TUBONGE KIUME: Uzi maalumu wa Kijiwe cha Wanaume

TUBONGE KIUME: Uzi maalumu wa Kijiwe cha Wanaume

Mbinu tatu za kumkomesha mwanamke anayewaalika marafiki ukimtoa ‘out’​



Kwa kuonyesha mahaba unaamua kumtoa ‘out’ mpenzi au mchumba wako kumpeleka sehemu mkapate vinywaji na msosi wa tofauti kidogo na ule mliozoea, ili pia mpate fursa ya kupiga soga za tofauti na zile mlizozoea na mkuze uhusiano wenu muwe maswahiba, ili hata mtakapofikia kuwa wanandoa muungano wenu uwe wa amani.

Lakini kwa sababu duniani kuna wanawake wengi wenye akili za kushikiwa kama ilivyo kwa wanaume wasiokuwa na akili kabisa, unashangaa mwanamke anakuja na kikosi. Anakuja na shoga zake watatu, wawili aliosoma nao chuo na mmoja mfanyakazi mwenzake jumlisha na binamu yake wa Tegeta.

Unabaki unajiuliza kweli huyu ndiye mwanamke ninayetaka kumuweka ndani, mwanamke mwenye akili hizi? Na isitoshe hao waandamanaji aliokuja nao si watu wa mchezo mchezo wanajua kuagiza kupita maelezo. Unaweza ukakuta kasichana ‘chembachemba’ lakini kakaagiza kuku mzima yaani kanakula kama Didier Drogba na ‘hakafanyagi’ mazoezi hata ya kukimbia nusu uwanja.

Kuna ambao wameshakutana na tukio kama hili na walilishughulikia kwa njia walizoona zinafaa.

Wewe ambaye linakutatiza ukikutana nalo hizi hapa njia tatu unazoweza kutumia kulishughulikia tukio kama hili.

Njia ya kwanza ni ya ‘Kidemokrasia’ inahusisha uhuru wa kuzungumza na kujielezea lakini pia inakupa haki ya kugoma ukiona kuna ulazima wa kufanya hivyo

Yaani ukiona kaja na timu, unamwambia ukweli mbele ya kikosi chake kwamba hujaridhishwa na tabia aliyoifanya, huu ndiyo uhuru wa kuzungumza. Lakini pia unaweza kuamua kutonunua chochote na mtoko ukafia hapohapo hii ndiyo tunasema haki ya kugoma.

Njia ya pili ni ya ‘Kitapeli’ unafahamu tapeli akishakuingiza mjini anavyokuacha kwenye mataa? Basi hivyo ndio unatakiwa uwafanyie na wao uwaache kwenye mataa. Yaani waache waagize, waagize, waagize tena na waagize zaidi. Kisha omba kwenda msalani halafu ukiwa huko tafuta upenyo wa kutimka zako.

Watakusubiri sana na mwisho wa siku watagundua tu kwamba tayari umeshatokomea hivyo watatakiwa kujilipia na kama hawana uwezo huo, basi jiandae kusikia stori ya namna walivyoosha vyombo na ‘makucha’ yao marefu ya kubandika.

Njia ya tatu ni ya ‘Kidiplomasia’ hii inahitaji utumie propaganda zaidi. Unachokifanya ni kumtumia salamu mpenzi wako kuwa hujapendezwa na tabia yake bila hata kumwamba kuwa ‘sijapendezwa’.

Unachotakiwa kufanya hapa ni rahisi angalia rafiki yake mzuri zaidi katika ile timu aliyoileta, kisha papo hapo mbele ya mpenzi wako anza kutengeneza ukaribu na kuonyesha kwamba umevutiwa naye kwa urafiki wa kawaida tu.

Msifie, mwambie mzuri na hakikisha unasifia vitu vya ukweli ambavyo hata mpenzi wako anaviona. Kisha ikiwezekana muombe hata namba ya simu, mwambie; “Shemu inabidi tuwasiliane bwana. Nipe namba zako.”.

Ndugu yangu, kwa njia hii, kuna uwezekano mkubwa watu wakaomba kuondoka kabla ya kumaliza mlivyoagiza na siku nyingine atakuja peke yake kwa heshima na adabu.
 

Ndoa ingekuwa mtu ingefanana hivi​

Watafute watu kadhaa walio kwenye ndoa, mathalani watu 10 hivi.

Kisha waambie unataka kuumba mtu mwenye taswira ya kufanana na ndoa, hivyo wakusaidie kupata picha kwamba mtu anayefanana na ndoa anaweza kuwa anaonekanaje? Niamini mimi, utaumba mtu mbaya kiasi kwamba kama marehemu, gwiji wa muziki wa Tanzania Dk Remy Ongala angekuwa hai, angesimama mbele ya vyombo vya habari na kutangaza kuacha kujinasibu kuwa ana sura mbaya kuliko wote.

Kwa nini? Kwa sababu leo hii tunaishi katika dunia ambayo kila mtu anayeongea kuhusu ndoa anaizungumzia kwa taswira za kutisha. Mama, bintiye anapoolewa atamwambia; mwanangu, ndoa si lelemama, ina changamoto nyingi sana, misukosuko, ugomvi, purukushani na makorokoro ya kila namna, kwa hiyo inahitaji uvumilivu wa kiwango kikubwa sana.

Baba naye, wakati kijana wake anaoa atamuelezea ya kufanana na hayo. Mwanangu ndoa ngumu, wanawake wana matatizo mengi, kuishi nao kunahitaji moyo wa kustahimili na akili kubwa sana, changamoto ni nyingi.

Watu hawa wawili wakikutana ndani ya nyumba ni kama Chadema na CCM kama sio Simba na Yanga, upinzani wa kufa mtu. Kila mtu kwa nafasi yake akili yake imejazwa habari hasi kuhusu ndoa. Habari hasi ambazo kimsingi zinaweza kuwa za kweli, lakini zinasemwa sana, kiasi kwamba ndoa inaonekana lazima iwe hivyo tu. Kwamba kuwa na furaha ndani ya ndoa… Mungu wangu, huo ni muujiza.

Lakini ni kweli iko hivyo? Au labda kwa misingi ya kidini tuseme Mungu aliamuru tuoane ili iwe kama adhabu kwa Adamu na msaidizi wake Hawa ya kuyapinga maagizo pale Edeni, sitaki kuamini.

ndoa inastahili kuwa tulizo kubwa kuliko kawaida, inastahili kuwa kimbilio kuu kwa mwanandoa mmoja anapopata matatizo mazito.

Mke akikumbwa na janga akimbilie kwa mumewe, akumbatiwe vizuri tu na kwa upole apewe maneno ya kutia nguvu na kuibua upya imani yake. Na ni hivyo kwa mume pia, purukushani anazokumbana nazo siku nzima ziyayushwe kama barafu juani kwa upendo wa daraja la juu sana kutoka kwa mkewe.

Ndoa haistahili kabisa kuwa namna ambayo watu wengi wanaifikiria kwamba ni ngumu. Labda tuamue, tuseme sisi ndiyo wagumu. Tusiipake matope ndoa.

Hata nakumbuka kuna kichekesho kimoja kuhusu ndoa, tuliwahi kukiongelea hapa hapa. Kwamba mwanaume akifa, akiwa mbinguni, kitu cha kwanza kuulizwa kabla ya kupimiwa dhambi zake ni kwamba Je duniani ulikuwa umeoa? Jibu likiwa ndio, Mungu atasema “mpelekeni peponi moja kwa moja mtu huyu. Moto alishaupata huko huko duniani.

Hapana, ndoa haistahili kuwa moto bali kinyume chake. Yaani pepo.
 

Fedha zinatupa wanawake wepesi​


Kabla hatujafika mbali naomba turudie kusoma kichwa cha habari. Kimeandikwa ‘Pesa zinatupa wanawake wepesi’ hakisemi ni dhambi kuwa na pesa au kutafuta pesa.

Pesa ni nguvu, na nguvu ni kitu muhimu kuliko kitu chochote hapa duniani. Hata kabla ya kuanza mfumo wa pesa za karatasi tunazotumia leo, pesa zilikuwa zinatumika.

Binadamu wa kale alitumia nguvu na maarifa kama pesa, ili apate chakula ilibidi atumie vitu hivyo viwili kuwinda sungura au kupanda juu ya mti kuangusha fenesi kwa wakati ule hiyo ndiyo ilikuwa pesa.

Ukiweka pembeni kazi za Mungu tu, pesa inaweza kufanya kila kitu kingine kinachobaki chini ya jua kununua muda, kununua akili, kununua afya bora, kununua heshima, kununua pesa zingine yaani inaweza kufanya kila kitu.

Ukiwa na fedha utakuwa na marafiki wengi, utapendwa na kila mtu, utaheshimiwa na utathaminiwa. Lakini changamoto inakuja ni kwamba, ukiwa na fedha kuna baadhi ya mambo huwezi kuyapata kiuhalisia. Kwa mfano, kupata mwanamke ambaye unatamani ni vigumu.

Kwa nini? Kwa sababu fedha ina kawaida ya kutojificha, ukiwa na fedha lazima watu watafahamu kwa jicho la kwanza watakaloelekeza kwako. Hata ukijiweka katikati ya kundi kubwa la watu, fedha itakuchomoza juu na kusema nipo hapa, kwa huyu bwana.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba kila mtu uliyemzidi pesa atataka kuwa rafiki yako. Kila mtu ataigizia kukuheshimu, kila mtu ataigiza kupenda na kutamani kuwa karibu yako. Maana yake ni kwamba hata kama leo hii ukimtaka mwanamke ambaye yeye binafsi hakuwa na sababu ya kuwa na wewe kwa maana ya upendo atakukubali kwa sababu kuna kitu kingine anaweza kupata ambacho ni pesa zako.

Na hii ndiyo sababu tunasema fedha zinatupa wanawake wepesi.

Mwanamke imara na mzuri ni yule ambaye anahitaji pesa sana sana, lakini hayuko tayari kufanya kinyume na matakwa yake au kufanya vitu visiyompendeza ikiwemo kuwa na mtu ambaye hampendi ili tu apate hizo pesa anazozihitaji sana.

Mwanamuziki wa Tanzania, Wakazi aliwahi kuandika. ‘Mwanamke mzuri ni mwenye tabia njema na mapenzi ya dhati, na mapenzi hayanunuliki kwa fedha. Unaweza kununua tendo la kufanya mapenzi, lakini si upendo’ huu ndiyo ukweli.

Na hii si kwamba tunawalaumu wanawake kwamba wanapenda pesa, hapana. Ukweli ni kwamba tunaongelea wanawake kwa sababu hii kolamu ni Tuongee Kiume, lakini hata wanawake wenye fedha pia, fedha zao zinawapa wanaume dhaifu.

Wanaume walioshindwa kutafuta vyao, wanaotegemea kuhudumiwa.

Mambo mawili muhimu ya kumalizia; kwanza si vibaya kuwa na mweza mwenye fedha, lakini cha kujiuliza ni je uko hapo kwa sababu ya fedha zake, au una sababu iliyo mbali sana na hiyo nguvu yake kiuchumi.

Na pili ni tusiokuwa na hela angalau ya nusu ya tunazozitaka, tuendelee kutafuata kwa jasho na akili.
 

Mzee Baba Kwa nini uliamua kuoa?​


Je, ni kwa sababu ulikuwa unampenda mwanamke huyu zaidi ya kitu chochote duniani au alikuwa karibu yako wakati hamu ya kutaka kuanzisha familia imekushika?

Au pengine ulipelekwa kwake na upepo wa kisulisuli, kufumba na kufumbua ukajikuta ndani ya ndoa. Au labda muungano huu ulikuwa nje ya matakwa yako, wazazi wako walitaka muwe mke na mume au familia yake ililazimisha muoane. Au inawezekana ulimjaza ujauzito, ukatakiwa umuoe mkalee mtoto utake usitake. Au huenda ulikuwa na hali mbaya kiuchumi, katika kutapatapa kwako ukajikuta unaishi chini ya hisani yake, matokeo yake ukalazimika kuoa ili uendelee kusaidiwa au ukaamua kuwa mume kama malipo ya fadhila aliyokupa kipindi chote?

Au basi tuseme mwanamke huyu ni mzuri sana, ukimtazama hivi kuna baridi fulani unapata unahisi ni kama umeshinda jackpot hivyo ukaona huna sababu ya kuacha aolewe na baharia mwingine, ukachukua hatua na ukalipa mahari ukamuweka ndani. Au inawezekana hana huo uzuri isipokuwa ni mchapakazi, hana tamaa za kisichana wala mambo mengi ya ujana, ana maadili na mshika dini anayejua kutunza mume, watoto, wakwe na familia?


Ulioa kwa sababu gani?

Au kwa kuwa swahiba zako wote walikuwa wameingia kwenye ndoa, ukajisikia vibaya kuona umebaki mwenyewe huku nje, ukaamua utafute mtu harakaharaka uoe. Au itakuwa kila siku familia ilikuwa inakuuliza utaoa lini, ukachoka hili swali ukaona bora uoe.

Au umeshachangia sana harusi za wenzio kwa hiyo ili kurudisha fedha zako ukaona uoe fasta fasta ili uchangiwe.


Inawezekana kuna lengo ulikuwa unasubiri litimie ndiyo uoe kwa hiyo sasa imekuwa hivyo. Labda ulijisemea nikijenga au nikinunua gari au nikifungua biashara yangu nitaoa na kutulia niangalie familia au pengine mwenyewe ulijiwekea muda kwamba ukitimiza miaka 30 tu unaoa.

Kwa nini una mke?

Kwa sababu ya mafundisho uliyopewa kanisani yanasema inabidi uoe au labda wewe unafuata ulichoelekezwa na masheikh kwamba ndoa ni nusu ya dini? Au umeoa kwa sababu hutaki uzeeke ukiwa bachela kwa kuwa watu watakucheka na kutokuheshimu au basi tuseme umeoa kwa sababu ya kupata mtu wa kukusaidia kazi za nyumbani kama kupika, kufua na kadhalika.

Itakuwa umeoa kwa sababu dini yako inakataza zinaa. Kwa kuwa tendo la ndoa ni muhimu na la kibaiolojia na kihisia hivyo umeamua kupata mtu wa kushiriki naye kwa halali?

Kuna sababu nyingi sana zinazotuingiza wanaume kwenye ndoa na kwa kawaida sababu hizi ndiyo kitu pekee huamua itakuwa na hali gani.

Ukiona ndoa yako ina matatizo kaa chini tulia, rudisha akili yako nyuma kumbuka uliingia kwenye ndoa hii kwa sababu gani tatizo kubwa linaweza kuwa liko hapo.
 

Sayansi nyuma ya kuchuja kwa mkeo​


Kupoteza mvuto, kufifia au kuchuja kwa mkeo ni hali ambayo nyuma yake imeficha sayansi ndogo sana inayosababisha kuchuja huko.

Iko hivi; mara ya kwanza ulipomuona mke wako alikuwa ni mdada fulani hivi mzuri. Anang’aa, amependeza hata ukajiaminisha kwamba kama itatokea utakufa bila kuzungumza naye siku hiyo – basi utakufa sawa sawa na mtu ambaye hajawahi kufanya jambo lolote la maana duniani.

Alikuwa na nywele safi, ndefu, ulifahamu sio za kwake halisi lakini zilikuvutia. Usoni alikuwa amepakaa kila kitu, yaani kama pilau lililotiwa viungo vyote hata sasa kauso kakawa kama ka mwanasesere. Gauni alilovaa pia, hata ukahisi kwamba alilinunua Dubai ingawa ulikuwa na uhakika uwezo huo hana.

Ulipomsogelea, kabla ya kusema neno lolote ukapokelewa na harufu nzuri ya unyunyu, hapo ukajiambia kimoyomoyo, kumbe zile stori za kwamba mbinguni kuna malaika ni porojo tu, malaika wako duniani na huyu ni mmoja wao.

Mkasalimiana, akakuruhusu iwe salamu ya kumshika mkono, na ulipothubutu kufanya hivyo ukafanikiwa kushika mkono laini kweli kweli hata ukawa na wasiwasi kwamba inawezekana huyu mwanamke hajawahi kufanya kazi yoyote ngumu – hata kubeba kisado cha maji.

Mkazungumza siku ile, urafiki ukaanzia hapo na baadaye ukabadilika kuwa mapenzi; mapenzi yakazaa mazoea, mazoea yakazaa uchumba, uchumba ukazaa ndoa na sasa mnaishi pamoja na watoto wenu kwa miaka kadhaa.


Lakini sasa hivi mkeo si yule uliyemuona siku ya kwanza, zile nywele safi, ndefu, hazipo tena, sasa unachoshuhudia ni kipilipili cha ajabu ambacho hata hujui wapi kimetokea. Ile sura nzuri iliyopakwa kila kitu kama pilau lililotiwa viungo vyote imeyayuka kabisa, sasa unaiona sura yake ya halisi, na umegundua kuwa kumbe kwa mbali anafanana na baba mke wako.

Harufu ya unyunyu nayo imetoweka, jasho lililochanganyika na harufu ya jikoni ndiyo unavyovinusa zaidi kwa sasa kiasi kwamba hujisikii hata hamu ya kuwa karibu naye mara kwa mara. Ule ulaini mikononi nao hata hufahamu ulipoendea, amekuwa na mwili mgumu kana kwamba huwa mnakwenda pamoja kufanya kazi nzito. Kwa kifupi mkeo kachuja.

Sasa sayansi inasema hivi; kama mkeo kachuja kuna mambo mawili tu nyuma yake. Kwanza ni labda umepata mwanamke aliyeamua kubweteka, kutojitunza baada ya kuolewa – kwa hiyo anachuja kwa sababu haoni umuhimu wa kufanya hivyo

Lakini pili ambalo linaweza kuwa ndiyo sasabu kuu, ni kwamba labda wewe hujui kutunza, unapenda wanawake wenye nywele nzuri, sura iliyokolezwa kila kipodozi na harufu za unyunyu wa bei mbaya lakini ubaya ni kwamba hujui kugharamia hivyo.

Hapo ndipo kosa linapoanzia, tunatamani vizuri ambavyo kwa kawaida vingi ni vya kutengeneza. Hivyo kumbe, tunaweza kuvitengeneza pia na kuvileta ndani.

Yaani badala ya kutamani mwanamke mwenye nywele nzuri nje, unaweza ambazo ni za kununua, unaweza kununua na kuzirudisha ndani ukaangalia zinakaaje.
 

Desemba, Januari miezi ya wanaume kula kwa jasho​



Huko kwenye maandiko imesimuliwa baada ya Adam na Hawa kula tunda la mti wa kati Mungu aliwaadhibu; akamwambia Hawa atazaa kwa uchungu na Adam atakula kwa jasho, muda wa kuthibitisha andiko hilo kwa upande wa wanaume umeanza.

Siku zote tunakula kwa jasho letu, lakini kula kwa jasho kwa kiwango kilichoandikwa kwenye maandiko matakatifu tunapaishi Januari. Katika mwezi wa kwanza maneno kama sina hela, niko vibaya ndiyo msimu wake. Watu wanakuwa weupe, akaunti zinasoma kama namba za mawimbi ya redio 88.5 jasho linatutoka kweli kweli.


Januari si ngumu

Kila gonjwa na chanzo chake, gonjwa la kusota tunakosota Januari linasababishwa na mwezi huu.

Januari wala si ngumu kiasi hicho, ina siku 31 tu kama tunavyoona kwenye kalenda, lakini kiuhalisia huwa inafikia hadi siku 42 au 47 kwa sababu ya Desemba.

Mwezi huu una mambo mengi sana . Mwezi huu una likizo, watoto wanatakiwa wapelekwe kijijini kwa bibi yao. Bibi naye ni mgeni njoo mwenyeji apone, anategemea akitembelewa, wakati anakuja kukupokea stendi akukute umebeba vifurushi na mia mbili tatu za kununilia mafuta ya taa. Na kumbuka hadi watoto wakifika hapo, maana yake umeshawalipia nauli ya basi iliyopanda bila sababu za msingi kwa sababu tu ni Desemba.



Ukisema watoto wabaki mjini tu si kwamba ndo utakuwa umejiokoa, hapana. Hiyo Waswahili wanaita ‘umeruka majivu umekanyaga moto’. Desemba ina sikukuu kibao na ikikuta mjini maana yake ni pesa lazima itumike. Watoto watataka kuvaa nguo mpya wapendeze, watataka kula mapilau kuku, na bado watataka uwapeleke sehemu wakafurahi, yote haya yanahitaji pesa.

Sasa jambo la kuchekesha ni mambo yote haya yanayoongezeka yenyewe tu kamshahara kako kanabaki vile vile.


Unaingia Januari na viraka

Ili tuweze kuimudu Desemba na sikukuu zake, wengi inabidi tukope.

Maana yake ni kwamba mkopo huu tutaulipa na mshahara wa Desemba. Tukilipa tunajikuta hatujabakiwa na kitu, matokeo yake unaanza mwaka mpya na viraka, huna chochote mfukoni.

Hapo sasa ndio ugumu wa Januari unapoanza kwa sababu pesa ambayo ulijua utaitumia kufanya manunuzi ya kuwaandaa watoto kurudi shule Januari ulishaitumia kulipa madeni ya pesa ulizotumia sikukuu. Kuanzia hapa sasa ndiyo ile mwanaume atakula kwa jasho lake inaanza kuonekana kwa picha kubwa.

Kwa hiyo muhimu ni kabla hujaanza kula sikukuu za Desemba hebu jaribu kuipata picha kubwa ya kinachofuata Januari.

Mwezi wa Bebi nikwambie kitu.

Bachela mwezi huu ukipokea meseji ya ‘Baby nikwambie kitu’ usiijibu kwa sababu kifuatacho baada ya hapo itabidi uzame mfukoni ununue wigi jipya.
 

Wanawake na madada wa kazi ni kama wanasiasa na vyama​


Wanawake na madada wa kazi ni wanasiasa na vyama.

Kwenye siasa tumeshazoea, si tatizo kabisa. Kwa mfano, historia inaweza ikaanza Lowassa akiwa mwanachama hodari wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Atazunguka nchi nzima, atakwenda Kaskazini Arusha kisha atarudi Kusini Mtwara, atapita Mashariki Dar es Salaam halafu atapanda treni hadi Magharibi Kigoma – kote huko anapita akiwahubiria Watanzania wenzake kwamba kama wanataka kuishi katika nchi ya ahadi waendelee kuchagua CCM.

Kisha kuna siku, ataamka na kututangazia kuwa nimehamia chama kingine cha siasa. Labda kwa mfano, atasema nimehamia Chadema. Na sababu atakayotuambia ni kwamba hana imani tena CCM, kwa hiyo kama na sisi Watanzania tunataka kuishi ndani ya Paradiso tukiwa hapahapa duniani, tuchague chama chake kipya, Chadema.

Miaka miwili mitatu itapita, mara asubuhi moja ataamka tena, atatutangazia kuwa amerudi CCM. Kwa sababu amegundua kuwa kumbe ndiyo sehemu halisi ya kutufanya Watanzania na Tanzania yetu iwe yenye maendeleo ya kustaajabisha.

Mfano huu ukitokea kweli kwenye siasa ni sawa kabisa. Kwa sababu kwenye nchi ya kidemokrasia unaruhusiwa kuhama chama cha siasa kadri utakavyo, kama Muumini Mwinjuma alivyokuwa akihama bendi za muziki.


Lakini wake zetu wameigiza hii tabia nyumbani – kila kukicha wanabadilisha madada wa kazi kama vyama. Na ukiuliza sababu, mara nyingi si ambazo zilikuwa na ulazima sana wa kufanya wanachofanya.

Jana mlikuwa na Mariam kutoka Kondoa, kesho atamtimua kwa sababu eti muda wote anashinda kwenye TV akizama tamthilia na Bongo Movie. Keshokutwa atamleta Neema kutoka Iringa, naye atakaa Jumatatu, Jumanne kisha Jumatano atamtimua, ukiuliza sababu utaambiwa hafanyi kazi, kutwa nzima anashinda akichezea simu mliyompa kwa ajili ya kuwasiliana na nyie mkiwa kazini. Kisha Ijumaa atakwambia anakwenda kumpokea Fatuma kutoka Mtwara, naye atakaa wikendi tu kisha atarudishwa kwao Namtumbo kwa makosa ya kufanana na wenzake waliotangulia.

Labda hizo sababu zote ni za kweli, lakini wanachoshinda kuelewa ni kwamba, tatizo lao mara nyingi wanachukua dada wa kazi wenye umri mdogo, ambao hawajawahi kufanya kazi sehemu yoyote kabla, na hata hawana hamasa ya ndani inayowasukuma kufanya kazi, yaani hawana watoto wanaosomesha wala hawana kodi za kulipa, ni watu ambao mara nyingi wanafanya kazi kama ratiba tu hivyo ule umakini wa mfanyakazi kwa ofisi yake hauwezi kupatikana.

Na isitoshe hawa madada wa kazi wametoka vijijini huko, kwenye maisha magumu kiukweli ambako hakuna bomba la maji, hakuna umeme, hakuna TV wala simu binafsi za mkononi. Kwa hiyo anapokuja kwako na kukuta kuna TV na king’amuzi kilicholipiwa mwezi mzima, hiyo kwake si nyumba, ni peponi, kwahiyo atahakikisha anaitumia fursa ambayo aliikosa miaka yote tangu kuzaliwa kwake.

Ninachosema ni huenda kosa linaanzia kwa namna tunavyowapata hawa wadada wa kutusaidia. Lakini suala la kubadilisha kama vyama si zuri sana kwa sababu kuna siku tutaajiri majambazi watusaidie kazi majumbani mwetu.
 

Hawapendi hela, wanapenda wanaume wenye hela​


Wimbo wa Taifa wa wanaume wa Tanzania ndiyo huo; wanawake wanapenda hela ooooh! wanawake wanapenda hela jamani! Karibu kila mwanaume unayemgusa, ukimuuliza hupendi mwanamke wa aina gani? Atakujibu, “sipendi mwanamke anayependa hela” na ukimuuliza unapenda mwanamke wa aina gani atakujibu kuwa, “napenda mwanamke asiyependa hela.”

Na siyo kama watu wanazungumza hivi kwa kufuata mkumbo, hapana. Wana sababu za msingi kabisa. Hapo kila anayezungumza ni muathirika wa kunakoitwa kupenda hela kwa wanawake — wengine bado waathirika wapya, vidonda vibichi kabisa; na wengine wamebaki na makovu, waliyokumbana nayo baada ya kukutana na wanawake wapenda hela. Ni mazito. Hao nd’o hawataki hata kusikia kuhusu kuzihusisha hela zao na wanawake.

Huko kwenye mitandao ya kijamii, vijana wanakoshwa na machapisho ya aina mbili. Kwanza picha nzuri za wanawake na pili ni maandiko yanayowasema vibaya wanawake kuhusu kupenda hela — likiwekwa hilo la pili, linapata wachangiaji ‘kama wote’. Kila mtu anachangia uzoefu wa maumivu yake.

Wakati watu wazima wenye hekima wao wanaendelea kutafuta hela kwa sababu wanayatazama maisha kwa uhalisia sio nadharia. Wanaelewa hakuna mtu yeyote anapenda hela duniani; sote tunapenda huduma zinatokana na hela.

Ukitaka matibabu mazuri unahitaji kuwa nazo, kujenga nyumba nzuri, gari ya kisasa, nguo bora, kulea watoto vizuri, kula ujana na kila kitu kizuri utakipata ukiwa na hela. Cha bure kwenye dunia hii ni pumzi tu, hata salamu inalipiwa.

Ubaya sasa unakuja ili upate hela kuna mchakato mchungu na mgumu unatakiwa upitie; Yaani unatakiwa ufanye kazi, na mara nyingi kazi haifurahishi.


Unatakiwa uamke mapema asubuhi ujiandae kwenda kazini, na ili uamke mapema unatakiwa ulale mapema, maana yake nini, kama mwanamke aache kutazama tamthilia na Shilawadu ili kesho yake awahi kazini. Na ukifika kazini hakuna kulala, ni mchakachaka mwanzo mwisho, jumlisha makelele na matusi ya mabosi pasua kichwa — na ikifika muda wa kulipwa, ni vipesa kiduchu tu ambazo atanunua vigauni vitatu na kwenda saluni mara moja baada ya hapo anabaki mweupe kama sufi.

Sasa wanawake wakajiongeza; kwa nini wateseke kiasi hicho, watoe jasho kubwa kwa malipo yasiyolingana nguvu iliyotumika. Wakatafuta njia fupi ya kurahisisha maisha na wakaipata. Wakaanza kupenda wanaume wenye hela ili wapate huduma kwa urahisi na kila kizuri wanachokihitaji.

Hilo lilipokuja kwa wanaume tukalipokea vibaya tukiamini wenzetu wanapenda hela na kuanza kuwapachika majina.

Narudia wanawake hawapendi hela, wanapenda huduma zinazopatikana. Kwa hiyo kama unapenda mwanamke, hakikisha unapenda kutafuta hela pia. Achana na kuishi kwa nadharia kwamba anayekupenda hajali— hakuna aliyewahi kula mapenzi akashiba.
 

Mwambie binti yako kuwa, kutokuolewa si dhambi​


Ukipata muda kaa na binti yako na umwambie kuwa kutokuolewa si dhambi na haijawahi kuwa dhambi. Kwa sababu huku mtaani wenzie wamechanganyikiwa kwa kuwa wamefikia umri wanaodhani ndiyo wa kuolewa, lakini bado hawajazipata hizo ndoa. Wanahisi wana gundu na bahati mbaya, wanahisi si wazuri wa kutosha au labda hawana tabia nzuri au kuna kitu wanakosea.

Kaa mwambie binti yako kuwa, akifikia umri huo na hajaolewa si kwamba ana gundu au bahati mbaya. Kuolewa hakuna uhusiano wowote na bahati nzuri kwa sababu ndoa si kitu kizuri wala si kitu kibaya hakibebi hali yoyote kati ya hizo mpaka itakavyoamuliwa na mhusika. Ukiamua kuona ni nzuri basi ni nzuri, ukiamua kuona kinyume, huwa hivyo pia.

Asidhani yeye si mzuri, mwambie ni mrembo sana lakini ndoa haziji kutokana na uzuri wako, zinakuja kutokana na makubaliano ya wawili walioamua kuoana ndiyo maana kuna wanawake wazuri walioolewa na kama wapo wabaya, basi wapo waliolewa pia.

Labda hana tabia nzuri ila mweleze kuwa ndoa si mshahara wa tabia njema. Na mwambie kwamba hatakiwi kuwa na tabia nzuri kwa sababu ya kuolewa, anatakiwa awe hivyo kwa sababu yeye ni binadamu. Mpe mfano kwamba uasherati si tabia mbaya kwa sababu hakuna mwanaume anayetaka kuoa mwanamke mwasherati, bali ni tabia mbaya kwa sababu uasherati ni uchafu.

Msisitizie kwamba jeuri, kiburi, mvivu na vitabia vyote vichafu, si vichafu kwa sababu wanaume watamuogopa, ni vichafu kwa sababu ataogopwa na kila binadamu hakuna bosi anayetaka mfanyakazi kiburi, hakuna shangazi anayependa mpwa jeuri kama ambavyo hakuna mwanaume anayependa kuoa mwanamke wa hivyo, mweleweshe awe mtu mwema si kwa sababu ya ndoa, bali kwa sababu dunia inahitaji watu wema.

Hakikisha husahau kumdadavulia kuwa kutokuolewa ni dhambi kwa wanawake wasiojielewa kwa nini wapo duniani. Ajue kuwa siku zote wanawake wasiokuwa na ndoto zozote, ndoto yao huwa kuolewa.


Mwanamke ambaye hana mpango wa kuja kuwa mmiliki wa gazeti kubwa la fasheni Afrika Mashariki, ndoto yake huwa ni kuolewa. Mwanamke ambaye hana ndoto kubwa ya kuwa Spika wa Bunge au mwanasiasa mkubwa msaidia watu, ndoto yake kubwa huwa ni kuolewa. Mwanamke ambaye hajui yupo duniani kwa ajili ya nini, huishi kwa ajili ya kuolewa, kubebeshwa mimba, kuzaa, kulea watoto na kuzeeshwa, kufariki na kuzikwa.

Sijakwambia umwambie ndoa ni kitu kibaya au asiolewe, hapana. Mwambie ndoa inaweza kuwa kitu kizuri lakini kamwe asikae chini kuisubiri. Aendelee na maisha yake, aendelee kufukuzia ndoto zake, ndoa itakuja itamkuta huko huko mbele ya safari.
 

Sababu tatu kwa nini mzee, mtu mzima hatakiwi kuoa binti mbichi​


Tukisema binti mbichi tunamaanisha mtoto mdogo, msichana ambaye umri wake unafanana na watoto wako wa kuwazaa, kama huna watoto basi tofauti ya umri kati yenu wawili ni kubwa kiasi kwamba mnaweza kuwa baba na mwana kabisa. Na leo tunaambiana sababu tatu za kwa nini mzee, mtu mzima unatakiwa uoe mwanamke wa aina hiyo.

Wanasema umri ni namba tu, lakini kama unataka kula pensheni yako gerezani tafuta binti mdogo mwenye miaka 20 oa. Kwa nini? Kwa sababu asilimia kubwa ya ndoa za namna hiyo huwa ni za kupangwa, siyo kwa ajili ya mapenzi, mtoto wa miaka 20 akupende wewe kwa lipi?


Ukifanikiwa kuoa mtoto mdogo namna hii tarajia ndoa isiyokuwa na uaminifu hata kwa asilimia 20, labda umfungie nyororo pembeni ya kitanda asitoke ndani kwako, ukioa ndoa ya namna hii tarajia migogoro kila kukicha, ugomvi kati yako na vijana wadogo wa umri wake wanaommendea kwa sababu ndiyo watu rahisi zaidi yeye kuvutiwa nao. Akiwa karibu nao wana mengi ya kuongea kuliko akiwa na wewe, hii wala haihitaji sayansi kuielewa, wewe ni wa kizamani, yeye ni wa kisasa. Na matokeo yake ni nini? Leo utamkuta kasimama kichochoroni na vijana wenzake wanaokusalimiaga shikamoo, kesho atakurudia nyumbani usiku bila sababu, kesho kutwa utamkuta ndani kwako na vijana hao hao. Utaua, Serikali ya mama Samia itakushughulikia.


Pia oa mtoto mdogo kama unataka kifo chako kisababishwe na mtu mwingine. Dini zinatuambia kila mtu ataonja umauti, sayansi inatuambia hivyo pia na kuongeza kuwa watu waliokula chumvi zaidi wana uwezekano mkubwa wa kutangulia kwa vifo vya asili kama vile magonjwa. Lakini kama unaona mtindo huo unakuchelewesha oa mtoto mdogo ili akupe msongo wa mawazo, presha ipande ichanganyike na sukari utangulie kabla ya siku zako.


Na tatu oa mtoto mdogo kama umechoka kuishi kwenye familia yenye amani. Kuna wazee wanaishi vizuri na familia zao, lakini siku wanaamka tu na kuhisi wanahitaji mke mwingine, tena binti mdogo. Na kwa sababu familia nyingi za Kiafrika wanaume tukiamua jambo hakuna wa kutuzuia, basi wanafanikiwa kuoa.


Sasa mke akishangia ndani ya nyumba familia inatibuka, mifano lukuki tunayo kwenye maisha yetu. Kwa hiyo kama umechoka kuishi maisha ya amani na familia yako, ingiza mke mdogo mdogo.

Lakini nisichoelewa zaidi ni sisi wanaume tuna shida gani? Tufanye una miaka 50 au unakaribia umri huo, halafu unakwenda kuoa mtoto mdogo, unakuwa unataka kugundua nini ambacho hukukiona kwenye miaka 50 ya maisha yako?
 
Samahani kwa kuingilia kijiwe chenu wanaume, nimevutiwa na mada zako.
 
Tuwaache watoto wetu watimize ndoto zao


Karibu kila mzazi anatamani mwanaye awe kama Mbwana Samatta, Barack Obama, Diamond au Billgate — hapa tunaongelea kiwango cha mafanikio. Na waswahili wanakwambia, hakuna mtu anayependa ufanikiwe kweli kama mzazi wako. Wengine wanapenda ufanikiwe ndio, lakini sio ufanikiwe kuwazidi wao.

Na mzazi naye anapenda ufanikiwe kwa sababu nyingi, lakini moja ya sababu kubwa ni kwamba mafanikio yako ni yao. Yaani anaamini ukiwa na nyumba nzuri, kuna uwezakano mkubwa wa yeye kutoka kwenye kinyumba anachoishi sasa hivi, kuja kuishi ndani ya kasri lako. Au atibiwe kwenye hospitali nzuri akiumwa kwa sababu tu mwanaye aliyekusomesha kwa jasho lake uko vizuri kiuchumi.

Mafanikio si kitu rahisi na ndiyo maana si kila mtu anayo. Na ubaya ni kwamba, unapozungumzia mafanikio, kila mtu anayapima kulingana na malengo yake au mtazamo wake.

Kwa mfano, unakuta una ndoto ya kwamba hadi kufikia mwaka 2025 uwe mfanyabiashara unayemiliki kiwanda au kampuni ya nguo yenye thamani ya bilioni moja. Lakini hadi mwaka 2024 unaweza kuwa uko nusu ya hapo.

Kwa wanaokutazama nje wanaweza sema umefanikiwa, lakini wewe binafasi ambaye unajua malengo yako unaelewa zaidi umesimama sehemu gani, kwamba bado kuna jambo la ziadi unahitaji kulifanya.

Hapa najaribu kukupa picha ya kukuelewesha kuwa watoto wetu nao wana malengo na ndoto zao kubwa, lakini wengi bado hawajazifikia. Ingawa kwa nje, akina sisi tunaona tayari wanaishi nchi ya ahadi kwa sababu hatujui undani wa nchi ya wanayoitafuta.

Sasa tatizo linakuja kwa wazazi wengi, hasa wanaume kwa watoto wetu wakiume kwa mtazamo wetu, tunataka kuanza kufaidi matunda makubwa ambayo unakuta kumbe yako nje ya uwezo wa mtoto, yaani hawezi kumudu kwa huo. Au hata kama anaweza kumudu, basi anaweza kupitia anguko baada ya hapo.

Yaani mfano, kama mtoto ana milioni 30 ya kuboresha biashara yake. Na wewe unatamani akujengee nyumba. Akikujengea maana yake unataka biashara yake ibaki palepale ilipo, maana yake asiendelee, au asifanikiwe kama mafanikio kwake ni kuboresha biashara.

Kama mfano huo ni mzito, ushushe hata kwa daraja ya kununuliwa shati jipya na mtoto anayefanya biashara ndogo ya mtaji kiduchu.

Hatusemi unakosea kutamani vizuri kutoka kwa mtoto, ni haki yako kwa sababu hata Mungu anawakumbusha watoto kuwatunza wazazi wao. Lakini ni vizuri zaidi kama hautaharakisha hilo litokee mapema kabla mambo ya mwanao hayajasimama kisawasawa.

Wenzetu- kwa maana ya mama. Wanawaelewa sana watoto wao na ndiyo maana hili huwezi kuliona kwao. Wanaelewa, wanaheshimu na wanawapatia watoto wao muda.

Tuwape vijana wetu na mabinti zetu nafasi ya kufanya ndoto zao ziwe kweli. Mambo yakikaa vizuri, tutafaidi. Hakuna mtoto anayependa kumuona mzazi wake juu ya mawe - watatusaidia.

Sent from my M2101K6G using JamiiForums mobile app
 

Tuoe tabia nzuri au wazuri?​


Wanaosema tuoe tabia nzuri, wanadai uzuri ni kitu cha muda, mwanamke mzuri huwa hivyo katika umri fulani pekee, hasa ujana. Kwa hiyo kadri umri unavyosonga ulimbwende nao unapukutika. Hii maana yake ni kwamba kama utaoa kwa sababu ya uzuri, kuna uwezekano mkubwa wa kuichoka ndoa uzuri ukimuisha mwenzio. Lakini tabia, weee! Hizo hata akizeeka zitabaki palepale.

Tena wanakwambia wanawake wazuri hawajui maisha. Kwamba kwa sababu wanafahamu wanavutia macho ya wanaume wengi, basi wanakuwa na kujiamini kulikopitiliza. Maana yake ni anaweza kuwa hata hakusikilizi kwa sababu anaamini hata mkishindwana dakika hii, akitoka nje hatembei hatua tano anapata mwingine.

Na unaambiwa ukioa mwanamke mzuri pia inabidi uwe na nguvu sana ya kulinda ndoa yako kwa sababu wanaume wote duniani tunapenda vitu vizuri, kwa hiyo tutamsumbua sana — atatongozwa kazini, kwenye daladala, sokoni, dereva wa bodaboda na karibu na kila mwanaume atakayepata ukaribu wake. Swali ni Je, ataweza kukwepa mishale yote hiyo? Ukizingatia mingine inatoka kwa watu waliouzidi kila kitu? Wanawake wanaopendwa na wengi mtihani.



Wanaosema tuoe uzuri

Wanakwambia kabla ya kuoa fikiria vitu vingi. Fikiria jinsi utakavyokuwa unamtambulisha mkeo kwa rafiki na ndugu zako. Ukiwa na mwanamke mzuri, wala huhitaji kuongeza sifa wakati wa kumtambulisha, ukisema ‘huyu ndo mke wangu mtarajiwa.’ inatosha. Lakini ikiwa hawa wengine, inabidi uchombeze na sifa zisizoonekana kwa macho kama ‘huyu ndo mke wangu mtarajiwa. Usimuone hivi, anafahamiana na viongozi wengi huyu.”

Pia fikiria jinsi picha zenu za harusi zitakayoonekana. Fikiria watoto mtakaopata watakavyokuwa. Vyote hivi haviwezi kukuumiza kichwa ukiona mwanamke mzuri, utakuwa na amani.


Na ukitoka kibaruani, umeshagombana na bosi, umegombana na wateja, umegombana na konda kwenye daladala, ukirudi nyumbani unatakiwa upate kitulizo. Yaani ukute mwanamke mzuri anakusubiri. Mwanamke ambaye ukimuangalia tu, unasahau magumu yote uliyopitia mchana. Sio unarudi unakutana na kitu yenye ‘sura ya mjomba wake’. Ukiangalia, badala ya kupoza machungu ya siku unajikuta unapandwa na hasira upya hii inaweza kukupa magonjwa ya uzeeni ukiwa bado na umri mdogo sana.

Pia wanauliza kama tabia mbaya ni tatizo, hata wewe una tabia zako mbaya lakini amekubali kuolewa na wewe. Hii maana yake ni kwamba, hakuna mtu mwenye tabia zote nzuri. Kwa hiyo unaweza kuvumilia tabia zake mbaya ukadumu.



Tuoe yupi?

Inawezekana lengo la Mungu kutupa kila mtu roho yake ni kwamba kila mtu aishi maisha anayotaka. Wewe unataka nini? Uzuri wa sura au tabia? Fanya unachoona kinakufaa.

Mwisho wa siku fahamu kwamba uzuri sio kitu halisi, ni fununu tu. Hakuna kipimo cha aidha uzuri wa sura au tabia. Ni mitazamo pekee ndiyo inayoamua kwamba tabia hii au mwonekano huu ni mzuri au mbaya.
 

Dalili ndoa yake ilishakufa​


Kuna ndoa zimekufa lakini bado wanandoa hawajatengana au kutalikiana. Wanaendelea kuishi chini ya paa moja la nyumba, kulala chumba kimoja, wengine hata kitanda na shuka bado wanachangia.

Wapo wanaofanya hivyo kwa makusudi, kwamba wanajua ndoa zao hazina uhai tena lakini wanajitoa ufahamu kwa kuamua kutofanya chochote kuhusiana na ndoa yao. Na wapo ambao wenyewe hawana habari kabisa kwamba kati yao hakuna ndoa tena, kuna watu waliowahi kuoana na sasa wanaishi kama familia. Hawa wenyewe wanaweza kuona mambo yanavyokwenda vibaya lakini wasijue kwamba ndiyo angamio linaendelea hivyo wanahitajika kufanya kitu ili kuokoa ndoa au maisha ya wanandoa.

Kwa kukumbushana tu — hizi ni baadhi ya dalili ndoa yako imeshakufa.

Unaishi kama hujaoa

Wakati unaoa ulibadilisha mtindo wa maisha, kuna baadhi ya tabia uliachana nazo. Lakini sasa ghafla tu unajikuta umezirudia bila kujituma. Unaweza ukachelewa kurudi nyumbani bila taarifa, wengine hadi hawarudi kabisa. Unazungumza na wanawake wengine hovyo hovyo kwa ajili ya kuonana nao kimapenzi, marafiki wako wa ajabu ajabu umewarudia na makorokoro mengine yote ambayo hayapendezi kufanywa na mtu aliyeoa.

Na hii inatokea tu, unaweza kusema bila kukusudia kwa sababu roho ya ndani tayari inafahamu kwamba wewe haupo kwenye ndoa tena, ni kapera. Ukiona dalili hii kubwa, angalia namna ya kutafuta suluhisho kwa namna ya kuwafaa nyote wawili.


Kutomuamini mpenzi wako hakukuumizi tena

Kipindi ndoa yenu iko hai ilikuwa ukihisi kutomuamini mke wako unakumbwa na wivu na wasiwasi. Mfano, alikuaga akitoka kazini, kabla ya kurudi nyumbani atapita sehemu lakini atawahi kurudi. Lakini mara anapitisha muda. Unaamua kumpigia simu, mara ya kwanza inaita hapokei, mara ya pili hapokei, ya tatu hivyo hivyo na ya nne ndiyo hapatikani kabisa. Unaingiwa na wasiwasi, sio wasiwasi kwamba inawezekana kapata ajali au tatizo, bali kwamba labda yuko sehemu anavunja uaminifu.

Lakini ndoa yenu ikiwa mfu-hai. Apokee simu au asipokee wewe unaona sawa tu, arudi nyumbani au asirudi yote heri kwako, zaidi unaweza kuitumia kama chachu ya kuzusha ugomvi nyumbani lakini ndani yako ukielewa kabisa kwamba sio kwa sababu ulitaka awahi kurudi bali unataka tu ugomvi.


Mipango yako haimuhusishi

Mwanzo mlikuwa na mpango wa kupanga fremu mbili, kisha kuzitoboa katikati na kutengenezea duka kubwa, na mipango mingine mingi ya kimaendeleo. Lakini ghafla unajihisi kama humuhitaji tena kwenye mipango ya namna hiyo. Unahisi unaweza kufanya mwenyewe, bila msaada wake.

Kimsingi ni kweli unaweza kufanya mwenyewe na hata mara ya kwanza wakati unamshirikisha ilikuwa unaweza kufanya mwenyewe pia. Ila kilichokufanya ugundue hilo kwa sasa ni kwa sababu nafsi yako ndani haimchukulii tena kama mwenza wako. Bali mtu tu.
 

Kukosa kazi kunachangia kuharibu mahusiano​


Tunaposema mahusiano tunamaanisha mahusiano ya kila namna. Ndoa, urafiki, uchumba, mzazi na mwana, ukwe, ushemeji na kila namna ya mahusiano.

Na tunaposema kazi tunazungumzia kitu kama ajira au biashara au labda tuseme shughuli yoyote ambayo inakuingizia pesa kihalali kwa lugha rahisi tungeweza kuweka kichwa cha makala hii kuwa, ‘kukosa ajira au biashara inayokupa chochote mfukoni kunaongoza kuvunja mahusiano’.

Usipokuwa na kazi ndoa yako itayumba tu, hata kuwe na upendo wa kiasi gani kati yako na mkeo. Atakupenda leo, kesho na keshokutwa baadaye atagundua kuwa yeye na watoto wana mahitaji muhimu ambayo hayawezi kutimia bila pesa, na pesa huwezi kuipata bila kazi au biashara.

Mkeo naye ni mtu sio mbao, ana akili kichwani sio barafu, hivyo ataamua kutafuta namna ya kukusaidia bila kupunguza upendo wake kwako kwa sababu anajua utakuwa nayo kesho. Hapo ndio utaanza kuwaza vitu vingine katoa wapi pesa au ananichukuliaje hivi ambavyo mahitaji ndani anatimiza yeye kwa kiasi kikubwa na taratibu upendo utaanza kupungua kutoka kwako kwenda kwake, na usipokuwa makini uhusiano au ndoa itaharibika.

Kuhusu marafiki nao, Waswahili wanakwambia akufaae kwa dhiki ndiye rafiki kwa enzi hizi, kutokuwa na pesa ni dhiki kubwa zaidi, kwa hiyo marafiki zako wa kweli hii ndiyo itakuwa tiketi yao ya kukuonyesha upendo wa dhati walionao juu yako.

Watakusaidia watakutumia pesa kwenye simu, watakununulia pombe mtalewa na mtafurahia tu.



Lakini zikipita wiki mbili tatu wataanza kukuchoka, wataanza kukuona kama kupe au kunguni, unawanyonya tu kwa sababu zamani walikuwa wanakupa na wewe unawapa sasa hivi huna.

Matokeo yake ni kwamba urafiki utaharibika kwa sababu utakuwa ni urafiki wa upande mmoja na tangu dunia imeanza urafiki wa namna hiyo haujawahi kudumu. Kwa ndugu unaambiwa ukiwa huna hela, kwenye vikao vya familia hata hawakuulizi unatumia kinywaji gani, utashangaa tu umeletewa ‘mirinda nyeusi’. Na ukitaka kuchangia hoja kuwa makini na sauti yako, ukiipandisha kidogo tu wanaweza kukwambia unafanya fujo.

Ukweli ambao unaweza kuamua kuukataa ukipenda ni kwamba usipokuwa na pesa ya kutatua matatizo angalau madogo madogo ya familia, unakosa kuheshimika kwa sababu kwa dunia ya sasa watu wanathamini vitu kuliko utu.

Mwisho wa siku tusikubali kukaa bure, pia tuwakumbushe na watoto wetu umuhimu wa kutokukaa bure. Wanapotoka vyuoni, waache kukaa nyumbani kusubiri ajira ziwafuate. Itafikia mahali kinamama wataanza kuwatuma vitunguu magengeni bila kujali ni wavulana au wasichana.

Ukifanya shughuli yoyote atakuagiza uje na vitu kama mkate, maziwa, sukari, badala ya kukuita kwa jina lako atakuita baba au mama.
 

Watoto wa kike wanatusahaulisha kuwa tunao pia watoto wa kiume​


Tunawachunga na kuwalinda sana watoto wa kike hadi tunasahau kama tuna vijana wa kiume pia, hii si nzuri tena ipo kwenye ngazi zote, kuanzia kitaifa hadi familia.

Sikiliza televisheni, tazama redio, soma gazeti, ingia mtandaoni, ukikuta harakati hazihusu kulinda watoto kwa ujumla wao, basi lazima zitakuwa zinahusu kulinda watoto wa kike pekee, lakini kukuta za mtoto wa kiume kuna ugumu hili ni tatizo.

Majumbani mwetu tuna sheria lakini hazifanyi kazi kwa usawa kwa watoto wote. Binti akichelewa kurudi nyumbani ni vita kuu ya tatu ya dunia na ni tatizo kubwa kuliko deni la taifa, ni gharika zito kama upepo wa kisulisuli lakini akichelewa kurudi mtoto wa kiume hakuna tatizo, na hata likiwepo basi ni tatizo la kawaida sana, la kuambiwa maneno makali mawili matatu na likapita.

Tunaamini tunafanya hivi kwa sababu si kwamba tunawapenda watoto wetu wa kiume zaidi, hapana, bali tunaamini tunawalinda mabinti zetu tunaamini kwamba msichana yuko kwenye hatari zaidi ya kukumbwa na majanga kuliko mvulana. Lakini jambo ambalo labda tunashindwa kulielewa ni kwamba kwa sasa tunaishi dunia ya tofauti sana.

Mtoto wa kiume na wa kike, mvulana na msichana, wote wapo na viwango sawa vya kukumbwa na hatari katika ujana au utoto wao.

Kama unaogopa binti akichelewa kurudi nyumbani anaweza kukutana na manyang’au watakaomchezea na kumjaza ujauzito na kumtoa nje ya reli uliyokuwa unajaribu kumtengenezea.


Basi unatakiwa pia uogope hivyo hivyo kwa mwanao wa kiume akichelewa kurudi huenda yuko sehemu anakula mihadarati na atarudi akiwa teja, anaiba na atarudi akiwa maiti kama sio mfungwa, ananunua kahaba na atarudi na gono kama sio kaswende na Ukimwi, anatumika kama mwanamke au mwanaume katika mapenzi ya jinsia moja na atarudi akiwa mtoto ambaye hutokuwa unajivunia hata kumtambulisha mbele za watu kuwa ni mwanao.

Anaweza pia akawa hayuko darasani kama alivyokuaga, na utagundua hilo akirudi na sifuri nyumbani.

Haya tunayoyazungumza hapa si hadithi za kubuniwa, kwa sasa tunaishi kwenye dunia ya namna hiyo. Fuatilia habari zinazoendelea mijini utaelewa. Hatuyasemi kwa sababu ya kutishana au ili kuifanya dunia ionekane ni hatari, hapana. Tunasema ili tuwe makini na kufuatilia nyendo za watoto wetu kwa karibu na kuwakumbusha namna ya kuwa mtu bora, kuwaeleza ukweli kwamba dunia haijawahi kuwa mbaya wala nzuri, dunia iko katikati, ambapo sasa walimwengu ndiyo huamua waipeleke wapi.

Wakiwa wabaya, inakuwa mbaya na wakiwa wazuri huwa hivyo pia.
 

Michepuko mjiongeze kidogo​


Tazama mfano huu.

Umerudi kazini, umekaa na mama watoto, kashika simu yake kageukia kule, wewe umeshika yako umegeukia huku unaperuzi mtandaoni. Mara unakumbana na kavideo fulani hivi kanakuvutia, unakatazama kanakuchekesha, unacheka sana, sana kama mwenda wazimu hadi machozi yanakutoka. Unasema hapana, hii kitu lazima na mke wangu naye aone tucheke pamoja.

‘Njoo uone’ unamuita. Anakugeukia, anasogea karibu yako, unamsogezea simu unamuonyesha ulichokuwa unaangalia. Video inaanza, sekunde ya kwanza, ya pili, ya tatu, mara kinaingia kimeseji wakati video inaendelea na kama unavyojua ‘smartphone’, meseji ikiingia, hata kama unafanya vitu vingine kwenye simu, yenyewe inajitokeza pale kwa juu ikionesha jina la aliyeituma na alichokiandika.

Basi, kwa sababu Mungu aliwapendelea wanawake vipaji vya kufanya mambo mawili mawili kwa wakati mmoja; mkeo kwa wakati huo huo anaotazama video unayomuonyesha, anasoma jina la mtumaji na meseji... baby kesho usinidanganye kama leo meseji kutoka kwa Jack Sinza.

Kuanzia hapo hakuna tena video ya kuchekesha, sebule inachafuka, mambo yanaharibika, nyumba inawaka moto, mzee unawekwa kizimbani ujitetee utetezi ambao hata ukinena kwa lugha haitatokea ueleweke.


Kusuluhisha

Kesi kama hizi zinatukuta, na ni ngumu sana kupata suluhisho zikishatokea, kwa hiyo unachohitaji ni kinga tu, ni kuhakikisha hazitokei. Na kuna njia mbili za kujikinga nazo.

Ya kwanza ni kujiongeza wewe na mchepuko wako, mkawekeana sheria na mipaka ya mawasiliano, mfano kwamba ikifika saa 2 usiku mwisho wa kupigiana simu na kutumiana meseji.

Na kama kukiwa na shida ambayo anaona ni lazima muwasiliane, basi mnaweza kuwa hata na meseji ya kuzuga. Kwa mfano, ikishafika saa 2 usiku, akitaka kukupigia au kukutumia meseji aanze kwa kuandika ‘Naweza kupata kazi hapo ofisini kwenu? ukijibu Sawa. Nitakujulisha zikitokea. Ajue kuwa ulipo, hakuna usalama kwa wakati huo.

Yaani kwa kifupi, hapa cha kulinda ni simu tu kwa sababu matatizo yote yanaanzia hapo siku hizi. Ndiyo maana kuna wanaoenda kuoga na simu au wanazificha, hazionekani hadi watoke bafuni. Wengine simu zina nywila ngumu kama zimeficha mafaili ya siri ya ufisadi wa EPA. Wengine wana ‘laini’ maalum ya michepuko, akiingia nyumbani anaitoa kwenye simu... Yaani ni shida tu.

Sasa kama hutaki purukushani zote hizo tumia njia ya pili ambayo ni kutokuwa na mchepuko kabisa ukiweza hii, magonjwa ya moyo, na presha presha za ajabu zitachelewa sana kukupata kwa sababu utakuwa na amani muda wote, unajiamini hakuna cha ajabu atakachokiona.
 

Wanaume tuna nafasi kubwa kukomesha ukahaba​


Mfikirie Mohamed Dewji… majuzi tu alitajwa na jarida la Forbes kama bilionea mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika. Na ukipata swali la hii imewezekana vipi? Jibu la haraka laweza kuwa ni kutokana na biashara anazomiliki au kuziendesha ambazo chimbuko lake ilikuwa ni baba yake mzazi.

Mo anauza soda, juisi, maji ya kunywa, khanga, vitenge, mafuta ya kupikia, sabuni, vipodozi, sembe, ngano, sukari, pikipiki, nishati. Anajihusisha na kilimo cha mkonge, chai, pamba, korosho… kwa kifupi anagusa karibu kila biashara inayohusu mahitaji muhimu ya kila siku ya binadamu.

Lakini jiulize vipi yote haya yangewezekana kama Mo angekuwa anaishi dunia ya peke yake? Nani angevaa vitenge anavyouza? Samaki wa nani wangekaangwa kwa mafuta anayotengeneza? Nguo za nani zingefuliwa kwa sabuni yake au ngano anayosaga na kusindika ingepika chapati za kuliwa na nani?

Kwa hiyo kumbe Mo anahitaji watu wa kuwageuza kuwa wateja ili kuingiza Mabilioni kwa mwaka, ili jina lake lifike hadi Forbes.

Yaani wateja ndiyo sababu ya biashara kuwepo au ndiyo roho ya biashara. Wateja wanaweza kuipa biashara yako matokeo wanayotaka. Wanaweza kukupandisha na hata kukushusha wakiamua.

Sasa majuzi jeshi la polisi lilikamata machangudoa 118. Nakusisitizia tu, stori kama hii unaweza kuisema hivi; majuzi jeshi la polisi lilikamata wanawake 118 wakijiuza – hii haileti picha nzuri kabisa hasa ya mwelekeo wa maadili yetu.


Tusiongelee nini kimewapelekea kuwa hapo, kwa sababu nina uhakika kila mmoja kati ya hao 118 atakuja na stori yake – lakini ukizijumlisha zitarudi kwenye mzizi wa kwamba maisha magumu, kazi hakuna, wakaamua kupita njia fupi.

Katika hili wanaume tunaweza kufanya jambo likawasaidia dada zetu. Kwa sababu tumeshasema wateja ndiyo sababu ya biashara kuwepo. Na wateja wa hawa mama na binti zetu ni sisi wanaume.

Tuwasaidie kwa kuacha kuwanunua, kwa sababu kama watatoka majumbani kwao usiku na kwenda kujipanga barabarani na kwenye chochoro zenye giza – kisha wakasimama hapo usiku mzima waking’atwa na mbu na kugongwa na baridi bila kusememshwa na mwanaume hata mmoja, ni wazi kwamba asubuhi watarejea nyumbani bila senti mfukoni.

Kisha kesho na kesho kutwa na wiki nzima ikijirudia hali hiyo hiyo hakuna tena mwanamke atakayekuwa na nguvu za kutoka nyumbani kwenda kusimama tena barabarani ili awe chakula cha mbu bila malipo hata kwa mkopo.

Tuna nguvu kubwa sana ya kuwaokoa hawa binti zetu, dada zetu, mama zetu, shangazi zetu na zaidi. Bila kutumia jasho, wala bunduki wala askari polisi kama ilivyokuwa juzi. Tuache kuwanunua, waache kujiuza, watafute njia nyingine za kupata kipato za halali zaidi.
 

Siku wanawake wakigundua jambo hili, tumekwisha​


Tumezichezea sana akili za wanawake. Tulianza kwa kuwaambia kuwa sisi ni bora zaidi yao. Wakanywea, wakawa wadogo wakiamini hakuna kiumbe duniani chenye ‘manguvu’ na ‘maakili’ ya ajabu zaidi yetu. Wakatusujudia, wakatuona ni miungu mtu, tena labda sio kutuona ni miungu mtu, bali mungu wa pili.

Na nguvu tuliyoitumia kuhakikisha hili linafanikiwa si ndogo. Tumetumia vitabu vya dini, vinavyosomeka kwamba Mungu mwenyezi baada ya kuumba kila kitu, akatuumba sisi wanaume na kutupa uwezo wa juu ambao hata malaika hawakuwahi kuwa nao, yaani kama ingekuwa enzi hizi za kiteknolojia tungesema Mungu katengeneza mashine yenye programu toleo jipya.

Kisha vitabu vya dini vikasogea sentensi kadhaa mbele ndipo neno mwanamke likajitokeza, sentensi zikasomeka kwamba mwanamke akatokea ubavuni mwa mwanaume yaani sawa na kusema bila mwanaume, kusingekuwa na mwanamke.

Ikaendelea mbele, ikaandikwa mwanamke akashawishiwa na shetani ili akamshawishi mwanaume wale tunda la mti wa kati na ikawa hivyo; hii ikamaanisha mwanamke alikuwa ni mdhaifu, tukaibeba na kuileta hadi leo mwaka 2019, na bado kuna wanawake kupitia sisi wanaamini wao ni wadhaifu.

Vitabu vikaendelea kuandika kuhusu mashujaa waliokuja kutetea ulimwengu, karibu asilimia 98 ya mashujaa wote walikuwa wanaume. Nuhu mwanaume, Musa mwanaume, Yesu (Isa bin Mariam) mwanaume, Yusufu mwanaume, Muhammad (S.A.W) mwanaume. Kisha asilimia kidogo tukawazungumzia wanawake, huku karibu asilimia 60 ya wanawake waliotajwa wakiwa ni wa upande mbaya.

Tukaweka vitabu vya dini pembeni, tukaja na historia. Tukawaambia kuhusu uhuru wa taifa kubwa kama Marekani, kisha tukawachorea michoro inayosema kuwa uliletwa ama kupiganiwa na wanaume kwa asilimia 98.

Uhuru wa Tanzania pia, wa Kenya, Uganda, Afrika Kusini na karibu wa kila taifa duniani ulipiganiwa na asilimia 98 ya wanaume. Kwa maana ya kwamba sisi ndiyo viumbe wenye nguvu au ni vipi?

Tukaja kwenye maendeleo ya dunia, tukasema kila kitu kiliigunduliwa na sisi wanaume. Gari, ndege, kompyuta, mashine ya kuchapisha magazeti, viatu hadi sufuria na vijiko, vyote ni sisi wanaume. Kwamba kwa kipindi hicho wanawake walikuwa wanafanya shughuli gani?

Matokeo ya yote hayo leo hii wanawake wanahangaika kulazimisha kufanana na sisi, kitu ambacho ni ujinga kwa kiasi fulani. Kwa sababu kama unataka kupiga hatua, kama unataka kuwa bora zaidi, hutakiwi kupambana kwa kiasi sawa na aliye bora. Unatakiwa kuhakikisha unakuwa bora zaidi ya aliyekuzidi ubora. Yaani kama wanawake wanataka kufanya mageuzi, wasihangaike kuwa kama sisi, au kuwa sawa na sisi, wahangaike kuwa bora zaidi ya sisi wanaume.

Tuwafundishe hili mabinti zetu, kuna mabadiliko yatakuja.
 
Back
Top Bottom