Ziwa chala nakumbuka sana mwaka 1995 tuliokuwa tunahitimu form four mwaka huo katika shule ya sekondary iiliyojulikana kama MKUU DAY SECONDARY SCHOO Madume tu peke yetu tuliamua kufanya kile tulichokiita PICNIC YA WAGUMU katika ziwa hili, nakumbuka wasichana walilia sana tuende nao ila tulikataa kwani picniki hiyo haikuwa na baraka kutoka kwa walimu wala walezi. Tulijiandaa kwa vyakula vingi akiwemo mbuzi wa kuchinja na vinywaji vingi vikiwemo vileo. Hatukupima kabisa hatari zozote ambazo zingeliweza kutokea kule na kweli wengi wetu tulinusurika hatari nyingi mfano binafsi ilikuwa almanusura nizame wakati nikiogelea kwani lile ziwa ni la ajabu mno, ukiwa mita moja unajiona huwezi kuzama lakini sogea kidogo tu utashangaa! Lina slope kali na kukosa wenzangu waliokuwa wanajua kuogelea leo nisingelikuwepo hai.Ziwa lipo chini kina kirefu kutoka juu na mpaka ulifikie siyo mchezo unashuka kama upo juu ya mlima vile.
Baada ya kuogelea na kununua samaki kwa wenyeji waliokuwa wakivua ili tukachome jioni kabla hatujalala, usiku huo kuna hatari nyingine ilitokea ambayo hatukuiarajia, lilifumuka joka kubwa kusikojulikana na kutokomea bila shaka eneo tulipokuwa tumeweka kambi lilikuwa karibu na makazi yake, bahati halikumdhuru mtu. Usiku tulienjoy sana huku tukicheza miziki ya reggae hasa Bob marley na Lucky dube baada ya kula vyakula vyetu supu ya mbuzi na mazagazaga mengine kibao, Kesho yake kama saa 4 asubuhi hivi tukaanza safari ya kurudi shuleni huku tukiwa tumeacha historia kubwa Wilaya nzima ya Rombo katika Mashule mengine yote yaliyokuwepo wakati huo kama Ibukoni, Mashati, Shauritanga na Namfua tuliacha waliokuwa form 3 wakipanga na wao mwaka uliofuata wende lakini nafikiri hawakuweza kutimiza lengo hilo.
Wote tulirudi salama salimini na siwezi kuisahau siku hiyo, kama yupo mtu tuliyekuwa naye siku hiyo tafadhali ikiwezekana kama ana picha tulizopiga siku ile tuwasiliane ikiwezekana tuzilete hapa JF. Ziwa hili Wachagga wa Mkuu-Rombo wana simulizi nyingi kuhusiana na kutokea kwake wengine hudai ziwa mwanzoni lilijitokeza maeneo fulani ya msituni huko kijiji cha Maharo eneo ambalo hadi leo inasemekana pana dimbwi kubwa na ukirusha chochote pale kama shina la mgomba au mti husafiri mamia ya kilomita mpaka ziwa chala chini kwa chini. Lakini pia inasemekana kuwa maji ya ziwa hili hupita chini kwa chini kutokea Mlima Kilimanjaro na kuja kutua hapo chala, si hivyo tu kutoka tena hapo chala maji hayo hupita chini kwa chini mpaka ziwa jingine jirani liitwalo ziwa JIPE na ndio maana baadhi ya watu wanaozama katika ziwa hilo wengine huenda kuokotwa ziwa Jipe. Ziwa pia lina mamba hatari na wenyeji walitusihi sana tusiingie ndani sana wakati wa kuogelea wakatuonyesha maeneo salama. Upande wa Kenye kulikuwa kunaonekana Hoteli nzuri tofauti na Tanzania kwa wakati huo.