Inaaminika kwamba kitabu cha Ufunuo kiliandikwa mwaka 96 CE. Kwa muktadha huo, hata Yesu angerudi leo hawezi kuwa amerudi "upesi" wakati imeshapita miaka karibu 2000 tangu aseme hayo.
Kwa Bwana miaka elfu ni kama siku moja (2 Petro 3:8-9)
Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili...kwa Bwana...miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali anawavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote watubu.
Yesu alipaa mbinguni takriban mwaka 33 BK.
Huu ni mwaka 2025, hivyo tunaweza kusema amekaa mbinguni kwa miaka 1992
Tukibadili hiyo miaka kuwa siku (kwa mujibu wa 2 Petro 3:8), miaka 1992 duniani ni sawa na siku 1.992 (1992÷1000 = 1.992)
Kwahiyo tangu Yesu apae mbinguni hadi sasa Machi 2025, amekaa mbinguni kwa takriban siku 1.9 tu!
Hii inaendana na unabii wa Hosea 6:2
Baada ya siku mbili atatufufua...
Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba kuja kwa Yesu sio jambo la mbali, tuko karibu sana na siku ya pili, aliyoinena Nabii Hosea, ambayo wengi wanaamini ni wakati wa kuja kwa Yesu!
Kwa hesabu hiyo na kwa unabii huo wa Hosea, ni wazi Yesu yuaja upesi kama alivyoahidi katika Ufunuo 22:12, kwakuwa atakuwa amekaa mbinguni siku 2 tu!
Hatujui siku wala sasa ya kuja kwake. Tunachotakiwa tu ni kukesha maana kwa siku na saa tusiyodhani, Yesu atakuja(Mathayo 24:42).
Kukesha ni kuhakikisha tunaishi maisha matakatifu na kujiepusha na usingizi wa kiroho(Ebr 12:14).