Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SABINI NA NNE
SONGA NAYO................

“Mheshimiwa!”
“Unaweza ukanipa sababu ya kwanini ulirudi pale wakati ulijua kabisa mimi na wewe tulitoka pale pale?”
“Kwa sababu nilitaka kuwa na uhakika zaidi juu ya jambo lile, pia nilijua kama mwanamke yule angehisiwa kuwa mhusika wa jambo lile basi huenda kuna watu wangekuwa na sababu kubwa ya kuweza kumvamia hivyo nilihitaji nipate majibu ya uhakika hivyo nilienda pale kwa ajili yako”
“Kwa ajili yangu?”
“Ndiyo”
“Kuna kazi ambazo huwa unazifanya kwa siri kwa ajili yangu mimi?”
“Hapana mheshimiwa, kwa wakati ule nilijua haupo sawa, ulitoka kumpoteza mkeo hivyo kama mkuu wa majeshi niliona kabisa kwamba kuna umuhimu wa kuwajibika kwa ajili ya raisi wangu”

“Okay, uliishia wapi baada hapo?”
“Nilichelewa kufika eneo la tukio kwa sababu ilikuwa imeshatokea tayari”
“Kwahiyo unataka upewe medali kwa hilo?”
“Hapana”
“Ila?”
“Nahitaji umjue muuaji wa mkeo”
“Nakusikiliza”
“Sarah Martin ndiye binti aliye husika kwenye mauaji ya mkeo mheshimiwa”
“Mhhhhh! una ushahidi upi juu ya hili?”
“Kwa sababu eneo la tukio lilikutwa ganda la risasi. Kuna kosa moja ambalo mhusika nadhani alilifanya kwenye kazi yake huenda kwa bahati mbaya ama kwa kuto kujua. Alishika risasi kwa mkono wake hivyo baada ya kupima finger prints na DNA zimekutwa zake moja kwa moja na taarifa za awali ni kwamba ile risasi ilikuwa inatumika kwenye silaha ya mdunguaji wa ngazi za juu na binti yule ni mmoja wao”
“Kumbukumbu zangu zinaniambia kwamba lile ganda lipo kwa mkemia mkuu na hakuna mtu mwingine ambaye nilitoa ruhusa ya kuweza kulipata, inamaanisha ulienda nyuma ya mgongo wangu na kufanya hili?”
“Nisamahe mheshimiwa ila ni sehemu ya jukumu langu”
“Mke wangu ni jukumu lako kwa namna ipi labda?”
“Kwa sababu wadunguaji wote ambao wamewahi kuwa na uwezo mkubwa hili taifa wanatokea jeshini, mimi ndiye mkuu wa majeshi na jambo hili nahesabia kwamba limetokea kwa uzembe wangu wa kushindwa kuwaweka vijana wangu kwenye mstari hivyo nilijiona kuwa mwenye hatia ndiyo maana nikaamua kulifuatilia mwenyewe hili suala”
“Una muda gani tangu ulifahamu hili?”
“Nilikuwa nina hisia tu na uvumi ila sikuwa na uhakika bado leo hii ndipo nimepata uhakika kwa asilimia zote”
“Huyu binti sina kumbukumbu sahihi kama namfahamu ila ni wewe ambaye uliniambia kwamba ndiye pekee ambaye alipona kule Kenya, au sio huyu?”
“Ni yeye mheshimiwa”
“Kwahiyo ni jambo gani linaendelea hapa?”
“Ndiyo maana imekuwa sahihi yeye kuhusika na mauaji haya kwa sababu kuna uhusiano wa haya matukio”
“Kivipi?”
“Huyu binti siku ile alidaiwa kwamba ndiye pekee alikutana na Gavin Luca na kuachwa hai. Swali la msingi ni kwamba kwanini iwe yeye pekee ndiye aweze kuishi kwenye hilo? Maana yake watu hawa huenda walikuwa wanafahamiana kabla ya siku hiyo. Wenzake wote waliuawa isipokuwa yeye, kulikuwa na kitu nyuma ya pazia ambacho alituficha yule binti”
“Enhe! nakusikiliza”
“Kwahiyo baada ya lile kuisha inaonekana kuna makubaliano waliyaingia na baadae ndipo alikuja kuyafanyia kazi”
“Makubaliano yapi hayo?”
“Ya kumuua mkeo”
“Huyu binti kuna sababu gani ambayo imefanya mpaka aweze kumuua mke wangu”
“Inasemekana kwamba hii amri imetoka kwa yule mama Aurelia, na imekuwa rahisi kwa sababu ndiye mama wa Gavin hivyo Sarah hakuwa na namna zaidi ya kukubali kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa”
“Aurelia?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Kuna sababu gani mpaka yule mwanamke akubali kifanya hii kazi? Mimi kumhoji sikuwa na maana kwamba nina uhakika kahusika”
“Kwa habari chache nilizokuwa nazo ni kwamba wawili hawa waliwahi kuwa na ugomvi huko nyuma kwa sababu hawa wamezaliwa sehemu moja. Pole sana kama nitakuwa naongea jambo ambalo halipo kwenye matarajio yako kwa sasa ila nadhani unastahili kujua hili mheshimiwa”
“Nakusikiliza”
“Nmepitia historia yao hawa wawili inaonekana kabisa waliwahi kusoma shule moja, hawakuwahi kuwa vizuri tangu wakiwa wanasoma na baadae mkeo akaja kukutana na wewe wakati huo Aurelia aliingia jeshini ambako alifanikiwa mpaka kuwa kanali wa jeshi, ilikuwa ni moja ya hatua kubwa kwake.
Kumbuka kwamba hawakuwa sawa hivyo kila mmoja hakuwa anataka kuona mwenzake akifanikiwa kuliko yeye, wakatengeneza uhasama mkubwa baina yao. Jambo hilo likapelekea mkeo kuanza kumletea visa Aurelia ili afukuzwe jeshini ila alikuwa makini sana, hakuwahi kufanya kosa hata moja ila jambo hilo lilizidi kumletea kisasi kizito kweye moyo wake. Baadae sana nadhani ulizisikia zile taarifa za mwanamke huyu kuipoteza familia yake kabla hajaanza kusumbuliwa na lile tatizo la akili ambalo aliamua kutuigizia”
“Nakuelewa, endelea”
“Sasa kwenye lile tukio mtu ambaye yeye anaamini kwamba ndiye aliruhusu zile risasi kwenda kwa familia yake ambapo alimpoteza mumewe na mtoto ni mkeo. Kwahiyo alikuwa anatafuta sababu ya kulipa kwa namna yoyote ile kuhakikisha anamuua siku moja mpaka sasa ambapo aliona ni muda wake sahihi wa kufanya hivyo”
“Umesema mke wangu ndiye aliua familia yake?”
“Kwa jinsia ambavyo yeye anaamini, ndiyo”
“Ile kazi walitumwa vijana kuifanya, sasa mke wangu aliingia vipi hapa?”
“Huenda ni kweli endapo kama aliwazuia vijana kwenye hatua za mwisho na kufanya lile, kumbuka alikuwa anajua kila kitu mheshimiwa na alikuwa karibu yako na kwa wakati ule ulikuwa moja ya wanasiasa wenye nguvu kubwa nani angemzuia kama angetaka kulifanya hilo kwa amri yako?”
“Hizi habari wewe umezitolea wapi?”
“Kuna msamaria mmoja ambaye amenipatia taarifa hizi kwenye simu muda ule ambao nimekupigia simu kwamba nahitaji kuonana na wewe ndiyo maana nilivyo zipata tu nikaona kuna umuhimu wa kuonana na wewe ili ujue mheshimiwa”
“Msamaria huyo ni yupi?”
“Bado sijajua kwa sababu amegoma kutaja jina lake japo amedai kwamba kama mimi na wewe tunahitaji kupona kwenye hili hatuna budi kukubali masharti yake ili aweze kutusaidia”
“Kutusaidia mimi na wewe?”
“Ndiyo”
“Kwenye nini?”
“Anaamini kwamba huyu mtu ambaye sisi tunatafutana naye, hakuna namna tunaweza kuishi mbele yake”

74 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SABINI NA TANO
SONGA NAYO................


“Raisi wa nchi ndiye ambaye hawezi kuishi mbele ya raia wa kawaida?”
“Hayo ni maneno yake mheshimiwa”
“Na wewe umemuamini?”
Hapana sijamuamini ila huwa sidharau maneno hata kama yametoka kwa mjinga hususani kwenye jambo la mhimu kama hili la kupigania uhai. Ni jambo la hatari sana kiongozi”
“Nipe namba hiyo vijana wangu waweze kuidukua wajue ni wapi alipo ili akachukuliwe haraka aje anipe sababu za msingi za mimi kuendelea kumuacha akiwa hai”
“Hilo halina shaka mheshimiwa”
‘Halafu huyu binti umemhifadhi wapi kwa sasa”
“Sijakuelewa mheshimiwa”
“Umesema kuna binti kamuua mke wangu”
“Ametoroka mheshimiwa”
“Whaaaaat?”
“Nilituma vijana wakamkamate amewaua wote na kutokomea yeye na familia yake”
“Savato umekuja hapa usiku wote huu nikujua umemaliza kazi halafu kazi yenyewe imekushindwa mwanzoni tu?”
“Mkuu hili jambo nalimaliza mwenyewe, huyu binti mpaka sasa ana kesi ya mauaji na kingine ana familia hivyo hakuna mahali anaweza kwenda ndani ya ardhi hii nisimpate kikubwa naomba nipe masaa ishirini na manne tu namleta kwako”
“Nitakupa hayo masaa ili nione kama naweza kuendelea kukuamini au nikufute kwenye hesabu zangu lakini Savato angalia, kama kuna taarifa hapa umeipika kwa sababu zako ambazo unazijua mwenyewe, nakuapia nitakufanyia jambo baya sana”
“Mimi nitakuwa mtiifu kwako siku zote mheshimiwa”
“Unaweza kwenda”
“Bado nina jambo la mwisho mheshimiwa” bwana huyo alikuwa amejipanga haswa kwenye kuucheza huo mchezo.
“Kuna jambo gani jipya?”
“Ni mkurugenzi”
“Amefanyaje?”
“Bila shaka nina uhakika ulikutana naye mheshimiwa”
“Ndiyo, kuna tatizo juu ya hilo?”
“Hapana, wewe unaweza kukutana na mtu yeyote na wakati wowote ambao unataka lakini yule mtu anajua sana na amekuwa hatari kwa upande wetu, amekuja kunipa onyo kuhusu mwisho wetu mimi na wewe. Anaelekea sehemu mbaya”
“Najua hilo ndiyo maana anatakiwa kufa kesho usiku baada ya mazishi ya mke wangu”
“Ulilipanga hili mheshimiwa?”
“Ndiyo, leo nimekutana na kiongozi mkuu wa huu umoja wetu hivyo najua ambacho ninakifanya”
“Unamaanisha umekutana na bosi mwenyewe?”
“Ndiyo”
“Naweza kufahamu ni nani ambaye tumekuwa tukimtumikia miaka yote hii?”
“Itakuwa hatari kwako na kwangu, kama kutakuwa na umuhimu basi kuna siku ataonana na wewe”
“Sawa mheshimiwa, nitaisubiri hiyo siku”
“Nenda kaniletee huyo binti haraka kisha Aurelia nitajua namna ya kudili naye mwenyewe”
“Hilo hesabia kwamba limeisha mheshimiwa”

Raisi aliacha maagizo na kuondoka akimwacha bwana huyo hilo eneo akiwa mwenyewe anatabasamu. Alikuwa mzandiki sana mkuu wa majeshi, alikuwa anacheza michezo ya hatari mno kwa kuzigeuza taarifa.
Baada ya kukutana na raisi hapo alizipika taarifa kwa usahihi kiasi kwamba ilikuwa ni ngumu kwa mtu kuweza kumsoma. Alitoa siri ya mzee Hasheem, alikubali mzee huyo asimmalizie baadhi ya taarifa za msingi kwa kumtoa sadaka kwa sababu mambo yalimfika shingoni na kama angecheza vibaya basi ni yeye ambaye angekufa, jambo ambalo alilifanya wakati ameenda kukutana na mzee Hasheem mara ya mwisho kuna simu aliiacha kwenye ile nyumba akiwa ameiwasha.

Namba ya kwenye ile simu ndiyo alimkabidhi raisi ili vijana wake waweze kuidukua ambapo alikuwa na uhakika kwamba lazima watu hao wangeenda huko ili kumkamata mzee huyo kuweza kumhoji kuhakikisha anaeleza kila kitu ambacho alikuwa anakijua lakini wakati wao wanafanya jambo hilo alijua huo muda alitakiwa kuutumia kumuua mzee huyo. Aliinyanyua simu yake ndogo na kuipiga mahali ambako alikuwa anakujua mwenyewe, simu ilipokelewa haraka sana akatamka tu
“Kill him” simu ilipokatwa, alitabasamu kwa mara nyingine akaiweka nguo yake vizuri na kuanza kutoka ndani ya jumba jeupe.

Siku zote watu wenye akili kubwa ndio ambao huwa wanaishi kwa muda mrefu kwa sababu wanakuwa makini kwenye kila jambo ambalo wanalifanya, kwao akili huwa zinaanza kwanza ndipo yanakuja matumizi ya nguvu kwa baadae. Aliwahi kuambiwa mara nyingi kwamba hakuwa mtu mwenye akili kabisa, alidaiwa kuwa mtu wa kutumia zaidi mihemko ila sasa ulikuwa ni wakati wake sahihi kabisa wa kuweza kuwaonyesha kwamba hakuwa mtu wa kubahatisha kama ambavyo wao walikuwa wanadai bali alikuwa mtu ambaye alitakiwa kuaminika kwa sababu angeweza kufanya mambo makubwa ambayo huenda yangemuacha kila mtu mdomo wazi.
Mwanaume huyo pia alielewa kuhusu suala la kifo cha mke wa raisi, yeye ndiye ambaye alitakiwa kuwa mhanga mkuu lakini tangu mwanzo alipiga hesabu za mbali kuweza kumtumia Sarah, alielewa madhara ambayo yangejitokeza baadae ndiyo maana hakukurupuka. Kwa wakati huo aliwauzia kesi wanawake wawili kwa wakati mmoja, kwa sababu alijua kwa muda huo wote raisi asingeweza kuwapata na mwenye uhakika wa kuja kupatikana angekuwa ni Sarah, hakuwa fala. Aliamini kwamba yeye ndiye alitakiwa kuwa mtu wa kwanza kabisa kumpata mwanamke huyo na baada ya kumpata alitakiwa kumuua kwa mkono wake kabla raisi hajampata kwa sababu kama ingetokea hivyo basi lazima binti huyo angetema nyongo kwa kusema ukweli. Swali la msingi kwake wakati huo ilikuwa ni kwamba Sarah yuko wapi kwa wakati huo? Bado kilibaki kuwa kitendawili ambacho kilihitaji majibu kutoka kwake mwenyewe.


********
Aliyafumbua macho yake, alikuwa kama katokea kwenye kifo, hakuamini kama bado alikuwa hai na mzima. Mwili wake ulikuwa na maumivu kwa mbali ambayo hayakumpa mushkeli mkubwa wa kumfanya asiweze kuuona mwanga kwa mara nyingine.
Alimshukuru Mungu kwa kumpendelea wasaa mwingine wa kuweza kupata nafasi ya kuyaishi maisha mengine hata kama ingekuwa ni kwa wiki tu lakini jambo hilo kwake lilikuwa zaidi ya upendeleo na alishukuru sana kuipata nafasi hiyo ambayo wengi hawakuwa na uwezo wa kuipata.
Baada ya kufumbua mboni zake na kutazama sehemu aliyokuwepo, ilikuwa ni sehemu ya kisasa isivyokuwa kawaida, ilikuwa ni tofauti na mazingira ya nyumbani kwake ambayo aliizoea, vitu vilivyokuwa humo ndani vilikuwa vya bei ghali kupita kiasi. Hapo ndipo akili ilianza kurudi na kumkumbusha kwamba hakuwa kwake, bali alikuwa eneo geni kabisa na nyumbani.
Mara ya mwisho alikuwa kwenye kipigo kikali tena kutoka kwa mtu ambaye binafsi alichagua kumuamini kwa maisha yake yote, Nick. Alisikitika na kughafilika moyoni, alisonya akiwa na hasira na kula kiapo ndani mwake kwamba kama kuna siku ingetokea akaja kuonana na bwana huyo basi angekuja kumfanyia jambo baya ambalo hatalisahau kamwe kwenye maisha yake. Usimwani sana binadamu kupitiliza hususani mtu ambaye mmekutana tu kwenye maisha haya ya utafutaji ama kupambana, watu wanabadilika na sio lazima mtu afanye vile unataka wewe kwa sababu naye ana vipaumbele vyake.

75 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SABINI NA SITA
SONGA NAYO................


Usimchukie mtu kwa sababu kakuumiza, hajakupenda ama hajafanya kama vile ambavyo wewe unataka afanye, mtu hana muda wa kuishi maisha yake kwa kukufurahisha wewe wakati naye anatakiwa kupambana kuitafuta furaha yake. Ukiona sehemu hutakiwi ama unaona mtu anajaribu kuwa na wewe lakini hawezi acha ujinga wa kulalamika na kujifanya spesho sana, tafuta mahali ambapo mtakutana watu wawili wenye kufanana vitu, vingi punguza kujikuta wewe ndiye mwana wa MUNGU ambaye unastahili kila kitu na ukipate kila ukitakacho. Huo ni ujinga, kwani wewe ni nani bwana! Acha kusumbua watu. Aliyakumbuka maneno ambayo waliwahi kufundishwa kipindi wapo jeshini, hapo alituliza komwe lake kwa sababu kosa halikuwa kwa mtu mwingine bali kwake mwenyewe, yeye ndiye alimfungulia Nick milango ya kuingia ndani mwake halafu alitaka kuanza kulalamika tena. Alitulia japo hakuona kama ni sababu ya msingi ya kuweza kumsamehe bwana yule, angelipa kwa aliyo yafanya.

Akiwa yu mbali anawaza hayo, alishtuliwa na sauti ya tv ya kisasa ambayo ilibandikwa ukutani, tv hiyo ilikuwa inatoa taarifa ambazo zilikuwa zinaendelea nchini na duniani hususani kwa asubuhi hiyo. Jambo hilo likampa umakini kuweza kufahamu kama kuna habari imhusuyo ama ya kumfariji ilikuwa imetokea Tanzania.
Habari ya kwanza na kubwa zaidi ilikuwa ni juu ya mazishi ya mke wa raisi, mwanamke ambaye ni yeye kwa mkono wake aliyabeba maisha yake. Mwanamke huyo alikuwa anazikwa siku hiyo hivyo ilikuwa inasomwa ratiba ya mazishi yake na namna yatakavyo fanyika, alisikitika kwa sababu hiyo lakini ilikuwa imesha tokea tayari hivyo masikitiko yake hayakuwa na msaada wa aina yoyote ile japo ilikuwa inamuumiza sana kuua mtu bila kujua sababu za msingi za kuweza kumuua mtu huyo.

Taarifa hizo hazikuwa mbaya kwake, bali taarifa ambazo zilifuatia baada ya hapo ndizo ambazo zilimtoa pale kitandani akajikuta amesimama huku akitoa mipira ya maji kwenye mwili wake, zilimchanganya pakubwa mrembo huyo ambaye alibaki ameduwaa asielewe ni jambo gani alitakiwa kulifanya kwa wakati huo.

Taarifa ambayo ilikuwa inatolewa kwenye vyombo vya habari wakati huo ilikuwa ni ya muuaji wa mke wa raisi, alikuwa ni mwanajeshi mwenye mafunzo ya hali ya juu mno kwenye udunguaji. Mtu huyo alidaiwa kulisaliti jeshi kwa muda mrefu sana kwa sababu tukio hilo ndilo lilifanya waanze kuungananisha matukio yaliyokuwa yametokea nyuma kabla ya siku hiyo.
Binti huyo baada ya kuhisiwa kuhusika na jambo hilo walitumwa wenzake kuweza kumpekeka makao makuu ili akahojiwe lakini matokeo yake aliishia kuwaua wote kikatili akiwepo mwenzake ambaye alikuwa karibu naye, Nickson! Ambaye siku kadhaa nyuma walionekana wakiingia kwenye nyumba pamoja eneo ambalo mmoja wao alikuwa akifanya kazi, bila shaka walikuwa wapenzi lakini hilo halikumzuia mwanamke huyo pia kumuua bwana huyo.

Picha ya mwili wa Nickson ilikuwa imekuzwa kwa ukubwa ikiwa imezibwa usoni, yalikuwa yakionekana majeraha tu mengi kwenye mwili wake. Hivyo mtu huyo alikuwa anatafutwa kwa kuhusika na mauaji ya mke wa raisi lakini pia wanajeshi wenzake na raia waliombwa kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kupatikana kwa mtu huyo kama kuna sehemu wangemuona kwani watu kama hao ndio ambao walikuwa wanalifanya taifa liendelee kuingia kwenye machafuko makubwa.

Sarah ndiye ambaye alikuwa ndani ya chumba hicho, alihisi kuchanganyikiwa kabisa. Hakujua ni kwanini kesi hiyo ilimgeukia vibaya kwa namna kama hiyo, huenda alitarajia baadhi ya mambo kama hayo kutokea ila sio kwa namna kama hiyo ambavyo yalikuwa yanatokea. Aliishiwa hata la kufanya, mpaka muda huo alikuwa ameyaharibu maisha yake na ya familia yake kwa ujumla, alijua kabisa watu hao hawakuwa na nia ya kumkamata kama ambavyo walikuwa wanaongea kwenye mitandao bali popote pale ambapo wangemuona basi wangemuua yeye na familia yake yote.
“Mamaaaaaa!!!!!” aliita kwa nguvu huku moyo ukiwa unamuenda mbio, alikumbuka kwamba mpaka muda huo alikuwa kwenye mikono ya wauaji ndiyo maana alikurupuka. Kuita kwake kulisindikizwa na yeye kushindwa kutambua namna ya kutoka ndani humo alimokuwemo kwa sababu chumba kizima kilikuwa na vioo vya shaba kiasi kwamba akawa hata haelewi mlango ulikuwa wapi.
Akiwa ameshika kichwa haelewi afanye nini, angeenda kule na kurudi huku akiwa kama mtu ambaye alikuwa amepoteza kila kitu kwenye maisha yake, chumba hicho kilianza kama kujiupdate na kubadika badilika mpaka kilipo tulia kilikuwa kwenye hali ya kawaida, hapo aliuona mlango wa mninga, alitamani kuusogelea lakini alirudi nyuma baada ya kuona kinayongwa kitasa, bila shaka ni mtu alikuwa anaufungua kutokea nje. Alimeza mate kwa hofu na tahadhari kwa sababu hakujua nani alikuwa kamtembelea.

Aliingia mwanaume mmoja ambaye alikuwa mwembamba ila mwili wake ulizungumza mengi juu ya ule wembamba wake, alimwangalia mwanamke huyo kwa umakini kuanzia juu mpaka chini kisha akatoka mlango ukiwa bado upo wazi. Hazikupita hata sekunde tatu, mama yake aliingia humo ndani akiwa wa afanya kabisa, alimkimbilia na kumkumbatia, angalau moyo wake ulianza kutulia baada ya kugundua mama yake ni mzima wa afanya na bila shaka hata mdogo wake alikuwa hivyo hivyo. Alimshukuru Mungu kwanza kwa ajili ya familia yake.

“Mama” aliongea kwa hisia chozi likiwa linamshuka. Angalau yeye kwenye maisha yake alipata bega la kuegamia wakati akiwa kwenye uchungu namna hiyo, ilimsaidia kupunguza maumivu makali aliyokuwa anayapitia wakati huo.
“Najua mwanangu, najua mambo hayawezi kuwa kama mwanzo, najua kila kitu kimebadilika”
“Mama unaamini kama mimi ni muuaji?”
“Hapana mwanangu najua ulifanya yote kwa sababu ya familia na mimi sikulaumu kwa lolote lile” mama yake alimkalisha mwanae na kuhitaji waongee kama watu wazima sasa, kwa sababu mambo yalikuwa yameharibika lakini mwisho wa siku maisha mengine yalitakiwa kuendelea hivyo mpaka wakati huo walitakiwa kujua nini ilikuwa hatima ya maisha yao.
“Nakusikiliza mama”
“Kwanza tunapaswa kuwashukuru watu hawa mpaka sasa kuhakikisha sisi tupo salama na wazima wa afya japo wamedai wataongea na wewe ukiwa sawa”
“Mimi nipo sawa mama, nahitaji kuongea nao saivi”
“Inategemea na majibu ambayo daktari wao atawapa kuhusu wewe ndiyo yataamua kama unaweza kukutana na kiongozi wao”
“Tupo wapi hapa?”
“Hata mimi sijui, ilikuwa ni usiku sana na nilikuwa nahofia zaidi kuhusu hali yako ila bila shaka itakuwa Dar es salaam”
“Dar es salaam”
“Ndiyo”
“Hapana mama, hili eneo sio salama tena kwetu, hii ni sehemu ambayo inaweza kuyabeba maisha yetu muda wowote kuanzia hivi sasa”
“Tuliza kwanza akili mwanangu ujue ni kipi unakitaka kwa sasa, usalama wako ndio ulikuwa jambo la msingi kwanza haya mengine tutayaweka sawa”
“Yatakaaje sawa mama wakati mimi hapa natafutwa kwa kuhusika na mauaji ya mke wa raisi? Nimesingiziwa kuhusika na mauaji ya watu wale wakati najua kabisa ni njama za kunipoteza mimi. Nimekosa nini mimi kustahili haya yote?”
“Mwanangu kumbuka kipindi kile tuna maisha magumu hakuna mtu alikuwa na muda na sisi. Kwa juhudi zako mama yako nimeishi maisha mazuri, mama yako nimekuwa mtu mbele za watu. Dunia ipo hivyo mwanangu jinsi unavyozidi kufanikiwa ndivyo pia unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuweza kuchukiwa na watu kwa sababu kila mtu anakuwa anakupiga jicho baya, unakuwa sio kipenzi kwa watu tena, unakuwa adui wa watu mpaka siku wahakikishe wamekupoteza ndipo wanakuja kukupa pole ya kinafki kama kukusanifu tu. Hao ndio wanadamu ambao tunaishi nao hivyo huu sio wakati wa wewe kulia bali ni muda wa kuonyesha uimara wako na kuhakikisha hili tunalivuka kwa pamoja”
76 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SABINI NA SABA
SONGA NAYO................

Mama alikuwa anaongea maneno mazito lakini yenye nguvu, haukuwa muda wa kukaa na kuanza kulia lia juu ya mambo ambayo yalitokea, ulikuwa ni muda wa wao kukaa na kukubaliana namna sahihi ya kuweza kulimudu jambo hilo. Mama aliamini kwamba hakukuza mtoto mayai mayai bali alikuza binti ambaye alitakiwa kila siku ajivunie kuwa mwanae ndiyo maana wakati huo alitamani kuweza kumuona akiwa imara.

Sarah alitamani kuongea neno baada ya kumsikia mama yake akimpa moyo wa kupambana wakati huo ambao walikuwa kwenye wakati mgumu lakini hakufanikiwa kufanya hivyo baada ya mlango kufunguliwa. Aliye muona mbele yake ni mdogo wake, walikumbatiana kwa furaha lakini hakuwa mdogo wake tu pekee bali mwanaume mwingine, Othman chunga, yule yule muuaji ambaye alikuwa amemsaidia ule usiku ambao ulikuwa umepita na bila bwana huyo huenda asingekuwa hai. Ujio wa mtu huyo haukuwa kuja kupiga naye soga bali alikuwa anahitajika haraka na kiongozi wa watu hao, Gavin mwenyewe.

Sarah alinyanyuka na kuanza kumfuata bwana huyo akiwa ndani ya jengo ambalo hata hakujua kabisa kwamba lipo wapi na kuanza kumfuata, akiwa njiani alitamani kuyajua machache kuhusu watu hao.
“Haya maisha mmeanza kuyaishi lini?” Othman alitabasamu na kumwangalia mwanamke huyo kwa makini
“Ya kuogopwa, kuua ama kuishi kama familia?”
“Namaanisha yote kwa ujumla”
“Naweza kusema ni muda kidogo tangu bosi alipotukusanya pamoja”
“Alipo wakusanya?”
“Ndiyo”
“Kivipi labda?”
“Mara ya kwanza hatukuwa hivi, kila mtu alikuwa anaishi maisha yake. Sisi ni watoto wa familia ambazo zilipenda haki, familia ambazo zilipenda kuiona Tanzania mpya na bora kutoka kwenye mikono ya hawa wazandiki lakini hawakuwa tayari kwa hilo, taifa linaongozwa na watu wenye tamaa, watu ambao wanawaza matumbo yao tu, watu ambao hawana muda kabisa na hali ngumu wanayo ipitia watanzania. Familia zetu ziliuliwa kwa sababu ya kulipambania taifa lakini kwa bahati iliyokuwa mbaya sana wakati hayo yanafanyika, hawakuua wazazi wetu tu bali walibeba kila kitu ambacho walikuwa nacho wazazi wetu
Tulibaki bila mwelekeo, hatukuwa tunajuana hivyo kila mtu alikuwa anakufa na hali yake, wote ambao tupo humu ndani tumezaliwa kwenye familia ambazo zilikuwa na uwezo lakini kwa sababu ya watu hawa kila kitu kilibadilika, kila kitu kilibaki kuwa cha kufikirika na ni wakati ambao mimi binafsi nilijifunza kuiheshimu hata punje moja ya wali. Maisha yakiwa kwenye njia yako huwezi ukawaelewa watu ambao wana uchungu na chakula mpaka siku moja ukiingia kwenye hiyo hali ndipo utawaelewa vizuri. Nakiri kwamba baada ya kifo cha wazazi wangu kila kitu kilipotea hivyo nilianza maisha na moja tena nikiwa mwenyewe. Ukumbuke sikuwahi kuishi maisha magumu halafu nilitakiwa kuyaanza haya maisha mwenyewe nikiwa sijui nianzie wapi, unaweza ukaelewa kidogo njia ambazo nilipita”

“Kwanini usingejaribu kwenda mahakamani kupata mustakabali wa mali za wazazi wako?”
“Wewe ni mwanajeshi na unaelewa haya mambo yanavyo isha, hakuna sehemu mahakama ipo kwa ajili ya maskini kwenye taifa hili. Ni mtu wa ajabu pekee ambaye anaweza akakaa na kuziamini hizo habari, ni watu wa kufikirika ndio ambao wanaweza kupoteza muda wao kuanza kuamini huo ujinga. Hawa watu wameshika kila sehemu, wapo kila kona, wana watu kwenye kila shina la nchi hii mpaka Ikulu ambayo ndiyo ofisi kuu, wanaiendesha wao sasa utapitia wapi na hiyo haki unaipatia wapi Sarah? Unabaki kufanya maombi ambayo hayana matumaini
Niliishi maisha magumu ambayo sikuwahi kuyafikiria kabla, hakuna kazi ngumu ambayo sikuifanya kwa wakati ule kwa sababu ndiyo ilikuwa njia pekee ya mimi kuweza kuishi. Nilibeba zege, nilikesha kwenye mabar kutafuta vibarua hata vya kuchoma nyama, ajabu kipindi chote hichi kulikuwa na nyumba yetu maeneo ya Tabata, nyumba walidai kwamba nitaruhusiwa kuitumia kipindi wakimaliza kufanya uchunguzi wao ila mpaka hivi ninapo ongea na wewe ile nyumba imebaki kama gofu, haina mtu na hakuna mtu anaruhusiwa kukaa na ndiko huko aliko zikwa baba yangu.

Nilikata kabisa tamaa ya kuendelea kuishi, maisha yalikuwa magumu sana upande wangu mpaka nikafanya maamuzi ya kutoka kujitoa uhai. Ule ulikuwa ni uamuzi wa mwisho kabisa mimi kuufanya. Niliona ni bora niende nikapumzike kaburini na wazazi wangu lakini kabla sijafanya hayo maamuzi ndipo kwa mara ya kwanza nikapata neema nyingine, MUNGU alimtuma malaika wake aje kuniokoa. Stori ya maisha yangu ilibadilika kabisa nikawa mtu mwingine kuanzia pale, ni baada ya kukutana kwa mara ya kwanza na Gavin Luca.
Sikukutana naye kwa bahati mbaya bali alinitafuta mwenyewe, kiukweli ni kwamba sikuwahi kabisa kuonana naye wala kumfahamu kabla ya pale hivyo hata sikujua vizuri aina ya mtu ambaye nilikutana naye. Kwa mara ya kwanza nilijua ni wale wale wamekuja kunimaliza na mimi ila bwana yule alinishangaza, alinipatia kiasi cha milioni mia moja mkononi akinitaka nianze maisha mapya, maisha ambayo natakiwa kufanya maamuzi sahihi kama nitakuwa tayari kuwa chini yake anisimamie na kama nilikuwa na kisasi cha kulipa basi angenisaidia mwenyewe kufanya hivyo.

Nilipigwa na butwaa, mtu akupe milioni mia moja kwa maisha haya, ni nani huyu? Milioni mia moja ni pesa nyingi sana kwa maisha ya mtanzania, ni pesa ambayo unatumia miaka mingi mno kuwa nayo na kuna wengine watakuja kufa bila hata kuishika hiyo pesa. Niliipokea kwa sababu ya njaa zangu ila nilikuwa naogopa mno maana vitu vya bure huwa ni vibaya sana hususani ukufika wakati wa kuweza kuvilipia, licha ya kuogopa hilo sikuweza kuikataa pesa, niliipokea. Mtu huyo alipotea akidai kwamba angekuja kunitafuta baadae ila nilitakiwa kuishi bila kutambulika kwamba nina pesa kwa sababu ingekuwa tatizo kwa upande wangu.
Ilipita miezi kadhaa mpaka nikaanza kusahau kuhusu kukutana naye ndipo alinitafuta kwa mara ya pili, mara hii sasa alikuja na mpango mezani wa kunitaka nifanye maamuzi kama nataka kusaidika na kuwa mtu mwingine ama kama nahitaji kumfuata yeye kisha niwe mtu wa tofauti na maisha yangu yabadilike ila alinisisitiza kwamba kama nikimfuata basi sitakuwa mtu yule yule tena na hakutakuwa na kurudi nyuma. Sikuwa na cha kupoteza kwenye maisha yangu hivyo nilikubaliana naye moja kwa moja na kuyaanza maisha chini yake.

Mara ya kwanza nilihisi kwamba nipo mwenyewe ila baadae niligundua kwamba sikuwa pekeyangu kweye ule mpango na ule mpango ulikuwa na kesi ambazo zinafanana. Alitutafuta wote ambao familia zetu zilifanyiwa mambo ya kikatili akatuweka pamoja, alimtaka mtu ambaye anatamani kuwalipa wale ambao walimfanya yeye kuishi maisha magumu abaki kwake yeye angempatia kila kitu ambacho kingemsaidia kulipa kisasi na kwa ambaye hakuwa tayari kufanya hivyo basi alikuwa tayari kumsaidia kupata pesa yoyote ambayo angeihitaji ili akaanze maisha yake popote duniani.
Kwenye dunia ya leo kupata ofa kama hiyo ni jambo adimu mno kama kuona vimondo vikidondoka, kila mtu alikuwa na kisasi ila hakuna ambaye alikuwa ana uwezo wa kulipa kwa sababu hatukuwa na uwezo. Wote tulikubali kuwa naye, tulimuomba sana atusaidie siku moja tulipe kisasi kwa watu ambao walikuwa wamehusika kufanya unyama kwenye familia zetu. Safari ya maisha yetu ilianzia pale.

Ile miaka ambayo ilitumika yeye kutafutwa baada ya jina lake kuwa maarufu halafu akaja kupotea, ni miaka ambayo alituingiza kambini msituni kutufanyisha mazoezi makali na magumu yeye mwenyewe. Hakuonekana kuwa binadamu wa kawaida, alikuwa ni mtu hatari mno kwenye ulimwengu wa mapigano. Kuna siku moja niliamka usiku wa manane nikiwa sina usingizi kabisa nikalazimika kutoka nje, nikiwa nje nilisikia upepo ukiwa unavuma kwa kasi ndani ya msitu, ikanilazimu kwenda huko. Kitu nilicho kishuhudia kule kilinifanya mpaka leo namuogopa sana, alikuwa anaweza kuukusanya upepo kwa mkono wake kisha akautumia kuzoa vitu na kuvitupa mbali, alikuwa ni mwepesi muda mwingine hata macho ya kawaida kumuona ni ngumu, mpaka leo sina imani kama ni binadamu aliyezaliwa na mwanamke.

77 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SABINI NA NANE
SONGA NAYO................


Mikono yake ilikuwa na nguvu za ajabu, alikuwa anatembea juu ya miti kama naangalia drama za wakorea. Mkono ulikuwa ukitua kwenye mti basi mara moja mti unabonyea. Nilitamani kupiga makelele ila nilijizuia na kukimbia eneo lile kurudi kulala, nilitamani kumjua kiundani zaidi ya alivyokuwa ametueleza kuhusu yeye, nilitaka kumjua upande wake mwingine kwamba ana kitu gani hasa kiasi kwamba ana uwezo wa ajabu namna ile ndipo nikaja kuyajua mambo magumu sana kuhusu yeye mambo ambayo sikuwahi kumshauri mtu mwingine yeyote aweze kuyajua kwa sababu ni hatari mno tena yanaweza kufanya mtu amuogope maisha yake yote”

“Mhhhhh simulizi ya maisha yako inasikitisha sana, nimejisikia vibaya kwa ambayo yamekukuta lakini hilo la bosi wako halionekani kuwa jambo la kawaida”
“Ni kweli sio jambo la kawaida ndiyo maana kuna vitu hautakiwi kujua kuhusu yeye kwa sababu inaweza kukufanya usije kukaa karibu naye tena, itakufanya umuogope maisha yako yote. Mambo mengi kuhusu yeye nilikuja kuyapata baada ya kuisoma diary yake, ameandika mpaka namna atakavyokuja kufa”
“Whaaaaat?”
“Yeah, ndilo jambo ambalo linanitisha kuhusu yeye. Kuna muda natamani asiimalize hii vita mapema kwa sababu siku akiimaliza tu ndiyo siku ameandika kwamba ni lazima afe”
“Anajua kama wewe unajua kuhusu hili?”
“Hapana, niliisoma kipindi yeye hayupo na hajui kama niliiona hiyo Diary yake”
“Kuna muda huwa anaondoka au?”
“Ana familia ambayo kwa sasa ameileta karibu huku japo ni eneo la siri sana ilipo”
“Unamaanisha nini kusema ana familia?”
“Ana mke na mtoto”
“Bila shaka ndio udhaifu wake mkubwa”
“Kila mwanaume udhaifu wake mkubwa ni familia yake Sarah”
“Naweza kujua sababu gani ambayo imemfanya mtu huyo ajitabirie kifo?”
“Watu ambao anajua anaenda kukutana nao sio wa kawaida nao, ni watu hatari sana ambapo lolote linaweza kutokea lakini kuna kitu ambacho kinamfanya hata baada ya hili kuisha apange kuyabeba maisha yake mwenyewe”
“Anataka kujiua?”
“Ndiyo”
“Kitu gani hicho?”
“Ana nguvu za ajabu kwenye mwili wake ambazo utafika wakati hatakuwa na uwezo wa kuweza kuzimudu tena hivyo zinaweza kuja kuwa hatari kwa huu ulimwengu”
“Nguvu gani hizo?”
“Hauwezi kunielewa, ni nguvu ambazo amekatazwa kuweza kuzitumia na kama ikilazimika akizitumia basi hatakuja kuwa binadamu wa kawaida tena ndiyo maana amepanga hadi namna ya kufa kwake ambapo hataki kabisa familia yake ije kuona mwili wake. Amepanga kufanya hivyo kwa sababu siku anamaliza kazi yake anajua itamlazimu kuzitumia nguvu hizo kwahiyo akizitumia kwa kiasi kikubwa uwezo wa kuzihimili utakuwa mdogo, itampelekea kupoteza kumbukumbu na kuwa muuaji, hapo anaweza kuja kuanza kuua kila mtu hata ambao alikuwa anawajua na kuwalinda, hataki kabisa kufikia hatua hiyo ndiyo maana amepanga kupotea kwenye nyuso wa walimwengu kabisa baada ya kazi kuisha” Sarah alikuwa anasisimka na kuogopa kwa wakati mmoja kipindi anapewa simulizi ya maisha ya mtu ambaye wakati huo ndiye alikuwa anaenda kukutana naye.
“Hizi nguvu anazo kabla au baada ya kuwa na mtoto?”
“Mtoto wake ni wa juzi tu hapa, hizo nguvu anazo hata kabla ya kuwa kabisa na familia”
“Kuna namna hizi nguvu zinaweza kuhamia kwa mtoto kwa njia ya asili?”
“Hilo jambo hajaliandika humo ndani japo huenda inawezekana ila sijui”
“Kama hilo linawezekana basi kuna hatari nyingine hata mtoto wake akaja kuwa nazo kwa baadae, hizi nguvu za asili huwa zinakuwa na nguvu zaidi kutokana na namna zinavyozidi kuhama kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.”
“Hilo tuliache kwa sasa, unaweza kwenda kuonana naye” maongezi yao yalikuwa yanafanyika nje ya lango moja kubwa sana, walikuwa wamefika sehemu ambayo Sarah alikuwa anatakiwa kwenda. Simulizi fupi ya maisha ya akina Othman aliyopewa pamoja na nguvu ambazo alikuwa nazo Gavin Luca alijikuta anatetemeka huku jasho likiwa linamtoka kwa wingi kwenye mwili wake licha ya kiyoyozi kuwepo kila kona ya jengo hilo.
“Kwanini umeamua kuniambia haya yote Othman?”
“Mpaka tumekuleta ndani ya hii sehemu ujue umeaminika na sidhani kama kuna lolote unaweza kulifanya juu ya nilicho kwambia”
“Mpo wangapi ambao aliwachukua kwa ajili ya kuwasaidia?”
“Jumla tupo wanne”
“Wote mpo humu ndani?”
“Hapana. Mmoja ni mlinzi wa mama, mmoja ni mlinzi wa mke wa bosi, mmoja ni mlinzi wa mtoto wa bosi na mimi hapa mara nyingi huwa nipo kwa ajili ya kumlinda bosi inapobidi lakini mara nyingi huwa ni ngumu kutuona jambo ambalo huwa linafanya mtu yeyote asijue kama tupo mahali husika”
“Na wote mmeshalipiza visasi vyenu?”
“Wote kwa sasa tumemaliza, bado mmoja wetu ambaye ana deni na mkuu wa majeshi japo hataki kumuua kwa mkono wake, bila shaka hamalizi masaa ishirini na manne atakuwa amemaliza kisasi chake hapo itabaki zamu ya bosi mwenyewe”
“Mnataka kumuua mkuu wa majeshi?”
“Ndiyo”
“Ni jambo gumu sana”
“Hilo ni gumu kwako, hauwajui watu ambao upo nao hapa wakati huu namna walivyo hatari Sarah, kakutane naye utaanza kunielewa” mwanaume huyo aliongea huku akiwa anaweka jicho lake ukutani kwa ajili ya kulifungua lango hilo. Lilifunguka, ndani kulikuwa na vitu vya thamani sana, pembezoni alionekana mwanaume mmoja akiwa amekaa kwenye sofa anaziangalia picha kadhaa ukutani. Ilikuwa kwa mara ya pili yeye kukutana na Gavin Luca mwenyewe, Sarah alikuwa anaogopa hata kuingia ndani ya eneo hilo, mwanadamu ambaye alikuwa anaenda kukutana naye hakuwa wa kawaida kama walivyo wengine, alikuwa ni mtu ambaye anatisha isivyokuwa kawaida ila hakuwa na namna.

Taratibu alianza kuzirusha hatua zake kuelekea kukutana na mtoto wa mfanya biashara wa dawa za kulevya ambaye alifanikiwa kuujenga mji wake mwenyewe na kulisaidia taifa kwa kulipa zaidi ya pesa za kimarekani zaidi ya bilioni kumi lakini kwa bahati mbaya sana akaishia kuuawa na mtu ambaye hakuwahi kujulikana alitoa amri, ndiyo kazi kubwa aliyokuwa nayo Gavin kuweza kumpata mtu huyo ambaye alitumia miaka mingi kuishi gizani mpaka siku hiyo hakuwa amemjua bado lakini kwenye mkono wake alikuwa na jina la Medrick Savato, mkuu wa majeshi.
Huyo alitakiwa kumpa majibu yote pindi akimtembelea na ni huyo ambaye aliahidi kwamba akirudi kutoka huko Singida ambako alienda kuifuata familia yake na kumwambia ukweli wa maisha yake mkewe alitakiwa kudili naye.

78 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
Respect [emoji120][emoji120]
 
Mwandishi niwie radhi kwa yale maneno ndugu yangu.

🙏🙏🙏🙏🙏🙏
 
Leo ni leo[emoji91][emoji91][emoji91]

Sent from my ZTE T1002 using JamiiForums mobile app
 
Leo ni leo[emoji91][emoji91][emoji91]

Sent from my ZTE T1002 using JamiiForums mobile app
IMEACHIWA tayari mkuu..

Collection imekamilika

1. IDAIWE MAITI YANGU
2. THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA - SAFARI YA GAVIN LUCA (LIONELA)
3. SIKU ZA MWISHO- THE DARKNESS OF AN ANGEL (Hii imeachiwa alasiri ya leo) 🔥🌹🌹
 
IMEACHIWA tayari mkuu..

Collection imekamilika

1. IDAIWE MAITI YANGU
2. THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA - SAFARI YA GAVIN LUCA (LIONELA)
3. SIKU ZA MWISHO- THE DARKNESS OF AN ANGEL (Hii imeachiwa alasiri ya leo) 🔥🌹🌹
Weka Link hapa mkuu
 
Respect mkuu kazi nzuri
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…