TAHARIRI YA GAZETI LA MTANZANIA (5/1/2007) NI YA KISHABIKI NA YENYE KUPOTOSHA KAULI YA KWELI YA MBOWE KUHUSU MAKAMBA NA CCM
CHADEMA tunatambua uhuru na mchango wa vyombo vya habari kama mhimili muhimu wa kuleta demokrasia na maendeleo. Hata hivyo tumekuwa pia wakati wote tukisisitiza kwamba vyombo vya habari vitangulize mbele ukweli na maadili ya sekta ya habari. Tumeshangazwa na maoni ya mhariri ya gazeti la Mtanzania la Januari 5 mwaka 2007 hasa tukizingatia kwamba gazeti hili ni moja ya magazeti ambayo yamejijengea sifa huko nyuma.
Inasikitisha zaidi kwamba tahariri hiyo huitwa Maoni Yetu ikiwakilisha maoni ya bodi ya wahariri, kwa yoyote ambaye amesoma tahariri hiyo atakuwa atakuwa amejiuliza kama kweli ni timu ya watu makini imekaa na kuandika maoni hayo ama ni mawazo ya mtu binafsi.
Mosi, maoni hayo yamejaa ushabiki wa kisiasa yakiwa na vionjo mbalimbali kwa ziara ya CHADEMA inalenga kuwashukuru wananchi waliokipa chama kura chache na kujipitisha kuonyesha kwamba chama kipo bado , Mbowe anaupotosha umma kwa kuzusha mambo ambayo si ya kweli na kwa kufanya hivyo kuwachonganisha wananchi dhidi ya chama tawala na serikali yake waliyoiamini pasipo na shaka yoyote(mhariri alipaswa kufahamu kuwa CCM haikushinda kwa asilimia mia na alipaswa kujua pia kwamba Rais Kikwete ametangaza kuwa hapendi kupewa sifa za uwongo na amekiri wazi kuwa kuna mapungufu kadhaa katika mwaka mmoja wa utawala wake), Mbowe hasemi ukweli na hii ni hatari sana kwa mustakabali wa ustawi wa siasa katika nchi hii nk.
Lakini pili, maoni hayo hayana ukweli wowote na ni dhahiri kwamba yalilenga kupotosha. Na ushahidi wa suala hili uko katika maoni yenyewe ya mhariri !. Tahariri imeanza kwa kujenga mazingira kwa msomaji ya kudhihaki ziara ya CHADEMA lakini pia kujenga picha kwa msomaji kwamba Mbowe anatishia mustakabali wa Taifa, lakini kichekesho ni kuwa tahariri inatolea mfano suala moja tu ambalo linamfanya Mbowe atishie mustakabali wa Taifa nalo ni kusema kuwa Kwamba Makamba hajui siasa inavyokwenda na wala kwamba hajawahi kugombea nafasi yoyote ya kisiasa ya kupigiwa kura na wananchi.
Hivi kauli hii hata kama ingekuwa si ya kweli inatishia maisha kiasi gani hata kuchambuliwa katika maoni ya mhariri ?. Wasomaji tumezoea kuwa maoni ya mhariri ni mahali kwa wahariri kujadili na kutoa maoni yako kuhusu masuala nyeti ya kitaifa. Ukurasa wa mbele wa gazeti la toleo ya siku hiyo ulibeba habari ya msiba wa Waziri Akukweti(Mungu amlaze mahali pema), IGP kucharukia wauza nguo zinazofanana na sare za Jeshi na Kawawa kuitaka SUA isipoteze maana ya kuanzishwa kwake.
Masuala haya na hii kauli ya Mbowe kuhusu Makamba kipi kilipaswa kutolewa maoni na wahariri kwa maslahi ya taifa ? Katika mazingira ya kawaida ilipaswa baada ya Mbowe kama mwanasiasa kutoa kauli Makamba naye ajibu kama mwanasiasa badala ya ukurasa wa mhariri wa maoni yetu kutumika kama ofisi ya itikadi na uenezi ya CCM ama mhariri kuwa kama mwandishi wa habari wa Makamba!
Lakini kubwa kuliko yote ni kuwa kauli aliyoitoa Mbowe ni ya kweli, na tahariri yenyewe imetoa ushahidi wa ukweli huo. Katika sehemu ya kwanza ya kauli yake Mbowe alisema kwamba Makamba hajui siasa inavyokwenda, tahariri imesema kwamba muktadha wa Mbowe kusema hayo ni kauli ya Makamba kwamba vyama vya upinzani vitakufa.
Hivi kiongozi mwandamizi akisema vyama vya upinzani vitakufa anajua kweli siasa inavyokwenda ? Mhariri amekwenda mbali zaidi kutoa ushahidi wa uwezo wa Makamba kujua siasa ni kuwa alitunga na kuimba nyimbo nyingi wakati wa TANU! Ushahidi wa namna hii ulilenga kumsafisha au kumdhihaki mheshimiwa Makamba ? Kwa ushahidi kama huu mwanasiasa kama Mbowe anakuwa na kosa gani kusema kwamba Makamba hajui siasa inavyokwenda?
Sehemu ya pili kauli ya Mbowe amenukuliwa akisema kwamba Makamba hajawahi kugombea nafasi yoyote ya kupigiwa kura na wananchi. Mhariri anatoa ushahidi kwamba Mbowe hajasema kweli na kwamba Makamba amewahi kugombea ujumbe wa halmashauri kuu ya Taifa CCM akiwakilisha mkoa wa Tanga?
Hivi mjumbe wa NEC CCM anachaguliwa na wananchi ? Ni wazi anachaguliwa na wanachama wa CCM na si wananchi. Kwa mantiki hiyo, kati ya Mbowe na mhariri nani hajasema kweli ? Kwa hiyo ni ukweli kwamba Makamba hajawahi kuchaguliwa na wananchi hata nafasi ya mwenyekiti wa kijiji.
Kwa upande wake Mbowe alichaguliwa na wananchi kwa asilimia kubwa kuwa mbunge wa jimbo la Hai kuanzia 2000 mpaka 2005. Katika hali hiyo gazeti linapaswa ama kukiri mapungufu hayo ama wasomaji wa Mtanzania watapata hisia kwamba gazeti hili linatumika kubomoa CHADEMA na itakapobidi tutachukua hatua za kufaa na inapobidi kuwataka wanachama wetu kuacha kununua, kusoma ama kutangaza katika gazeti hili. Na rahisi kuwa na hisia hizi kwa kuwa taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba gazeti hili sasa linamilikiwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM na si mara ya kwanza kutoa taarifa potofu kuhusu CHADEMA. Na kama hivyo ndivyo basi gazeti lieleze upya sera yake kama bado ni katika kusimamia ukweli na haki ama ni mashine ya propaganda za kisiasa za CCM na serikali yake !
Mwisho :
Tunasikitika kwamba tumetumia muda wa wananchi kusoma taarifa hii ndefu. Kodi za wananchi zilizomo kwenye ruzuku ya chama na michango ya wanachama kutoa tamko hili. Tumetumia vile vile muda katika kuandaa taarifa hii ambao ungetumika kwa shughuli nyingine za kuleta demokrasia na maendeleo nchini.
Hii yote inatokana na watu waoamua kupotosha. Na tunasikitika zaidi CCM na taasisi nyingine zinapotumia fedha za umma na wanachama wao kusambaza uzushi. Tumeamua kujibu tukiamini kuwa ukweli ni uhuru! Tungependa kuwakumbusha watu wa jamii hii kwamba siasa sio uadui, CHADEMA kama chama mbadala ni chombo kinachopaswa kuheshimiwa na watanzania wote wapenda maendeleo.
CHADEMA kwa upande wake kitaendelea kutimiza wajibu wake. Tumemaliza ziara awamu ya kwanza. Tutaanza tena mchakato wa kwenda maeneo mbalimbali kujenga oganizesheni ya chama na kufanya uchaguzi ndani ya chama kupitia mpango wa CHADEMA ni Msingi. Tunajiandaa vilevile kwenda awamu ya pili ya ziara ambayo itahusisha mikoa iliyobaki. Aidha wakati wote tutaendelea kushirikiana na raia wote bila kujali itikadi kuhakikisha serikali iliyoko madarakani inatekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi. Hakuna kulala, mpaka Kieleweke.
CHADEMA : Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli
Imetolewa 6/1/2007 :
Erasto Tumbo
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
0713 47 47 07
info@chadema.net
www.chadema.net