Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA SABA
SONGA NAYO................

“Maana yangu ni kwamba wewe hapo haujui uimara wako uko wapi, unahisi kwamba jeshi ndiyo uimara wako jambo ambalo sio la kweli. Wale ni wanadamu ambao wananunulika mbele ya pesa, wakionyeshwa begi zilizo jaa wale wanakuuza mchana kweupe hivyo unatakiwa kuelewa uimara wako upo kwenye kichwa chako pamoja na kwenye rasilimali ulizo nazo. Moja ya rasilimali kubwa ambayo wewe unayo kwa sasa na unatakiwa kuwa nayo makini ni mimi hapa, hautakiwi kunipoteza bwana mkubwa
Lakini jambo la pili ni kwamba hujui udhaifu hata mmoja wa watu ambao unashindana nao na anguko lako lipo kwenye hili eneo ila kama utafanya vile ambavyo nataka mimi basi nitakusaidia kwenye hili. Umenikatili usingizi wangu naenda kupumzika tutakutana wakati mwingine kuweza kuelezana kwa mapana” mzee huyu alijikatia mapande na kujipa nafasi lakini wakati huo alinyanyuka na kuondoka hilo eneo ili aweze kwenda kulala.
Kulikuwa kumeanza kupambazuka, mkuu wa majeshi alibaki hilo eneo akiyatafakari yale maneno kisha nae akatoka nje kuweza kuondoka hilo eneo baada ya kuyapata majibu kadhaa ambayo aliyajia hapo.




*********
Ismail Mhammed alikuwa kwenye biashara zake, alikuwa na maduka ya jumla ya vifaa vya umeme ambayo mara nyingi alikuwa akipenda kuyasimamia mwenyewe kule Zanzibar, zilikuwa ni miongoni mwa biashara zake nyingi ambazo alikuwa nazo.
Ni siku kadhaa tangu mwanae Zara aweze kuuawa hakuwa ametembelea biashara zake yeye mwenyewe hivyo akaamua kwenda huko kuhakiki mahesabu yake na biashara zake zinaenda vizuri lakini siku hiyo akiwa anafanya hayo yote kuna mtu alikuwa anamfuatilia tajiri huyo kila sehemu ambayo alikuwepo, kuanzia ulinzi wake na kila shughuli ambayo alikuwa akijihusisha nayo kila dakika ambayo ilikuwa inaenda.
Hakuonekana kuwa mtu ambaye alipenda kuupoteza muda wake huenda ndiyo moja ya sababu ambayo ilimfanya kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa, muda ni mali bwana! Ukiupoteza hovyo basi nao utakudhalilisha mwisho wa siku, hakutaka kuwa mfano mbaya kwenye hilo ndiyo maana akafanya kila namna kuhakikisha kwamba jambo hilo linamuendea safi kabisa kama alivyokuwa amepanga yeye.

Slyvanos ndiye ambaye alipewa kazi ya kumteka mzee huyo na ndiye ambaye muda huo alikuwa anakula naye sahani moja kuhakikisha kwamba ndani ya muda mfupi uliokuwa unafuata alikuwa anarudi naye Dar es salaam. Aliifuatilia mizunguko ya siku nzima ya tajiri huyo mpaka alipokuwa na uhakika na hesabu zake, akasubiri jua lizame ndipo atekeleze jambo lake huku akiwa makini kuhakikisha kwamba hakuna hatua hata moja ambayo anaifanyia jambo la kijinga la kumuingia kwenye matatizo kabisa.

Saa tatu kasoro usiku mzee huyo alikuwa ndani ya gari yake na walinzi wake wawili ambao alikuwa akitembea nao mara nyingi. Zanzibar kulikuwa na amani tele, hakuwa na haja ya kutembea na kundi la watu kwa ajili ya usalama wake huenda ni moja ya sehemu ambayo alifanya kosa kujipa imani ya namna hiyo. wakiwa wanatembea kuelekea kwake, kuna sehemu walikutana na toroli barabarani, ikamlazimu dereva kusimamisha gari kisha mlinzi mmoja akashuka kwenda kuangalia sababu hasa ya lile toroli kuwepo pale.
Alishangaa kukutana na mwili wa mtu basi ikabidi awaite wengine mpaka bosi wake, walisogea pale kwa pamoja, lilikuwa kosa. Yule mwanaume ambaye alikuwa ndani ya lile toroli mithili ya mtu aliyekufa alinyanyuka ghafla tena kwa kasi kubwa na kutua kwenye shingo la mwanaume mmoja, alizamisha sindano na kugeuka na kiganja ambacho kilitua kwenye shingo ya mwingine wote wakazima.
Alibaki dereva na tajiri mwenyewe ambaye alitaka kukimbia, dereva alirushiwa sindano ya shingo akadondoka hapo hapo akiwa anakoroma kwa mbali, akawa amebaki tajiri.
“Nakukumbuka wewe, ulikuja nyumbani ukidai ni afisa upelelezi, ndivyo mnatumwa kuifanya kzi yenu kwa namna kama hii tena kwa mtu kama mimi?”
“Mzee sina muda wa kukueleza sababu za mimi kuwepo hapa lakini ni wakati wa mimi na wewe kuondoka pamoja kwa amani”
“Unajua madhara ya kuja kunivamia mtu kama……” hakumaliza sentensi yake, aliguswa kwenye shingo yake akapoteza fahamu. Slyvanos aliwabeba wale vijana wa yule mzee na kuwapakiza kwenye gari kisha akampakiza na mzee huyo akaondoka naye kuelekea bandarini, boti ilikuwa imeandaliwa hivyo hakuwa na muda wa kusubiri tena alitakiwa kuwahi Dar es salaam. Alilitelekeza gari hilo karibu na bandarini huku akitokomea na tajiri huyo kama ambavyo maelekezo yalikuwa yanamtaka afanye.

Mzee huyo alikuja kushtuka baadae sana shingo ikiwa inamuuma, alijihisi uchovu kwenye mwili wake ila hakujua alikuwa wapi kwa wakati huo. Macho yake yalikuwa yamshawishi kuendelea kulala lakini hakuwa na huo uwezo wa kufanya hivyo ingali hakuwa na uhakika kabisa na usalama wake. Aliangaza kila kona ya sehemu ambayo alikuwepo, kilikuwa ni chumba kikubwa kilichokuwa na baadhi ya vifaa vya kuhesabu huku sehemu kubwa ikiwa ni meza na viti viwili ambapo yeye alikuwa amekalia kiti kimojawapo.
Ndipo kumbukumbu zake zilipo rejea vyema namna alivyoweza kufikishwa ndani ya hilo eneo, aligundua kabisa kwamba alikuwa ametekwa ila sababu za kutekwa na kuwekwa hapo bado hakuwa amezipatia jibu lake. Kutekwa kwake kulikuwa ni ishara mbaya kwani kama watu hao wangehitaji kuzungumza naye kwa amani basi wanemfuta nyumbani kwake kama ilivyokuwa mwanzo.

Nje ya hapo alipokuwepo, kuna watu walikuwa wanamwangalia kwa umakini mkubwa, walikuwa ni THE INVISIBLE wenyewe, walikuwa wanaisoma akili yake kwa namna alivyokuwa anahangaika kuweza kuyapata majibu sahihi ya kile kilichokuwa kinaendelea.
“Huyu lazima kuna mambo atakuwa anayafahamu, ana wasiwasi mno”
“Huenda ni wasiwasi baada ya kukamatwa”
“Sidhani, watu kama hawa kukamatwa kwao sio tatizo kubwa sana kwa sababu anajua hawezi kumaliza masaa ishirini na manne atakuwa huru ila sababu ya yeye kuwepo hapa huenda ndiyo inampa wasiwasi mkubwa”
“Unahisi anaweza kusema ukweli ambao tunauhitaji?”
“Sina uhakika na hilo labda mpaka tukipata sababu ya msingi ya kumtishia mpaka aweze kusema ukweli kabla muda haujaisha. Yakifika masaa ishirini na nne hajaonekana popote lazima habari zitasambazwa kila kona juu ya kupotea kwake”
“Ikiwa na maana kwamba tumebakiwa na masaa ishirini tu kuhakikisha tunapata tunacho kihitaji”
“Ndiyo lakini pia kumuachia kirahisi ni tatizo kwetu, vipi kama ikijulikana kwamba tulikuwa naye halafu Gavin akampata? Si tutakuwa kwenye skendo mbaya sana ya kuteka watu”
“Kama angekuwa anamtaka nina uhakika mpaka sasa angekuwa amempata”
“Kama anajua alihusika kwanini asiwe amemkamata au kumuua mpaka sasa?”
“Kuna uwezekano mkubwa huyu anatumika kama chambo kuwapata samaki wakubwa. Lengo lake sio huyu ni wale ambao wapo nyuma yake. Amewaua wengine huenda kwa sababu sio mhimu sana kama huyu, kama huyu ni mhimu kwake maana yake kuna sababu kubwa ya yeye kumuacha hai mpaka wakati huu. Hivyo tunatakiwa kujua kwamba ni kwanini hajamuua yeye, kwanini alimuua mwanae halafu tujue watu ambao wapo nyuma yake huenda ndio hawa watatupa muongozo sahihi wa hatua ambayo tunatakiwa kuifuata mbele kabla hayajatokea madhara mengine huko mbele”
“Nadhani hilo ndilo jambo la msingi kwa sasa, sasa nani atamhoji?”
“Nitaongea naye mwenyewe” Dayana aliongea akiwa anaanza kuzitupa hatua zake kuelekea kwenye kile chumba ambacho yule tajiri alihifadhiwa. Walikuwa wanafanya maongezi yao juu ya hatua ambazo walitakiwa kuzifuata lakini walielewa kabisa kwamba walimkamata mtu huyo kwa nguvu hivyo walivunja haki zake za msingi kisheria na kama jambo hilo lingefahamika lingewaletea sifa mbaya huenda hata kusimamishwa kabisa kazi lakini hawakuwa na namna, huyo bwana alikuwa ni mhumu sana kwa wao kuweza kuzuia kila lililokuwa linaendelea nchini kwa wakati huo.

Akiwa anaendelea kutafakari sehemu aliyokuwa ameishia tajiri Ismail, alihisi kuna mtu anakuja humo ndani. Ni baada ya mlango kuguswa na kitasa kunyongwa taratibu, mbele yake alimuona mwanamke mrembo isivyo kawaida, alimeza mate akiwa haamini kama alikuwa hilo eneo kwa ajili ya kuonana na mwanamke ambaye hakuelewa alikuwa na lengo naye lipi. Mwanamke huyo alikuwa ameva suti ya blue huku koti la suti likiwa wazi, lilikuwa limepenya mpaka ndani kabisa ya kifua ambapo palikuwa na shati jeupe lililokuwa limeyachora maziwa yake saa sita kwa ufasaha zaidi.

57 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA NANE
SONGA NAYO................
“Wewe ni nani bibie na kwanini nipo hapa kinguvu?”
“Usiwe na haraka ya kuhitaji kunijua mimi, kwanza nataka nikukumbushe historia yako. Miaka kumi na mitano iliyopita wewe uliingia kwenye orodha ya majina ya wahalifu ambao walikuwa wanatafutwa sana kwenye taifa hili, unakumbuka ni kwanini uliingia huko?” Dayana swali lake lilikuwa la mtego lakini tajiri huyo lilimchanganya, hakuelewa binti huyo alikuwa na maana ipi kuuliza hilo swali.
“Kwanza natakiwa kujua nipo wapi, bila shaka kwa swali lako wewe ni mtu wa usalama na unajua kabisa ni kosa kisheria mimi kuwa hapa bila taarifa hivyo kama kuna ulazima wa mimi kuongea na wewe hakikisha unampigia simu mwanasheria wangu”
“Uhalifu wako ulikuwa ukihusiana na wewe kuhusika kwenye biashara haramu ya kusafirisha viungo vya binadamu na kutakatisha fedha. Kesi hii iliibuliwa na afisa mmoja wa polisi Zanzibar ambaye alikujulikana kwa jina la Ashrafu, hii kesi baadae ikaja kufutwa kwa amri ya jaji mkuu Emilia Clark ambaye ameuawa kwa sasa. Lakini haukuishia hapo bali pia ulimuua yule afisa wa polisi na familia yake yote kwa kukuingiza kwenye skendo chafu, kwa sababu bado jaji mkuu alikuwa upande wenu basi ile kesi hakuna mahali ilipelekwa, mzalendo yule akakosa haki yake ya msingi na kuishia kufa halafu mpuuzi mmoja kama wewe upo mpaka leo unadunda. Unaelewa maana ya haya yote?” Dayana alilipuuzia swali la tajiri huyo na kumpa machache kuhusu yeye ambayo alikuwa akiyafahamu
“Hahaha hahahaha hahaha bibie nina imani utakuwa haupo timamu kuanza kutengeneza kesi zote hizo ambazo hazina uhalisia wowote na hazijawahi kunitokea kwenye maisha yangu yote. Kama ningekuwa nafanya haya mambo basi mpaka leo nisingekuwa uraiani muda huu”
“Sipo hapa kutaka ukubali kuhusu hilo, jambo ambalo nalihitaji ni muunganiko wa haya mambo kwa sababu kwa hesabu zangu ni kwamba hata wewe umebakisha siku kadhaa tu jina lako liweze kubadilika kuwa marehemu”
“Unanitisha mimi?”
“Wala sikutishi, nipo hapa kutaka kujua ukweli ambao unaweza kuwa msaada wa kukulinda hata wewe pia”
“Hahahaha hahahaa hahah wewe hapo ndo unadai unataka kunilinda mimi?”
“Naonekaan kama nakuchekesha mzee?”
“Huna lolote binti, wewe muda huu ulitakiwa uwe unamkatia kiuno bwana yako kitandani” hiyo kauli ilimuuma sana Dayana, alinyanyuka na kwenda kuufunga mlango, wakati anafunga wenzake walishtuka na kuhitaji kuuwahi lakini walichelewa. Alisogea kwenye kamera na kuiangalia kwa umakini akijua wazi kwamba wenzake walikuwa wakimtazama kwa nje, alivuta kisanduku kimoja na kwenda kukitua pale mezani hali ambayo ilianza kumpa mashaka Ismail.
“Ni kweli mzee wangu, huenda mimi natakiwa kuwepo kitandani kumkatia bwana angu viuno muda huu lakini kwa bahati mbaya mimi ni miongoni mwa watu wachache ambao hawalali kuhakikisha tu taifa linakuwa salama kutoka kwa watu wazandiki kama wewe. Unajua kwanini nimefunga ule mlango?” aliongea akiwa anamzunguka zunguka mzee yule ambaye hakuwa na jibu la kuweza kumpa.
“Kwa sababu mimi huwa sijui mambo ya fair Play, habari za viungo kwenye mpira mimi sina hizo mambo. Kuna watu wanatutazama nje hapo, wale wanajua kabisa njia ambazo huwa nazitumia kupata kile nakitaka kwa mtu na njia zangu hazijawahi kuwa na mwisho mwema hivyo kama mlango ungebaki kuwa wazi maana yake ni kwamba wangekuja hapa kunizuia nisikuumize ila kwa sasa hawawezi kuingia tena humu ndani mpaka nimalize kazi yangu na kama watatumia njia ya ziada basi ni dakika thelathini ambazo bila shaka mimi na wewe tutakuwa tumemaliza mazungumzo yetu kwa sababu natarajia yatakuwa mafupi na sahihi”
“Bibie una familia au mtoto labda?”
“Ndiyo njia ambayo huwa mnaitumia kutishia watu ambao wanaingia kwenye maslahi yenu sio?”
“Kwa sababu nitakifuta kizazi chako chote, haujui aina ya watu ambao unaingia nao kwenye hii ligi bibie, bosi wa bosi wako analijua hili ndiyo maana wenzako wamekaa pembeni muda wote sio kwamba hawajui ila wanaheshimu mipaka ambayo wamewekewa. Jiangalie kwa sababu kuna wanaume wana hamu ya kuwaingilia wanawake wa aina yako. Hahaha hahahah hahahaa” bwana huyo licha ya kuonekana kuwa mtu wa dini lakini bila shaka ndani yake kulikuwa na ushenzi ulio tukuka na wakati huo alianza kuudhihirisha waziwazi.
“Utatamani ungenisikiliza mapema” Dayana aliongea akiwa analivua koti lake na kuliweka ukutani na kuikunja shati yake. Mzee huyo hakuwa anamjua mwanamke huyo, huenda angeelewa sababu ya yeye kuwa ndiye kiongozi wa kundi lililo jaa wanaume basi angekuwa anaongea naye kwa heshima kubwa. Dunia ilikuwa inaenda kumpa somo la maisha.

Dayana alichomoa praizi na mkasi, alimwangalia mzee huyo usoni akiwa anatabasamu, mzee huyo naye alikuwa anamwangalia kwa dharau lakini sura yake ilibadilika ghafla baada ya kushtukizwa bila kutarajia. Mkasi ulizama kwenye kidole kwa nguvu kama mtu anausimika kwenye udongo, praizi ilizamishwa kwenye kucha na kuanza kuing’oa kwa lazima huku akiwa anazungusha zungusha ili kumpatia maumivu. Mzee Ismail alipiga makelele kama mtoto mdogo mpaka inang’ooka alikuwa ameshusha machozi na kamasi zilikuwa zinachuruzika.
Dayana aliviweka vyote mezani na kusogea nyuma akainamia kwenye siko la mzee huyo.
“Bila shaka kwa sasa tunaweza kusikilizana vizuri na kuongea kiutu uzima sasa maana tulikuwa hatujuani mwanzo na sikulaumu kwa hilo” aliongea akiwa anairushia mezani picha kubwa, sura ilikuwa ni ya Gavin Luca, mzee huyo alipatwa na wasiwasi mwingi baada ya kuiona hiyo picha mbele yake.
“Ninajua kwamba wewe ni miongoni mwa wahusika ambao wanatafutwa sana na huyo bwana, kuna mambo ambayo mliyafanya miaka ya nyuma huko ambayo mliudanganya ulimwengu na watu wakawaamini. Leo hii kupitia mambo hayo mmejichumia utajiri wa kutosha lakini mwenye vyake amekuja kukusanya kila deni ambalo mlilikopa wakati huo sasa nina mambo machache ambayo nahitaji kuyajua kwako” Dayana alikuwa amebadilika mpaka sura, alitulia na kumsoma mzee huyo usoni ambaye alikuwa ana presha, ilionekana kwa jinsi alivyokuwa akizivuta pumzi zake.
“Nataka kujua kwamba ni nani anayefuata baada ya hapa, nataka kujua aliye muua Emilia, nataka kuijua sababu ya msingi ya wewe kuwa hai mpaka sasa wakati huna ulinzi wowote wa maana na nataka kujua sababu ya kwanini mtu huyo alimuua binti yako na sio wewe” maswali yalikuwa yanaeleweka vizuri na hata mzee huyo aliyasikia kwa usahihi kabisa.
“Nasikitika kwamba hakuna swali hata moja ambalo naweza kukujibu hapa binti yangu”
“Mimi sio binti yako, unahisi nipo hapa kukubembeleza?”
“Hayo maswali yapo nje ya uwezo wangu”
“Inaonekana haupendi amani kabisa” Dayana aliongea akiwa anatoa mashine ndogo ya kutindulia, ilikuwa inaweza kutindua hata miamba, ilitakiwa kuzama kwenye mwili wa mzee huyo. Alibaki akihaha na kuhema kwa nguvu kwa sababu alijua hatua zilizokuwa zinafuta.
“Kama nikisema lolote basi lazima nife na familia yangu itauawa”
“Hakuna mtu atajua kuhusu hili, haya ni makubaliano ambayo wewe unaingia na shirika la kijasusi la taifa hili”
“Hauelewi binti, hawa watu wapo kila sehemu, wapo na watu kila kona ya sehemu nyeti kwenye taifa hili hata humu ndani huenda lazima kuna mmoja wao yupo nao sasa unaniaminisha vipi kwamba hili litabaki baina yangu mimi na wewe? Sioni kama hili lina maana yoyote kwa sasa”
“Kama ni hivyo basi hakuna haja ya makubaliano na mimi, utatakiwa kusema tu kwa sababu hauna chaguo, kumbuka kwamba hakuna mtu hata mmoja ambaye anajua kwamba wewe upo hapa hivyo tunaweza kukufanya lolote lile”
“Una uhakika kwamba hakuna mtu anajua kwamba nipo hapa?” ile kauli ilimshtua Dayana, ni kama hakumuelewa mzee yule.
“Una kifaa kwenye mwili wako?”
“Ndiyo, yakipita masaa saba bila kujulikana kwamba niko wapi basi lazima nitaanza kutafutwa na hapo watajua sehemu nilipo” Dayana alitabasamu, wau hao walikuwa wamejipanga kwa kila kitu.
“Safi kabisa kwa sababu bado kuna masaa matatu mpaka watu hao waweze kukushtukia kwamba haupo, kwa maana hiyo mimi na wewe tuna muda mrefu wa kuwa pamoja humu ndani” mzee huyo alimeza mate kwa shida kubwa akiwa hana ujanja zaidi ya kutoa ushirikiano kwa watu hao.

58 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA TISA
SONGA NAYO................


“Emilia ni watu wetu walimuua”
“Watu wenu?”
“Ndiyo”
“Wewe na nani?”
“Hili jambo ni zito sana sidhani hata kama unatakiwa kulijua”
“Ndiyo maana nipo hapa kwa sababu nahitaji kulijua”
“The Immortals”
“Ndio akina nani?”
“Huu ni mtandao mzito ambao ndani yake una watu wengi mno, wapo mpaka viongozi wakubwa wa taifa hili”
‘Unamaanisha kama raisi na mkuu wa majeshi?”
“Umezipatia wapi hizi habari?”
“Unahisi muda wote sisi tunakuwa tumelala na hatuoni kinacho endelea?”
“Kama ni hivyo kwanini upo kunihoji hapa?”
“Kwanini walimuua Emilia?”
“Kwa sababu alikuwa na siri nyingi mno na yule alikuwa mtu wa wazi, taarifa za Gavin Luca kuendelea kuwa hai hazikuwa njema kabisa ndiyo maana ikalazimika Emilia kuuawa ili siri zibaki kuwepo kwa sababu kama angepatikana yule basi kuna mambo mengi angeweza kuropoka ambayo yasingewafurahisha wakubwa”
“Ilikuwaje watu hawa wakajua Gavin Luca yupo kwa takribani miaka mitano iliyopita halafu hawakuwahi kuonekana kuwa na usiriasi na jambo hili kiasi kwamba akawa analisiamamia mkuu wa majeshi mwenyewe?”
“Kwa sababu kila mtu alikuwa ana uhakika kwamba mtu yule alikufa, huyu mwingine ambaye alianza kujiita hilo jina iliaminika kwamba ni mtu tu ambaye aliamua kupita na upepo kwa kujifanyia upasuaji ili afanane na bwana yule hivyo hakuna mtu ambaye amewahi kuchukulia kwa uzito kwa sababu mhusika tuliamini amekufa”
“Kipi kiliwapa uhakika kwamba alikuwa amekufa?”
“Kwa sababu aliye muua aliye muua alituonyesha picha na video zake”
“Huyo mtu ndiye huyo Douglas Shenzi?”
“Ndiyo”
“kwa sasa ni jambo gani linaendelea baada ya kuwa na uhakika kwamba bado anaishi?”
“Tunasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa juu”
“N hao viongozi wa juu ni akina nani?”
“Siwajui”
“Haiwezekani usiwajue viongozi wako”
“Sijawahi kuwaona hata siku moja, huwa tunaenda kwenye mkutano tu lakini anaye tupa amri hatumuoni, huwa tunasikia sauti yake tu”
“Hiyo sauti umewahi kuisikia mahali popote?”
“Hapana”
“Na raisi ana nafasi gani huko?”
“Raisi huko ni kibaraka kama mimi tu”
“Unataka kusema kwamba raisi sio miongoni mwa watu wa juu huko?”
“Hapana, hata yeye anapokea amri na ndiyo watu ambao wamemuweka pale Ikulu na wana uwezo wa kumtoa hata leo wakiamua”
“Mnakutana tena lini?”
“Walisema tujiandae muda wowote kuanzia sasa ila hatujui”
“Mkutano huwa mnafanyia wapi?”
“Sijui”
“Kila kitu haujui?”
“Kwa sababu huwa tunafungwa macho tukifika bandarini, tukifika mahali tunabebwa na halikopta ila kiualisia sijawahi kujua kwamba ni wapi”
“Mpango wenu wa sasa ni upi?”
“Bado sijajua ila nahisi ni huu wa kumpata huyu mtu kwa gharama yoyote ile”
“Kwahiyo hata viongozi wenu waliamini kwamba huyu mtu amekufa?”
“Sina uhakika juu ya hilo”
“Kwanini wewe hauna ulinzi wa maana na bado mtu huyu hajakujia? Kwamba hakufahamu?”
“Sijajua sababu ya yeye kutokuja kwangu ila kuja kwangu litakuwa ni kosa kubwa analifanya nadhani hata yeye analitambua hilo”
“Ndiyo maana alimtumia binti yako kama kitisho kwako?”
“Ndiyo japo mpaka wakati huo sikujua kama yupo hai”
“Kuna uhusiano wowote wa binti yako na haya mambo yako ambayo unayafanya?”
“Ndiyo”
“Anahusikaje?” hilo swali lilimfanya mzee huyo aanze kusita sita
“Yeye ndiye alikuwa anasimamia biashara zangu” Dayana alibaki anashangaa
“Huyu mwanao alisemekana kwamba alipotea miaka miwili ambayo ilikuwa imepita”
“Hapana hakuwahi kupotea, ni mimi ambaye nilitengeneza huo mchezo kwa sababu mwanangu muda wote alikuwepo Zanzibar”
“Kwanini ulifanya hivi?”
“Biashara muda mwingine inahitaji maamuzi magumu sana kuweza kufanikiwa”
“Kuna sababu ipi ya msingi kiasi kwamba umtoe sadaka mwanao? Kwa sababu hiyo sababu ambayo unanipa hata hainiingii kabisa akilini”
“Nilihitaji mtu wa kuweza kumrithisha biashara zangu, watoto wote walionekana kuwa na moyo mlaini na binti yangu ndiye alionekana kuwa shujaa kati ya wanangu wote hivyo nilimuita mezani kuweza kumwelekeza kila jambo. Nilifanya hivi kwa sababu nilijua kuna siku naweza kufa na kupotea ghafla hivyo bila kuweza utaratibu wa kueleweka lazima mali zingekuja kupotea kwa kukosa usimamizi wa kueleweka hali ambayo ingekuja kuifanya familia yangu kuishi maisha magumu kwa baadae”
“Unamaanisha ni wewe uliandaa hata mpango wa kufa kwake?”
“Hapana, nisingetumia miaka yote hii kumuandaa ili nije kumuua, hakuna mzazi mpuuzi duniani ambaye anamuua mwanae kwa mkono wake afisa. Umeuliza swali la kipuuzi sana”
“Sasa mwanao alikufaje?”
“Sina jibu la hilo swali kwa sababu hata mimi natamani kwamba ningekuwa na majibu yake ila mpaka sasa sijui”
“Wakati mwanao anakufa kuna kitu alikwambia kabla?”
“Hapana”
“Yule mtu alionekana kuwa mpenzi wake mpaka wanaingia hotelini. Kwanini hakumuulia nje akasubiri waingie hotelini ndimo akatekeleze jambo hilo”
“Sina majibu sahihi juu ya hilo”
“Huna majibu au hutaki kunijibu?”
“Kwa sababu ile hoteli ni yangu”
“Ni hoteli yako?”
“Ndiyo”
“Binti yako alikuwa analijua hilo?”
“Hapana”
“Ulikuwa unajua kwamba ana mpenzi mpya?”
“Hapana”
“Alikuwa analindwa?”
“Ndiyo”

59 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA SITINI
SONGA NAYO................



“walinzi wake wako wapi?”
“Mpaka sasa sijui walipo kwa sababu hawakupatikana tena baada ya lile tukio”
“Kama Gavin ni mwenyewe alifanya lile tukio kwanini hakukujia wewe moja kwa moja akamtumia mwanao?”
“Nahisi huenda anajua kila kitu kuhusu mimi”
“Unamaanisha nini?”
“Baada ya kutokea huyo mtu ambaye sisi kwa mara ya kwanza tuliamini kwamba anajifanya kuwa Gavin, ulitengenezwa mtego wa kuja kumkamata kama itafikia hatua akawa hatari kwa kundi hili. Ilijulikana kwamba kuna siku taarifa zangu zinaweza kuvuja na kama zikivuja basi mimi nitakuwa kawaida tu bila ulinzi mkali, sababu hiyo ingemfanya mtu huyo kujileta kwangu bila mahesabu maana yake ambapo angejileta kwangu basi angekuja kukamwatwa kirahisi tu kwa sababu ingekuwa ni kama kujitokeza hadharani. Anajua hili ndiyo sababu hajawahi kunifuata mimi”
“Kama ni hivyo, kwanini amuue binti yako?”
“Binti yangu alirithi kila kazi yangu chafu ambazo alikuwa anazifanya kwa niaba yangu, mimi nilikuwa nampatia kila kitu lakini sikuwahi kumuonya kuhusu mapenzi au kutojichanganya na wanaume nahisi huko ndiko alimpatia mpaka kufanikiwa kumuua”
“Bado haujajibu swali ambalo nilikuuliza”
“Siwezi kukwambia afisa”
“Unataka turudi kule kule mwanzo kwenye kupunguzana viungo?”
“Kwa sababu Zara alimuua mama mwenye mtoto na mimba”
“Kwa sababu zipi?”
“Alimjibu vibaya na kumtukana”
“Sasa Gavin anaingiaje hapa?”
“Nina uhakika mpaka amemuua rafiki yangu wa damu waziri wa mambo ya ndani maana yake hata mimi alikuwa ananifuatilia kwa nguvu kubwa na maisha ya familia yangu. Kwahiyo hata binti yangu alikuwa anafuatiliwa na mtu huyo ambaye nina imani kwa mazingira yalivyo huenda aliigiza na kumrubuni mpaka kuwa mpenzi wake kwahiyo baada ya kujua uhalisia uliopo nyuma yake na kile alicho kifanya akaamua kumuua”
“Sasa kwanini amuulie kwenye hoteli ambayo unadai ni yako?”
“Lengo lilikuwa ni kufikisha ujumbe kwangu kwamba anajua kila ninalo lifanya”
“Ili iweje?”
“Alijua nitapaniki na kuhitaji msaada wa haraka, hilo ndilo alikuwa analitaka”
“Ili iweje sasa?”
“Kwa sababu kupitia hilo angejua moja kwa moja mahali ambako naenda, angejua watu ambao mimi nina muunganiko nao hivyo ningekuwa namrahisishia kazi yake ya kujua aliye nyuma ya mambo haya”
“Unamaanisha kwamba ukiacha ile sababu ambayo umenipa mwanzo, hii ni sababu ya kukuacha hai kwa sababu anajua ipo siku utajisahau na kumuongoza kwa watu wako?”
“Ndiyo”
“Kama wewe haupo kwenye hesabu zake za kukuua kwa sasa, ni nani ambaye anafuata?”
“Siwezi kuwa na jibu la hilo swali lako”
“Jibu ni lazima uwe nalo kwa sababu hili halitakuwa ombi ni lazima unipe taarifa zote ambazo mimi ninazihitaji”
“Kwa mkanganyiko wa matukio ulivyokaa nina uhakika kwamba mtu ambaye anaweza kufuata kwa sasa ni mkuu wa majeshi”
“Kwanini?”
“Kwa sababu kama amemuua yule kijana kule Afrika ya Kusini basi atakuwa anaujua uhusika wa mkuu wa majeshi kwenye hili. Yule kijana moja kati ya watu ambao walikuwa wakimsimamia alikuwa ni mkuu wa majeshi ambaye ana taarifa nyingi zaidi yangu mimi lakini ukitaka taarifa zaidi basi kaeni na raisi wenu”
“Kwahiyo mkuu wa majeshi na raisi ndiyo wanaujua ukweli juu ya hili kundi na viongozi wake?”
“Ndiyo”
“Kuna mtu mwingine kwenye hili?”
“Watu wapo wengi hata mimi wengine siwajui”
“Lengo hasa la hili kundi ni lipi?”
“Kisasi”
“Kisasi?”
“Ndiyo”
“kwa nani?”
“Kwa familia ya Gavin”
“Kisasi kilisha isha nadhani?”
“Sio kama Gavin yupo hai”
“Mlijua alishakufa, hivyo hiyo sababu yenye mashiko, kipi kilikuwa nyuma ya hili?”
“Pesa”
“Zipi?”
“Za yule mfanya biashara wa madawa ya kulevya”
“Kwa hiyo hili kundi linazihitaji zile fedha na halina?”
“Ndiyo”
“Na hizo fedha mnahisi kwamba zilienda wapi?”
“Alikuwa anatafutwa mtu ambaye atakuwa nazo kwa sababu Gavin iliaminika amekufa ila mpaka sasa imetambulika kwamba hizo pesa zipo kwenye mkono wake bado”
“Hapa tunazungumzia kiasi gani?”
“Ni pesa ambazo hata calculator haina uwezo wa kuziandika”
“Utajiri wote wa baba yake unamaanisha upo kwenye mkono wake?”
“Ndiyo”
“Oooooh Mungu wangu, ndiyo maana anaogopwa sana kwa sababu ni mtu tajiri sana”
“Nadhani nimemaliza majibu yako Ofisa, kumbuka pale bandarini kuna kamera hivyo hata kama mtachelewa kuniruhusu kuondoka au msipo nirudisha kabisa kijana wako sura yake itaonekana wakati unafanyika msako hivyo niache niondoke kwa usalama wenu”
“Siwezi kukuacha uende mpaka uniahidi kwamba kilicho tokea hapa kitabaki humu humu ndani bila kwenda sehemu nyingine yeyote”
“Siwezi kukuahidi hilo”
“Basi huenda usilione jua kwa mara nyingine”
“Mimi na wewe wote tunajua kwamba hamuwezi kuniua, nimekujibu maswali yako nataka kuondoka”
“Kwa leo nakuruhusu uende ila kumbuka kwamba nikikuhitaji basi tutaonana kwa mara nyingine tena”
“Kama utakuwa hai mpaka wakati huo bila shaka tutaonana”
“Unanitisha?”
“Sijakutisha, nakwambia ukweli kwa sababu umevuka mipaka, kuna watu kama wakijua hili basi hawatapendezwa akiwemo raisi wako, najua wewe ni afisa wa kawaida tu ambaye unjitutumua kuonyesha unalipenda taifa lako lakini mabosi zako hawajali kabisa kuhusu hilo. Unahisi kama wakijua haya itakuwaje ofisa?”
“Nitakutafuta tena kwa haya ambayo umeyafanya Ismail”
“Kama umerekodi mazungumzo yangu na wewe nikiwa nakwambia haya ukahisi utatumia kama ushahidi kuniangamiza basi utakuwa hauna uwezo wa kufikiri vizuri. Kwanza hakuna jaji atakubali kusimamia kesi ya aina hii lakini pia nina uwezo wa kuyakana mahakamani kwa kudai kwamba mlinilazimisha hivyo sikufanya kwa mapenzi yangu bali kwa kulazimishwa jambo amabalo nina uhakika nitakuwa na hiyo haki kabisa ya kugoma. Baada ya hapo naweza kufungua kesi ya nyie kuniteke kwa nguvu bila ridhaa yangu, hilo linaweza kupelekea wote kufutwa kazi na kufunguliwa mashtaka lakini binafsi mimi na wewe tumeingia makubaliano kwamba jambo hili halitakiwi kufika popote tena kwa hiyo nategemea hivyo pia kwako. Lakini kumbuka umeniumiza binti hili halitaishi hivi hivi kuna siku utakuja kulilipia tu”

60 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
Mkuu kongole chuma kimetulia kama kimeandikwa na senior strategist wa CIA ungechapisha vitabu kwa hakika vingeuza.
 
Back
Top Bottom