STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA SITINI NA NANE
SONGA NAYO................
Masaa hayasimami, muda unazidi kujongea, kesho yake ilifika Ezra hakuwa na utani kabisa juu ya hiyo ari yake mpya ya kuhitaji kufanikisha alichokuwa anakihitaji. Aliwahi mapema kwenye jumba la sinema ambalo alikuwa ameelekezwa, lengo lake alihitaji kuonana na mzee huyo ambaye alikuwa anaitwa Miraji. Watu walikuwa ni wengi ndani ya eneo hilo lakini haikumpa shida kumtambua mtu wake kwa sababu alitakiwa kusubiri mpaka watu wote waishe ndipo angeweza kuonana naye moja kwa moja.
Muda ulivyozidi kwenda ndivyo watu walianza kupungua hususani baada ya ile tamthiliya ambayo iliwapeleka pale kuisha. Baada ya watu kutawanyika alibakia mzee mmoja ambaye alikaa katikati kabisa ya ukumbi. Taa zote zilizimwa ikabaki moja tu ambayo ilikuwa imefifia lakini kutokana na kiza kikali ambacho kilikuwepo, taa hiyo ilisaidia kuweza kuangaza na kufanya amuone alipokuwa. Ethan alijua kabisa yule ndiye alikuwa mtu wake haswa ambaye alikuwa akimhitaji, alitembea taratibu mpaka mstari wa nyuma kutoka pale alipokuwepo mzee yule.
“Bila shaka unapata kumbukumbu bora ambazo mwisho wake haukuwahi kuwa mwema mzee wangu” ilisikika sauti nyuma yake ambayo ilimfanya mzee huyo kugeuza shingo yake kutazama nyuma kumwangalia mtu ambaye alikuwa anamwongelesha kwa sababu hakumsikia wakati anafika eneo hilo.
“Ni muda gani tangu umekaa hapo nyuma yangu?”
“Nina sekunde kadhaa tu”
“Bila shaka umekuja kwa ajili yangu hapa?”
“Ndiyo mzee”
“Tunafahamiana kabla?”
“Hapana”
“Sasa nakusaidiaje kijana?”
“Kwanza pole kwa kukukatisha kwenye kumbukumbu za kumkumbuka kijana wako ila nimefanya jitihada kubwa mno mpaka kufanikiwa kufika hapa ili kuweza kuonana na wewe, nina imani utanisikiliza kwa hili”
“Bado haujaongea shida yako”
“Ninahitaji taarifa za bwana mmoja ambaye alipata kuitwa Dato Pazu” jina halikuwa geni kwa mzee huyo ila mtu ambaye alilitamka ndiye alikuwa mgeni, alilazimika kusimama na kugeuka ili amwangalie kijana huyo vizuri usoni, alimwangalia kwa dakika nzima akiwa anausoma uso wake kisha akarudi tena kuketi chini.
“Wewe ni nani?”
“Ukweli ni kwamba mimi ni ofisa wa polisi ambaye napeleleza kesi ya kifo cha waziri wa mambo ya ndani kwa siri kwa sababu hakuna anayejali kuhusu kazi yangu”
“Kwahiyo unataka kuwadhihirishia kwamba una uwezo?”
“Hapana nafanya kwa sababu nahisi kabisa ni jukumu langu kufanya hii kazi”
“Simjui huyo mtu kijana hivyo hakuna msaada ambao naweza kukupatia” mzee huyo hakuonekana kuvutiwa na hiyo maada, aliongea huku akinyanyuka na kuanza kuondoka hilo eneo.
“Fikiria kama angekuwa mwanao, bado ungemjibu hivyo? Najua umempoteza mwanao wa pekee na eneo hili huwa unalitumia kwa ajili ya kumbukumbu bora ambazo alikuachia akiwa hai, msaidie kijana mwenzie basi kukamilisha kumbukumbu yake, nina imani hata huko aliko atajivunia wewe kuwa baba yake” alipewa maneno ya familia ambayo yalimgusa kwa ukubwa, maneno ambayo yalimuingia vilivyo alirudi kukaa tena kwenye kiti.
“Unataka kujua kuhusu nini kwenye hilo jambo?”
“Nataka kuyajua maisha ya Othman chunga, nina uhakika uliiona video ya mauaji ya waziri hivyo lazima unamjua mhusika ambaye namuulizia hapa”
“Una miaka mingapi kijana?”
“Thelathini”
“Wewe bado ni kijana mdogo ambaye bila shaka una ndoto nyingi za kuweza kuzitimiza. Una uhakika unataka kuivaa hii kesi ambayo unaiulizia muda huu?”
“Mpaka nafika kwako basi ujue kabisa kwamba nimefanya maamuzi mzee wangu, natamani hata siku nikifa angalau niwe nimefanya jambo lolote la mhimu kwenye taifa langu”
“Huyo mtoto jina lake anaitwa Kanaan Dato Pazu ila hilo jina ambalo analitumia sasa nadhani alipewa ama ni yeye amejipatia. Baba yake mimi namfahamu sana kwa sababu nimefanya naye kazi kwa muda mrefu kabla ya kustaafu na amewahi kuwa bosi wangu pia hivyo namjua vyema hata huyo mtoto wake japo kuna wakati alikuja kutoweka
Baba yake udadisi ndio ambao ulimponza, udadisi wa kutaka kujua mambo ya wanasiasa. Slyvester Mboneka alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa washenzi ambao walikuwepo kwenye taifa hili, bwana huyo alikuwa akijihusisha na biashara haramu. Kuna kipindi kesi yake ilifika kwenye mikono ya Dato ambaye hakuichekea, licha ya kila mtu kumkanya na kuikataa hiyo kesi yeye alidai kwamba alitaka kuitumia kama mfano ili wanasiasa waweze kupata somo kuhusu kuheshimu sheria za nchi hivyo akaipandisha mahakamani akiwa na ushahidi wa kutosha.
Kesi ile haikuwa na mwisho mwema kwake kwa sababu iliyabeba maisha yake muda mfupi tu baadae na kesi yenyewe ikaishia hewani tu kwahiyo haikuwahi kuendelea tena. Lakini enzi za uhai wake alikuwa na mtoto huyo wa kiume ambaye hakuwa akimuweka hadharani ila ni watu kadhaa ambao tulikuwa tunamjua, hii ni kwa sababu aliamini kwamba kupenda kwake haki kungemfanya kuwa na maadui wengi hivyo angekuja kumletea matatizo mtoto wake ndiyo sababu ya msingi ikamfanya amuondoe kwenye mfumo wa utambulisho wake kabisa. Kijana huyo tangu baba yake afe hakuwahi kabisa kuonekana tena, alipotea jumla mpaka baada ya miaka kadhaa ndipo alikuja kuonekana nyumbani kwangu, alikuwa kabadilika mno na wakati amekuja kwa sababu alijua mimi nilikuwa miongoni mwa watu wa karibu zaidi na baba yake alinipa machache kuhusu maisha yake.
Walikuwa wapo chini ya mtu mmoja ambaye anaitwa Gavin Luca, bwana huyo inadaiwa kwamba aliwakusanya wote ambao waliwahi kuonewa na hao wanasiasa wakubwa kisha akawataka vijana hao walipe hayo madeni yao kama wangetaka yeye angewasaidia, uliwahi kusikia mtu amjue mdeni wake, akapewa nafasi ya kumfanya amlipe halafu akamuacha? Hawezi kufanya hivyo kwahiyo vijana hao walikubali kulifanya jambo hilo lakini huyo mtu ambaye alidaiwa kwamba ndiye aliwakusanya na kuwapa tumaini jipya la maisha ukizingatia karibia wote walikuwa na maisha magumu, anadaiwa kuwa mtu hatari sana na mimi nimekuja kumfahamu vizuri siku kadhaa hizi ambazo zilipita ndipo nikaikumbuka ile simulizi ya yule muuza madawa maarufu hapa Tanzania kwamba huyo bwana aliye wakusanya ndiye bosi wake.
Kwahiyo huyo ndiye ambaye aliwapa mafunzo mwenyewe, ndiye kawatengeneza hawa vijana kwa mkono wake na ndio hawa ambao wanayafanya haya mambo ambayo yamekuleta wewe hapa.
“Amewapa? Kwamba ni wengi?”
“Inaonekana sio mmoja kwa sababu hata yeye wakati ananiambia habari hizi alikuwa anatumia wingi”
“Naweza kumpatia wapi Kanaan mzee wangu”
“Kijana unatarajia kabisa kwamba nimuuze mtoto wa rafiki yangu kirahisi namna hii?”
“Hilo nalitambua lakini mimi nataka nikutane naye nimhoji, wala hili jambo halitafika popote kwa sababu hata mabosi zangu hawajui kama nafanya haya, hii kesi nimepokonywa”
“Nihakikishie kwamba hakuna kibaya kitamkuta Kanaan”
“Siwezi kufanya kibaya kwake mzee, kama kutakuwa na ulazima basi naweza kuwa msaada mkubwa kwake” mzee huyo alimwangalia sana kijana huyo, alimtaka ampe kalamu ya wino na karatasi, aliandika mahali ambapo angeweza kumpata kijana huyo.
“Baada ya hapa sitegemei kutafutana tena, najua kama nisingekupa taarifa hizi ungenitisha kwamba unenda kuniripoti kwa sababu nilishuhudia baadhi ya matukio ya huko nyuma ila baada ya hapa ni matumaini yangu kwamba mimi na wewe hakutakuwa na ulazima wa kuweza kuonana kwa mara nyingine”
“Roger that, sir!” Ezra moyo wake ulikuwa unafurahi, alikuwa anapiga hatua kubwa ya mwendo wake ambao alikuwa ameuanza, hakukuwa na kitu cha kuweza kumzuia kufanya alichokuwa amekusudia wakati huo, kila kitu kilikuwa upande wake, alianza kuuona mwanga taratibu wa kesi yake.
68 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.