Mikakati na mitafaruku iliyozaa Muungano wa Tanzania III
..
Joseph Mihangwa
Toleo la 317
25 Sep 2013
..
KATIKA sehemu ya pili ya makala haya, tuliona jinsi juhudi za Marekani, Uingereza na Mwalimu Julius Nyerere, za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki kwa lengo la kuimeza Zanzibar, zilivyogonga mwamba.
Tuliona pia kushindwa kwa mpango wa Marekani na Uingereza kuivamia Zanzibar kijeshi na kuibuka kwa wazo mbadala la kuunda Shirikisho la Zanzibar na Tanganyika kwa lengo hilo hilo la kuimeza Zanzibar ya Wakomunisti. Tuendelee na sehemu ya mwisho kuona jinsi Shirikisho la Tanganyika Zanzibar lilivyozaliwa katikati ya mitafaruku hii.
Muundo gani wa Muungano uliofikiwa?
Aprili 21, 1964, Frank Carlucci, alituma taarifa kuelezea hali ilivyokuwa akisema: Viongozi wakongwe wamefanikiwa kumshawishi Karume kuzihesabu Marekani na Uingereza kama marafiki wema wa zamani walioisaidia Zanzibar, na amekubali kuzipa fursa zionyeshe urafiki huo; Karume ameishukuru Marekani kwa zawadi ya majengo ya mradi wa zebati na jenereta alizopewa. Huu ni wakati mwafaka wa kutoa misaada zaidi; ombi la Karume la kumsomesha mwanaye nchini Marekani ni ishara ya imani kubwa aliyo nayo sasa kwa Marekani.
Naye Balozi Leonhart aliripoti akisema: Kuzorota kwa hali na kuongezeka kwa ushawishi wa Babu na Wakomunisti wa Kichina (CHICOMMS) Visiwani,kumeifanya Tanganyika ione umuhimu wa kuishirikisha (kuiunganisha/incorporation) Zanzibar kama njia pekee ya kulinda usalama wa Tanganyika, na kwamba Zanzibar isiende kwa Wachina. Muundo wa ushirikiano uliokubaliwa ni wa Shirikisho mithili ya uhusiano kati ya Serikali ya Uingereza na Ireland Kaskazini.
Huku akionesha wasi wazi juu ya Muungano huo, Leonhart alisema: Mradi (mpango) huu haujakaa sawa, na hatari zake ni dhahiri. Hoja kuu hapa ni (a) kupata suluhisho la Kiafrika kwa tatizo la Kiafrika (b) kigezo cha kisiasa (ni kile) alichobuni Nyerere (c) Usiri utumike kutekeleza mpango huu ili kunufaika na kutokuwapo kwa Babu nchini (alikuwa safarini Indonesia) na kuzuia CHICOMMS kujiimarisha.
Na kuhusu hali Visiwani alisema: Kwa siku chache zijazo, hali itakuwa tete (alitabiri Jeshi la Zanzibar kuasi); Serikali ya Tanganyika inaimarisha vikosi vyake Visiwani, lakini uwiano ni wa kutilia shaka kutokana na ukweli kwamba, kambi ya Babu inamiliki silaha za kisasa zaidi (ilizopata kutoka China na Urusi) zikiwamo magari ya vita, mizinga na bunduki za rashasha.
Akaendelea kusema: Serikali ya Tanganyika inafahamu utayari wa Uingereza wa kutoa misaada kwake iwapo itaombwa na Zanzibar pamoja na Viongozi wa Tanganyika; kikosi cha Jeshi la Nigeria kilichopo Dar Es Salaam (kufuatia Jeshi kuasi Januari 20, 1964) hakiwezi kutumika nje ya Tanganyika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi hizo mbili.
Tena akasema: Tumependekeza vikosi vya Marekani viwekwe katika hali ya tahadhari; tumekubaliana na Balozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam aandae zana muhimu za kivita
.kwa wakati huu tupunguze kutoa kauli juu ya Tanganyika Zanzibar, na tuongeapo na Viongozi wa Kiafrika, tuepuke maneno yenye kujenga hisia za vita baridi, tusisitize tu kwamba, hizi ni juhudi za Kiafrika kutokana na uamuzi wa Watanganyika na Wazanzibari wenyewe.
Jeshi Zbar lilijiandaa kupindua serikali mpya
Imeelezwa kuwa, siku Mkataba wa Muungano ulipotiwa sahihi, Aprili 22, 1964, Mkuu wa Jeshi, Kanali Mahfoudh, aliandaa Jeshi la Ukombozi la Zanzibar (Peoples Liberation Army PLA) kufanya Mapinduzi, lakini wanasiasa wakamzuia kwamba Si busara kupoteza watu (Wazanzibari 300,000 kwa maslahi ya watu -Watanganyika milioni 10.
Waanzilishi wa PLA waliofunzwa Kijeshi, walikuwa ni makada wa Umma Party walioshiriki kwenye Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kiongozi akiwa Kanali Ali Mahfoudh aliyefunzwa Cuba. Jeshi hili ndilo lililodhibiti silaha zote zilizopokelewa baada ya Mapinduzi. Lilitaka kufanya Mapinduzi kwa sababu halikujulishwa juu ya mpango mzima wa Muungano.
Siku hiyo, Dean Rusk alituma simu ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam akisema: Toa ushauri haraka kama Zanzibar na Tanganyika zitahitaji vifaa kama vile mabomu na silaha nzito ili kukabili maasi yanayoweza kutokea.
Naye Balozi Leonhart alituma simu Washington akisema: Mbwambo (Mkuu wa Itifaki Tanganyika) amenipigia simu kuwasilisha ombi la Nyerere na Kambona kwamba Marekani ijiepushe kuzungumzia lolote juu ya Tanganyika Zanzibar; naelekeza ushauri wa Nyerere uzingatiwe, lugha iwe juu ya Shirikisho la Afrika Mashariki na si vinginevyo.
Aprili 24, Frank Carlucci alitaarifu Washington akisema, hapakuwa na sababu ya kupeleka silaha Zanzibar kwa kuwa hali ilikuwa shwari, lakini tu kwamba,
.Nyerere apewe misaada aliyoomba; kwa sasa ameshika hatamu, tumwache adhibiti hali mwenyewe ila pale tu itakapoonekana mambo yanamwia vigumu.
Karume aliamini wameunda Shirikisho
Aprili 26, 1964, dunia ilitangaziwa juu ya kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar. Siku hiyo, Leonhart alitoa taarifa Washington kwa furaha akisema: Sina shaka sasa Serikali ya Wakomunisti Zanzibar itamezwa ndani ya tumbo la Tanganyika isiyofungamana na upande wowote
. Ni muhimu Nyerere akaendelea kupewa misaada kimya kimya aweze kujiimarisha.
Juu ya aina ya Muungano uliofikiwa, Carlucci aliripoti akisema: Habari za kuaminika zinasema, Karume bado anaamini ametia sahihi Mkataba wa kuunda Shirikisho lenye Serikali tatu Serikali kuu ya Muungano kwa mambo 11 ya Muungano; na kwamba Serikali za Tanganyika na Zanzibar zitabaki kusimamia mambo yote yasiyo ya Muungano.
Licha ya kwamba Karume alitia sahihi Mkataba huo bila kupata ushauri wa kisheria, lakini alikuwa na kila sababu kuamini kwamba Muungano uliofikiwa ulikuwa wa aina ya Shirikisho kwa sababu nyingi, zikiwamo, kwanza; ibara ya 4 ya Mkataba imeweka bayana mambo kumi na moja tu yatakayoshughulikiwa na Bunge na utawala (uongozi) wa Muungano. Pili, ibara ya tano ya Mkataba inatamka wazi kuwa, Sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.
Tatu, kwamba, Rais wa Kwanza wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere, alipashwa kuongoza Serikali ya Muungano kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano, akisaidiwa na Makamu wawili wa Rais, na Mawaziri wengine na Maafisa ambao angeteua kutoka Tanganyika na Zanzibar, watakaohesabiwa kuwa Watumishi wa Jamhuri ya Muungano.
Nne, kwa mujibu wa ibara ya 7 (b) ya Mkataba wa Muungano, utaratibu wa kutunga Katiba ulimtaka Rais wa Muungano, kwa kukubaliana na Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye chini ya Mkataba huo, ndiye pia Rais wa Zanzibar, kuitisha Bunge la Katiba lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar kwa idadi hao wawili watakayokubaliana.
Karume alikosa ushauri wa Kisheria kabla ya kusaini Mkataba kwa sababu, kama tulivyoona mwanzo, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado, alipewa likizo ya siku saba siku mbili tu kabla ya Mkataba kutiwa sahihi. Naye Mshauri mbadala aliyeitwa kuja kushauri, Dan Wadada Nabudere (Uganda), aliwasili akakuta Mkataba umetiwa sahihi.
Mshauri pekee mwenye kuaminika na msomi, ambaye pia alikuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Salim Rashid, hakukubalika kwa Nyerere, kwani ilitokea katika moja ya mazungumzo kuelekea utiaji sahihi Mkataba huo, alizuiwa mlangoni na Walinzi kwa amri ya Nyerere kwa sababu ya kuwa na ndevu nyingi, na kuamriwa kwenda kwa kinyozi akazinyoe. Aliporejea, alikuta tayari Karume amechakazwa kwa hoja na kusalimu amri kwa shinikizo la Nyerere la kuunganisha nchi hizo.
Aprili 27, Leonhart alifurahia jinsi Nyerere alivyoweza kuteua Baraza lake la Mawaziri kwa ufundi mkubwa ili kuwanyamazisha Wazanzibari machachari, alisema: TumpeRais Nyerere majibu ya hoja alizowasilisha; tumhakikishie tutaipa Serikali ya Muungano pauni milioni mbili kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar; michango mingine itafuata kutoka Uingereza na Ujerumani Magharibi.
Baraza jipya la Mawaziri la Muungano alilolisifia Leonhart, ukiwaondoa Mawaziri kutoka Tanganyika, lilikuwa na Wazanzibari wafuatao:Mzee Abeid Amani Karume, aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais; Aboud Jumbe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais; Kassim Hanga, Viwanda na Nishati, na Abdulrahman Babu, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Kurugenzi ya Mipango.
Wengine walikuwa ni Hassan Nassoro Moyo, Sheria; na Idrissa Abdul Wakil, Habari na Utalii.Babu, Hanga na Moyo, ambao kwa hisia za nchi za Magharibi walikuwa sehemu ya mhimili wa Ukomunisti Visiwani, ilikuwa lazima waondolewe kwenye viambaza vya Zanzibar kufanya Karume na Nyerere wapumue.
Mikakati na mitafaruku hiyo, iliyochukua siku 100 tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964 hadi kufikia Muungano, ilikamilika kwa kutiwa sahihi Mkataba wa Muungano Aprili 22, 1964 kwa ushindi wa nchi za Magharibi dhidi ya Ukomunisti Visiwani.
Lakini pamoja na hayo, Zanzibar ya Muungano, kama ilivyokuwa Zanzibar ya kabla na baada ya Muungano, haikugeuka asprin kutuliza maumivu ya kichwa kwa Nyerere na Watanzania kwa ujumla, kama inavyothibitishwa hadi leo na ugonjwa tishio wa kuuwa, uliokosa dawa; ujulikanao kama Kero za Muungano.
Sio tu kwamba Muungano wa Tan-zan-ia umekosa mwelekeo wala kukidhi madhumuni yaliyokusudiwa hadi leo, bali uliwaumiza vichwa hata waasisi wenyewe wakafarakana; hasa baada ya Karume kugundua kwamba mwasisi mwenza, Mwalimu Nyerere, alipanga kutekeleza Muungano wa Serikali mbili kuelekea Serikali moja, badala ya Shirikisho la Serikali tatu, kama tulivyoona.
Nia hiiinathibitishwa na kuongezwa kinyemela kwa mambo ya Muungano, kutoka kumi na moja ya awali, hadi (sasa) 23 kulikomfanya Karume agongane na Mwalimu mara nyingi kiasi cha kusema:Muungano ni kama koti, likikubana unalivua, kama ishara ya kuchoshwa na Muungano huo.
Uhasama wa Viongozi hao uliwafanya wasiwasiliane ana kwa ana ila kwa njia ya wapambe wao Bhoke Munanka [Nyerere] na Aboud Jumbe [Karume]. Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Salim Rashid alipotaka kujiuzulu kazi Serikalini siku moja kabla ya kuuawa kwa Karume, [Karume] alimzuia asifanye hivyo kwa sababu yeye [Karume] alikusudia kuvunja Muungano lakini muda haukumruhusu.
Kwa nini Muungano?
Hapana shaka kwamba, chimbuko la Muungano ni hofu ya Mwalimu dhidi ya hatari kwa Zanzibar kama nchi, kuwa mlangoni mwa Tanganyika; hofu ambayo awali alipendelea ipate ufumbuzi kwa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) ili Zanzibar imezwe ndani ya Shirikisho.
Kushindikana kwa EAF kulimlazimu Mwalimu Nyerere kuanzisha mchakato mpya wa Muungano wa Tanganyika Zanzibar kwa madhumuni hayo hayo. Mchakato ulirahisika zaidi kufuatia Mapinduzi Visiwani, yakiongozwa na Wanaharakati wa Kikomunisti [Babu na wenzake] kushika dola na kuzitia hofu nchi za Magharibi [Marekani na Uingereza] na kuungana na Nyerere dhidi ya Ukomunisti.
Kwa nchi hizo, hofu haikuwa juu ya kupinduliwa kwa Serikali ya ZNP/ZPPP iliyowekwa madarakani na Waingereza, bali ilikuwa juu ya kueneza kwa Ukomunisti Afrika kupitia Zanzibar.
Ni kwa kiasi gani Muungano huo ulifanikiwa kupoza maumivu ya kichwa kwa Mwalimu juu ya Zanzibar? Jibu sahihi linatolewa na Mhariri wa gazeti la The Economist la Juni 1964, kwamba, Rais huyo [Nyerere] amemudu nusu tu ya kazi ya Chatu [ya kumeza]; amefanikiwa kummeza Mnyama [Zanzibar] lakini bila kuzivunja nguvu za Mnyama huyo ambaye bado yu mzima tumboni akiyeyushwa. Ukali wa mateke yake na maumivu yanaonekana dhahiri ndani mwa Tanganyika, na yanaweza kuuwa.
Maumivu haya kwa Muungano (Kero za Muungano) si ya kisiasa bali ni ya Kikatiba. Kujaribu kutibu maumivu haya kisiasa, ni kujaribu kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe. Na ili kutibu ugonjwa huo, kunatakiwa Katiba (mpya) yenye kuzingatia historia sahihi ya Muungano na kile kilichokusudiwa na kama bado kina mantiki hivi leo.