Zitto ampigia debe
Dk. Rashidi Tanesco
*Adai ni mtendaji makini, asiyeyumbishwa na wanasiasa
*Apuuza tuhuma zake za rada, ang'ang'ana tena na Dowans
MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
WAKATI kukiwa na hisia ya kuwepo mtandao unaofanya jitihada za kuhakikisha kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco), Dk. Idris Rashidi, anateuliwa tena kushika nafasi hiyo nyeti, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe, ameibuka hadharani kumpigia debe Rashidi katika mazingira yanayoongeza utata kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa mbunge huyo katika siku za karibuni.
Katika hali isiyotarajiwa, Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, amedai kuwa Dk. Rashidi ni mmoja wa viongozi bora zaidi wa mashirika ya umma waliopo Tanzania, licha ya tuhuma zinazomwandama na utendaji wake ambao umewakera Watanzania wengi.
Zitto, ambaye alipachikwa jina la "Mr Dowans" na baadhi ya watu mapema mwaka huu baada ya kuchukua mtazamo wa aina yake wa kutetea mpango tata wa Dk. Rashidi wa kutaka kununua mitambo yenye kutu ya Dowans kwa bei kubwa kuliko hata waliyoitumia Richmond kuinunua awali, sasa amejitokeza na kudai kuwa kiongozi huyo ni lulu.
Kauli hiyo ya Zitto aliyoitoa kupitia mtandao wa mijadala wa Jamii, imekuja ikiwa ni baada ya gazeti hili kubainisha kuwa jina la Idris limepenyezwa Ikulu ili ateuliwe kuendelea na wadhifa huo, hali ambayo imesababisha mgawanyiko katika Bodi ya Tanesco ambako baadhi ya wajumbe wameukana uamuzi huo kuwa si wao.
................................................
SOURCE: KULIKONI, Novemba 27, 2009