Nnachoona ni kuwa wengi wanachangia huku wakiwa hawajaelewa profesa amezungumzia nini!
Nilivyomuelewa ni kwamba
Hakusema kama Waarabu hawakushiriki Katika biashara hiyo ila ushiriki wake sio kama unavyoonyeshwa katika historia ya sasa mashuleni, kwa asilimia kubwa anayehusishwa ni Mwarabu, huku mzungu mhusika mkuu akiwekwa pembeni.
Na bahati nzuri ushahidi upo wazi Kwa sasa, huko uzunguni ngozi nyeusi inaongoza kuliko nchi za kiarabu, lkn Kwann atajwe sana Mwarabu hii leo?
Kama mzungu alikuwa anazuia utumwa, na watumwa waliopo huko kama walipelekwa na Waarabu mbona hatuoni Waarabu huko wakiwa wamezaliana ila tunaona ngozi nyeusi tu na wazungu.
Kama hili nalo wewe unaechangia mada kwa jazba hukuliona, jua ya kuwa hutumii akili kufikiri.
Maelezo mazuri kwa wanaotumia akili!
Huo ndio uongo tunao upinga. Sijui mlisoma historia gani lakini niliyosoma mimi ilizungumzia sana uhusika wa wazungu katika biashara ya watumwa iliyovuka bahari ya Atlantic. Kwa wao ilikuwa rahisi zaidi kwenda Ghana mpaka Angola kuchukua watumwa kuwapeleka kwenye himaya zao Amerika ya Kusini, Amerika ya Kati, ya Kaskazini na Carribean. Wazungu wenyewe wanakiri hili na wanakubali kuwa babu zao walifanya ukatili mkubwa sana.
Waarabu, kwa sababu ya ukaribu wao na Afrika Mashariki walihusika sana katika biashara ya utumwa ya pande hizi. Ushiriki wao ulianza hata kabla ya Seyyid Said kuhamia Zanzibar. Wahindi walihusika kwa kuwakopesha fedha za kununulia vitu ambavyo wangenunulia watumwa. Baadhi ya makabila yetu yalihusika na walikuwa washiriki wa waarabu katika hiyo biashara dhalimu. Wazungu walianza kuja kufuata watumwa maeneo yetu biashara hii ilipopigwa marufuku na waingereza na hivyo kuwazuia kuchukua watumwa kutoka maeneo yaliokuwa sehemu ya himaya ya Uingereza. Hao watumwa anaosema walipelekwa Brazil wengi walichukuliwa kutoka Angola ambalo lilikuwa koloni la Ureno.
Waarabu kutokana na ukaribu wao, ndio walikuwa vinara wa biashara ya utumwa Afrika Magharibi iliyowapeleka watumwa Afrika Kaskazini. Dhana ya kuwa watu weusi ni watu wa kutumikishwa inaendelea bado Mauritania, Libya na Sudan.
Huyu profesa anashupalia vikatuni wakati kuna picha nyingi tu zikionyesha watumwa wakiwa katika majahazi ya waarabu. Simulizi la kilio cha watumwa Bagamoyo sio za kutungwa. Kuna ushahidi wa maeneo walikokuwa wakihifadhiwa. Kushamiri kwa tamaduni za kiarabu katika njia kuu ya utumwa ni ushahidi mwingine. Tamaduni hizi zilipelekwa na waarabu ambao anasema kwa zaidi ya miaka 1000 hawakudiriki kuingia ndani ya Afrika.
Kutuambia kuwa watu weusi walifanywa watumwa uarabuni ili kuwapikia chai waarabu ni matusi ya nguoni.
Hiyo hoja ya kusema kuwa kwa sababu kuna watu weusi wengi Marekani kuliko uarabuni haina mashiko. Watu weusi wapo uarabuni. Tofauti na Marekani ni kuwa waarabu waliwatambua watu weusi wenye damu ya kiarabu kuwa ni waarabu. Seyyid Said alizaa na waethiopia na watoto wake walitambuliwa kama waarabu. Huko Sudan, Janjaweed wengi ni weusi tii lakini kwa sababu wana damu ya waarabu wanajihesabu kuwa waarabu. Iraq weusi wapo. Kuwait wapo. Tofauti ni kuwa hawaitwi weusi bali waarabu.
Wazungu walikuwa tofauti. Wao mtu yeyote mwenye damu nyeusi alikuwa mweusi ( one drop rule) . Kwa sababu hiyo hawakuona taabu kuwafanya watumwa watoto waliozaa na watumwa wao. Mmoja wa waasisi wa taifa la Marekani, Thomas Jefferson alikuwa na familia kubwa tu ya watoto weusi aliozaa na mtumwa wake. Watoto pamoja na mama yao walibaki watumwa wake mpaka alipokufa.
Sababu nyingine ya kutokuwa na watu wanaohesabiwa weusi wengi uarabuni ilikuwa ni kuwa wengi hawakufika uarabuni na walifia njiani kutokana na mazingira ya kikatili waliyokuwa wakisafirishiwa.
Nyingine ni kuwa wale watumwa wa kiume waliokuwa wanafanya kazi za kuhudumia wanawake wa kiarabu walihasiwa.
Nyingine ni kuwa wengi waliingia kwenye Uislamu na hivyo kufunguliwa njia ya kutoka utumwani kwa sababu Uislamu unakemea kumfanya Muislamu mtumwa. Mara nyingi hili lilipuuzwa kwa watumwa weusi lakini Seyyid Said aliitumia kukataza kuwafanya wasomali watumwa. Wazungu wao hawakujali kama wewe mkristu au la. Kwa wao rangi ya ngozi yako ndio iliyowapa haki ya kukufanya mtumwa.
Ni uongo kusema kuwa historia inasema kuwa waarabu ndio waliopeleka watumwa Marekani na Carribean. Wazungu wanakiri kuwa ni mataifa ya Ulaya ndio waliopeleka watumwa maeneo hayo. Kuchukua kipicha kilichotumiwa na mtu asiyejua historia kama ushahidi kuwa wazungu walisema kuwa waarabu walipeleka watumwa Carribean ni kutaka kutuchezea akili. Hao waliochora hizo picha ni watu wasiojua historia. Wakosolewe kwa kutokujua kwao.
Waarabu na washiriki wao wanafanya juhudi kubwa sana kutaka kutuaminisha kuwa wao hawakuhusika katika biashara hii haramu bali ni sisi watu weusi tulijipeleka utumwani baada ya kuvutiwa na ukarimu wao! Watu kama huyu profesa wanajaribu kupunguza scale ya udhalimu huo kwa sababu wanajua ushahidibupo wa ushiriki wao kwa hiyo hawawezi kuukana jumla.
Tofauti na anavyosema huyu profesa, chuki katika jamii yetu inapandikizwa na watu kama yeye ambao wanataka tuangalie kila kitu kwa misingi ya dini. Na wanaweza kufanikiwa kwa sababu sasa hivi mtu unaweza kuishi maisha yako yote bila kushirikiana na mtu wa dini nyingine. Unaweza kusoma kuanzia chekechea hadi chuo kikuu katika shule zinazomilikiwa na watu wa dini yako. Unaweza kufanya kazi katika makampuni yanayomilikiwa na watu wa dini yako. Watu kama hawa inakuwa rahisi sana kuwachukia watu wa dini nyingine. Tunaona humu jinsi watu wanavyotupiana matusi ya nguoni linapotokea suala linalohusu dini zao.
Ndio maana najiuliza kama hawa watu kweli hawana marafiki na ndugu wasio wa dini yao? Watu kama huyu profesa wanatupeleka kubaya.
Amandla...
JokaKuu Nguruvi3