Ferruccio Lamborghini
JF-Expert Member
- Apr 15, 2020
- 1,667
- 2,595
Usiku kwenye daladala, saa ya simu yangu inaonyesha ni saa 4:47. Najilazamisha kuacha kusinzia, mara nasikia sauti za wanawake wawili wakizungumza viti vya nyuma yangu… stori zao zinanisaidia kukimbiza usingizi wangu.
Nasikia mmoja anamwambia mwenzake; “basi wakati namalizia kuosha vyombo akaja, eti ananiuliza vipi sasa? Nikajifanya sijui kinachoendelea, nikamuuliza vipi kuhusu nini? Akanambia nilichokuomba mchana, nikamuuliza kipi? Yaani nilikuwa najifanya kama vile nimesahau kila kitu, sikumbuki chochote.
“Basi akajizugisha zugisha pale ndio akanambia, nilikuomba namba yako. Nikamuuliza ya nini? Akanambia maswali gani hayo, nikamwambia si namba yangu, nitakupaje bila kujua ya nini. Akanambia kuna vitu nataka tuongee. Nikamwambia si uviongee hapa hapa. Akaniuliza kwani tukiongea kwenye simu kuna shida gani? Na mimi nikamuuliza kwani tukiongea hapa hapa huku tunaonana uso kwa macho kuna tatizo gani?
“Akaishiwa maneno, akanambia haya, nimeshindwa mimi, akaondoka.”
Nikiwa kwenye kiti changu nikajikuta natamani kugeuka kuwatazama hawa wanawake wawili angalau nijue wanaonekanaje, lakini tatizo ni kwamba, kama ningefanya hivyo ingeonekana wazi kwamba nawasikiliza na mimi nilikuwa sitaki tufikie huko nikaamua kujituliza, nikaishia kutengeneza picha ya namna walivyo nikitumia sauti zao na aina ya mazungumzo waliyokuwa wanayaongea kwa sauti bila soni kwenye usafiri wa umma.
Basi nikasikia yule mwanamke mwingine akicheka, yule msikilizaji; “He he heeee! Umemkomesha. Yaani hiyo ndio dawa ya vijanaume vya siku hizi. Vinapenda penda lakini havijui kutongoza, yaani tangu zimekuja simu na meseji wanaume hawajiamini kabisa kuongea mubashara. Wanakimbilia kuomba namba ya simu ili watume vimeseji vyao vya ajabu ajabu.”
Mwenzake akadakia; “Na emoji za kopa kopa.” kisha wote wakacheka kwa sauti utasema kwenye gari hakuna abiria wengine.
Ukiachana na kukosa aibu kiasi kwamba wanaweza kuongea mazungumzo ya aina hii kwenye usafiri wa umma, kitu walichokuwa wanakiongea huenda kina ukweli, wanaume siku hizi hatujiamini sana, hatujui kucheza na maneno kabisa, hususan uso kwa uso.
Ndiyo, tunajua vigori wenyewe siku hizi hawaelewi maneno makavu, kama ni mwanamume suruali utaimba mashairi yote, kuanzia ya hayati Sheikh Shaaban Robert mpaka ya William Shakespeare hutopata kitu, lakini hiyo haitunyimi uhuru wa kuonyesha makali yetu ya kusimama uso kwa uso na mrembo na kumuelezea yaliyojaa kwenye mtima wako.
Unajua uzuri wa kurusha makombora uso kwa uso ni kwamba ukikutana na kichwa ngumu anakuzodoa unaondoka umenywea, lakini bado ndani unajiona kidume. Na hiyo kuzodolewa ndio vijana siku hizi wanachoogopa, ndio maana wanakimbilia kuomba namba za simu, ili hata wakizodolewa iwe kwa njia ya meseji haiumizi kama ya ana kwa ana. Ebu tuache woga bwana.
©Mwananchi