Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani bungeni, Mheshimiwa Mbowe, aliwaagiza wabunge wa Chama chake wasusie Bunge kushinikiza Bunge liwekwe kwenye 'lockdown' kwa ajili ya corona. Baadhi ya wabunge wake walitii agizo hilo, baada ya kuwa wamekwishapata posho ya kuhudhuria Bunge. Hivyo, Spika amekuja na agizo kwamba wote wanaosusia Bunge, warudishe masurufu waliyopewa kwa siku ambazo hawakuhudhuria vikao. Hili limezua mjadala, 'for and against'.
Nina maoni kadhaa katika suala hili.
Mheshimiwa Mbowe ana hoja ya msingi. Ubaya wake ni jinsi alivyoitoa. Alipaswa kuwasilisha Bungeni muswada wa dharura kuomba kusitisha shughuli za Bunge. Bunge lingejadili muswada huo kwa kulinganisha manufaa na madhara yatakayotokana na hatua hiyo. Upande unaoafiki watasema hatua hiyo itathibiti kuenea kwa ugonjwa. Wanaopinga watasema madhara kiuchumi na kijamii ni makubwa zaidi kuliko manufaa yatakayopatikana, kwani mpaka sasa ueneaji wa ugonjwa siyo mkubwa sana. Muhimu, watu kufuata tu masharti yanayoelekezwa na Serikali, kama kuvaa barakoa, kutosongamana kwa watu wengi, n.k. Aidha, wanaopinga muswada wataleta hoja kwamba Bunge liko ukingoni mwa muda wake na linabidi kukamilisha shughuli zake kabla ya kuvunjwa, kupisha uchaguzi mwishoni mwa mwaka. La sivyo, huenda ikalazimika kuahirisha uchaguzi, kitu ambacho sidhani kama upinzani watakipenda.
Zote hizo ni hoja nzuri (za kuunga mkono na za kupinga) na zinastahili kujadiliwa. Bunge lingezijadili na kufikia uamuzi. La muhimu ni kwamba kitu kinachoamuliwa ndicho hicho kiwe. Ninaamini kama Bunge lingeamua kusitisha shughuli baada ya kujadili hoja za pande zote mbili, Spika asingesita kusitisha Bunge. Kama hoja ya Mbowe ikishindwa, upinzani ingebidi watii maoni ya wengi, na hiyo ndiyo demokrasia. Siyo kwa sababu tu maoni yako hayakukubalika basi unaamua kufanya utakavyo, hata kama ufanyacho kinakinzana na maoni ya wengi.
Badala ya kupeleka muswada wa dharura, Mbowe alikwenda kwenye vyombo vya habari na kutolea huko maoni/maamuzi yake na kuwaagiza wabunge wa chama chake wasitishe kuhudhuria vikao vya Bunge. Hili halikumpendeza Spika na akaamuru wabunge wote wasiohudhuria vikao warudishe posho waliyopewa kwa siku ambazo hawakuwa bungeni.
Uamuzi huu nakubaliana nao kwa asilimia 100. Unapewa posho ya kuhudhuria vikao. Kama hukuhudhuria kikao, hustahili kulipwa posho. Kuna wachangiaji humu ambao walionyesha kushangaa kwa nini posho ilitolewa kabla ya vikao kufanyika. Hakuna la ajabu hapo. Mfanyakazi yo yote anaposafiri kwenda kikazi nje ya kituo chake cha kazi, hukadiria atakaa huko siku ngapi, malazi ni kiasi gani kwa siku, na vivyo hivyo kwa chakula. Hesabu zinapigwa na anapewa masurufu kulingana na hesabu hizo. Unategemea mtu huyu alipiaje malazi na matumizi mengine ya kujikimu akiwa huko nje ya kituo chake cha kazi kama hukumpa hela 'in advance'? Akirudi ana-'retire imprest' aliyopewa kwa kutoa vielelezo jinsi alivyotumia masurufu aliyopewa. Hela ambayo hawezi kuitolea maelezo inabidi kuirudisha. Hiki ndicho kinachofanyika kwa maofisi yote, likiwemo Bunge. Bunge linapangwa kuchukua siku kadhaa na posho ya mbunge ni kiasi fulani kwa siku. Hivyo mbunge anapewa posho hiyo 'in advance' kama 'imprest'. Hakuna cha ajabu hapo. kwa kuwa wabunge wa Chadema walihudhuria vikao kwa baadhi tu ya siku zilizopangwa, ile posho ya siku ambazo hawakuhudhuria inabidi irudishwe. Period.
Tatizo lilitokana na Mheshimiwa Mbowe kutumia njia zisizo za kiofisi (vyombo vya habari) kueleza mawazo yake. Kama hatua aliyochukua ilikuwa kwa ajili tu ya kuhofia afya ya wabunge, na si kwa kujipatia sifa za kisiasa, hawezi kuona shida kurudisha hayo masurufu ya siku alizokosekana bungeni. In fact angejizolea sifa sana kama angerudisha posho hiyo kabla hata Spika hajasema hivyo. Watu tungeelewa kwamba kweli mtu huyu amechomwa moyoni na hoja yake kiasi kwamba yuko radhi hata kurudisha posho yake. Sasa unasusia vikao lakini posho unaing'ang'ania. Kwa misemo ya wahenga: 'Baniani mbaya lakini kiatu chake dawa'; au 'Kigeugeu na kisebusebu papo'.