STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA SITINI NA MBILI
SONGA NAYO................
Zilisikika hatua za watu zikiwa zinakuja kwa mbali, aligeuka kuangalia hatua hizo lakini hakuziona, alihisi kama anaota mpaka pale alipogeuka tena alitaka kukimbia. Aliwaona watu watatu wakiwa mbele yake, hakuelewa watu hao walifikaje kwani hakuzisikia kabisa hatua zao wakiwa wanakaribia hilo eneo, ule mshtuko ulimfanya adondokee nyuma hatua kadhaa akiwa anahema kwa nuvu na jasho likimtoka mfululizo mwilini.
Mshtuko haukuwa tu kwa sababu ya kuwaona watu mbele yake ila ni mtu ambaye alimuona, bado alihisi hakuwa hai, huenda alikuwa amefika kuzimu ila sio kweli! Alikuwa na uhakika kabisa kwamba alikuwa hai, sasa jambo hilo liliwezekana vipi? Ni mtu alikuwa anaichezea akili yake? Akakumbuka kwamba yeye ni raisi mtu hawezi kucheza na hiyo akili yake kirahisi namna hiyo hivyo kwa namna yoyote ile kile ambacho alikuwa anakiona mbele yake haikuwa ndoto bali ulikuwa ni uhalisia.
Natron Vinza ndiye mtu aliye muona mbele yake, huyu alikuwa ni raisi wa Tanzania miaka ya zamani sana, huyu ndiye ambaye alipigishwa magoti na Lucas muuzaji wa madawa ya kulevya ili aweze kukubali kulisaidia taifa, huyu ndiye yule ambaye alipewa amri ya kujiuzulu ili taifa lisaidiwe na akafanya hivyo. Huyu ndiye yule bwana ambaye alidhalilishwa mno na muuza madawa ya kulevya yule baada ya kuhitaji robo ya utajiri wa bwana yule.
Ni miaka mingi iliyopita kila mtu alijua kwamba bwana huyo alikufa lakini haikuwa kweli, bwana huyo kakufa kama ambavyo dunia na Watanzania waliamini. Mtu ambaye alikuwa na njaa ya mafanikio kama yeye asingeweza kuyaondoa maisha yake kijinga eti kwa sababu tu ya kumhofia muuza madawa ya kulevya, hakuwa amefikia hatua ya ujinga wa kipuuzi namna hiyo ila yeye ndiye ambaye aliuhadaa ulimwengu ukaamini kupitia mtego wake aliokuwa ameuweka.
Aliiaminisha dunia kwamba amekufa na kweli dunia ikaamini hivyo, aliufanya ulimwengu uamini kwamba historia yake ilikuwa imezikwa kwa miaka mingi sana ila haikuwa kweli, bwana huyo alikuwa mzima tena yu buheri wa afya kabisa kuliko hata alivyokuwa miaka ya huko nyuma. Mwili wake haukuonekana umekaa kihasara kama alivyokuwa anashinda kula bata kipindi yupo Ikulu, mwili wake ulikuwa umekomaa mno, mwili ambao ulionekana kuwa na nguvu zisizo za kawaida akiwa ndani ya kanzu safi nyeupe ambayo ilimkaa vizuri.
Sasa bwana huyo alikuwa ni nani hasa kwenye hiyo dunia mpaka raisi wa nchi ajikute anaingia kwenye mikono yake na kuuhitaji msaada wake kwa ukubwa namna hiyo? Pembeni yake alikuwa amezungukwa na maninja wawili ambao walikuwa makini kwenye kila hatua yake ambayo alikuwa anaipiga. Alikuwa analindwa mno bwana huyo.
Huyo ndiye alikuwa mwanzilishi na kiongozi mkuu wa hilo kundi la THE IMMORTALS, huyo ndiye alikuwa msingi wa hilo kundi na ndiye ambaye alikuwa na kauli ya mwisho juu ya kila kitu. Mtu huyo alikuwa anaishi nyuma ya pazia kiasi kwamba watu wake hawakuwahi kujua wanamtumikia nani lakini raisi siku hiyo aliipata hiyo bahati.
Alikuwa ana wasiwasi isivyokuwa kawaida, alikuwa mtu wa mashaka mno akiwa bado anahisi yupo ndotoni. Kiongozi wa zamani ambaye binafsi alihisi alishakufa mpaka watu walishamsahau alikuwa hai bado. Kwanini yeye? Aliogopa sana.
“Mheshimiwa?”
“Naona umeshtuka sana kuniona nipo hai George” alimeza mate akiwa anaogopa hata kujibu baada ya kuisikia ile sauti ya kukwaruza isiyokuwa na utani ndani yake.
“Mheshimiwa ulikufa na nilihudhuria mazishi yako, sasa inakuwaje upo huku na upo mzima wa afya kabisa?”
“Una uhakika mimi nilikufa?”
“Ndiyo, niliona na mwili wako”
“Wewe ni raisi George, unaamini kuna jambo haliwezekani hapa duniani?”
“Hapana kiongozi”
“Nyanyuka ukae kwenye kiti kwa sababu mimi na wewe leo tunaenda kuwa na mazungumzo marefu kidogo”
“Asante kiongozi” alinyanyuka na kwenda kukaa kwenye kiti cha dhahabu ambacho hakikuwa mbali na pale ambapo alikuwa amedondokea.
“Mimi sikufa wala sijawahi kufa George”
“Sasa aliyekufa alikuwa nani?”
“Alikuwa kijana wangu ambaye alikubali kuifanya kazi ile ili familia yake iishi maisha mazuri”
“Ambayo uliwapa?”
“Huwa siishi nje ya ahadi yangu, yeye alikufa lakini familia yake imeishi maisha mazuri mpaka leo”
“Naheshimu hilo lakini sikutegemea kama ni wewe ndiye ambaye ningekukuta hapa”
“Ulitegemea kukutana na nani?”
“Sijajua lakini haukuwa akilini kabisa”
“Unakumbuka zamani nikiwa raisi?”
“Ndiyo kiongozi”
“Ni jambo gani ambalo lilikuwa linaongelewa sana mtaani kuhusu mimi?”
“Kwamba ulipenda sana starehe”
“Kitu ambacho ni sahihi hata wewe uliamini kwamba ni kweli si ndiyo?”
“Ndiyo kiongozi”
“Lakini unajua kwanini kuna baadhi ya watu wanapenda starehe?”
“Hapana kiongozi”
“Kuna vitu vingi vinafanya baadhi ya watu wanafanya hayo mambo lakini kuna mambo makuu ambayo ndiyo hupelekea yote hayo. Jambo la kwanza ni kupata vikubwa ambavyo nafsi yako inaamini kwamba haukustahili, huwa inambadilisha mtu moja kwa moja na kumfanya kuwa wa hovyo huku yeye akiona kwamba ni fahari kufanya hayo. Jambo la pili ni kukosa mambo ya mhimu ya kufanya, mimi nilikuwa nagawa majukumu tu kwa watu wengine ila sikuwahi kuhitaji niyatimize mwenyewe, kugawa majukumu yote kwa watu wengine wa chini yangu kulinifanya muda mwingi nisiwe na la kufanya
Siku zote ukiwa hauna la kufanya hata akili haiwezi kutulia na kupambana na mambo ya maana, hapo ndipo akili huwa inaanza kuwaza mambo mazuri kama wanawake warembo, kufika sehemu nzuri za gharama na za kupendeza duniani, unajikuta haujali tena kama wewe ni raisi wa kuwaongoza raia wako. Hilo ndilo ambalo mimi nililifanya na nina uhakika hata wewe unafanya hivyo, sijawahi kukuingilia kwa sababu najua unakilinda ambacho kilikufanya uwe hapo
Lakini bwana George hayo yote huwa yanabadilika pale tu ambapo unakuwa na sababu ya msingi ya kukufanya uwe na jambo la kuwaza. Mimi niliachana na hayo mambo baada ya kufanya maamuzi magumu ya kufa kwa watu, yaani dunia ilitakiwa kuamini kwamba mimi sijawahi kuishi tena baada ya maisha yake, lakini unaijua sababu ya msingi?
Sababu ilikuwa ni watu, mimi kama raisi nilidhalilishwa mno, kama raisi nilionekana toi la kuchezea na baada ya siku ile hakuna mtu ambaye angeniheshimu tena, wote wangekuwa wananicheka kila ninapopita ndiyo maana niliamua kupotea kabisa kwenye nyuso za watu ili nije kuishi sehemu ambayo sitakuwa na mtu wa kumuogopa
Hata vijana siku hizi wanashindwa kupata mafanikio kwa sababu ya kushindwa kuielewa hii formula. Ukitaka kufanya mambo makubwa kwa amani bila presha, nenda eneo ambalo wale watu wanao yajua madhaifu yako hawawezi kukuona. Hautakuwa na mtu wa kumuogopa tena, utayafanya mambo yako kwa amani na uhakika kwa sababu huna jambo la kupoteza ila kuendelea kupambana sehemu ambayo watu wanayajua zaidi madhaifu yako?
Hiyo inakuwa ni hatari kwako kwa sababu asilimia kubwa utafeli tu na asilimia za kufaulu ni ndogo mno George
Mimi niliamua kuja kuishi huku kwa sababu ya yule mtu ambaye ndiye aliifanya heshima yangu kupotea kabisa. Niliishi na kisasi kizito kwenye moyo wangu kwa miaka mingi nikiamini kwamba ingefika siku ningekuja kulipa, nadhani unayakumbuka maisha ya zama zile George”
62 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.