisha akamwangalia na Hamza aliekuwa nyuma.
“Wewe kumbe bado upo tu , nimesikia umekuwa msaidizi , hio nafasi inakufaa sana kwenye maisha ya Regina”Aliongea.
Hamza alimwelewa alichokuwa akimaanisha , hakutaka kukubali yeye na Regina ni wapenzi
Regina upande wake hakutaka uhusiano wake kutambulika kwa walinzi hivyo alimwambia James ampishe apite.
“Regina achana na ukauzu wako , najua haupo kwenye mudi leo lakini hayo ni maswala ya kibiashara, maswala yetu binafsi hayawezi kuathirika”
“Hakuna maswala binafsi kati yangu na wewe”
“Kinachokukasirisha ni kuikosa Omega, wasiwasi wa nini , mimi na wewe tukishaoana familia yenu na yetu itaungana , nimeandaa mahali tayari ambayo familia yako itaipenda”
“James acha kwenda mbali , upo ndani ya maegesho ya kampuni yetu , Mkurugenzi anataka umpishe, sijui unanisikia?”
“Nisipompisha utanifanya nini wewe Mal**ya”
“Unanitukana wewe mwanaharamu”
Yonesi hakutaka kujizuia tena , hakupenda matusi na aliona amshikishe adabu lakini Regina alimzuia.
“Yonesi punguza hasira”
“Mkurugenzi .. amenitukana umemsikia..”Aliongea lakini aling’ata meno yake kwa hasira na kutulia.
“James unachotaka kutoka kwangu ni nini mpaka unatoa matusi hapa?”Aliuliza Regina.
“Sitaki chochote , kwanini nitake kitu kutoka kwa mwanamke ninaempenda kama wewe, nataka ukubali kutoka na mimi usiku kwa ajili ya chakula”
“Sijisikii vizuri”
“Kama hujisikii vizuri nitakupeleka hospitalini”Regina aliishia kumwangalia kwa macho ya hasira , hakupenda uking’ag’anizi wa James hata kidogo.
“Regina unatakiwa kujua tayari umeshindwa, kama ukiendelea kuhangaika kama hivi , hali itakuwa mbaya zaidi kwako na kwa watu wanaokuzunguka , kama una akili kubali kuolewa na mimi na tuishi maisha ya furaha , nakuhakikisha hototeseka”
Mara baada ya kuongea hivyo alinyoosha mkono akitaka kumshika Regina kidevu.
Yonesi mara baada ya kuona tukio hilo alimkinga Regina na mwili wake.
“Acha ukichaa wako , huruhusiwi kumsogelea Mkurugenzi”
“Fu**ck , wanaumee, hebu muondoen huyu ch*ko”’
“Yes sir”
Mabodigadi wawili waliovalia suti nyeusi walisogea mbele kwa ajili ya kumtoa Yonesi.
Walinzi waliofika na Yonesi , mara baada ya kuona kapteni wao anasogelewa na wao walisogea na kuwakinga wale mabodigadi.
Mabodigadi wa upande wa kampuni ya Dosam walikuwa wanne na walishindana na mabodigadi wawili aliofika nao James, walikuwa wengi na walikuwa maveterani wa jeshi hivyo ilikuwa faida kwao.
Yonesi mara baada ya kuona maadui zake wanazidiwa aliruka na teke na kumpiga moja ya bodigadi na akaenda mzima mzima chini na palepale wale wengine walimdhibiti yule mmoja.
Regina mara baada ya kuona walinzi wake wameweza kufanikiwa kushinda alivuta pumzi ya ahueni.
Lakini James hakuwa na wasiwasi wowote na aligeuza shingo yake na kumwangalia yule mzee.
“Master Konki huyu mwanamke sio wa kawaida , hata kama ukimshambulia haiwezi kuonekana unamnyanyasa maana ni mwanajeshi”Aliongea James.
Yule Mzee alieitwa Master Konki alimwangalia Yonesi kwa macho ya kumchunguza na aliishia kwenye kifua chake akithaminisha urembo wa mwanamke huyo.
“Mwanamke mrembo kama huyu lakini anataka kushindana nguvu na wanaume , hebu ngoja nimfundishe adabu kidogo aanze kufikiria namna ya kumhudumia mwanaume”Aliongea hukuwa akiwa na tabasamu la kifedhuli.
Yonesi mara baada ya kuona mzee huyo anamsogelea uso wake ulizidi kuwa siriasi , alijua kitendo cha James kuja hapo akiwa anajiamini akiongozana na mwanaume huyo basi lazima atakuwa na uwezo wa juu.
Hamza palepale alipitisha macho yake ya ki uchunguzi kwenye mwiali wa mzee huyo na aliweza kuona kitu kilichomfanya kukunja sura na kumuonea huruma Yonesi matatizo anayojitafutia
“Nina wasiwasi naweza nimshindwe huyu mzee”Aliwaza Yonesi kwa hofu.
“Kapteni huyu mwanaume amezeeka lakini bado anaonekana kuwa na tamaa , nipe nafasi nimfundishe adabu mimi”Aliongea moja ya mlinzi wa kampuni.
“Sogea mbali , mimi ndio kiongozi wewe ni msaidizi tu nitamshikisha adabu mimi”Aliongea Yonesi kwa kujigamba.
“Kapteni kuwa tu makini , mimi nitakushangilia ukishinda”Aliongea Hamza huku akicheka.
“Huna haja ya kuongea”Alijibu.
“James nadhani ushanipa ruhusa ya kumkamata huyu mwanamke na kuondoka nae”
“Usiwe na wasiwasi Master Konki , mimi shida yangu ni mchumba wangu Regina , huyo mwanamke unaweza kumfanya chochote ukishamshikisha adabu, nakuhakikishia hivi , hakuna kitengo cha usalama cha aina yoyote ndani ya taifa hili kitakuuliza”
“Vizuri sana kijana , nimekaa mafunzoni kwa muda mrefu bila kuonja nyama tatu , kwa urembo wa huyu binti atakidhi kabisa matamanio yangu”Aliongea Konki.
“Na uzee wote huo lakini unaongea bila busara , usamehewe bure , isitoshe mpaka kuja na James hapa inaonyesha ni kwa namna gani huna akili”Aliongea Yonesi kwa hasira.
Dakika hio hio Yonesi aliamua kukaa mkao wa kijeshi , huku akimwangalia Mzee Konki na macho ya tahadhari.
“Sogea mrembo nione ni kipi una cha kunishangaza”
“Umeomba mwenyewe usije kunilaumu”Aliongea Yonesi na palepale aliinua mguu wake na kudhamiria kumpiga yule mzee lakini kabla hata hajamfikia Konki alikuwa ashainua mkono wake na kuzuia lile teke huku vidole vyake vitatu vikitengerneza umbo kama kucha za Tai na kwa ustadi wa hali ya juu alimchoma na vidole vile eneo la mguuni.
“Arghhhhh..”
Yonesi alijikuta akipiga ukulele wa maumivu na bila ya kupenda alirudi nyuma huku akisikiliza maumivu , hakuamini vidole vitatu tu vinaweza kumletea maumivu makali ya namna hio.
“Mbinu ya kimapigano ya kucha za Tai”Aliongea huku akiwa na mshituko, Yonesi hakutarajia mzee kuwa na uwezo huo , kwa kawaida Yonesi alikuwa mzoefu likija swala la mbinu za kimapigano , wakati alipokuwa jeshini alishahudhuria kozi ya kimapigano katika taifa la Thailland na China.
Unachopaswa kujua likija swala la mapigano kama vile Kung fu , unachoona mtaani au kwenye filamu mara nyingi ni kwa ajili ya maoneysho tu lakini likija yale mapigano halisi , mbinu zake ni ngumu sana kuona zikitumika mfano wake ni kama mbinu ya hio ya vidole vya Tai, ni mbinu ambayo anaejifunza anafundishwa kuua siku zote na mara nyingi unamlenga mtu katika maeneo dhaifu ya mwili.
Licha ya Mzee Konki kuonekana mzee lakini spidi yake haikuwa ndogo na nguvu ya vidole pia haikuwa haba mpaka kufanikiwa kumsabishia Yonesi maumivu makali.
Mzee Konki hakuacha kushambulia , alizidi kumsogelea Yonesi huku akiwa na macho ya uchu, kama sio uwezo wake wa kukwepa pengine vidole vingeweza kumtoboa eneo la kifuani.
Regina ambae alikuwa akiangalia mpambano huo aliishia kukunja sura , hakuamini James ameenda mbali mpaka kukodi mtu wa aina hio.
“Mzee Konki usiwe sana siriasi , nataka umshikishe tu adabu nisije onekana mtu mbaya mbele ya mchumba wangu”Aliongea James.
“Msichana nimependa sana hio miba hapo kifuani kwako , kubali tuondoke pamoja kuliko kuendelea kuwa mlinzi”Aliongea Mzee Konki.
“Kwenye ndoto zako”Aliongea Yoinesi na kuzunguka na teke akimlenga kumpiga Konki kwenye shingo lakini mguu wake ulishikwa.
“Haipendezi kwa mrembo kama wewe , ila ngoja tu nikuvunje mguu mmoja , tuone kama utaendelea kuleta ukinzani hehe..”
Aliongea Master Konki huku akicheka na palepale aliweka vidole vyake katika mkao wa kucha za Tai ili kumponda nazo Yonesi kwenye mguu.
Dakika ambayo Yonesi anawaza anakwenda kuvunjwa mguu wake na kuishia kufumba macho alikuja kugundua hakuna kilichomtokea.
“Hamza?!”
Yonesi alimkodolea macho Hamza , bila hata ya kujua Hamza alikuwa ashatokea pembeni yake na kushika mkono wa Mzee Konki.
Mzee Konki alikunja sura na kujaribu kusogeza mkono wake lakini aligundua hakuweza hata kujitoa na aliishia kuachia mguu wa Yonesi na mkono mwingine aligeuza kuwa vidole vya Tai na kujaribu kumshambulia Hamza kwenye macho.
Lakini ile mkono unamkaribia Hamza na yeye alikuwa ashatengeneza staili ileile ya vidole vya Tai na Mzee Konki mara baada ya kwenda kugusana na vya Hamza alijikuta akitamani kutoa ukulele kwa maumivu yaliozidi mpaka vidole vikashikwa na ganzi, kidogo tu vidole vyake vivunjike.
Hamza mara baada ya pale alimsukuma nyuma yule mzee na kumfanya ajikokote asidondoke.
“Wewe Mzee , Kapteni Yonesi ni kama mjukuu wako lakini huoni aibu unataka kumvunja mguu”Aliongea
Mzee Konki alibakia katika mshituko wa ajabu huku akimwangalia Hamza , hata kwa Regina na Yonesi walikuwa wamepatwa na mshituko , James muonekano wake ulikuwa ni ule wa kukakamaa.
“Unaijua sanaa ya ndole za Tai pia!!?”Aliuliza Mzee Konki huku akiwa na mshituko kwani Hamza alitumia mbinu yake.
“Kwani hii mbinu ina ugumu gani kutumia?”
“Unaongea ujinga , hii ni mbinu ya sanaa ya kucha za Tai , ngoja nikuonjeshe utamu wake”
Mzee Konki aliona ni kama udhalilishaji hivyo kwa hasira aliruka hewani kama mshale huku akitanguliza mkono wake wenye staili ya kucha za Tai kumlenga Hamza katika shingo yake.
Hamza alivyosimama kizembe ni kama vile amekosa cha kufanya na anasubiria shambulio hilo , lakini ile Mzee huyo anamkaribia na yeye alinyoosha mkono wake katika staili ya kucha za Tai na kumzuia kwa kubananisha vidole vyake na vya yule Mzee.
Baada ya kuvibananisha katika vidole vyake alizungusha kwa nguvu na kwa hasira kali.
“Arghhhhhhhhh..”
Mzee Konki alitoa ukulele wa aina yake , mifupa ya vidole vyake ilisikika ikitoa mlio wa kuvunjika kutokana na nguvu aliotumia Hamza na mara baada ya kutua chini aliangalia mkono wake akiwa katika maumivu makali huku akimwangalia Hamza katika mshangao.
“Wewe mtoto .. umejifunzia wapi hii mbinu!!?”
Mzee Konki alikuwa akiamini kwenye taifa la Tanzania hakuna mtu ambae anaweza kumshinda likija swala la mapigano bila ya siraha , hasa katika kutumia mbinu yake hio ya Kucha za Tai.
Alikuwa amefika bongo na mpango wake ni kwenda kushindana na wanajeshi wote ambao wanajita makomandoo , alikuwa akitaka kujihakikishia yupo mwenyewe mwenye mafunzo makali ya kimapigano, lakini kwa bahati mbaya anakutana na Hamza kabla hata ndoto yake haijatimia na anashikishwa adabu , kitu cha kumshangaza zaidi aliemshikisha adabu alikuwa ni kijana mdogo sana kuliko yeye ambae amejifunza kwa miaka mingi kuimaster hio mbinu.
Regina ,Yonesi na wengine pia walikuwa wanamwangalia Hamza kwa maswali , walishaona Yonesi hakuwa na uwezo wa kumzidi huyo mzee licha ya kupitia kitengo cha special forces jeshini.
James mara baada ya kuona tukio lile aliishia kupiga hatua moja kurudi nyuma , alikumbuka baba yake alichomwambia kuna uwezekano huyo Hamza asiwe mwepesi na sasa ndio anaamini.
“Mtu alienifundisha ni maarufu sana dunia nzima , anajulikana kila kona ya dunia kutumia hii mbinu, nikikuambia jina lake unaweza kupatwa na mshituko”Aliongea Hamza.
SEHEMU YA 29.
“Acha makusudi ya kujikweza , sheria namba moja katika ulimwengu wa mapigano ni kujitambulisha wewe na shirka lako , mimi ni mwanafunzi kutoka Shirka ya Tai Mweusi, jitambulishe Shirka lako na wewe kama ujasiri huo unao , udhalilishaji wa leo utalipwa mara mia zaidi”
“Nimefundishwa na Master Kato Hawk ushawahi kumsikia?”Aliuliza Hamza
“Kato Hawk , mbona sijawahi kumsikia ni raia wa wapi?”Aliuliza Mzee Konki akionyesha kutomjua.
James mara baada ya kuona Mzee Konki anaanza kuuliza maswali ya kipuuzi alitamani kwenda na kumpiga , ila uwezo huo hakuwa nao.
James alikuwa akimjua Kato Hawk, mtu yote mpenda filamu za angemfahamu Kato Hawk.
“Ushawahi kumsikia mtu anaeitwa Kato Hawk huko jeshini?.”Aliuliza Regina ki udadisi swali hilo likienda kwa Yonesi.
Yonesi na wenzake walikuwa wakimjua ndio lakini hawakutaka kumwelezea Regina na walishangaa kwanini hamjui.
“Taja jina la Shirka ulilojifunzia, sijawahi kusikia jina la mtu uliemtaja?”
“Kama hujawahi kumsikia mtu maarufu kama huyo , basi sioni haja ya kukuambia nenda kaulize”Aliongea Hamza akiwa na muonekano wa kejeli.
Mzee Konki alikuwa na hasira mno , kama sio kuumia mkono wake angejaribu kuzipiga tena na Hamza , alijua kuvunjika kwa vidole vyake hawezi kupona ndani ya siku kadhaa.
“James , turudi kwa leo ila naahidi , nisipokuja kulipiza hili labda sio mimi Konki Master”Aliongea Konki kwa hasira , hakuamini miaka yake yote ya kujifunza mapigano na kutia mguu Tanzania anakuja kukutana na udhalilishaji.
James mara baada ya kusikia hivyo alifurahi , alijua lazima mzee huyo atakuja tu kulipiza kisasi.
James ashaona kabisa Hamza sio saizi yake hivyo aliondoka kimya kimya
Regina alimwangalia Hamza kwa macho ya kiulizo na alijiambia ndio maana aliweza kumuokoa kiwepesi tu, hali hio ilimfanya kukosa hiari ya moyo wake na kujisikia hali isioelezeka.
Wakati wa kurudi nyumbani kulikuwa na foleni kubwa mno hivyo gari ilisogea taratibu taratibu.
“Kwahio Master wako ndio anafahamika kwa jina la Kato Hawk , umefahamiana nae nje ya nchi nini?”Aliuliza Regina.
Swali lile lilimfanya Roma kushituka na kidogo tu akanyage kwenye pedeli tofauti na breki kugonga magari ya mbele yake.
“Regina inamaana hujawahi kusikia hilo jina?”
“Ningekuuliza kama najua , hata Yonesi nimemuuliza ameonekana hajui”
Hamza alijifikiria na kujiambia inakuwaje hawamjui , lakini hata hivyo aliona kwa mwanamke kama Regina ni haki kutokumjua.
“Nilikuwa nikiongea ujinga tu pale , usichukulie siriasi”Aliongea Hamza.
“Kwanini unakuwa hivyo ,unaona aibu kuwa na Master eh?”
“Haha.. nimeongea kumugopesha tu yule usichukulie siriasi”
“Usiponiambia nitatafuta mtandaoni na lazima nitajua tu”Baada ya kuongea hivyo alichukua simu yake na kuingia kwenye mtandao wa google na kuandika jina la Kato Hawk.
Hamza aliishia kutingisha kichwa tu na kujiuliza kwanini huyu mwanamke ana shauku ya kujua siri zake namna hio.
Ndani ya nusu dakika tu , Regina mashavu yake yalikuwa mekundu na aliishia kung’ata lips zake na kuweka simu chini bila kuongea chochote.
Hamza mara baada ya kuona muonekano wa Regina alijua tayari ashaujua ukweli kuhusu Katona alitamani kucheka kicheko kikubwa.
“Hehe, nilikuambia mimi usitafute haya ona sasa?”Aliongea Hamza huku akicheka.
“Muhuni sana wewe..”Aliongea Regina akiwa na hasira , hakuaminni alikuwa ameuliza swali hilo kwa Yonesi na wenzake , alijihisi kuona aibu
“Nilishakuambia nilikuwa nikiongea ujinga, halafu kingine Kato Hawk hawezi kuwa na vigezo vya kuwa master wangu , uwezo wangu wa mapigano kwa kutumia vidole ni wa juu mno”
“Kimya , endesha gari” Regina hakutaka kumsikiliza tena , alitamani kumsogelea na kumpiga kibao.
“Basi ngoja nikuambie ukweli , kama usiponiamini unaweza kujaribu kutafuta tena”
“Ukiongea ujinga tena nitakata mshahara wako”
“Sawa Madam , kama hutaki kusikia basi nitakaa kimya”Aliongea Hamza huku akitamani kucheka.
****
Upande mwingine wa jiji kulikuwa na kikao kilichojumuisha kundi la watu wenye mafunzo ya kimapigano lifahamikalo kwa jina la Tanzania Martial Art Association.
Kundi hili halikuwa la kihalifu lakini kwa namna moja lilitafsirika kama la kihalifu kutokana na usiri mkubwa wa ajenda zao , unaweza kusikia kuna kundi hili lakini huwezi kujua ni kitu gani wanachokifanhya wakikutana.
Kuna wanaosema kundi hilo hufadhiliwa na Binamu , hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa madai hayo., lakini taarifa ya kuaminika hata baadhi ya wanajeshi wenye vyeo vya ukomandoo jeshini walikuwa ni wanachama na hawakujiunga kwasababu walitaka bali walipambanishwa na wenzao na kukidhi vigezo na kuingia katika umoja huo na kulikuwa na faida kubwa sana ya kimaslahi kwa kila mwanachama wa kundi hilo.
Sasa katika moja ya jumba la kifahari lililopo Tegeta kulikuwa na kundi la watu ambao walikuwa wamevalia mavazi ya suti na walikuwa wamekaa eneo la sebule yenye masofa mengi ya thamani ya juu.
Kwa muonekano wao ilionyesha kabisa hawakuwa watu wadogo katika jamii , mmoja ambae alikuwa katikati ndio kiongozi alifahamika kwa jina la Fanueli Yowe au unaweza muita Kanali Yowe.
Ndio alikuwa ni Komandoo wa jeshi la taifa lakini pia mwanachama wa umoja huo wa sanaa ya mapigano.
Ukiziangalia sura zote zilizokuwa ndani ya eneo hilo usingeamini kama walikuwa na uwezo wa kupigana wa hali ya juu na baadhi yao ni makomandoo wa jeshi.
“Nadhani kila mmoja wenu amesikia , mwanachama wetu mpya Mzee Konki amekutana na mtaalamu wa hali ya juu wakati alipokodiwa na Mzee Benjamini wa kampuni ya Zena?”
“Hii maana yake ni kwamba mpaka sasa hakuna mmoja wetu hapa anaemuweza mtu huyu , maana tunajua fika Mzee Konki ndio mwanachama wetu mpya ambae ametushinda wote kimapigano, hii ni taswira mbaya kwa umoja wetu na maslahi yetu kwa ujumla katika nchi hii, kwa kusema hayo nimeitisha kikao hiki ili kuwauliza mnaonaje hili swala?”
“Kwa mtazamo wangu lazima mtu huyo atakuwa si wa hapa Tanzania na hata kama ni wa Tanzania basi amerudi hivi karibuni na pengine ameajiriwa kulinda kampuni ya Dosam”
“Mimi pia nadhani huyu ndio mtu alieripotiwa kwetu na Amosi , unajua Amosi licha ya kutokuwa na uwezo wa hali ya juu lakini ana macho ya kuona mtu ambae ana uwezo mkubwa , nasikia baada ya hapo Amosi alipokea vitisho kutoka kundi la Chatu aache kabisa kumchokoza yule mwanamke mfadhili wetu anaemtaka”
“Unamaanisha Dina ndio aliingilia , nadhani kadri siku zinavyoenda ndio anasababisha matatizo zaidi”Aliongea mwanaume mwingine aliefahamika kwa jina la Gosu au Mzee Gosu ni mstaafu kutoka polisi.
“Kwanini mnampa bichwa yule msichana ,tunajua wote hapa hatumuwezi lakini hatuwezi kumsujudia pia”
“Mimi nadhani tuachane na swala la Dina , na Mzee Konki mwenyewe atuelezee ni kwa namna gani tutarudisha heshima yetu , wenzetu kutoka nje ya nchi wakisikia kuhusu hili watadharau na hawatukubali kufanya biashara na sisi”
“Nadhani kwanza tumfahamu ki undani ni nani , alitaja Master jina la Master aliemfundisha lakini sikuweza kumfahamu , nadhani kati yetu hapa kwenye huu umoja lazima atakuwa amesikia jina hilo , amesema anaitwa Kato Hawk na ni maarufu sana”
“Eeh!!
“Watu wote walikaa kimya na kufanya hali itulie na kitendo kile kilimfanya Mzee Konki kushangaa.
“Mbona kila mtu amekaa kimya?, au inamaana mnamjua tayari?”
“Mzee Konki nadhani ni kweli umechoka mno , unaonaje ukiingia chumbani kupumzika kwanza”
“Mkuu kwanini nipumzike , hiki kikao si kinanihusu mimi na yule mpuuzi?”
“Mzee Konki acha kututania , yaani unatuambia mcheza filamu za ngono anaejitamba mtandaoni kuwa ni Bruce lee ndio mtaalamu wa mbinu ya kucha za tai.”
“Nini !!, Mcheza filamu za ngono , mnamaanisha nini?”
“Mzee Konki hatukulaumu , wewe ndio mzee hapa hivyo hutumii sana mtandao wa internet hivyo ni rahisi kutomfahamu Kato Hawk, huyo mtoto inaonekana alikudanganya makusudi , haina haja ya kuwa siriasi hivyo”Aliongea Mzee Fanueli Yowe.
Mzee Konki mara baada ya kuagalia sura ya kila mmoja alijikuta akishindwa kuzuia kicheko na muda huo huo watu wote walimuunga mkono na kuanza kucheka na ghafla tu akaacha na wote wakaacha.
“Mpuuzi sana yule mtoto , nitamchuna ngozi”Aliongea kwa hasira , hakuamini haikuwa swala la kupigwa tu lakini vilevile ametajiwa mcheza filamu za utupu kama Master.
Kato Hawk kabla ya kuwa muigizaji wa filamu za kimapigano alifahamika kama Gerald Lupe alikuwa ni mcheza filamu za ngono maarufu sana , kitendo cha kubadilika kutoka ugiizaji wa filamu hizo na kuingia katika sanaa ya mapigano huku akijifananisha na Bruce lee ndio alijibatiza jina la Kato, uhusika wa Bruce lee katika filamu ya Green Hornet(1966) ,hakuna mtu ambae alikuwa akiamini kama Gerarld Lupe au Kato alikuwa akijua mapigano , kilichomfanya kuwa maarufu sana hadi Tanzania ni wakati alipofika nchini katika uigizaji wa filamu huko Ngorongoro na kupewa mapokezi makubwa kwa kigezo cha kutangaza utalii, kilichomfanya pia kuwa maarufu dunia nzima ni namna ambavyo alikuwa akijibrand kwa kutengeneza vidio fupi fupi katika mtandao wa Tiktok na Reel Instagram akionyesha staili mbalimbali za mapigano kama Bruce Lee lakini ikaja kujulikana anafanya Editing huku kile watu walichokuwa wakiona sio uhalisia.
Skendo hio ya kufanya editing ilimfanya kuzomewa na watu wengi mtandaoni huku wakimuonya asitumie utambulisho wa kusema yeye ni Bruce lee aliezaliwa(Recarnated) katika mwili wa Gerald Lupe kwani ni kuchafua hadhi ya kumbukumbu za kishujaa za Bruce lee.
Hivyo ukiingia mtandaoni ukiandika jina la Kato Hawk ni Gerald Lupe mcheza filamu za ngono maarufu anaedai ni Bruce lee aliezaliwa katika mwili wa Gerald Lupe.
“Mzee Konki haina haja ya kuwa na hasira , tunachopaswa kuamini kwasasa ni kwamba huyu mtoto sio wa kawaida , kama ni hivyo unadhani kwanini hajatoa jina la Shirka analotokea.
“Kesho mapema narudi Thailland kwenye Shirka langu , nipo tayari kualika hata wataalamu wa hali ya juu wa kimapigano kwa ajili ya kumshikisha yule mtoto adabu”Aliongea kwa hasira.
Kauli ile iliwafnaya wote waliokuwa hapo ndani kufurahi , walijua fika Mzee Konki kama ninja wa daraja la juu lazima atakuwa anafahamiana na maninja wengine wa uwezo wa juu.
“Mzee Konki tutasubiria kurudi kwako kama ndio hivyo , ruhusa unayo kutoka kwetu”Aliongea Mzee Yowe.
******
Siku iliofuata ilikuwa ni jumamosi , Kwasababu ilikuwa wikiend haikuwa lazima kwenda kazini mapema , hivyo Hamza alitoka nje kwenye uwanja wa bustani ya nyumba na kuanza kuchukua mazoezi.
Mazoezi yake Hamza hayakuwa ya kawaida hata kidogo , hayakuwa ya kukimbia wala ya kuruka ruka.
Ilikuwa ni kama vile anakata mauno kwa jinsi alivyokuwa akifanya , lakini utofauti ulikuwa kwenye viungio vya miguu yake vilikuwa vikipinda katika mjongeo wa aina yake.
Kwa lugha nyepesi ni kama vile anajaribu kucheza cheza tu kupoteza muda , hakukuwa na kitu cha kushangaza sana kwa kile anachokifanya na mtu asiejua anachokifanya angeishia kucheka , kilichokosekana ni mziki wa saida Karoli wa Maria Salome tu.
Lakini Hamza alikuwa siriasi mno , alikuwa tena amefumba macho kabisa huku akiendelea kukata mauno.
“Wewe, wewe umekuwa chizi , kwanini unakata mauno asubuhi asubuhi yote hii ?”Ilikuwa ni sauti tamu ya Regina na ilimfanya Hamza afumbue macho yake.
Regina alikuwa amevalia tisheti ya rangi ya pink iliomfanya chuchu zake kuchomoza kama miiba , kikaptura cha rangi nyeupe na raba aina ya Converse , alionekana kama vile ni mwanafunzi wa chuo anaejiaandaa kwenda Jogging.
“Mbona unanikodolea na macho yako?”Aliuliza Regina huku akiona aibu za kike.
“Regina kumbe na wewe una ratiba za kuchukua mazoezi”
“Wiki nzima kazini , siku mbili za mazoezi , unadhani ukiwa na shida ya mwili unaweza kufanya vizuri kazini , halafu acha kubadilisha topiki , kwanini unacheza kibwebwe asubuhi asubuhi?”
“Kibwebwe ndio nini , hii sio mchezo ni mbinu yangu ya mazoezi , ina nguvu ya ajabu mno”
“Mh ,mbingu gani hio ya mazoezi ya kukata viuno , jina lake inaitwaje?”
“Jina lake .. dah hata sijawahi kulifkiria.. kwa mtu wa kawaida anaweza kuona nacheza au kufanya maigizo lakini usichokijua ni kwamba nisingeweza kuwa na uwezo niliokuwa nao leo hii kama sio hii mbinu”
“Unajaribu kumdanganya nani , mimi nadhani ni kwasababu tayari wewe ni kichaa hivyo hata sikulaumu ukikata viuno asubuhi asubuhi”Aliongea Regina na alijua kabisa Hamza anaendelea na mchezo wake wa kumdanganya.
“Unadhani nadanganya , ijapokuwa kuna maelezo mengi ambayo naweza kukuelezea mpaka uelewe ila hii ni mbinu inayokuwezesha kuwa na muunganiko wa kimapigano”
“Acha uongo wako , kama ukiona kichaa kishaamka tafuta sehemu ya mbali ucheze midundiko yako , usije kumuua Shangazi kwa presha”Aliongea Regina na hakutaka kuongea nae zaidi bali alitoka nje ya geti na kuanza kukimbia katika barabara ya ufukwe wa bahari kuchukua mazoezi.
Mara baada ya Regina kutoka Hamza hakujali kejeli za Regina kabisa aliendelea kucheza kama vile ni mchawi , alikuwa akicheza anapanda juu anaenda mpaka chini halafu anarudi tena na kutingisha kiuno , kwa namna alivyokuwa akifanya ungeishia kucheka tu na kujisemea bangi ya asubuhi asubuhi sio nzuri.
Baada ya lisa kupita hatimae Regina alirudi akiwa anakimbia na kwa kuangalia mwili wake tu alijua Regina hakuwa mzembe kabisa na ilimshangaza na kujiuliza kwanini hakuona hilo mapema, au ni kwasababu ya urembo wake ndio maana hakumchunguza, Hamza aliishia kuguna tu na kujiuliza Regina ana siri gani na kuwa na mwili wa kijeshi.
Hamza mara baada ya mazoezi aliamua kuingia ndani na kujisafisha na kisha alikaa mezani kwa ajili ya Breakfast ambayo ilikuwa imeandaliwa na shangazi.
Regina na yeye alikuwa ndio wa mwisho kukaa mezani , kama kawaida ya tabia ya wanawake kujiremba ndio maana alichukua muda mrefu na mara baada ya kukaa mezani alikula kidogo tu tena nusu kikombe cha maziwa.
Wakati Hamza akiwa bize aliweza kuona simu ya Regina inaita kupitia kio chake , ilikuwa ni ya Linda sekretari wa Regina.
“Linda Mr Frei amefika tayari?”Aliuliza Regina mara baada ya kupokea.
“Ndio Mkurugenzi , Mr Ferney ndege yake imekwisha kutua, anajiandaa kuelekea Hotelini , nasikiliza maelekezo yako?”
“Haina haja ya kumsumbua kwasasa , atakuwa amechoka sana , tukiongea nae sasa hivi anaweza asitoe ushirikiano mzuri,tuma barua pepe kwa msaidizi wake na muulize ni saa ngapi tunaweza kukutana”
“Sawa madam”
Mara baada ya kukata simu Regina alimgeukia Hamza aliekuwa bize kumalizia vitafunwa vyote.
“Nimekuandalia nguo kadhaa na zimewekwa kabatini chumbani kwako , kazivae kama zilivyo muda si mrefu tunaondoka”Aliongea Regina.
ITAENDEEA