SEHEMU YA 4
"Sitti sikuachi tuondoke wote." "Hapana kwanini unanifuata unadhani kwamba mzee atanielewa?" Mzee akimaanisha yule mganga mkuu anayekaa naye pale nyumbani, mueleze matatizo yangu huwenda akanisaidia. "Unadhani basi ninaimani sana na mambo haya ya kishirikina?" Sitti alijifanya kwamba hana imani sana na waganga lakini mimi moyoni mwangu nilijua fika kwamba yeye anaweza kunisaidia juu ya jambo hili kwa hivyo nilikata shauri la kumfuata mpaka pale alipokuwa akiishi. Kagiza ndio kalikuwa kakianza kuingia na unavyojuwa hali kijijini giza linawahi kuingia haraka na usiku huwa ni mrefu na wa kutisha mno.
Nilimshika Sitti mkono mpaka pale alipokuwa akiishi tulifika ilibidi aniache nje kwanza barazani ili aende akaongee na yule Mzee Mganga. Ni mganga aliyekuwa maarufu sana hapo kijijini sito mtaja kwa jina ili kuficha hadhi yake lakini kila siku hayakuacha kupaki magari yasiyopungua matano ya wateja waliokuwa wakihitaji huduma yake, nilifika nikasikia kuna mteja alikuwa akimalizia kumtibu niliketi barazani kwenye benchi na mara kidogo niliitwa na kuingia ndani, Siti alinitambulisha na baada ya utambulisho niliona yule mganga akitazama kwenye kioo chake na kisha baadaye akaongea kwa upole.
"Kuna watu wanakufuatilia, na hata hapa ulipo wapo mimi nimewaona?" "Wako wangapi?!" niling'aka kwa mshtuko. wapo wawili nilihisi huwenda kuwa ni wale vijana wa mzee Samasimba ndio wametumwa kunifuatilia, ni kweli Mganga alinieleza kuwa hao vijana wametumwa na mzee fulani ambaye hato mtaja jina na lengo lao ni kuangalia nyendo zangu na kisha kumpelekea yule mchawi taarifa. "Wewe huwezi kuwaona kwasababu huna nguvu za kuwaona," alisema kwa upole na kwa utulivu mno.
Nilikuwa nipo ndani kwenye chumba maalum cha uganga, koroboi iliyokuwa hapo chumbani ndiyo iliyokuwa ikitoa mwanga kwa wakati ule. Chumba kilitapakaa harufu ya udi ambapo mganga alikuwa ndio kwanza anaanza kupandisha maruhani yake alisimama akaanza kutetemeka mwili mzima mithili ya mtu aliyepigwa na shoti ya umeme. "Enyi wazee na mizimu ya wakulu njooni mumuokoe huyu m'bwanga, asije kudhulika na walimwengu wenye roho mbaya. aliongea kwa sauti kali sana kisha kuchukua tunguli yake akiisha kuitikisa sana akaipuliza na hapo ikatokea sauti kama ya filimbi. Aliizungusha kichwani kwangu na kuniwekea kichwani kwa dakika kadhaa kisha kuitoa na kuivaa shingoni kwani ilikuwa na ukamba wake.
Huyo mganga alikuwa amejifunga kaniki kwa mtindo wa lubega tu na kiunoni alifunga mkanda wa shanga za makombe ya baharini. Chumba chake kilijaa zana za kazi basi alichukua kikamba kama bangili yenye mafundofundo akanifunga mkononi ilikuwa ni kama hirizi ndogo, kisha akanipaka dawa kidogo kutoka kwenye ile tunguli na kunishika mkono kutoka nje huku akiwa ameshikilia pembe ndefu pamoja na mwengo (kama mkia wa ng'ombe) alizunguka nyumba mara nyingi huku akiimba na kisha akaniambia nimfuate nyuma twende nyumbani kwangu kuzuza. (kukagua usalama wa nyumba yangu).
Nilimfuata nyuma alikuwa akikimbia kwa kasi japo sio sana, niseme tu labda ni kile kihirizi alicho nifunga ama ile dawa aliyonipaka usoni kwani kuanzia hapo nilianza kuona mambo ya ajabu mno na yakutisha. Niliweza kuona mwanga kama vile kuna taa za umeme kijiji chote pia mandhari ya kijiji ilibadilika ikawa ni yakuvutia mno ni kama vile macho yangu yalipigwa kiini macho. Niliwaona watu wakiwa katika maumbo ya ajabu ajabu wengine wakitembea huku wakiwa uchi wa mnyama!
Kila tulikopita niliona vitu ambavyo nisingeweza kuviona kwa macho ya kawaida wale vijana walikuwa wakitufuatilia kwa nyuma baada ya muda sikuwaona tena. Tulitembea usiku na baadaye kuingia kwenye njia ya kuelekea mashambani ni njia ya mkato kuelekea nyumbani kwangu lakini njia hii hupitia kwenye makaburi ya kijiji. Ghafla nilimuona yule mganga akipunguza mwendo na hapo akatembea kwa mwendo wa kunyata, alinisubiri mimi nilikuwa nyuma nikimfuata, jasho lilikuwa limenitoka mpaka kulowesha nguo yangu ya ndani, niliingiwa na woga mkubwa. Alinishika mkono tukatembea kidogo kuyakaribia makaburi tukachuchumaa chini ya mbuyu, nilistaajabu nilicho kiona.
Mwanga mkali wa moto uliokuwa umekokwa hapo makaburini wachawi walikuwa wakicheza kwa furaha huku wakiuzunguka moto ule. Mara nikamuona Mzee Samasimba akija huku akiwa amepanda juu ya mnyama fisi, wote walitulia kumsikiliza, niliwaona pia wale vijana waliokuwa wakitufuatilia wakiwa pamoja naye. Aliongea mengi ambayo sikuyasikia kwani alitumia lugha ya asili (kizigua) mwisho nilisikia jina langu na la Mzee Kingalu yakitajwa mara nyingi sana sikuelewa lugha iliyokuwa ikitumika nilimuona yule Mzee akilia sana huku akiongea kwa uchungu. Ijapokuwa alikuwa akiheshimika na wachawi wenzake lakini safari hii ilionekana kama aliudhika mno.
Wachawi hawana kazi, maranyingi hutafuta visababu tu ili kuanzisha ugomvi, ni watu wanaopenda kuheshimiwa na kuabudiwa kama Mungu bila kujua kwamba hapa duniani tunapita tu. Ndivyo ilivyokuwa kwa jamii ile niliyo kutana nayo amahakika nilijuta sana kuifahamu jamii ile na tamaduni zake. "Hapa ndipo sherehe na vikao vya kichawi hufanyika, inaonekana leo hawatokula nyama ya mtu ila kuna mtu wanamtafutia sababu, ni ama wewe au mzee Kingalu lakini mwenzako ni gwiji wa mambo haya wewe pangupakavu tia mchuzi watakuramba kama karata!" alisema yule mganga kwa sauti ya kunong'ona mwisho aliniambia tuondoke tunaondokaje aliniambia nimshike upindo wa ile kaniki na mara tukatokea mbele ya nyumba yangu.
"Kwa leo hatutoweza kufanya hili zoezi, lala kesho ukitoka kazini upitie nyumbani." Akimaanisha zoezi la kukagua nyumba na kuizindika, sikumjibu nilielekea mlangoni kwangu, niliufungua mlango na kuingia ndani kisha kuwasha kibatari nilipakaa ile dawa niliyopewa jana na mzee Kingalu utosini ilinisaidia kuzuia nguvu za kichawi, lakini ile hirizi niliyopewa na Mganga wala sikuivua. Nilizima kibatari na kulala ilikuwa yapata majira ya saa sita usiku. Niliomba pakuche haraka ili niwe salama. Sikusikia tatizo lolote kwa usiku huu ila baadaye nilisikia sauti ya bundi akilia juu ya bati langu alilia sana mpaka nikapitiwa na usingizi nilimsikia akilia kwa mbali na kupotea.
ITAENDELEA...
Sitosahau yaliyonipata kijijini Kwamsisi-5