MP's wapigwa stop kumjadili Kikwete.
Shauku ya wabunge kuichambua hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa bungeni wiki iliyopita imekwama, baada ya uamuzi wa kuijadili kuzuiwa kwa sasa.
Hatua ya kuzuiwa kwa mjadala huo ambao ulitangazwa kwa mbwembwe na Spika Samuel Sitta wiki iliyopita, tayari kumeibuka mgawanyiko wa mawazo miongoni mwa wabunge ambao baadhi yao wanaielezea hali hiyo kuwa inayotokana na shinikizo au maelekezo ya serikali.
Tamko la kusitishwa kwa mjadala huo lilitangazwa jana na Sitta mwenyewe, ambaye alisema uamuzi huo umeahirishwa kutokana na kile alichokieleza kuwa ni kutokukamilika kwa kitabu cha hotuba kilichokuwa kikiandaliwa kwa ajili ya wabunge.
Katika maelezo yake Sitta, alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya mambo aliyozungumza Rais Kikwete kutokuwa katika mpangilio wa hotuba yake, hali iliyosababisha haja ya kufanyika kwa marekebisho.
Alisema wamelazimika kuipeleka hotuba hiyo Ikulu, ili ikafanyiwe marekebisho hayo, hivyo haitaweza kupatikana mapema kwa sababu Kikwete mwenyewe anatarajia kuanza ziara nchini Marekani kuanzia kesho.
Alisema badala yake hotuba hiyo sasa ambayo ilikuwa ijadiliwe Alhamisi hii itapangiwa wakati mwingine kwenye mkutano wa 13 wa Bunge, unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Akizungumzia hatua hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, aliielezea kuwa ni ya kushangaza na itakayosababisha kushuka kwa morali wa wabunge.
"Kusema ukweli, kuchelewesha kujadili hotuba hii si jambo jema kwa wabunge, kwani wangependa waijadili sasa kuliko kungoja hadi Novemba ambapo itakuwa imepoa," alisema Hamad.
Alisema wabunge walikuwa bado wana fursa ya kuijadili hotuba hiyo kwa kutumia kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) badala ya kusubiri kuchapishwa kwa vitabu hivyo.
'‘Kwa hatua hii na kwa jinsi hali ilivyo, kuna mambo yanatengenezwa pamoja na kusogeza muda ili yale yaliyosemwa kuhusu wezi wa EPA, hasa wale waliopewa muda wa kurejesha fedha hizo ambao inawezekana wakazirejesha kabla ya muda waliopewa, hivyo wabunge hawatakuwa na
jipya kuhusu EPA," alieleza kiongozi huyo wa upinzani bungeni.
Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Dk.Willibrod Slaa, alisema kuahirishwa kwa mjadala huo kuna athari kubwa kwa taifa, kwani kuna baadhi ya watu wamejitokeza na kuanza kufanya maandamano ya kupongeza hotuba hiyo kwa lengo la kuficha ukweli kuwa ilikuwa na upungufu.
Alisema hotuba hiyo ilipaswa ijadiliwe ingali moto bila kutoa nafasi kwa serikali kujipanga na kufanya mambo yao kisiasa zaidi na hivyo kuipa fursa CCM iendelee kuwa kichaka cha mafisadi ambao kila kukicha huwaza namna ya kutafuna rasilimali za taifa.
"Kuna watu wanaolichukulia jambo hili kijuu juu na wanafikiri kupindua mambo ndiyo ujanja. Hii ni hatari kwa taifa, kwani tuna nyaraka za kutosha kuhusu EPA na mengineyo, hivyo ni vyema wakakaa chonjo," alionya Dk. Slaa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliungana na Hamad na kusema amepigwa butwaa kusikia sababu zilizotolewa na spika ambazo alidai kuwa si za msingi, kwani hotuba hiyo ipo kwenye kumbukumbu za Bunge ‘hansard' na lingekuwa jambo rahisi kutumia kumbukumbu hizo kuijadili.
Alisema kama Bunge litaendelea kushindwa kufanya kazi kwa kutegemea maagizo ya serikali ambayo kimsingi inapaswa kuwajibika kwa Bunge, litakuwa jambo la ajabu na aibu, na huo ndio utakuwa mwanzo wa kudidimia kwa demokrasia na kufifia kwa makali ya Bunge yaliyoanza kushika kasi katika siku za hivi karibuni.
Alisema mpaka sasa, kuna viporo vingi vya taarifa ambazo zinapaswa kutolewa kwa wabunge, lakini hazijatolewa.
Alitaja baadhi ya ripoti hizo kuwa ni ripoti ya kwanza na ya pili ya EPA, ripoti ya kamati ya madini na sasa ni hii ya hotuba ya Rais Kikwete,ambayo alisisitiza haoni sababu yakutojadiliwa sasa.
"Ni lazima tufike mahala, Bunge liache kupokea maagizo ya serikali, kwani sababu zilizotolewa haziridhishi, Bunge lina kumbukumbu zake, zilipaswa zitumike hizo kujadili hotuba ya rais," alisema Zitto.
Naye Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, alisema kuahirishwa huko kwa hotuba hiyo kutatoa nafasi kwa wabunge kuipitia kwa makini ili watakapoijadili, waweze kugusa maeneo yote.
Alisema kwa jinsi hali ilivyo, macho na masikio ya wabunge wengi yalijielekeza katika EPA wakati kama wakipata nafasi zaidi, wataweza kuichambua kwa umakini na kutoa mawazo yatakayoweza kujenga nchi.
Mbunge wa Maswa, John Shibuda (CCM), alisema uharaka wa Watanzania katika mambo mbalimbali, ndiyo sababu ya kutopatikana kwa suluhu nzuri, na wamekuwa wakitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani bila kujua kwamba kuna taratibu za kisheria ili mtuhumiwa apate fursa ya kusikilizwa.
Alisema tabia ya Watanzania kuhukumu watu kwa hisia, si jambo jema na Rais Kikwete katika hotuba yake kaligusia suala hilo kuwa si vema kumhukumu mtu kwa lengo la kumdhalilisha, kumfedhehesha na kumchafulia jina.
"Rais Kikwete katueleza wazi kuwa nia yake ni kuona watu hawabambikizwi kesi, sasa ni vema tukaacha tabia ya kuhukumu kwa hisia," alisema Shibuda.
Wiki iliyopita Spika Sitta, alipokuwa akizungumza na Tanzania Daima alisema hotuba hiyo itajadiliwa wiki hii, tena ingali moto, kwani kama ikisubiri kipindi kijacho, itakuwa imepoa na wabunge wanaweza wasichangie vema.
"Bwana mdogo, hotuba ya rais itajadiliwa katika mkutano huu, kwani mchuzi unywewe ungali moto, na nimemuagiza katibu wangu aingize jambo hilo katika ratiba, kabla ya kuliahirisha Bunge," alisema spika wakati huo.
Aidha, katika hatua nyingine, akizungumza jana, Sitta alisema siku ya Alhamisi ya wiki hii (Agosti 28), Waziri Mkuu Mizengo Pinda, atawasilisha utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge, kuhusu kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond.