Mzee Mkandara, heshima yako na pole sana na hiki kisanga!
Binafsi, nitaandika makala kuhusu haki za Zitto na ikiwezekana niombe ichapishwe na gazeti lolote. Hata hivyo, ni vigumu sana kumtetea Zitto kwasababu dhamiri zetu zinatusuta. Mzee Mkandara, swali lako jibu ni hapana. Hili Bunge halina haki ya kumsimamisha Mbunge aliyechaguliwa na wananchi. Lingekuwa Bunge ambalo wabunge wote wamechaguliwa na wananchi, jibu lake lingekuwa ndiyo wanaweza.
Jamani, hili Bunge sio halali, kikatiba na kiutendaji, hivyo maamuzi yote yanayofanywa na hili Bunge sio halali. Utangulizi wa katiba ya nchi yetu umeweka msingi kwamba tunajenga jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Katiba inaendelea kusema kuwa misingi hiyo itasimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi. Hili Bunge lina wabunge ambao hawakuchaguliwa na wananchi hivyo hawawakilishi wananchi.
Leo hii tunajiuliza kwamba inakuwaje Bunge la namna hii limsimamishe Mbunge aliyechaguliwa na wananchi? Lakini tumewahi kujiuliza kwamba inakuwaje katiba ya nchi yetu inatoa mamlaka kwa vyama vya siasa kumfuta kabisa Mbunge aliyechaguliwa na wananchi? Yaani kamati kuu ya CCM ikimfukuzuza uanachama Mbunge yeyote, basi na Ubunge wake unakoma palepale. CHADEMA ikimfukuza uanachama Mbunge yeyote, basi na Ubunge wake unakoma papo kwa papo bila kujali amechaguliwa na wananchi au la. Haya yote yako kwenye maandishi na wabunge walichokifanya ni kuweka mojawapo kwenye matendo.
Leo hii tunaweza kuhoji uhalali wa Bunge kumfukuza mbunge bila kuhoji uhalali wa vyama vya siasa kumfukuza Mbunge? Yote tisa, kumi ni je, haki ya Mbunge inaweza kutenganishwa na haki ya wananchi? Jibu ni hapana. Je haki ya mwananchi inaweza kutenganishwa na haki ya Mbunge? Jibu ni ndiyo kwasababu viraka katika Katiba yetu vimeweka masharti katika haki ya mtu kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi. Nyerere alituasa kuwa dhambi ya ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu, ukisha kuitenda hautakoma.
Ndiyo maana ni vigumu sana kumtetea Zitto kwasababu yuko ndani ya Bunge linalowanyanganya watu haki zao kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa. Ubaguzi kumbe haukukoma kwa wananchi ambao sio wanasiasa bali umeanza kuwatafuna wanasiasa wenyewe ambao wako ndani ya Bunge. Wengine wanasema kuwa leo ni siku ya giza kwa taifa letu kwasababu Zitto amenyanganywa haki yake. Well, binafsi nadhani siku ya giza ilikuwa pale Bunge lilipo wanyanganya wananchi haki yao ya kuwawakilisha wenzao. Leo ni matokeo ya ile siku.
Sasa Zitto afanye nini? aende kwa wananchi katika jimbo lake? Atawambia nini? Aseme tuungane kudai haki yangu niliyopokonywa na Bunge? Akitoka mtu akamuuliza swali kuwa unasemaje kuhusu haki zetu ambazo hazikusimamishwa kwa muda bali zilifutwa kabisa ndani ya katiba na Bunge hilohilo ambalo wewe ni mjumbe, atasema nini? Je haki ya Mbunge ni bora kuliko haki za wananchi?
Tutafika mahala tutambue kuwa hakuna kitu kinaitwa maslahi ya taifa, hakuna kitu kinaitwa mgombea binafsi, hakuna kitu kinaitwa Mbunge, hakuna kitu kinaitwa nchi. Kuna kitu kinaitwa watu ambao wana haki zao za msingi walizozaliwa nazo. Hizi haki wamepewa na Mungu hivyo hakuna kiumbe yeyote mwenye haki ya kuzifuta. Watu ndio wanaunda Bunge, nchi, Taifa, n.k. Unapofuta haki za watu unakuwa umefuta maslahi yao ambayo ndio maslahi ya Bunge, nchi, na taifa. Huwezi kutenganisha maslahi ya watu na maslahi ya taifa.
Kwa mara nyingine, natoa wito kwa wabunge wenye nia njema kujiuzulu ubunge wao ili tuungane na wananchi kudai haki zetu ambazo zitaandikwa ndani ya katiba mpya. Juhudi zote za kulitoa Bunge mikononi mwa wanasiasa na kulirudisha mikononi mwa wananchi lazima ziungwe mkono na zisichukuliwe kiushabiki.