Usumbufu unaoletwa na Urusi ni sawa na ule wa kunguni au chawa tu kwa binadamu. Sababu za usumbufu huo ni tatu:
1. Urusi tofauti na USSR imegeuka kuwa "rogue state" isiyo na lengo kuu la kimfumo (strategic objective) zaidi ya kuwepo tu (mere survival/existence). USSR ilikuwa na lengo la kuigeuza dunia nzima kuwa ya kikomunisti kwa misingi la Marx/Lenin. Hiyo ilishindikana, USSR ikasambaratika na kupoteza ushawishi huo duniani kote. Leo hii Urusi inaongozwa na kikundi maslahi kilichokumbatia madaraka na kugawana fursa za kibepari kwa kubebana (cronyism & patronage). Ukomunisti ulishatupiliwa mbali; sasa ni ma-oligarchs tu yanayojuana na Kremlin. Kikundi hiki kinajua kabisa kuwa maslahi yake yanategemea Marekani na Ulaya. Huko ndiko kwenye uhakika wa uchumi wake. Leo hii nenda Central London utakuta wamiliki wakubwa wa ardhi na mali ni kutoka Urusi/Ukraine. Wamewekeza kweli huko Marekani na Ulaya. Hivyo kila wakati wanahangaika kuhakikisha watu rafiki (sympathetic) (Trump & co.) wanakuwa madarakani.
2. Muhimu sana hawa wahuni (akina Putin) wamerithi rasilimali nzito za kiteknologia ikiwa ni pamoja na za nyuklia, ardhi, maliasili na mifumo ya elimu ya hali ya juu toka USSR. Na hapo wanajitahidi sana kutoa upendeleo kwa watu wao wenye kuweza kuziendeleza rasilimali hizo ili wazitumia kupambana na Marekani na Ulaya. Kule kuwepo kwa miundombinu ya uhakika ya nyuklia na sayansi za anga ni kinga/tishio (deterrence) tosha kwa yeyote atakayefikiria kupambana na Urusi. Tena wakiwa "rogue state" hawajali hata kutoa mhanga idadi kubwa ya watu wao kwa maslahi ya kikundi tawala kilichopo Kremlin. Tofauti na Marekani na Ulaya ambao watu wao wana thamani kubwa sana, wanaojali maisha bora kwa kila mtu na kuna mifumo thabiti ya kusimamia haki za binadamu. Marekani wakijua wanapambana na "wehu" si rahisi kuwavamia Warusi huko Crimea, Syria na kwingineko bila kujihakikishia kutozuka vita ya nyuklia!
3. Marekani na Ulaya ni jamii zilizo wazi (open societies). Mambo yao ni hadharani. Marais wao wakifanya faulo wanapashwa hadharani. Wanachunguzwa hadharani (Robert Mueller on Russian collusion). Wateule wa Rais wanapigwa interview hadharani. n.k. Kwa urusi, hiyo ni sawa na kuanika nguo zao za ndani hadharani. Rais wao (Putin) ni sawa na mungu! Athari zake ni kuwa watu hatari wanapata mianya kibao ya kuendesha uhalifu Marekani na Ulaya. Warusi wanatumia fursa hiyo kujaribu kuhujumu nchi za jumuia ya NATO. Marekani na Ulaya wanalijua hilo lakini hawako tayari kujifungia ndani kama Urusi. badala yake wanajiimarisha kitaaluma kukabiliana na chokochoko za Urusi na wahuni wengine. Na kwa kweli wamefanikiwa. Karibu harakati zote za Warusi wanazijua. Kuna wakati wanajifanya hawana uhakika ili kuwaingiza kwenye mitego.
Akina Putin wanajua vizuri sana kwamba hawaiwezi Marekani na washirika wake wa Ulaya. Kwanza, huko ndiko wanakohifadhia utajiri wao wa kifisadi. Ndiko wanakosomeshea watoto wao na ndiko ambapo kila Mrusi aliyefanikiwa anaotea kuwa na makazi na kumiliki mali kama ilivyo kwa watu wengine wa dunia ya tatu. Kitu nachoamini ni kuwa Urusi wangekuwa na viongozi wenye maono ya hali ya juu, kwa uwezo na rasilimali walizo nazo, wangekuwa tishio sana kwa washirika wa NATO. Bahati mbaya, wanaongozwa na watu wenye tamaa ya mali, madaraka na sifa (ujiko) bila falsafa kuu ya taifa. Watu ambao wanategemea kubebwa na miundombinu iliyowekwa na USSR ambayo sujui kama wataweza kuiimarisha ishindane na ya magharibi huko mbeleni.