haya ni MAONI YA MH FREEMAN MBOWE KWENYE GAZETI LAKE LA TANZANIA DAIMA, NAOMBA TUISOME KWA MAKINI NA TUTOE MAWAZO YETU, LAKINI NI FIKRA MBADALA KWA KUSHINDWA VIBAYA KWENYE UCHAGUZI ULIOPITA.NCHI YETU NI NCHI YA DEMOKRASIA BW MBOWE ANA UHURU WA KUZUNGUMZA KWA KILE ANACHOKIONA, LAKINI YANA UKWELI, YANA MALENGO NA MWELEKEO MZURI KWA WATANZANIA? AU NI MILINDIMO MIZURI YA MIZIKI INAYOWATAKA WATU WATOKE KWENYE VITI ILI WAANZE KUCHEZA?
mSOME MHESHIMIWA MAWAZO YAKE HAPO CHINI
Freeman Mbowe
KAMA ilivyo kawaida, ukiandika ukatoa hoja, tarajia maswali, pongezi na hata kejeli kutoka kwa wasomaji. Majibu yatategemea aliyeguswa kaguswa vipi.
Leo, nitajikita kwenye swali moja ambalo nimeulizwa.
Waungwana wamesema: Mbowe tumekusikia na kukusoma hoja zako kuhusu mustakabali wa nchi yetu; sasa tufanye nini? Nashukuru kwa changamoto hii. Kama Mtanzania na zaidi kama kiongozi, nina wajibu wa kuweka fikra zangu wazi. Wenye hekima na busara wazitafakari. Wenye husuda wabeze!
Mawazo yangu si msaafu. Ni fikra mbadala ambazo zinakusudia kujenga hoja mjadala.
Ninaamini wako Watanzania wengi wenye uwezo mkubwa sana wa uongozi. Lakini mfumo wetu hauwapi fursa. Sasa si siri, nchi yetu imekwama. Ni dhahiri Rais Jakaya Kikwete amelemewa. Yeye hataki au pengine hana ujasiri wa kukiri kuwa chama anachokiongoza hakina jibu la umaskini wa Watanzania.
Taifa lolote lililokwama linahitaji mabadiliko. Mabadiliko hayo huweza kuja kwa njia mbili. Ama kwa mtindo wa kutumia nguvu, yaani mapinduzi (revolution), au kwa mtindo wa amani, yaani mageuzi (reforms).
Ni dhahiri kuwa Watanzania wanapendelea mabadiliko kwa njia ya amani, yaani reforms. Tangu tumepata uhuru, Tanzania imefanyiwa majaribio mengi sana ya kisiasa, kijamii na hata ya kiuchumi, lakini majaribio haya hayakutukwamua. Bado tumekwama. Yako maeneo machache tuliyopiga hatua kama taifa. Lakini mafanikio machache tuliyopata hayalingani na utajiri wa asili wa nchi yetu. Aidha, hayalingani kabisa na umri wa miaka 46 ya uhuru wetu.
Ni kweli subira huvuta heri, lakini subira inapoendelea kutumbukiza taifa kwenye lindi la umaskini, subira hii hukaribisha shari! Ni rahisi kufikiria kuwa kukwama kwetu leo ni tunda la ufisadi wa viongozi. Ni kweli hili linachangia. Tukumbushane historia kidogo. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliongoza taifa hili kwa miaka 25. Alikuwa kiongozi aliyependwa sana na watu. Hakuwa fisadi na wala serikali ya awamu yake haikuwa ya kifisadi. Pamoja na uadilifu wa Mwalimu, bado nchi hii, ilikwama sana kiuchumi na hivyo kimaendeleo!
Kama taifa, tuna wajibu wa kutafakari tumekwama wapi? Ni dhahiri kuwa kutokomeza ufisadi pekee si suluhisho pekee la kuipeleka nchi yetu kwenye neema. Na wakati mwingine nimekuwa nikihoji: Je, inawezekana amani yetu tunayojivunia ndiyo sababu ya kukwama kwetu? Sihitaji kujadili utajiri wa Tanzania. Wote tunaujua.
Katika kujadili kukwama kwetu na kupendekeza suluhisho, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, nilizungumza kwa nguvu kubwa mambo kadhaa. Leo nitaanza kujadili machache ya msingi kama changamoto kwa Watanzania. Nilijenga hoja: Kwamba mfumo wetu wa utawala ndiyo chimbuko la umaskini na kukwama kwetu. Kwamba hata ukimleta malaika ukamweka Ikulu awe Rais wa Tanzania, kwa mfumo wetu wa utawala uliopo, lazima atakwama! Kwamba utajiri wetu wa asili ndio utatumika kama chanzo cha kubomoa mshikamano wa taifa.
Kwamba, kwa matendo ya watawala wetu, ni wazi kwamba wamemsahau Mungu! Kwamba amani yetu ni tete! Sera iliyosikika sana wakati wa uchaguzi ni ile ijulikanayo kama sera ya majimbo. Sera hii ilikusudia (na inakusudia) kujibu hoja na hofu yetu kuwa mfumo wetu wa utawala ndio msingi wa kukwama kwetu.
Mada hii ni ndefu. Nakusudia kuijadili kwa kina na kwa mapana yake katika mfululizo wa makala kadhaa. Niliamini niliyozungumza wakati ule. Bado nayaamini. Hatimaye, nitayaandikia kitabu, ili dira yangu ibaki kama kumbukumbu kwa vizazi vijavyo. Kama ilivyotarajiwa kwenye ushindani wa kisiasa, wapinzani wangu wakiongozwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, walipotosha kisha wakabeza hoja zangu, tena kwa kejeli kubwa!
Kikwete aliponda asichokielewa. Alichokuwa anawaeleza wananchi si sera ya majimbo bali ni uzushi wa CCM. Natumaini naye sasa atasoma na aelewe. Kama ninavyosema siku zote, jamaa hawa kwa propaganda ni hatari!
Katika demokrasia ya mfumo wa vyama vingi, chama cha siasa kina wajibu wa kutoa dira ya nchi. Chama kinakuwa chimbuko la fikra. Fikra hizo zinatekelezwa na serikali. Chama kinaweka misingi ya kiitikadi, serikali inatengeneza sera na kuzitekeleza. Mageuzi yanayolikwamua taifa lolote huanzia kwenye mageuzi ya kifikra. Mageuzi ya kifikra hupatikana tu pale walio kwenye madaraka wanapotambua kwamba uongozi wa nchi ni dhamana na si miliki yao.
Ni pale tu wanapokubali ukweli kuwa rais na hata viongozi wengine wa juu peke yao hawawezi kuliletea taifa neema. Ni pale tu watakapoheshimu kuweka mifumo mizuri itakayotoa fursa kwa wote wenye uwezo wa uongozi kupata nafasi hizo kwa misingi ya chaguzi zilizo huru na za haki.
Kikwete na timu yake waliingia madarakani bila fikra wala dira. Ndiyo sababu alikiri kuwa wale wanaotegemea mabadiliko wasahau, kwani anataka kufuata yale ya waliomtangulia kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya! Waingereza wanasema business as usual! Yaani, mambo yaleyale! Kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, si dira! Si itikadi! Si sera! Ni kaulimbiu. Ni vibwagizo vya uchaguzi! Ni mbwembwe! Ni sanaa.
Watu waliopewa au kujinyakulia dhamana dhidi ya watu wao wanapokosa fikra na dira zao wanazoziamini, huwa watawala, na hivyo kusababisha utupu (vacuum) wa dira. Wanapokuwa na fikra zao wanazoziamini huwa na dira, nao huwa viongozi. Huongoza watu wao kuelekea kule wanakokuamini, hata kama ni kubaya.
Panapotokea utupu (vacuum) wa fikra za wenye dhamana, fikra za nje huziba utupu huo. Katika mazingira haya wanajitokeza wengi kujaza utupu huu kwa kuwa madalali wa watawala. Wanageuza Ikulu kuwa gulio. Hili ndilo linaloisibu nchi yetu. Tangu Baba wa Taifa aondoke madarakani, nchi imekosa fikra na dira. Viongozi wameacha kufikiri au hawana uwezo wa kufikiri? Utupu huu wa kukosa fikra mbadala za ndani, unawafanya viongozi wetu kila kukicha kutimkia nje ya nchi kusaka mawazo na fikra mpya. Ni dhahiri watu wa nje wakijaza utupu wetu, watajifaidisha kwanza wao!
Tahadhari! Katika historia ya dunia, hakuna taifa lililoendelezwa na fikra za taifa jingine. Kila taifa huvutia kwake kwa kuchuma kwa wengine. Fikra zitakazokomboa taifa hili lazima zitoke huku huku. Watu wapo! Vichwa vipo! Vimebanwa na mfumo. Nieleweke hapa! Sikatai wawekezaji. Ila sikubali kuwa ufumbuzi wa matatizo yetu ya umaskini utaletwa na wawekezaji na wafadhili wa nje. Sasa narejea kwenye hoja! Chimbuko la fikra ya hoja ya sera ya majimbo
Naam! Baada ya kutafiti kwa kina, kwa upande mmoja nilibaini kuwa ukubwa wa nchi yetu na utajiri wake wa asili vimelemaza taifa letu. Kwa upande wa pili, nilibaini na hivyo kuamini kuwa mfumo wetu wa utawala umeshindwa kutumia rasilimali watu na maliasili yetu kwa maendeleo ya taifa.
Kwanza, nilishangazwa na idadi ya Watanzania wasiojua ukubwa wa kijiografia wa nchi yao. Ni idadi ndogo sana ya Watanzania wanaojua kuwa nchi yetu yenye ukubwa wa kilometa za mraba laki tisa na arobaini na tano elfu (945,000 km2) ni zaidi ya ukubwa wa nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Lesotho na Swaziland zikichanganywa!
Tanzania kwa idadi ya watu (milioni 38) ni nchi ya 38 kati ya nchi 195 za dunia. Katika Afrika, Tanzania ni ya saba ikizidiwa na Nigeria (milioni 132), Misri (milioni 79), Ethiopia (milioni 75), Kongo (milioni 63), Afrika Kusini (milioni 44) na Sudan (milioni 41). Ni dhahiri basi kuwa Tanzania ni nchi kubwa ya kutisha, huku ikiwa yenye rasilimali za kupindukia. Ukubwa na utajiri huu kama hautawekewa mkakati, unaweza kuwa kikwazo kikubwa ambacho watawala wetu hawajaweza kukiona.
Aidha, kama hautadhibitiwa mapema, unaweza kuwa chanzo cha migongano ya ndani kwa ndani, kwani kuna utupu wa kutisha. Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea kila kitu kutoka Dar es Salaam!
Chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, chini ya mfumo wa utawala wa kijamaa, nchi yetu ilitawaliwa kutoka kati, yaani kutoka makao makuu ya serikali. Serikali ilisimamia na kumiliki njia zote kuu za uchumi (command economy), ambazo ni pamoja na ardhi, maliasili zote, biashara, viwanda, mabenki, majengo n.k.Hata mfumo wetu wa kiutawala ulipata maagizo kutoka Dar es Salaam na hivyo kufanya makao makuu ya nchi na kiongozi mkuu kuwa na mzigo mkubwa sana wa kusimamia rasilimali za asili za taifa.
Ujamaa ulikwama. CCM, tangu enzi za Mzee Ali Hassan Mwinyi, ikautelekeza kisirisiri. Jambo la ajabu! Itikadi kuu ya nchi inatelekezwa kisirisiri bila wananchi kujua. Hii ndiyo fedheha ya watawala wasio viongozi. Kwa upande wa siasa, nchi nayo ikaingizwa kichwa kichwa kwenye mfumo wa vyama vingi. Balaa likaanzia hapa!
Tangu wakati huo, mserereko wa uchumi wetu umekuwa wa soko (market economy). Ujamaa umebakia kuwa usanii wa kuombea kura kwa wananchi.
Sera za ubinafsishaji sasa zikaanza na baadaye kushamiri chini ya utawala wa Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin William Mkapa. Nchi yetu nayo haikusalimika na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi na kisiasa ya dunia. Hii ilitokana na kufa kwa vita baridi kati ya mataifa ya mashariki ya kijamaa na yale ya Magharibi ya kibepari.
Nchi yetu hapa iliingia kwenye mfumo wa uchumi wa soko kwa kushinikizwa bila maandalizi ya kutosha yaliyosababishwa na kukosekana kwa fikra za ndani. Rasilimali za taifa ghafla zikawa kama hazina mwenyewe. Viongozi wetu wakaanza kuzigawa kwa wageni bila kuweka mkakati wa ndani wa kuwezesha wazawa. Kupitia ubinafsishaji na sera za uwekezaji, viongozi wetu nao wakaanza kujikatia mapande yao. Familia zao, wapambe wao nao hawakucheza mbali. Wawekezaji wa sampuli mbalimbali nao wakaingia ulingoni.
Kama nilivyokwisha kusema, nchi sasa ikageuzwa shamba la babu, ambapo kila mwenye kapu huvuna, na babu hana nguvu ya kuzuia. Uongozi wa nchi sasa ukawa biashara. Ufisadi wa kutisha ukazaliwa rasmi. Kazi ya kugawa rasilimali ya taifa ikaendelea kufanyikia Dar es Salaam. Bunge likageuzwa kituko. Likawa idara ya CCM, na likatumika kupitisha maagizo ya wakubwa, si matakwa ya wananchi.
Mali za nchi zikawa zinagawanywa na kikundi kidogo cha watu chini ya Rais, huku kikidhani kina akili kuliko Watanzania wote. Watanzania tukaendelea kupewa matumaini ya neema. Kila kukicha zinatolewa takwimu tamu tamu za kuonyesha uchumi unakua. Ni kweli, pato la taifa lilikua! Lakini cha kujiuliza, lilikua kwa faida ya nani ilhali wananchi waliendelea na wanaendelea kuwa maskini?
Sasa, hebu tuchambue bila woga ufisadi uliofanyika chini ya utawala wa Awamu ya Tatu, na ambao Rais Kikwete ameahidi kuuenzi na kuulinda! Mwanzo wa kuelemewa kwake.
Itaendelea wiki ijayo!