SEHEMU YA 11
Baada ya mauzauza na maswahibu yale, siku moja nilikuwa nimekaa ofisini mwanafunzi mmoja akanijia, alikuwa ni mwanafunzi kama wa darasa la nne hivi, miguuni alikuwa peku na alikuwa amevaa sare chakavu. Alinifuata akaniambia, "Mwalimu naomba tuongee!" huku akinitazama machoni. Nilimtazama alikuwa amepauka nilimshika mkono nikatoka naye nje, nikatafuta eneo salama lenye faragha. "Niambie mtoto mzuri unasemaje?" nilimuuliza huku nikiangalia hali ya usalama kama kuna mtu yeyote anayetusikiliza ama kutufuatilia.
"Jana tulikula nyama ya mzee Kingalu, wazee wamesema kwamba anayefuata ni wewe!" Nilishtuka. "Mliwezaje kumla nyama wakati tuliiteka nafsi yake nikiwa na yule mganga niliye mwamini?" maneno hayo yalinitoka bila kutarajia. "Aliyekuwa akizuia yule mzee kuliwa alikuwa ni mzee Samasimba pekee, pamoja na kukosana naye lakini walikuwa marafiki hapo kabla na ndiyo sababu alikuwa akichelewesha asiliwe nyama. Yule mganga alikubali kuitoa nafsi ya mzee Kingalu baada ya kulipwa gharama kubwa," alisema.
"Gharama kubwa ya fedha ama ya nini niliwaza." Nililia sana niliposikia kwamba mzee Kingalu ameshaliwa kwahiyo matumaini yangu ya kumuokoa yalikuwa yamesha gonga mwamba. "Unaitwa nani wewe kwani?" nilimhoji yule mtoto kwa sababu ya ugeni sikuwajua watoto wengi pale shuleni. "Naitwa Kondo," alinitazama na kisha akageuka na kuondoka, kaptula yake ilikuwa imetoboka kwa nyuma nilimsikitikia.
Hawa wanakijiji wanamila za ajabu sijapata kuona. Baada ya taarifa hiyo niliogopa sana nilijua fika kwamba kumbe waganga nao sio watu wa kuwaamini. Wala hawana urafiki wa kudumu na mtu yeyote, wako tayari kuuza nafsi ya mtu kwa dau la fedha ndogo sana, kwao uganga ni kama biashara wanafanya kazi za mteja yeyote yule ilimradi iwe yenye maslahi kwao.
Sikuwa na mpango na Sitti kwa siku hiyo kutokana na yale mambo aliyonifanyia. Nilimwona akiwa amekaa pale ofisini, wala sikumsalimia nilikaa mbali naye hata walimu wenzangu walinishangaa kwanini sikuwa na mpango naye. Niliingia kwenye kipindi kufundisha, kama kawaida wanafunzi walikuwa wakinisikiliza kwa makini na hata nilivyokuwa nikiwaamuru kufanya jambo fulani walitekeleza bila kipingamizi chochote, walikuwa wakiniogopa sana, nilishangaa!
Nilitoka nikatembea kuelekea nyumbani, yule mtoto alinikimbilia akanishika mkono. "Mwalimu usipite njia hii kuna kitu wamekutetegea." Nikweli nilivyotazama mbele nilimwona Jumanne akifukia kitu alivyoniona alirudi nyuma akapotea. Ghafla niliona kitu kama upepo mkali ukinipulizia na hapo nilipoteza fahamu sikuona chochote kinacho endelea.
Baada ya muda nilishtuka nikiwa kwenye chumba kilichokuwa nakiza kinene mbele yangu kulikuwa na shimo refu na kwa pembeni yangu alikuwepo yule mtoto akiwa ameshika usinga. "Nimefikaje hapa?" nilimhoji. "Usiulize umefikaje, ni mimi nimekuleta nataka nikuingize kwenye chama chetu ili uweze kupambana na wachawi vizuri, bila hivyo watakumaliza hutoweza kuishi hapa kijijini." sikuwa na jinsi ya kupinga nilikaa kimya tu.
Huyu mtoto japokuwa alikuwa mdogo lakini nilikuja kugundua kuwa alikuwa na daraja kubwa kwenye jamii za wachawi, kwahiyo kumbe siku hii aliniteka kichawi akiwa na malengo ya kuniingiza kwenye chama chao. Nilikuwa sina jinsi zaidi ya kukubaliana na lolote atakalo nifanyia kwani nilijiona kuwa sina nguvu za kupinga jambo lolote atakalo niamuru kufanya. Aliniamuru kujirusha kwenye shimo hilo lililokuwa mbele yangu.
Bila kutarajia nilijirusha kwenye lie shimo na mara nikatokea kwenye mji mpya uliokuwa wa kisasa. Lakini mji huu haukuwa na mwanga wa kutosha na ulikuwa na asili ya rangi nyekundu kutokana na asili chanzo cha mwanga kilichokuwa pale, mwezi mwekundu uliokuwa aking'aa kutoka angani. Kulikuwa na majengo mazuri na magari pia sikutambua jina la mji ule.
Pembeni yangu alikuwepo yule mtoto na kwa mbele niliona geti kubwa nilipolisogelea likafunguka tukaingia na yule mtoto. Nilishangazwa kuona chumba kikubwa kilichokuwa na urefu wa kama mita kumi na upana wa mita tano, lilikuwa ni kama kanisa lililotelekezwa na kwa pembeni niliona mishumaa ikiwa imetundikwa kwenye viango vilivyokuwa ikitoa mwanga hafifu kulia na kushoto ya kile chumba.
Nilitembea mpaka mbele ya kile chumba kwa mbele nilimuona nyoka mkubwa mwenye vichwa vitatu alikuwa ameketi kwenye kiti cha dhahabu huku upande wa chini akiwa amejizungusha na kuketi kwenye kile kiti. Sauti ilisikika kutoka kwa lile joka, "Mimi ni malkia wa ufalme wa nyoka sema unataka nini nikusaidie!"
"Ewe malkia mkuu wa ufalme wa nyoka naomba unipatie ulinzi wako kwani nimeingia kwenye vita na wazee wa kijiji cha Kwamsisi nahitaji unipatie nguvu za kushinda hila zao na nia zao ovu." nilijikuta nikitamka maneno hayo bila kutarajia. "Ulinzi umeupata lakini usisahau kutoa sadaka," sauti ya mtetemo ilisikika. alinisogelea akanitemea mate yake usoni nilipatwa na upofu wa muda mchache yule kijana mdogo alinisogelea akanishika mkono, kisha nikahisi kitu cha baridi kikijinyonga kwenye mwili wangu. Nilimezwa na yule nyoka na kukaa tumboni kwake kwa muda wa siku tatu!
Baada ya kukaa kwenye mwili wa lile joka kwa muda wa siku tatu alinitapika lakini ilikuwa karibu kabisa na mazingira ya nyumbani kwangu na wala si kule kwenye mji wa ajabu, sikufahamu kwamba alifikaje hapo. Nilishuhudia akigeuka na kupotea kusikojulikana. Nilijikuta kuwa karibu ya nyumba yangu nikiwa nipo hoi bin taaban huku nikiwa nimevaa pete kidoleni, sikumwona yule mtoto nilitembea taratibu kuelekea nyumbani kwangu ikiwa ni usiku mnene. Nilifika nikawakuta watu kadhaa wakiwa wameizunguka nyumba yangu, niliwatazama nikawanyooshea mkono wenye kile kidole nilichokuwa nimevishwa pete ya maajabu na mara niliwaona wakipotea kila mmoja kwa njia yake nilitembea mpaka kwenye ile nyumba.
Nikaufungua mlango ili kuingia ndani kwa chini niliiona bahasha ya khaki iliyokuwa imeandikwa anuani na jina langu kwa juu, Mpendwa Soka! ilikuwa imedumbukizwa kupitia chini ya mlango wa kuingia ndani kwangu, sikuweza kuisoma kwa siku hiyo nililala fofofo nilikuja kuamka nikiwa nimechelewa sana hivyo sikwenda kazini nilichukua jembe na kuanza kusafisha mazingira ya nyumba yangu.
Nilikutana na vitu vya ajabu vikiwa vimetegwa juu yangu vikiwa vimezikwa ardhini. Niliving'oa na kisha kuvichoma moto, sikumwogopa mtu yeyote kwa kipindi hicho nilijisemea moyoni kwamba liwalo na liwe, kwa sababu nilisha choshwa na maisha ya kishirikina yaliyoshamiri kule kijijini. Yule mwanafunzi (Kondo) nilimwona akirudi kutoka shuleni huku akiwa amebeba begi mgongoni. "Mwalimu umeiona barua yako?" aliniuliza. Nilishtuka, ni ile barua niliyoikuta pale chini ya mlango, nilikurupuka kwenda ndani kuitafuta!
ITAENDELEA...