Coronavirus: Congo DRC yathibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya Corona
Haki miliki ya pichaREUTERS
Kisa cha kwanza cha virusi vya Corona kimethibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Msemaji wa wizara ya Afya amesema Jumanne.
Mgonjwa huyo ni Mkongo wa miaka 52 aliye na kibali cha kuishi Ufaransa, ambaye aliingia nchini humo siku mbili zilizopita na alikuwa amewekwa karantini baada ya uchunguzi aliofanywa katika uwanja wa ndege wa Kinshasa kubaini kuwa ameambukizwa virusi hivyo.
Alikuwa akipewa matibabu katika kituo cha zamani cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola mashariki mwa mji mkuu wa Kinshasa.
Wizara ya afya ya DRC imesema kuwa inajaribu kwatafuta watu wengine waliyesafiri na mgonjwa huyo ili wawekwe karantini katika juhudi za kudhibiti maambukizi.
Waziri wa afya Eteni Longondo ametoa wito utulivu na kuzingatia usafi kwa kuosha mikono yao mara kwa mara.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya 11 ya Afrika kuthibitisha maambukizi ya ugonjwa hatari wa Covid-19.
Ugonjwa huo ambao ulianzia China umewauazaidi ya watu 3 800. DR Congo kwa sasa imeimarisha uchunguzi katika viwanja vyake vinne vikuu vya ndege kwa kuwakagua kwa makini wasafiri walio na viwango vya juu vya joto- hatua ambayo imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya kupambana na maaambukizi ya virusi hatari vya Ebola.