MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 7.79 ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo iliyokuwa imejiwekea ya kukusanya Sh. Trilioni 7.42 katika kipindi cha miezi mitatu (julai -Septemba) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kamishna Mkuu TRA Yusuph Mwenda amesema ufanisi huo umefanya kuvuka lengo la kila mwezi kwa miezi yote mitatu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana Oktoba Mosi, 2024 Mwenda amesema katika kipindi cha mwezi Septemba mwaka wa fedha 2024/25, TRAi ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 3.02, sawa na ufanisi wa asilimia 105 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 2.88.
"Makusanyo haya ni ya kiwango cha juu kabisa cha ukuaji wa asilimia 77.6 kuweza kukusanywa na TRA katika mwezi Septemba, ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2020/21,"amesema Mwenda.
Ameongeza kuwa, ufanisi katika makusanyo yote umechangiwa na maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini kwa kushirikiana na walipakodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao pamoja na kukua kwa uchumi wa nchi na ongezeko la wawekezaji kutokana na uwepo na usimamizi wa sera nzuri za uwekezaji za serikali ya awamu ya sita.
Aidha amesema sababu nyingine ni kukua kwa ushirikiano na mahusiano kati ya TRA na walipakodi wote nchini kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na ushirikiano mkubwa na mahusiano mazuri wanayoendelea kupokea kutoka kwa viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini.
Amesema, Utendaji kazi mzuri, bidii na kujituma kwa watumishi ikiwemo kuwatembelea walipa katika sehemu zao za biashara siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) na kutatua changamoto zilizopo kumesaidia katika zoezi hilo kwani ushirikiano huo wa umewezesha zoezi zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Sambamba na hayo, kuendelea kuboresha mahusiano baina ya serikali na wafanyabiashara ikiwemo kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa ni siku maalum ya Kusikiliza Walipakodi' kupitia ofisi zote za TRA nchini kutaongeza hamasa ya walipa kodi kutimiza wajibu wao kwa hiari.
"Kuongezeka kwa usimamizi wa wafanyakazi kwa kukemea vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo kukemea vikali vitendo vya rushwa na kuchukua hatua kwa wanaopatikana na kuthibitika kuhusika katika vitendo hivi, kufuatilia na kuchukua hatua za haraka za kutatua changamoto za walipakodi wanazowasilisha moja kwa moja kwenye ofisi ya Kamishna Mkuu kupitia TRA SIKIKA APP iliyozinduliwa mwezi Agosti 2024," amesema Mwenda
Pia Mwenda amesema kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kwa kuhakikisha marejesho ya madai ya kodi yanafanyika kwa wakati ili kufanikisha fedha hizo kurejeshwa kwenye mzunguko wa shughuli za kiuchumi nchini kumesaidia ongezeko kubwa.
"Kuendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa na Serikali ikiwemo la utengenezaji wa mfumo wa kurahisisha ugomboaji wa mizigo inayoingia kwa utaratibu wa ufungishaji wa mizigo (consolidation).Kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu bidhaa nane ambazo zimewekewa bei elekezi (vitenge, mashati, nguo zingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti) na ni sababu iliyochangia,"amesema Mwenda.
