Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA NNE
SONGA NAYO................

*********
Mr George, raisi wa Tanzania alikuwa na siku ndefu mno, ni siku ambayo alimpoteza mkewe kipenzi, siku ambayo alienda kukutana na yule mwanamama Aurelia lakini huko akaishia kukutana na mambo ya ajabu. Ni wakati ambao hakuwa anampata hata mkurugenzi wa usalama wa taifa jambo ambalo halikuonyesha usalama wala hali ya kueleweka kwa upande wake.

Lakini pia muda ulikuwa umeenda mno akiwa kwenye ofisi yake kusubiri majibu ambayo hakuwa na uhakika tena kama atayapata. Aliwatuma vijana wake waende kumchukua mwanamama huyo huko Yombo lakini mpaka wakati huo hakukuwa na majibu yoyote ambayo yalipatikana. Alikuwa anampigia simu mlinzi wake bila mafanikio yoyote yale mpaka akahisi kuchanganyikiwa, mwili ulikuwa una joto jingi, hakuna kitu kilikuwa kinaenda kama alivyo hitaji yeye.
Simu pekee ambazo alikuwa anazipata wakati huo zilikuwa za viongozi wakubwa wa mataifa mengine ambao walikuwa wanampa pole kwa kumpoteza mkewe huku wengine wakiwa wanaahidi kuweza kufika msibani na wengine walidai wangetuma wawakilishi kwa ajili ya kuja kumfariji. Hayo yote hakuyajali kabisa kwa sababu kwa wakati huo hayakuonekana kuwa ya mhimu hali ambayo ilimfanya kuzima kabisa simu zote hizo za ofisi. Aliifungua pombe na kuimimina kwenye bilauri akiwa mwingi wa jazba tena mwenyewe, alikuwa anatamani kumpata mtu wa kuweza kumaliza hizo hasira zake lakini hakumpata.
Akiwa kwenye hizo hasira nyingi mheshimiwa ndipo alipata simu ambayo iliingia kwenye namba yake binafsi ambayo ndiyo pekee hakuwa anaizima hata siku moja, mtu ambaye alimpigia muda huo alikuwa na hasira naye kali mno ambazo asingeweza hata kuzielezea kwa lugha ya kawaida. Othman Micho, mkurugenzi wa shirika lake la TIGI ndiye ambaye alikuwa anampigia simu wakati huo. Alisonya kwa sauti kubwa na kuipokea simu hiyo, bwana huyo alimwambia kwamba ndani ya dakika kumi na tano angekuwa anaingia hapo Ikulu kwa sababu alikuwa na mambo ya mhimu ya kuzungumza na bosi wake.
Kwake ilikuwa ni habari njema kwa sababu alikuwa ana usongo mkubwa na huyo bwana, alihisi huyo alikuwa moja ya watu ambao waliisababisha hali ya hatari kuweza kutokea kwa mke we hivyo alihitaji kumalizia hasira kwake na kama ingewezekana angeweza kumuondoa kwenye hiyo nafasi.

“Othman kipindi nakupa hii nafasi uliapa kulilinda taifa hili kwa gharama yoyote na kuhakikisha amani muda wote, kwenye kulilinda taifa, moja kati ya majukumu yako makubwa ni kuweza kumlinda raisi wako pamoja na familia yake kwa ujumla. Lakini leo hii mke wangu amepigwa risasi alasiri, kwenye simu hupatikani mpaka unakuja wakati kama huu ambao mimi nipo kwenye majonzi makubwa. Unaweza ukaniambia labda ulikuwa wapi na kuna sababu zipi za msingi ambazo zitanishawishi mimi kuendelea kukuweka wewe kwenye hiyo nafasi mpaka muda huu?”
“Kwanza nikupe pole kwa kuweza kumpoteza first lady, huu msiba sio wako tu bali ni msiba wa taifa zima lakini hata hivi sipo hapa kukuomba msamaha mheshimiwa juu ya kile ambacho kimetokea alasiri ya leo”
“Umesema?”
“Mimi na shirika langu kwa ujumla hatuhusiki kwa lolote lile kwa sababu wewe una kitengo binafsi ambacho kinakulinda hivyo hao ndio ambao walitakiwa kuwajibika kwa namna moja ama nyingine sijajua kwa sababu gani unataka kuona kama mimi ndiye mhusika mkuu kwenye hili jambo”
“Naona umeanza kunikosea heshima siku hizi Othman, unakumbuka mahali nilipo kutoa?”
“Naheshimu hilo la wewe kunipa nafasi hii kubwa kuweza kulitumikia taifa langu ila sidhani kama ni sababu tosha ya kufanya mimi kuwa mhusika wa kila jambo hususani sehemu ambayo sitakiwi kupewa lawama”
“Unajua Othman wahenga walikuwa na maana kubwa kusema kwamba kuku akiwa mgeni unatakiwa kumfunga kamba mguuni kwa sababu kama akipotea kuna nafasi ndogo ya yeye kupatikana tena lakini ikitokea siku kuku huyo akayazoea mazingira basi mara nyingi unamuamini kwa sababu unajua hata kama ataenda wapi bado ni lazima tu atarudi nyumbani. Umeshakuwa kuku mwenyeji hivyo sikuwa na mashaka na wewe ndiyo maana sikutaka kukufunga kamba mguuni lakini naanza kuona sehemu ambayo nilifeli mimi kama raisi wa hili taifa”
“Mheshimiwa samahani, unamaanisha kwamba ulikuwa unataka kuanza kunichunguza mimi”
“Mpaka sasa unatakiwa kuchunguzwa kwa sababu sina imani kama naweza kukuamini tena Othman” mkurugenzi alijisikia hasira kali mno, ni siku hiyo ambayo alitoka kuhakikishiwa kwamba hata huyo raisi alikuwa ni miongoni mwa wale washenzi ambao walikuwa wanalihujumu taifa ambalo yeye alikuwa analipambania halafu muda huo alikuwa anaambiwa ujinga na raisi huyo huyo.
“Mimi niliapa kukulinda wewe kupitia hatari za nje, niliapa kulilinda taifa hili na kulipigania pindi liingiapo kwenye hatari kubwa lakini hakuna sehemu hata moja ambayo niliapa kuyalinda maslahi ya mtu binafsi mheshimiwa, hili ni jambo ambalo hautakiwi kulisahau hata siku moja unapo ingia ndani ya ofisi yako”
“Whaaaaat! Unamaanisha kumlinda mke wangu ni kuyalinda maslahi binafsi? Unatamani kufa Othman?” raisi alifoka kwa hasira macho yakiwa mekundu vibaya mno.
“Huenda upo sahihi kuniambia kwamba mimi nilikuwa kuku mgeni ila kwa sasa nimekuwa mwenyeji, najitawala, nastahili kufungwa kamba tena jambo ambalo mimi na wewe wote tunajua kabisa kwamba haliwezi kutokea mheshimiwa labda kama utaamua kuyatumia madaraka yako vibaya kulazimisha hilo sawa kwa sababu wewe ni raisi unaweza kufanya hilo. Lakini jambo la msingi ambalo limenileta hapa sio kifo cha mke wako bali sababu iliyo nyuma ya kifo chake inaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maisha yako binafsi”
“Unataka kusemaje Othman?”
“Kuna mambo mengi ya hovyo ambayo huwa unayafanya ila huwa siwezi hata kukwambia kwa sababu wewe ndiye bosi wa taifa hili, najua unaweza kufanya lolote utakalo kwa sababu taifa ni lako lakini mambo yote hayo mimi huwa nakulinda na mara kadhaa nimetengeneza mpaka taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari ili uwe salama na jina lako lisiwe baya kwa wananchi ila kilicho nileta leo hapa kwako ni kutaka kujua kama kuna mambo yako binafsi ambayo unahisi kwamba siyajui na napaswa kuyafahamu kabla mambo hayajaharibika zaidi ya hapa kwa sababu bila kujua kumbuka sitakuwa na uwezo wa kukulinda lolote likitokea na lawama zitakuja kwangu kama ambavyo wewe unanilaumu hapa”
“Kuna kitu gani ambacho unakifahamu Othman kuhusu mimi?”
“Ndiyo maana nipo hapa ili niweze kukifahamu kutoka kwako mwenyewe”
“Umekutana na nani ambaye amekulisha hii sumu?”
“Kama ningelishwa sumu basi nisingekuwa hapa muda huu mheshimiwa, nimekuja kukwambia na kutaka kujua ukweli kwa sababu inaweza kuwa njia pekee ya sisi kumaliza jambo hili. Najua viongozi wengine wanaogopa kukwambia ukweli kwa sababu unaweza ukazibeba nafasi zao ama kuwaua, mimi nipo tayari kwa hilo ila sipo tayari taifa liangamie kwenye mikono yangu nikiwa natazama, watu wanakufa kila siku, mauaji imekuwa kama kawaida siku hizi, viongozi kila siku wanapotea kwa sababu ya makosa ambayo yalifanywa huko nyuma ndiyo maana nataka kujua kama kuna jambo ambalo silijui kuhusu wewe napaswa kulijua ili nianze upya hesabu zangu kuhakikisha nalirudisha taifa kwenye hali yake ya mwanzo”
“Unataka kuniambia unahisi raisi wa nchi nahusika kulihujumu taifa langu mwenyewe?”
“Hakuna sehemu ambayo nimetamka hivyo mheshimiwa”
“Ila una maana gani kuja kunidhalilisha na kunianza kunisanifu wakati mke wangu ndo kwanza hata hajapumzishwa?”
“Kwa sababu ndiyo njia pakee ya kulirudisha taifa kwenye njia yake ya mwanzo na hii inaweza kuwa namna bora ya kumfanya mkeo akapumzika kwa amani” Raisi alicheka kwa sauti kubwa, mezani kwake kulikuwa na bastola, aliibeba na kumnyooshea kiongozi huyo wa usalama ndani ya taifa lake.

54 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA TANO
SONGA NAYO................


“Nipe sababu ya msingi ya kunifanya nisikuue Othman”
“Kuhusu kufa mimi hata siogopi kikubwa tu tafuta sababu nzuri ya kuweza kuwadanganya viongozi ambao wengine hawaendani na sera zako kuhusu kifo changu na uhakikishe vijana wangu pia wanaelewa kwanini nilikufa kwa sababu najua wengi wapo kwenye mkono wako lakini nina vijana wangu ambao wananisikiliza mimi kuliko mtu yeyote yule kiasi kwamba wapo tayari hata kufa kwa ajili yangu. Najua unaweza ukawatafuta na kuwaua lakini mpaka unafanikiwa kuwaua wote tayari jina lako linaweza kuwa limechafuka hivyo kama una mpango wa kuniua hakikisha unatafuta eneo lingine la siri sio kuniulia Ikulu, damu yangu italeta matatizo mazito huko mbele, nina uhakika wewe ni mtu mwerevu kabisa na unalielewa hili” raisi alimwangalia kiongozi huyo ambaye ni yeye alimuweka hapo, alikuwa anauwezo wa kumuua ndiyo lakini haikuwa sawa, maneno ambayo aliambiwa yalikuwa na mashiko, aliishusha bastola yake akiwa anamkadiria.
“What do you want?”
“Nataka kujua kama na wewe upo kwenye uhusika wa hii kesi ya Gavin Luca”
“Hapana”
“Wakati nazitafuta taarifa za historia ya mtu huyu jina lako limejitokeza mheshimiwa, kabla ya kufanya maamuzi yoyote yale nimeamua kuja kwako kwanza ili nisije nikakuingiza zaidi kwenye matatizo nijue namna ya kudili na hii kesi. Jina kujitokeza sehemu mbili tofauti ni hali ya hatari hii na haionyeshi kama hili jambo lipo sawa kama ambavyo wewe unanijibu hapa. Unawajua vijana wangu, hakuna taarifa ambayo watashindwa kuipata na ndani ya masaa ishirini na manne naweza kuwa na taarifa zote mheshimiwa, hilo unatakiwa kulijua mapema”
“Hizi taarifa umezipatia wapi?”
“Unamkumbuka waziri mkuu wa zamani wa Tanzania, mr Hassan?”
“Ndiyo jina lake lilikuwa maarufu kipindi kile cha madawa ya kulevya nchini hivyo siwezi kulisahau”
“Yule mimi ni rafiki yangu mkubwa wa maisha ambaye aliamua kupotea kwenye maisha yangu. Mtu yule alinipa nafasi ya kuja kuonana naye mara moja kwa maisha ya baadae na wakati ambao wewe unanipigia simu nilienda kuonana naye” raisi alibaki kama bado haamini kilichokuwa kinazungumzwa mezani wakati huo.
“Bado yupo hai?”
“Ni mzima wa afya kabisa, anajua mambo mengi kuhusu wewe na ndiye amenihakikishia kwamba ili kulilinda taifa hili natakiwa kuanza kwanza na wewe kabla ya kwenda kwa mtu mwingine yeyote yule”
“Yeye ni nani kwenye hii kesi ambayo unaifuatilia?”
“kwa sababu yule ndiye babu yake na Gavin Luca”
“Noooo, noo, nooo hii haiwezi kuwa kweli”
“Yule ni rafiki ambaye nimekua naye, ila hata mimi sikuwahi kulijua hilo mpaka siku ya leo ndipo nimefanikiwa kufahamu kuhusu hili, nimefahamu kwa kuchelewa lakini haiondoi uhalisia kwamba jambo hili ni la kweli na kila kitu ni sahihi”
“Kivipi iwe hivi?”
“Hassan alikuwa na mtoto wa kike ambaye alikuwa anaitwa Glady, mtoto yule ndiye alikuja kuwa mke wa yule mfanya biashara wa dawa za kulevya sasa wakati mambo hayo yanatokea waliifanya mkuwa siri na yule mwanamke ndiye alijifungua wale watoto wawili mapacha nd….”
“Samahani, umesema mapacha?”
“Ndiyo”
“Ukiwa na maana ipi?”
“wale walizaliwa wawili, hakuzaliwa mmoja. Kipindi hicho wakati familia yake inavamiwa aliye uawa ni mwenzake na huyu ambaye ndiye Gavin ndiye alibaki hai hivyo hawa watu wote ambao anawatafuta na kuwaua kikatili ni wale watu ambao walihusika kwenye suala zima la kuiteketeza familia yake. Kwa taarifa ambazo nimezipata ni kwamba hata kama mtu alihusika kwa udogo mno hawezi kumuacha hai na ataondoka mwenyewe pindi tu atakapo maliza kuwaua hawa watu wote”
“Huyo babu yake yuko wapi?”
“Sijui alipo”
“Umetoka kuonana naye halafu unaniambia kwamba haujui alipo?”
“kwa sababu nimefika huko kwa hatua na watu ambao wamenibeba walinifunika uso ila nina ukakika ni hapa hapa Dar es salaam ila kujua ni wapi ni ngumu”
“Huyo babu yake anatakiwa kupatikana haraka sana”
“Halafu?”
“Atahukumiwa kwa makosa mengi kwa sababu hata yeye anatakiwa kuwajibishwa kwa ule uhusika wa kwenye kesi ya yule muuza madawa ya kulevya kwa sababu kama aliruhusu mwanae akaolewa na mtu yule basi ana majibu ya mambo ambayo yalitokea kipindi kile ndiyo maana anatakiwa kupatikana”
“Hukuwa ukijua lolote kuhusu mtu huyu saivi ghafla tu unadai kwamba anatakiwa kupatikana?”
“Hiyo ni kazi yako kutafuta taarifa kama hizi Othman hivyo umetekeleza wajibu wako nami kama raisi ni kazi yangu kuhakikisha watu kama hawa hawaendelei kuwepo mtaani kusababisha hatari kubwa zaidi”
“Nadhani kwa sasa unapaswa zaidi kuyahofia maisha yako bosi wangu kuliko kuanzisha hizo kesi zingine ambazo hata hatujui mwisho wake utakuwaje. Jambo lililo nileta ni hilo, nilitaka kupata uhakika kama unahusika kwenye hili jambo ili nijue namna ya kukulinda kwa sababu sitapenda raisi wa nchi apate matatizo kwenye uongozi wangu. Kama hauna tatizo lolote wala huhusika kwenye hili basi sina haja ya kuhofia kabisa kuhusu usalama wako ila kama kuna kitu hauniambii kiongozi ukumbuke kabisa kwamba sitaweza kukulinda kwa sababu sitajua naanzia wapi. Uwe na usiku mwema mheshimiwa raisi wa Jamhuri ya Muungano”

Mkurugenzi aliinamna kutoa heshima kwa kiongozi huyo wa taifa lake na kutoka mpka nje ambapo alisimama nje ya mlango wa hiyo ofisi na kugeuka nyuma, aliuangalia kwa dakika nzima kisha akaamua kuondoka. Ndani raisi alihisi kuvurugwa, alipasua pasua vitu hovyo asielewe ni kipi alitakiwa kukifanya. Taarifa iliyokuja mezani wakati huo haikuwa njema kabisa kwake, ilikuwa ni taarifa mbaya mno kwanza alishangaa mtu anakuwaje anaishi kwa siri namna hiyo kiasi kwamba dunia ilisha msahau wakati alikuwa kiongozi mkubwa serikalini? Ilikuwaje mtu huyo akahusika kwenye jambo kubwa kama hilo na asijulikane? Lakini swali la msingi zaidi kwake ilikuwa ni kivipi awe ndiye babu yake na huyo mtu ambaye alikuwa hatari kwa taifa kwa wakati huo? Alipagawa.

Aliingia kwenye chumba kimoja kikubwa na kufungua kabati la siri, aliitoa simu moja huko na kuiwasha. Kulikuwa na namba moja ambayo alikuwa na tarakimu kumi na mbili. Aliipiga namba hiyo ambayo iliita mara ya kwanza ikakata, akakaa kwenye sakafu na kuegamia kabati akiwa ameishika kwenye mkono wake. Simu hiyo ilianza kuita, aliipokea kwa kiwewe mno.
“Kiongozi, naomba tuonane muda huu, hali imeanza kuwa mbaya sana. Nahitaji msaada wako” simu ilikatwa. Aliondoka kwenye hicho chumba kama vile anafukuzwa. Alipiga simu kwa walinzi wake waandae msafara kwa sababu alikuwa anatakiwa mahali muda huo kabla hakujapambazuka. Alihitaji kwenda kuomba msaada kutoka kwa mtu ambaye alionekana kumuogopa na kumheshimu isivyokuwa kawaida.



*****
“Valeria na Aurelia wanajuana kwa muda mrefu, wale hawajafahamiana leo wala jana mpaka kufikia hatua ya kuweza kuuana. Wawili hawa wote ni wazaliwa wa Dodoma, wagogo namaanisha, kwenye ukuaji wao hawakuwahi kuwa sawa tangu wakiwa wadogo nadhani mwanzoni ilionekana kama hali ya kawaida kwa sababu wanawake wengi huwa hawapendani lakini kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda ilikuja kuonekana kwamba wawili hao haukuwa wivu tu bali ugomvi wa kweli”
55 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA SITA
SONGA NAYO................


“Uhasama wao mkubwa ulisababishwa na kitu kidogo tu, wakiwa shule Valeria aliwahi kufanya kosa na Aurelia ndiye alikuwa dada mkuu wa ile shule hivyo alilifikisha lile kwa jambo kwa uongozi wa shule kitu kilicho sababisha Valeria kufukuzwa shule. Alitengeneza kisasi moyoni mwake juu ya Auleria na kuamini kwamba ungekuja kufika wakati alitakiwa kuja kulipa jambo lile”
“Baadae miaka ilienda na maisha yalikuwa yanaendelea kwenda kama kawaida mpaka pale ambapo wawili hapo walipokuja kufahamiana na kuonana baada ya kupoteana kwa kipindi kirefu. Mmoja alikuwa jeshini na mwenzake alikuwa ni mke wa kiongozi wa siasa ambaye ndiye raisi wa sasa lakini kipindi hicho ni kabla hajawa raisi wa taifa hili”
“Valeria aliitumia fursa hiyo kuanza kulipa kisasi ambapo alianza kumtengenezea matatizo Aurelia akiwa jeshini kwa kuhitaji kumuengua kwenye ile nafasi yake na jambo hilo hakuwahi kumshirikisha mtu yeyote hata mumewe hakuwahi kujua ambacho kilikuwa kinaendelea”
“Hali ile ilimfanya kuishi nyuma ya kivuli kwa muda mrefu japo fitina zake mpaka pale ambapo alikuja kuvuka mipaka kwa mwanamama huyo ndipo safari yake ya kifo ilipo anzia. Aurelia alimpoteza mumewe na mtoto wake, wawili wale walikufa ikiwa ni mpango wa THE IMMORTALS ambao na wewe ulihusika lakini siku ya ile familia yake inauawa mtu ambaye alipiga risasi alikuwa ni Valeria. Alitaka kuhakikisha mwenzake anaishi kwa maumivu ikiwa ni kama kisasi ambacho alikibeba kwa miaka mingi”
“Jambo lile liliyaleta maumivu makali mno kwa Aurelia, kama ambavyo unajua vita vya mtaani vinatakiwa kuishia mtaani yaani mnamaliza kama ambavyo aliye vianzisha ametaka basi hivyo hivyo naye Aurelia alihitaji kuja kuvimaliza. Hakutaka kumuua Valeria kwa uharaka namna ile ila ndiyo ilikuwa njia bora zaidi kuweza kufanya hivyo kwa sababu kulikuwa na ugumu wa kufanya jambo hili na hakutaka kabisa Gavin aelewe wala kumtumia, hili alihitaji kulimaliza yeye mwenyewe”
“Sasa hakutaka kuhusisha mkono wake moja kwa moja kuhusika kwenye hili ndiyo maana akaamua kukutumia wewe uweze kuhusika kwenye mauaji ya mke wa raisi, unayajua matokeo yake baadae?” mzee Hasheem alikuwa anampasha mkuu wa majeshi ambaye alikuwa makini kumsikiliza.
“Hapana”
“Kuna siku hili jambo litakuja kukugeukia kwa sababu lazima wakati anakupatia hii kazi kwa namna moja ama nyingine kuna ushahidi ameuandaa, unahisi itakuwaje kama raisi akija kujua kwamba ni wewe ambaye umehusika kuyabeba maisha ya mkewe kipenzi bwana Savato?” maelezo hayo yalimuamsha kwenye usingizi ambao alikuwa amelala kwenye akili yake. Alimtumia Sarah ili kujiweka kando lakini hata yeye alitumika bila kujua.
“Hawezi kunifanyia jambo kama hilo mimi”
“Ana walinzi wake ambao kama angeamua kuwatumia walikuwa na uwezo wa kufanya vile, unahisi kwanini alikutumia wewe?”
“Kwa sababu kuna mambo yetu binafsi ambayo tunajuana huko nyuma, alifanya vile ili aendelee kunilindia siri yangu”
“Unahisi ni hilo tu?”
“Ndiyo”
“Sijajua sababu ya msingi ya kwanini wewe unamuogopa yule mama lakini hatua zako ni za kipuuzi na siku moja zitakuja kukuingiza kwenye moto mbaya na huenda utakuja kukumbuka ukiwa umechelewa na hautakuwa na mtu wa kuja kumkimbilia. Mpaka sasa unajiweka kwenye hatari kubwa kwa viongozi wako, kuna kadi za mhimu unatakiwa uwe nazo kwenye mkono wako ili uweze kushinda hii mechi”
“Kadi zipi hizo?”
“Ya kwanza ni mimi hapa, mimi ndiye ambaye naweza kukufanya ukaishi maisha marefu, yule mama kukulea lea sio kwamba ameshindwa kukuua ila huenda kuna kitu ambacho wewe haukifahamu. Kumbuka baada ya kugundua kwamba mke wa raisi alihusika kuipoteza familia yake aliamua kumuua sasa sijui siku akikuamkia vibaya itakuwaje na mpaka wakati huu jiangalie usije ukaishia kwenye mikono ya Gavin. Nakuhakikishia hautafanikiwa kuliona jua kwa mara nyingine kama hali hii itajitokeza kwako”
“Ni kipi natakiwa kufanya kwa sasa?”
“Hautakiwi kufanya jambo lolote lile, tena kama unaweza usijihusishe kwenye mgogoro wowote ambao hauna ulazima”
“Hilo haliwezekani, mimi kama kiongozi mkuu wa jeshi lazima nihusike kwa ukubwa juu ya mambo yote ambayo yanaendelea ndani ya taifa”
“Inawezekana lakini kusiwe na uhusika wako wa moja kwa moja kwa sababu kama ukifanya hivyo unakuwa unajichimbia kwenye kaburi ambalo kwa baadae litakuja kutumika kukufukia wewe mwenyewe ukakosa pa kukimbilia”
“Mzee kuna kitu ambacho unakipigania mpaka unajitoa namna hii?”
“Mimi napigaia uhai wangu, nimeishi ile sehemu ambayo ni mbaya kwa muda mrefu, nimepata nafasi ya kuwa huku uraiani sitaki nirudi tena kwenye maisha kama yale hivyo nautumia muda wangu vizuri kwa sababu najua nimezungukwa na watu wa hovyo kama wewe”
“Kipi kinakuaminisha kwamba nitaendelea kukuweka hai?”
“Kwa sababu kwa sasa hauna sehemu nyingine ya kukimbilia na siku zote mtu ambaye hana upande wa kusimamia anakuwa kwenye wakati mbaya na mgumu kwani huelewei hata ambacho ni sahihi kwako. Sasa jifikirie muda kama huu ambao nina uhakika hata wewe haujui kabisa kwamba unatakiwa kusimamia wapi halafu uniue mtu kama mimi ambaye nina taarifa ulizo tumia miaka kuzipata, wenzako taarifa kama hizi wanazinunua kwa gharama kubwa lakini wewe unazipata bure”
“Mzee kama kuna siku nitakuja kugundua kwamba unanidanganya kuhusu hizi habari ambazo unanipa, basi niamini mimi nitakuua kwa mateso makali kiasi kwamba hautatamani kama ungekutana na mimi kabisa kwenye haya maisha yako marefu ambayo umeyaishi mpaka hii leo”

“Nisikilize kijana wangu, kuishi maisha marefu kunakufanya uone mengi, ushuhudie vitu vingi lakini pia inakufanya uwasome wanadamu wengi walivyo. Kwenye maisha yangu yote nimejifunza kwamba binadamu wengi huwa wanafanya makosa ambayo yanajirudia, angalia watu wengi ambao wamefeli kwenye maisha yao, wengi sababu ni zile zile ambazo ziliwafelisha wengine waliopita lakini kwanini wanayarudia makosa yale yale? Kwa sababu kutoka kwenye ule mstari wa makosa mpaka kusimama kwenye mstari ambao umenyooka ni kazi ngumu ambayo inahitaji moyo mgumu pia

Hayo makosa nayaona na kwako pia, wapo wengi ambao walikuwepo kwenye hiyo nafasi yako na sasa hawapo. Wengine walistaafu wenyewe, wengine waliuawa na wengine walifutwa kazi kwa sababu mbali mbali, kama unalielewa hilo basi unatakiwa kujua kwamba hiyo nafasi hata siku moja haitakiwi kukufanya ujisahau kabisa kwa kuhisi kwamba unamiliki kila kitu jeshini. Wewe hapo unaamini kwamba wewe ndo kila kitu kwenye jeshi, unahisi kama vile unalimiliki jeshi ila unasahau kwamba hiyo ni nafasi tu ambayo umepewa na anaweza kupewa mtu yeyote yule
Jeshi hata bila wewe litaenda vizuri tu ndiyo maana hata kabla hujazaliwa lilikuwepo na hata ukitoka kwenye hiyo nafasi ama ukifa bado litaendelea kuwepo bwana Savato, usisahau jambo hilo kila unapokuwa unajivuna na kuwa na majigambo kupitia jeshi”
“Bado sijaelewa dhamira halisi ya hayo maelezo yako”
“Maana yangu ni kwamba popote pale ambapo unaenda jitahidi usije ukawa unaiacha akili yako nyuma kwa sababu itakula kwako. Hii ni formula ambayo ni ya mhimu hata sokoni, kuna vitu viwili vya mhimu zaidi unatakiwa kujua uimara wa bidhaa yako sana lakini pia unatakiwa kuujua udhaifu wa bidhaa ya mshindani wako. Hivyo vitu ukivijua vizuri basi hakuna soko ambalo litakusumbua hapa duniani hata usipokuwa na mtaji utaingia popote
Ila kwa bahati mbaya wengi huwa hawajui kuhusu hilo na ambao wanajua huwa hawalizingatii kabisa kiasi kwamba huwa wanakumbuka pale mambo yakiwafika shingoni, nina uhakika haujanielewa bwana Savato kwamba sentensi hizi nimemaanisha nini?” mzee huyo aliongea akiwa anatoa tabasamu la masikitiko kwenye uso wake, mkuu wa majeshi alibaki ametulia tu kwa sababu aliambiwa ukweli kabisa, hakuwa amemuelewa.

56 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
Back
Top Bottom