Sehemu 02.
SEHEMU YA PILI
Bwana Oleg Gordievsky alizaliwa ndani ya KGB ,ikamkomaza,ikamtwist vilivyo na almanusura imhuharibie maisha . Kufanya kazi ndani ya idara kubwa ya kijasusi ndani ya muungano wa Soviet,kwake ilikuwa ni heshima kubwa sana na ni kazi iliyokuwa kwenye damu yake. Kwani baba yake amefanya kazi ndani ya shirika Hilo maisha yake yote. Familia ya Gordievsky iliishi kwenye apartment za shirika Hilo na walipewa special treatment na favor maalumu kwa kuwa wao walikuwa ni familia ya kitengo.
Shirika la kijasusi la KGB(komitet gosudarstvennoy bezospasnosti) kwa kiswahili sanifu ni kamati ya ulinzi la kitaifa, ilikuwa ni taasisi imara ya usalama kuwahi kuundwa hapa duniani. Shirika Hili lilizaliwa kutoka kwenye kikundi kidogo Cha majasusi watiifu wa mzee Stalin. Kazi Yake ilikuwa kukusanya taarifa nje na ndani ya muungano wa Soviet ,kutoa ulinzi ndani ya taifa ,pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya kijamaa.
Kwa kifupi shirika Hili lilikuwa limetawala nyanja zote za kimaisha kwa wale wote waliokuwa wapo chini ya muungano wa ki Soviet.
Lilikuwa ni shirika lililoajiri na kupandikiza majasusi duniani kote kwa ajili ya ,kukusanya ,kuiba ,na pia kununua taarifa mbalimbali za Siri ikiwemo za kijeshi, kisiasa, silaha pamoja na taarifa za kisayansi na teknolojia. Inakadiriwa kipindi hicho shirika likiwa katika kilele Cha mafanikio ilikuwa na ma agent takribani milioni na zaidi.
Kwa upande wa nchi za kimagharibi hii taasisi ilitazamwa kama zana ya kuwatia watu hofu,kutii wasichokijua,kuwatesa na kuwanyanyasa raia wake kidhalimu. Ilitazamwa kama kundi la kimafia chini ya mwavuli wa kikomunisti lenye kusambaza propaganda za kijamaa zilizopitwa na wakati .
Lakini kwa waliokuwa wanaishi chini ya muungano wa ki Soviet wao walichukulia KGB kama mlinzi wao,alama ya uzalendo na Utiifu kwa taifa na mamlaka,pamoja na ngao ya kuwalinda Raia dhidi ya umagharibi. Kuwa memba wa KGB ilikuwa ni heshima na sifa na pia alama ya ufahari kwa wakati huo.
Hivyo basi bwana Oleg hakuwa na la kupingana nalo zaidi ya kufuata nyendo za mshua wake bwana Anton lavrentyevich Gordievsky, na kuwa afisa wa KGB.
Baba yake Oleg kabla ya kuwa afisa wa KGB ,alikuwa ni mwalimu .lakini baada ya mapinduzi ya mwaka 1917 akaamua kujiunga na kuwa mwanachama rasmi wa chama Cha kikomunisti. Kilichomfanya baba yake Oleg kujiunga na ukomunist ni itikadi za mzee Stalin , ambazo zilikuwa Kali.
Alijiunga na chama Cha NkVD( baadaye sana ilimezwa ndani ya KGB) au taasisi ya kikomunisti kwa ustawi wa watu. Lengo la hii taasisi au chama ni kulinda maslahi ya kikomunisti ,kutoa ulinzi na vilevile kusambaza propaganda pamoja na kupambana na maadui wa urusi. Mzee Stalin alitangazia umma kwamba maadui wa urusi ni mabepari , mashoga,majasusi wa utawala uliopita,wayahudi , maofisa wa serikali wenye mrengo wa kibepari n.k. Hivyo bwana Anton alijitolea kwa udi na uvumba katika kulinda itikadi za kikomunisti. Alijitolea kufundisha propaganda kwenye kambi za kijeshi na taasisi za elimu . Tuseme kwa kifupi alikuwa ni mwenezi kama polepole.
Na katika kipindi hicho watu walianza kuonja ladha ya ukomunisti .watu walipotezwa, wengine walinyang'anywa Mali ,kufungwa na pia wengine walilazimishwa kuhama nchi. Na kubwa zaidi wengi walikufa na njaa kutokana na uzalishaji kuzorota mashamba na maghala kuchukuliwa na serikali. Japo mzee Anton alikuwa ni mwanachama mtiifu kwa chama na serikali lakini nafsi ilikuwa inamsuta.
Alimwoa Olga nikolayevna gornova mrembo wa miaka 24 aliyekuwa anafanya kazi kwenye ofisi za takwimu. Walihamia Moscow kwenye apartments zilizokuwa spesho kwa ajili ya maafisa wa NkVD. Mtoto wao wa kwanza aliitwa Vasili aliyezaliwa 1932. Mtoto wao wa pili alizaliwa miaka sita baadaye yaani 1938,aliyeitwa Oleg antonyevich Gordievsky tarehe 10 October.
Mtoto wao wa tatu aliitwa marina aliyezaliwa miaka Saba baadaye. Kwa kifupi ilikuwa ni familia ya kitengo. Watoto walikuwa vizuri na pia stahiki na treatment za kutosha walizipata kutoka serikalini kwa kuwa ni familia ya KITENGO. Familia ilikuwa na kulelewa katika itikadi za kijamaa ,na watoto walikuwa watiifu na wazalendo kwa serikali ya kisoviet. Waswahili wanasema kila familia Ina Siri zake . kwa nje familia ya mzee Anton ilionekana ni familia Bora na iliyostawi sana na majirani kuweza kuwa admire. Haikuwa hivyo. Mzee Anton nafsi ilikuwa inamsuta sana kwa mabaya aliyokuwa anayafanya kipindi Cha Stalin anashika hatamu. Mfano kupotezwa kwa watu,uporaji wa mashamba na vifo vilivyotokana na njaa.hii ilimsumbua sana nafsini mwake lakini alikausha na Siri yake moyoni. Mkewe , Olga hakuwahi kuukubali ukomunisti lakini atafanyaje ndio anaishi kwenye ndoa yenye itikadi hizo. Sababu ya kuchukia ukomunisti ni kwamba baba yake alinyang'anywa mashine zile za upepo za kuvuta maji ardhini na serikali,pia kaka yake alikamatwa kwa kosa la kupinga sera ya umiliki na kilimo Cha kwa pamoja na kupelekwa huko Gulag Jimbo lililoko mashariki mwa Siberia na kupotelea huko mazima. Pia aliwahi shuhudia majirani zake kipindi hicho wakifuatwa usiku na watu wasiojulikana na kuondoka nao asiwaone tena.
Familia ya mzee Anton kushoto na wanao wawili marina na Oleg wakiwa na umri wa miaka kumi hivi
Watoto wa mzee Anton Vasili,mdogo wao wa kike marina na Oleg Gordievsky.
Oleg na Vasili walitofautiana kwa umri wa miaka sita hivi.na walikuwa kipindi Cha vita. Kwa mfano Vasili akiwa mdogo, alishuhudia mateka wa kivita wa kijerumani wakipanga gwaride mitaa ya Moscow na kulazimishwa kutembea umbali mrefu wakinyanyaswa na kudhihakiwa kama wanyama. Baba Yao mara nyingi alisafiri sehemu mbalimbali za nchi kueneza propaganda za kikomunisti. Kwa upande wa Oleg ,yeye alikuwa ni mtu wa kujifunza na kusoma vitabu. Kwa umri wake mdogo alijifunza kusoma katekisimu ya ki orthodox yenye mrengo wa kikomunisti. Pia alikuwa ni mtu wa kujifunza lugha na hatimaye alionyesha uwezo mkubwa katika kujifunza kijerumani. Baba yake Oleg alikuwa kila akirudi lazima aje na magazeti yenye itikadi za kikomunisti hivyo akawa na wasaha wa kuyasoma. Ingawaje alikuwa anasoma vitabu vya propaganda dhidi ya magharibi alivutiwa na maswala, kadhaa ikiwemo lugha za huko. Rasmi Sasa Oleg alivyofika umri wa utineja akajiunga tuseme UVCCM ya huko iliyojulikana kama KOMSOMOL.
Oleg alikulia kwenye familia yenye upendo baba yake akiwa mwanachama rasmi wa KGB,na mama yake pia akiwa mke wa afisa ,mama wa nyumbani, lakini ndani ya mioyo Yao Hawa wanandoa wawili walikuwa wanafeki tu kwa nje lakini ndani mwao kulikuwa na vidonda kuhusu madhila ya mfumo mzima wa kikatili wa kikomunisti.hakuna aliyewahi jionyesha kwamba anadukuduku lake dhidi ya mfumo.
Kwa kipindi hicho Cha utawala wa Stalin familia ya Anton Gordievsky waliamini kwamba unaweza ukawa mtiifu kwa serikali ya kikomunisti , lakini ukawa una amini jambo lingine kwa Siri sana Japo ilikuwa ni jambo la hatari ya maisha. Kwa mfano hapa kwetu uwe mtiifu kwa serikali ya ccm lakini ndani ni mwanachama mtiifu kabisa wa upinzani.
Umahiri wa Oleg ulidhihirika akiwa na UVCCM Yao ya KOMSOMOL kwa kupewa medali ya silver kama kijana mwenye akili , shupavu,mwenye bidii katika michezo na vilevile mzalendo haswa kwa nchi yake .licha ya hayo yote Oleg Gordievsky alijifunza kuishi maisha ya aina mbili.