THE MODERN WAR
(Vita ya kisasa)
Sehemu ya...............36
Mtunzi: Saul David
Email:
saulstewarty@gmail.com
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA...
Walikuwa ni wanawake waliotembea kikakamavu sana Osward akiwa katika yao, walitembea na kuingia ndani ya helkopta iliyokuwa ikiwasubiri. Mara tu baada ya wote kuingia rubani alifanya kazi yake na mara helkopta ile ikazunguusha panga zake na taratibu ikaachia ardhi na kupaa hewani.
Je, nini kitafuata?
SASA ENDELEA...
[emoji294][emoji294][emoji294]
"Mama yako anarudi leo kutoka marekani, atafika saa saba mchana. Nahitaji kukamilisha ratiba zangu mapema kisha twende uwanja wa ndege tukampoke"
"Sawa baba, nitakuwa hapa nakusubiri twende wote"
"Vipi hauendi kusikiliza kesi ya mchumba wako Osward?"
"Ooh! Nilishasahau baba hivi ni leo?"
"Mmh! Mwanangu inaelekea huyo Inspekta Aron anakuchanganya sana mpaka umeanza kusahau mambo muhimu"
"Hapana sio hivyo baba mbona nimeshakuelekeza kila kitu kuhusu Inspekta Aron, yule ni rafiki yangu tu"
"Haya sawa, kesi yake inasikilizwa leo kwa mara ya mwisho na hukumu itatolewa nina imani atashinda na kuachiwa huru, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kama yeye ndiye aliyeua"
Haya yalikuwa ni maongezi kati ya Najma na baba yake Dokta Gondwe ikiwa ni asubuhi na mapema majira ya saa moja.
"Basi sawa nitaenda"
"Ndio mwanangu ni muhimu sana ukawepo pale ili msherehekee ushindi kwa pamoja"
"Sawa baba, vipi wewe hautokuwepo?"
"Mmh! Nikipata muda nitakuja ila asubuhi hii nakutana na waandishi wa habari kwanza baada ya hapo nitaenda kuonana na Rais ikulu, kama muda utakuwepo nitakuja mahakamani" alieleza Dokta Gondwe
"Waandishi wa habari unakuta nao mda gani?"
"Sio mda, saa mbili na nusu pale nje ya jengo la Maendeleo CFC"
"Sawa ni kuhusu ile kashfa si ndio baba"
"Ndiyo mwanangu, baba yako nimechafuliwa sana mitandaoni mimi na serikali yangu, nahitaji kutumia nguvu kubwa kusafisha jina langu na kuweka mambo sawa, mama yako amekasirika sana naongea naye hataki kabisa kuelewa"
"Ndio maana anarudi bila hata kuniambia?"
"Ndiyo Najma, ki ukweli mama yako ana hasira sana"
"Usijali baba kila kitu kitakuwa sawa, naamini hakuna ukweli wowote hapo tunaimani na wewe baba" Najma alijaribu kumpa maneno ya faraja baba yake, mwisho wakaagana Dokta Gondwe akaingia kwenye gari yake akiongozana na walinzi wake wawili safari ya kuelekea ukumbuki wa Maendeleo CFC sehemu aliyopanga kukutana na waandishi wa habari ikaanza.
Huku nyuma Najma nae alijikuta anatamani kuona namna baba yake atakavyokuwa akiongea mbele ya waandishi wa habari, alichukua fungua ya gari la familia aina ya Noah akaingia na kuanza safari akimfuata baba yake nyuma taratibu.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Wakati Dokta Gondwe akiwa bado njiani mara simu yake iliita alipoitazama namba ya mpigaji ilikuwa ni ile ya mtu aliyekubaliana nae kumpa vimelea vya V-COBOS mtu mwenye video yake chafu. Ilikuwa ni namba ya ajabu ambayo inapiga tu lakini yeye hawezi kupiga wala kutuma ujumbe wa maandishi, ni namba ambayo hutoweka hewani na kuwa namba ambayo haipo mara tu baada ya simu kukata.
"Hallo"
"Ndiyo Dokta Gondwe" sauti ya ajabu iliyojaa mwangwi na kitetemeshi kikubwa ilisikika upande wa pili, Tino ndiye aliyekuwa akizungumza lakini haikuwa rahisi kwa Dokta Gondwe kumtambua.
"Nakusikia ndugu yangu"
"Sisi tumeshamaliza kazi yetu, umebaki wewe tu. Tulikubaliana ndani ya siku tatu uwe umetupatia virusi vya COBOS la sivyo basi tusije kulaumiana"
"Naelewa ndugu yangu siwezi kuwageuka, mmenisaidia sana kupost ile picha ya pili isiyo na sura yangu hivi naenda kuongea na waandishi wa habari kwa mara nyingine baada ya hapo nitaanza mpango wa kuwaletea vimelea vya V-COBOS" Dokta Gondwe alijieleza kwa unyenyekevu mkubwa.
"Lini sasa"
"Leo jioni, nipigie simu leo jioni nitawambia ni wapi pa kukutana niwakabidhi vimelea"
Kauli hii ilimfurahisha sana Tino, alijiona kabisa namna anavyokwenda kushinda vita hii kwa kuvipata vimelea vya V-COBOS, hakujua kuwa mtu anaemtegemea tayari yupo hatarini kuuwawa ikiwa ni agizo kutoka ZMLST ya Mexico wamiliki wakuu wa vimelea vya V-COBOS. Ukiachilia mbali kuhusu hao wazungu wanaotaka kumuua waziri wa afya Dokta Gondwe lakini pia kulikuwa na balaa la Sultana na kijana wake wa kazi Jasusi Shadow ambaye alipanga leo hii kuvamia maabara kuu ya serikali na kuviiba vimelea vya V-COBOS, swali linabaki kuwa ni nani ataibuka mshindi.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Nyumbani kwa Inspekta Jada..
"Jada, vipi Annah bado amelala?" Aliuliza Aron
"Mmh! Nikikwambia kitu basi unaweza kuamini" alisema Inspekta Jada huku akitabasamu na kuangalia pembeni
"Nini hicho?"
"Huyu binti ndio ameingia sio mda kulala"
"Eeh! Una maana gani usiku wote alikuwa wapi? Au alikuwa analia?"
"Walaa"
"Alikuwa wapi sasa?"
"Alinitoroka chumbani akaja akakaa hapo"
"Hapo wapi?"
"Kwenye kona hapo ameshinda anakuangalia wewe usiku kucha"
"Nini? Annah huyu... Hebu acha utani wako basi"
"Wallah nakuambia ukweli Inspekta Aron, huyu binti naona anakupenda tena sio kidogo sana tu"
"Acha masihara yako basi Jada"
"Kweli tena"
"Haya hebu tuachane na hayo basi, ratiba imekaaje!?"
"Kesi itaanza kusikilizwa saa tano asubuhi, itakuwa sapraizi kubwa sana watakapomuona Annah yuko hai mtu wanaeamini kuwa walimuua"
"Sana tuombe mungu tu kila kitu kiende vizuri" alisema Aron
"Vipi kwani unawasiwasi Aron?"
"Yeah kiasi, unajua mpaka sasa sijui ni kwa nini kesi haikusikilizwa jana na badala yake wakataka iwe leo"
"Mmh! Kwa hiyo unahisi kuna kitu hakipo sawa?"
"Ndiyo hisia zangu zinaniambia hivyo"
"Sawa, muhimu ni kuongeza umakini tu Inspekta Aron, Annah ndio kete yetu ya muhimu kuliko vingine vyote, huyu ndio atakayefanya Osward afungwe lakini pia kumuweka hatiani Dokta Gondwe"
"Sawa Jada, kwa hiyo tunafanyaje twende na Annah ofisini tukae nae hadi mda utakapofika ndio twende mahakamani au tumuache huku tutamfuata baadae?"
"Mmmnh! Hapo mimi nawaza tumuache huku hadi muda utakapofika ndio tumfuate"
Walikubaliana hivyo lakini kabla ya kuondoka Inspekta Aron aliingia chumbani akitaka kwanza kufanya mazungumzo na Annah.
"Samahani nimekuamsha"
"Usijali Aron, niambie"
"Sisi tunatangulia kazini muda wa mahakamani ukifika nitakuja kukuchukua" alieleza Inspekta Aron
Annah alitulia kwa muda kisha akaongea...
"Aron"
"Yes Annah usijali naona kama unawasiwasi, niamini mimi kila kitu kitakwenda sawa nitahakikisha wote waliohusika na mauaji ya wazazi wako wanawajibishwa ipasavyo, leo tunaanza na Osward alafu baada ya hapo Dokta Gondwe na wengine watafuata"
"Tatizo sio hilo Aron"
"Ni nini Annah" aliuliza Inspekta Aron huku akimtazama Annah usoni, Annah naye akainua uso wake na kumtazama Aron wakatazamana.
"Ukweli siwezi tena kuendelea kujizuia Aron, haijarishi nini kitatokea huko mahakamani kushinda au kishindwa lakini sitoweza kuondoka na ndugu zangu, nataka kubaki na wewe Aron nakupenda, nakupenda sana. Nina hisia za kimapenzi kwako moyo wangu umeshindwa kabisa kuvumilia najua utaniona mwanamke wa ajabu lakini sio kosa langu Aron ni moyo, Nimekupenda" Annah alijieleza huku akiwa ametazama chini na kuchezea chezea vidole vyake.
Inspekta Aron alibaki ameduwaa kwa muda hakuwahi kuwaza kama siku moja Annah angekuwa na ujasiri wa kuongea maneno kama yale mbele yake licha ya kuona dalili za Annah kumpenda lakini hakuwahi kuwaza kama siku moja angekuja kutamka mwenyewe kwa kinywa chake.
"Annah" Inspekta Aron aliita
"Tafadhali usiseme neno lolote Aron, nilikuwa tu naeleza hisia zangu kwako najua haukuwa ukitegemea, nimeongea mimi leo wewe utaongea siku nyingine sawa baba" Alisema Annah huku akitembea na kwenda kukaa kwenye kona ya kitanda, Aron akataka kuzungumza lakini mara Inspekta Jada akaingia ghafula.
"Aron tuwahi kazini tafadhali kuna mambo mengi ya kufanya kabla ya kwenda mahakamani" alisema Jada huku akichukua koti lake refu kabatini, akalivaa na kutoka.
Aron alimtazama Annah usoni, Annah akampa ishara kuwa aende. Taratibu Aron alisogea karibu yake akamkumbatia kwa sekunde kadhaa...
"Nitarudi kwa ajili yako Annah, usijali" Alisema Aron kisha akamuachia na kuondoka.
Waliongozana na inspekta Jada kuelekea lilipokuwa gari lake.
"Si nilikwambia" alisema Jada
"Kuniambia nini?" Aliuliza Aron
"Kuwa haka ka binti kanakupenda"
"Aah! Kwa hiyo ulikuwa unasikiliza?"
"Hahah ndo maana nikaingia kukusaidia, mwanaume mzima unajiumauma unashindwa kutoa jibu, mtoto mbichu yule shauri ako, au usharusha nyavu kwa Najma nini?"
Alisema Inspekta Jada na hapo wote wakacheka kwa pamoja wakati huo tayari safari ya kuelekea kituo cha polisi cha kati Morton ilianza.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Rais mstaafu Profesa Cosmas Kulolwa alionekana amesimama juu kabisa ya nyumba yake yenye urefu wa ghorofa nne, alikuwa akilitazama jiji ikiwa ni asubuhi ya mawio wakati jua likichomoza, alichukua simu yake akapiga namba fulani na kuiweka simu sikioni.
"Hallo mkuu" sauti ya Osward ilisikika upande wa pili wa simu ile
"Nambie mambo yanaendaje"
"Kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa mheshimiwa, nitamuua Dokta Gondwe wakati anafanya mazungumzo na waandishi wa habari, Inspekta Aron atashughulikiwa na wale mabinti Malaika weusi tayari wapo kazini, baada ya hapo nitarudi gerezani kisha nitapelekwa mahakamani" Osward alisikika akieleza
"Sawa hakikisha hakuna anayekuona ukiwa nje ya gereza, saa nne kamili uwe umerudi pale tulipokutana usiku, yule askari atakusindikiza kukurudisha gerezani kwa siri kama ilivyokuwa mwanzo. Kila kitu kipo sawa usijali"
"Sawa mheshimiwa" alijibu Osward kisha simu ikakatwa.
"Oops! Rafiki yangu kipenzi tena wa kitambo sana, tangu tukiwa shuleni, tumesoma wote nje ya nchi, tumeingia kwenye siasa kwa pamoja nikawa Rais ukawa Waziri wa afya lakini leo nalazimika kuyaondoa maisha yako mimi mwenyewe, nisamehe sana Dokta Isaack Gondwe" Profesa Kulolwa alikuwa akiwaza huku akilegeza vifungo vya shati lake na kuvuta pumzi ndefu.
Je, nini kinaendelea kwenye mkutano wa Dokta Gondwe na waandishi wa habari?
Osward atamuua Dokta Gondwe?
Vipi kuhusu Najma ambaye atakuwepo eneo la tukio?
Vipi kuhusu kesi ya Osward mahakamani?
Wale wanawake watatu wanaojiita Malaika weusi watafanya nini?
Inspekta Aron atakuwa salama?
TUKUTANE SEHEMU INAYOFUATA...
Simulizi ni shillingi 1,000/= lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina saul au Airtel money namba 0788967317 jina saul kisha njoo WhatsApp inbox namba hizo hizo