Baada ya Wananchi na Wafanyabiashara kulalamika kuhusu hali duni ya mazingira katika Soko la Bombambili, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Abbas Ahmed Abbas, amefanya ziara ya kukagua soko hilo pamoja na masoko ya Manzese A na B yaliyopo Manispaa ya Songea.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa masoko ya Manzese A na B pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya Soko la Bombambili.
Brigedia Jenerali Abbas amesema ujenzi wa masoko ya Manzese A na B haujaanza licha ya mkandarasi kulipwa shilingi bilioni 3 kama malipo ya awali, huku mradi huo ukipangwa kuanza Julai 15, 2025 na kukamilika Julai 12, 2026.
Kutokana na hali hiyo, amemuagiza mkandarasi kuwasilisha maelezo rasmi kuhusu kuchelewa kwa mradi huo na hatua atakazochukua kuharakisha ujenzi.
Kwa upande wa Soko la Bombambili, ameelekeza barabara zinazoingia sokoni zirekebishwe, taka ziondolewe mara moja na usimamizi wa malori uimarishwe ili kulinda miundombinu.
Amesisitiza maagizo hayo yatekelezwe ndani ya wiki moja, akionya kuwa mazingira duni wakati wa mvua yanaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa na kuhatarisha afya za wananchi.