SEHEMU YA 23
Mara wifi akaanguka chini na kuanza kutapatapa kama mtu mwenye kifafa.
Hofu ikatawala ndani yangu, nikaogopa sana kwani sikujua cha kufanya kwa wakati huo na sikujua ni kitu gani kimempata wifi yangu.
Wakati nahangaika pale chini na wifi huku nikimuamsha kwa kumtaja jina, kaka alikuwa amewasili na kukimbilia pale chini nilipokuwa na wifi.
"Vipi tena Sabrina, wifi yako kafanyaje?"
"Hata mi sijui, ameanguka gafla tu na kuanza kutapatapa"
Nikaogopa kumweleza kaka jambo lolote huku nikihofia kuwa kaka ataniona mimi mbaya.
Kaka akamnyanyua wifi na kwenda kumpakiza kwenye gari yake ili kumpeleka hospitali, bora kaka yangu ni mwenye nguvu maana mi mwenyewe nisingeweza kumbeba wifi na ile mimba.
Kisha nami nikapanda kwenye gari kwa lengo la kumpeleka wifi hospitali.
Kufika hospitali, wifi alikimbizwa moja kwa moja kwa daktari. Nilitulia kusikilizia kinachoendelea mara kaka akanifata na kuniambia kuwa nirudi nyumbani ili niandae vitu vya wifi kama khanga na vitenge na nguo, akanikodia gari.
Nami nikaondoka na kurudi nyumbani nikajua tu kuwa wifi atakuwa anataka kujifungua ndiomana wanahitaji hivyo vitu.
Nilifika na kuandaa kila kitu, nikaona karatasi iliyokunjwa vizuri kwenye kabati la kaka ila kabla sijafungua kaka alikuwa amewasili ikabidi nimkabidhi zile nguo na kumuuliza.
"Kwani wifi anaendeleaje?"
"Anaendelea vizuri ila ni kifafa cha uzazi kinamsumbua, tumuombe tu Mungu ili ajifungue salama maana kifafa kibaya sana"
"Basi unipe taarifa za huko kaka, uwe unanipigia simu"
"Hakuna tatizo, nimeshamtaarifu na mama kwahiyo atakuja hospitali. Wewe baki tu mdogo wangu kila kitu kitakuwa sawa, Mungu atasaidia"
Basi kaka akaondoka na kuniacha pale nyumbani, hamu ya kujua kilichoandikwa kwenye kile kikaratasi ilinijaa, nilitamani kujua maneno yaliyomo.
Nikaenda na kukichukua, kiliandikwa hivi:
"Nampenda sana mke wangu Joy, namuamini kuliko chochote duniani eeh Mungu nashukuru kwa kunipa mke muaminifu kama Joy"
Nikakisoma mara mbili mbili na kujiuliza, je ni kweli Joy ni mwaminifu? Kama ni mwaminifu mbona akabeba mimba ya mtu mwingine? Je uaminifu wake umepimwa kwa yapi?
Yote hayo ni mapenzi yao na sikutakiwa kuyaingilia ila je nitakaa kimya bila ya kusema ukweli? Maswali mengi nilijiuliza bila majibu, nikaamua kurudi chumbani kwangu huku nikiendelea na mawazo yangu hadi muda wa kulala ulipofika.
Nilipokuwa nimelala nilimuona wifi akijifungua mtoto mzuri sana wa kiume.
Nikashtuka na kutabasamu na kujisemea kuwa kumbe mawazo yangu yalikuwa kweli kuwa wifi atajifungua mtoto wa kiume, ila kuangalia vizuri ilikuwa ni ndoto sema siku hizi nimeanza kuziamini ndoto zangu, nikawa nangoja kukuche ili nipate uthibitisho wa ndoto yangu.
Asubuhi na mapema kaka aliwasili sababu alilala hukohuko hospitali kwaajili ya mke wake.
"Wifi anaendeleaje kaka?"
"Anaendelea vizuri sana, amejifungua mtoto wa kiume saa kumi na mbili asubuhi"
Nikafurahi sana,
"Ndio umuandaliage uji na kila kitu naenda kumchukua hivyo, nitarudi hapa na mama"
"Yupo hospitali na yeye?"
"Ndio yupo, nitarudi nae hapa"
Nikawa nangoja kwa hamu hata yale mawazo mengine kuhusu wifi yakapotea.
Nikaandaa uji kama nilivyozoea kuandaa kwani sikuzoea uji wa mzazi unatiwa nini.
Wakati naandaa uji, simu yangu ikaita na mpigaji alikuwa Carlos.
"Nini tatizo Carlos?"
"Nakusalimia tu, utampa jina gani mtoto wa wifi yako?"
"Mmh! Sijui, kwani umejua kama kajifungua?"
"Ndio najua, tena mtoto wa kiume"
Nikaishia kuguna kuwa huyu Carlos licha ya kuwa na upeo mkubwa basi atakuwa na upeo tofauti na wengine.
Nikakata ile simu ila akanitumia ujumbe mfupi wa maneno.
"Fikiria jina la kumpa mtoto wa wifi yako kwamaana wewe ndiye umeteuliwa kutoa jina"
Nikaanza kujifikiria sasa kuwa mwanzoni kabla wifi hajajifungua nilimwambia kuwa kama akijifungua mtoto wa kiume basi tutamuita "James" ila kwa sasa jina hilto lilinipa utata na nikashindwa kufikiria zaidi kwani ndio jina la kweli la baba wa mtoto.
Baada ya muda waliwasili nyumbani wifi, mama na kaka.
Mtoto alikuwa mzuri sana tena alichangamka na alipendeza kumuangalia, mama alienda kumuweka vizuri wifi, mimi na kaka tulibaki na mtoto.
Muda wote kaka alitabasamu huku akisema.
"Dah dume langu hilo"
Nilimwangalia tu kaka bila ya kusema chochote kwani nilihofia kwamba nitaanzia wapi kusema ukweli.
Mchana wa siku hiyo mambo yakawa shwari kabisa, wifi alitulia huku akimnyonyesha mtoto wake, mama nae alitulia pembeni na kaka yani kila mmoja alikuwa na hamu ya kumbeba mtoto ukizingatia mtoto mdogo anavutia sana.
Kaka akamuuliza mama,
"Mama eti tumuite nani?"
"Mi sijui, wazazi ndio muamue"
"Basi mdogo wangu Sabrina achague jina la kumpa mtoto"
"Mmh kaka mchagulie mwenyewe tu"
"Mi ningempa jina la mtu wangu wa karibu ila kwavile toka mwanzo wifi yako alitaka mtoto aitwe jina lako kama akiwa wakike basi ni wakiume na utatakiwa wewe utaje jina la kumpa"
"Kuna jina nilichagua kabla labda mmuulize wifi kama litafaa maana mimi nimelisahau"
Ikabidi kaka amuulize wifi
kuhusu hilo jina.
"Mmh hata mimi nimelisahau"
"Basi hilo jina litakuwa ni zuri, ukilikumbuka Sabrina ututajie tena"
Yani kaka alikuwa na furaha iliyopitiliza kwa yeye kupata mtoto tena mtoto wakiume.
Watu mbalimbali walianza kufika na kumuangalia mtoto huku wakimsifia kuwa mtoto ni mzuri sana na kumpa hongera wifi na kaka.
Moyo ulikuwa waniuma kila nikimsikia wifi akisifia kuwa mtoto kafanana na baba yake kwani sikuelewa anamaanisha kaka yangu au huyo James.
"Yani huyu mtoto mtundu kama baba yake, ona na macho yake ni baba yake mtupu"
Nilikuwa nikimuangalia tu na kukosa cha kufanya, kaka alikuwa akifurahia muda wote hata hakwenda mahali popote leo akimshuhudia mtoto aliyejua kuwa ni mwanae.
Ilipita wiki nzima bila ya mimi kutaja jina la kumpa mtoto, ikabidi kaka ampe jina lingine.
"Napendekeza huyu mtoto aitwe James"
Wifi akashtuka sana na kuropoka
"Kwanini asiitwe Deo?"
Kaka akacheka,
"Aitwe Deo kivipi? Itakuwaje mtoto Deo na baba Deo? Kwahiyo atakuwa Deo Deo! Mmh hata haipendezi"
Kisha kaka akanigeukia mimi na kuniuliza.
"Eti Sabrina hebu ona eti Deo Deo ndio nini? Itapendeza kweli!"
Nikaishia kucheka tu, kisha kaka akaendelea
"James Deo ndio itapendeza sio Deo Deo bhana"
Nikaguna na kujisemea moyoni je James James inakuwaje? Nikaishia na swali langu moyoni.
Wifi alikuwa kimya kabisa akitusikiliza kisa na yeye akaamua kumuuliza kaka.
"Kwanini umechagua jina hilo mume wangu?"
"Kwanza ni zuri, pili nina jamaa yangu anaitwa James dah ana roho nzuri sana. Ni mpole na mcheshi"
Nami nikachangia mada hapohapo.
"Hata mimi nilichagua jina hilohilo kaka"
"Kumbe mawazo yetu yanafanana, vizuri sana mdogo wangu"
Wifi alipokea jina lile kishingo upande, ni mimi tu niliyejua kwanini amenyong'onyea kwa kusikia hilo jina.
Wanakwaya wenzie walikuja kumuona mtoto wa wifi na kama kawaida watu hupenda kuanza na jina la mtoto ila wifi hakuwatajia huku akisema mtoto bado hajapewa jina.
Jioni yake nikapigiwa simu na Carlos,
"Badae nitakuja kwenu Sabrina"
"Utakuja kivipi mbona muda umeisha?"
"Nilisahau kama muda umeisha, basi nitakuja kesho"
Nikamaliza kuongea na Carlos na kuendelea kufanya mambo yangu mpaka muda wa kulala ulipowadia nikaenda kulala.
Nilipokuwa nimelala, nilihisi kuna mtu amelala pembeni yangu, uoga ukanijaa kwani niliogopa hata kugeuka huku nikihisi kuona mtu kweli nyuma yangu.
Nikahisi yule mtu akinipapasa mgongoni, hapo uoga ukawa zaidi ya mwanzo na nikatamani kupiga makelele ila sauti iliishia njiani, nikasikia kama mtu akiniambia.
"Acha uoga Sabrina, kwanini unakuwa muoga hivyo?"
Hofu ikazidi na kujibu nikashindwa, nikajikuta nikifumba macho kwa nguvu ili ile hali ipotee lakini haikupotea kwani nilihisi uwepo wa mtu kweli mgongoni mwangu.
Mara gafla mlango wa chumba changu ukafunguliwa na uwepo wa yule mtu ukapotea, hapo nilishtuka na kujifunika na shuka zaidi kwa uoga huku nikiwa nimejikunja.
Aliyeingia alikuja moja kwa moja na kunitingisha mgongoni kama kuniamsha.
"Sabrina, Sabrina"
Nilipoisikilizia ilikuwa ni sauti ya wifi Joy, hapo nikainuka na kumkumbatia.
"Una nini Sabrina?"
"Hamna kitu wifi"
"Mbona unaonyesha uoga halafu ulikuwa unaongea na nini?"
"Hakuna mtu wifi"
Akanishika mkono na kunivutia sebleni, kisha tukashikana mikono na kuniambia kuwa tuombe.
Kwakweli sikuwa muombaji mzuri kwahiyo ni wifi mwenyewe aliomba.
Baada ya maombi wifi alianza kunieleza.
"Unajua nilipokuwa nimelala chumbani, mtoto alikuwa anashtuka mara kwa mara nikajua kuna kitu tu. Unajua hawa watoto ni malaika huwa wanaona mambo mengi na vitu vingi ambavyo wakubwa hatuvioni, ndomana nikaja kukuamsha ili tusali"
"Asante wifi"
"Nenda ukalale kwa amani sasa"
Nilienda chumbani kwangu na kulala hadi kunakucha ila swala la wifi lilizidi kunichanganya kwani nilishindwa kujielewa kuwa ilikuwaje wifi hadi akamsaliti kaka, nilijiuliza sana bila ya majibu.
Siku ya leo niliamua kuvunja ukimya na kwenda kumuuliza tena wifi ili kupata ukweli ulio kamili.
Nilivizia muda ambao tulibaki wawili tu tena wakati mtoto amelala.
"Wifi niambie ukweli au unataka niseme kwa kaka?"
"Usifanye hivyo Sabrina, nihurumie wewe ni mwanamke mwenzangu"
"Hata kama mi ni mwanamke mwenzako, kumbuka mumeo ni kaka yangu wifi! Ilikuwaje hadi ukamsaliti na kwanini ulimsaliti? Hivi unajua ni kiasi gani unapendwa na kaka yangu? Yupo tayari kwa lolote kwaajili yako halafu unamsaliti kwa vazi la ulokole, mlokole gani wewe msaliti?"
"Usinitusi Sabrina, hujui nini kilitokea ni shetani tu huyu anataka kuharibu imani yangu"
Akainama akifuta machozi,
"Acha kumsingizia shetani, kwani huyo shetani hajakupeleka wewe huko kwenye mambo ya ajabu"
"Ndiomana nakwambia hujui kilichotokea mdogo wangu hujui, sikupanga wala kutaka kumsaliti kaka yako ila shetani anapitia kuvuruga watu wa Mungu"
"Nimekwambia acha kumsingizia shetani wifi unajua viapo vya ndoa wewe? Mi sijaolewa ila ninajua, hakuna mahali panaporuhusu kusalitiana."
"Mi sijamsaliti kaka yako wifi"
"Kama hujamsaliti ilikuwaje ubebe mimba ya mtu mwingine? Huo ni usaliti wifi, tena usaliti uliowazi kabisa tena huku ukiendelea kumuongopea kaka kuwa mtoto ni wake"
"Sabrina nielewe tafadhari, yaliyonipata mimi yanaweza kukupata hata wewe nihurumie wifi yangu"
"Huruma yangu kwako ni kumwambia ukweli kaka"
"Tafadhari nihurumie Sabrina, nitaenda wapi mimi? Nani atanihudumia jamani!"
"Akuhudumie huyo James, kwani anashindwa nini?"
"James hawezi kunihudumia Sabrina hawezi, nisaidie mwanamke mwenzio nateseka mimi"
Huruma ilianza kuingia moyoni mwangu ila nikamkazia.
"Msaada wangu kwako ni huo tu, kumwambia ukweli kaka Deo"
Wifi akainuka na kupiga magoti mbele yangu huku akilia. Huruma ikanijaa
"Nihurumie wifi nihurumie"
Mara kaka akarudi na kutukuta katika hali ile.
Itaendelea