Oscar Kambona ni miongoni mwa viongozi mahiri na shupavu waliowahi kuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, kutokana na uongozi wake, hekima na busara.
Ndiye Mtanzania wa kwanza kuwa waziri aliyeongoza wizara mbili kwa wakati mmoja. Ndiye Mtanzania pekee anayeaminika kusimama kidete na kufanikiwa kulidhibiti jeshi lililoasi mwaka 1964.
Hata hivyo, pamoja na umahiri huo, lakini kubwa zaidi kutokuwa na tamaa ya kutumia nafasi ya uasi wa jeshi kushika madaraka ya nchi.
Pamoja na hayo mchango wake hauthaminiwi kabisa. Tofauti na viongozi wengine wa siasa au hata utamaduni, mpaka sasa hakuna barabara yenye ukumbusho wa jina la mwanasiasa huyu aliyefariki akiwa katika matibabu mjini London, Juni 1997 na mwili wake kurudishwa Tanzania kwa mazishi.
Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925, katika kijiji cha Kwambe kilichoko mwambao mwa Ziwa Nyasa, karibu na Mbamba-Bay, wilaya ya Mbinga, mkoani wa Ruvuma.
Alikuwa ni mtoto wa Kasisi David Kambona ambaye alikuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kupata upadri katika kanisa la Anglikana la Tanganyika, na kwa mama Miriam Kambona.
Akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo kumfanya Oscar kujawa na hamu ya kuitumikia nchi yake.
Msingi wa elimu yake aliupata nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao bado uko mpaka sasa), katika kijiji cha Kwambe, kwa kuwatumia wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.
Alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli na baadaye Shule ya Sekondari ya Alliance (sasa Shule ya Sekondari Mazengo), ambako alilipiwa ada na askofu Mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya pauni 30 kwa mwaka. Inasimuliwa kuwa kilichomvutia Mzungu huyo kukubali kumlipia Oscar ada ni baada ya kusali sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni kwa Kizungu.
Alichaguliwa kwenda ‘Tabora Boys Senior Government School ambako ndiko alikokutana na Mwalimu Julius Nyerere kwa mara ya kwanza. Wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya Kikatoliki ya St Marys.
Kukutana tena na Nyerere
Ilikuwa mwaka 1954, kwenye mkutano wa kitaifa wa walimu, ndipo Oscar Kambona ambaye naye alikuwa amemaliza shule na kufundisha katika shule ya Alliance, alikutana tena na Nyerere na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo harakati za chama cha TANU.
Oscar alishawishika kuitumikia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa muda si mrefu, bila malipo baada ya Mwalimu Nyerere kumweleza kuwa asingeweza kuajiriwa ndani ya chama kwa vile haikuwa na fedha.
Huo ulikuwa uamuzi mzito na mgumu mno, hasa kwa mtu kukubali kuachia nafasi ya ualimu ambayo alikuwa akilipwa vizuri na kufanya kazi bila malipo tena za chama ambacho ndiyo kwanza kilikuwa kikianza harakati za ukombozi.
Kwa miezi takriban sita, Oscar Kambona alifanya kazi ngumu ya kuzunguka sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili wanachama.
Kwa kipindi hicho huku akitumia fedha kidogo alizokuwa amejiwekea akiba yake, alifanikiwa kusajili wanachama 10,000 na haikuwa ajabu kuwa baada ya mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000.
Ili kutunza fedha za chama, Kambona alifungua akaunti ya kwanza ya TANU na kisha kwenda Butiama kumshawishi Mwalimu Nyerere achukue uongozi wa chama moja kwa moja kama mtendaji mkuu.
Mwaka 1957, Kambona alikwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza kwa ufadhili wa Gavana.
Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Tanganyika na mwenyekiti wa tawi la TANU la London.
Kukutana na watu mashuhuri
Mwaka 1958, Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri akiwemo George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa wa Waafrika duniani, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa Waafrika wote (All Africa's Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada ya kupata Uhuru.
Kambona alisafiri mpaka Ghana, wakati huo akiwa bado anaendelea na masomo yake nchini Uingereza na huko alipata nafasi ya kukutana na mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrika, Kwame Nkrumah.