Tujikumbushe watangazaji wa zamani wa Redio na TV

Tujikumbushe watangazaji wa zamani wa Redio na TV

msimsahau fundi mitambo Rwehamamu RTD idhaa ya biashara kipindi club raha leo na Julius Nyaisanga
 
baba yke chale ana maviraka kumi na mbili .....tuliimba tukiwa watoto kufuatiliza midundo ya kile kipindi cha?????
 
Salama Mfamao RIP
Aloysia Isabula
Aloysia Maneno
Peter Makorongo
Suleiman Kumchaya
Juma Ngondae RIP
Mshindo Mkeyenge
Abdallah Mlawa
Siwatu Luanda RIP
Salim Mbonde
Omary Masoud RIP
Pascal Mayalla
Adam Mwaibabile
etc....

hapo kwenye pasco mayalla huyihuyu wa ppr na jf au,huyu sio alianzia itv? kawahi kupitia rtd kweli?
 
Tangazo lingine ni WATOTO HAWA BWANA,....... KULA WANAKULA, KUVAA WANAVAA LAKINI MMMMMMMMHHHHHH
Tangazo la sabuni MSHINDI. SABUNI KOMOA. NA MBUNI. BILA KULISAHAU TANGAZO LA KIBUKU OYEE, KIBUKU HONGERA HONGERA

kuna tangazo la sabuni ya kodrai, kondraiiiiiiiiiii,....... lilikuwalinapigwa baada ya kipindi cha majira asbh.likinikuta nyumbani hili tangazo nilikuwa najua hapo tayari nimeshachelewa no skonga,maana kwa dk 4 au 5 zilizobaki nisingeweza kuwahi skonga.
 
Mahokaaaaa We mama mbavu zangu weeee we mama mbavu zangu weeee we mama mbavu zangu weee ha ha ha haaaaaaaaaa! Duh noma hapo jumapili napiga pasi uniform kwa ajili ya jumatatu pasi ni ya mkaa kama ya dobi mara mkaa au jivu linadondokea kwenye shati jeupe unaanza kufua kola upya enzi hizo electric iron ni luxurious item!

Lol,umenikumbusha mbali sana mkuu. Hivi kumbe kabla ya kicheko alikuwa akitamka maneno haya? sikuwahi kumuelewa kabisa!
 
1981 nikiwa sumbawanga kipindi jioni njema, unapigwa wimbo wa DDC mlimani park orch duniani kuna mambo! Sauti tamu ya bitchuka inanifanya niache kucheza chandimu nakimbilia ndani kuusikiliza toka hapo mimi na mlimani park ni damu damu! Rtd ya wakati ule ilikuwa nzuri sana! Kaka yangu alikua akiniamsha kumi na moja kasoro tunaoga sasa rtd kumi na moja inafunguliwa wimbo wa taifa kwa sala na swala halafu wimbo wa marijani rajabu kumekucha jama kumekucha, majogoo vijijini yanawika... Kumi na mbili kamili majira sisi ndo tunatoka regional block mie jangwani pr school my bro sumbawanga pr school no daladala umbali ni km ubungo mataa hadi mwenge unawahi asubuhi, saa sita mnarudi kula, nane kasolo mpo mstarini mnaingia tena kwa class. Hotuba za mchonga rtd lzm aanze na ndugu wananchi hahaa. Ila ilikuwa ikifika mwezh desemba nyimbo za xmass yaani utajua tu mwisho wa mwaka, kuna baba gaston kakolele viva xmass, ooh xmass oyee bonane baba noele kikumbi mwanza mpango aka king kiki na marquis, jim reeves.
 
Kuna mtangazaji nimemsahau alitangaza mechi ya Yanga na Milambo Kilimanjaro premium league kesho yake tukatangaziwa kafariki ilikuwa kama 1993/4. Nani anamkumbuka huyu mtangazaji?

Ni Chilambo Dominic kama sikukosea, kifo chake kilitikisa sana. Hapo kwenye bold sidhani kama ligi ilikuwa na wadhamini wakati ule
 
Mi nakumbuka tangazo la National bank of commerce ndio bank yetu sote na ni bank ya kisasa lilikua linaletwa wkt wa mchezo wa redio. Nlikua nakipenda sana kipindi cha wkt wa kazi, jambo na kile cha wagonjwa nshakisahau jina, apo huletwa nyimbo motomoto

Kipindi cha wagonjwa kilikuwa kinaitwa Ugua pole
 
Dah, kitambo sana enzi za kina Hendrick Maiko Libuda, lakini nasahau jina la yule
Mtangazaji alitangaza mechi ya simba na Atletico sports Aviacao ya Angola ambayo
ilikuwa na wachezaji wakali kama Kanka wemba, Abilio Amanali, Gito, Libenge, Bravo
Yanda, Nero sijui nelo n.k


Wakati huo simba ilikuwa ni kina Abdul Mashine, Mohammed Mwameja, Hussein Masha, Yamadhani Leny
Damian Kimti, Mteze John Rungu, Malota Soma, Edward Chumila n.k


Umenifanya nivikumbuke vipindi maarufu kama HISIA NA MUZIKI, MAHOKA, PWAGU NA PWAGUZI
PITIO LA KITABU NA SAIF D KIANGO N.K

Debora mwenda sitamsahau kamwe kwa kukifanya kipindi cha mama na Mwana
kipendwe hata na watu wazima......... acha Bwana hadithi tamu kama Ua Jekundu,
Binti chura, Kibibi jitu n.k Enzi zimepita sasa watoto wanacheza viduku.

Pia ninawakumbuka waigizaji kama Mzee MUNDU, Mshamu, Matuga n.k

Hiyo match ya Atletico Sportivo Aviacao nakumbuka ya marudiano Luanda alitutangazia Mikidadi Mahmood,Simba inaingia fainalii x 3 !!!
 
mnakumbuka kipindi cha mikingamo? Wakati huo mafisadi ndo wakitajwa humo ilikuwa noma. Kipindi cha michezo mbili kasoro, hapo mama ndo anapaalia wali kwa kuweka mkaa juu ya mfuniko basi njaa zinauma tunasinzia tu, ikifika mbili kamili ubeche tayari kwenye sina mtu km tano tumelizunguka hapo hasinzii mtu.
 
Kuleni kuku, mayai mboga samaki, maziwa. Pa kulala pawe bora!

Duh inanikumbusha enzi hizo primary school na vistori vyetu vya jokes eti kuna jamaa katoka bushi kuja mjini aksikia hili tangazo la kuleni kuku mayai mboga Sasaki maziwa pa kulala pawe bora eti jamaa akajuwa bora ile kampuni ya viatu enzi hizo kuwa inaprovide free accomodation akanunua kuku mayai zake na mboga Sasaki maziwa then akala alipomaliza kaenda duka la bora anauliza sehemu ya kulala! Basi tukipigiana hiyo story tunacheeeka utoto bwana kiboko
 
Kulikuwa na Fundi-Mitambo Ally Said Tunku. Nilikuja jua baadaye kumbe jina la mwisho ni Tunkumbe. Kweli ujana maji ya moto.
Mmenikumbusha mbali.

Pia kulikuwa na mfundi wengine wa mitambo Noel na Maloe, Samwel Kunjumu, Edward Kwilasa na Juma Bundara.
 
Julius Nyaisanga kwa sasa yupo mji kasoro bahari (Morogoro) katika ofisi za ATV habari akisimamia utangazaji wa taarifa za habari pale Aboud Television na Aboud FM radio, kule kwa waluguru. Mzee ndani ya suti na miwani anachomoka spidi mia na ishirini yaani hadi raha jamani( mtamkumbuka na mambo mseto radio one kila jumapili?)
 
Unikumbusha matango kama "vipi Rambo?"pancha bwana.pancha wakati kuna oko?oko ni dawa ya maji maji inayodhibiti pancha.
 
Sitawasahau CHILAMBO, HILLARY na JONGO. Kwanini? Nisikilize.....
Kwa kutambua umuhimu wa kila mmoja katika maendeleo ya soka au michezo kwa ujumla, leo nitawazungumzia watangazaji waliokuwa wakitangaza wakati huo ambao ufanisi wa kazi yao ulichangia kwa kiasi kikubwa msisimko wa soka.

Ikumbukwe, wakati huo teknolojia ya televisheni haikuwa imeenea kwa wingi, hivyo shabiki wa mpira wa kule Kigoma, Mpanda Rukwa, Nyamanolo, Mwanza, au Muleba, Bukoba, alipata taarifa kwa kusikiliza matangazo ya mpira kupitia redio.

Kutokana na umahiri wao katika utangazaji, mtu aliyesikiliza mpira akiwa kona yoyote ya nchi, aliweza kupata burudani ya kutosha na kuridhika kwa kile kinachotangazwa katika viwanja mbalimbali.

Hivyo basi watangazaji mbalimbali walifanya kazi nzuri kama Salim Mbonde, Bujaga Izengo Kadago, Halima Mchuka na wengineo ambao sijawahi kuwataja, lakini nitawazungumzia zaidi wale waliokuwa jirani zaidi na wachezaji wa soka.

Ni wazi, ukaribu wao na wachezaji, walikuwa kama ndugu na kwamba, licha ya ukaribu wetu na wao, hawakubadili mwenendo wa kazi yao kwa kutusifia tu pasipo sababu, bali walikosoa au kusifia palipostahiki.

Mfano, Dominick Chilambo ambaye kwa sasa ni marehemu, Charles Hilary anayetangaza Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Ahmed Jongo, aliyestaafu, ambao kwa hakika, sauti zao na ufasaha wa kuripoti kilichokuwa kikiendelea dimbani, vilitosha kuwa burudani kwa wasikilizaji.

Na hicho ndicho ambacho kimenifanya niwakumbuke watangazaji hawa ambao kwa hakika walitoa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya michezo, hususan soka katika enzi zetu.

Walipokuwa wakitangaza kwa mfano kwenye Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam ambao sasa unaitwa Uwanja wa Uhuru, wapenzi ambao hawakuwepo uwanjani, walijiona kama wako uwanjani wanashuhudia kinachoendelea.

Baadhi ya mashabiki waliofika uwanjani lakini wakashindwa kuingia kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosa fedha, wengi wao walibaki nje na redio zao ndogo wakifuatilia matangazo ya mechi na kupata uhondo kama wako jukwaani katika uwanja huo.

Wengi wa watu hawa, ni wale waliokuwa wakifika uwanjani, lakini wakishindwa kuingia kwa kukosa fedha, hivyo kusubiri dakika za kuingia bure, ambazo kwa lugha ya kimichezo, huita ‘fungulia mbwa’, yaani wasio na fedha.

Cha kushangaza ni kwamba, baada ya filimbi ya mwisho, wale walioingia dakika chache kabla ya filimbi ya mwisho huku wakifuatilia dakika zaidi ya 80 kwa matangazo ya redioni, ukimuuliza kuhusu mechi hiyo, walikuwa wakitoa maelekezo mazuri kuliko hata yule aliyeshuhudia mechi husika kwa dakika zote 90.

Huu si umahiri tu wa shabiki, bali ni ufasaha pia wa mtangazaji wa mechi kwa jinsi alivyokuwa akiripoti matukio ya mechi hiyo hata kumfanya msikilizaji kujiona kama yuko kwenye jukwaa akishuhudia mechi.

Nakumbuka jinsi baba yangu, mzee Luwongo, katika uhai wake alivyokuwa akitayarisha redio yake kujiwekea mazingira mazuri ya kusikiliza redio, utadhani yupo uwanjani akifuatilia!

Wakati wapenzi na mashabiki wakifurahia kupata maelezo ya mechi kwa ufasaha mkubwa, nasi wachezaji tulio wengi, sifa zetu zilikuwa zikinogeshwa na watangazaji hawa ambao licha ya kutangaza soka kwa kuwa na majina ya wachezaji, wao karatasi ilikuwa kama kutimiza wajibu tu.

Licha ya kuwa na karatasi za majina ya wachezaji, lakini wengi wao hawakuwa wakitegemea karatasi, kwani kutokana na kuwa karibu na wachezaji, waliwajua wengi kiasi kwamba, hawakuwasumbua hata katika kutangaza.

Binafsi, niliwahi kushuhudia Charles Hilary akitangaza mechi ya Sigara na Red Star katika Uwanja wa Uhuru bila kuwa na karatasi. Tukiwa katika chumba cha utangazaji pale Uwanja wa Uhuru, aliweza kutangaza kwa ufasaha bila hata ya kukosea majina.

Aidha, ndivyo ilivyokuwa kwa Dominic Chilambo, ambaye kwa sasa ni marehemu, ambaye katika uhai wake, ndiye alikuwa mwasisi wa jina la TP Lidanda. Hili lilikuwa jina la utani la Pamba ya Mwanza wakati huo ikiwika kwelikweli katika soka ya Tanzania.

Ninapokumbuka umahiri wa Chilambo, naishia kusema, Mungu amuweke mahali pema peponi! Amina.

Huku majina ya Khalfani Ngassa, Raphael Paul, Ali Bushiri, Hussein Marsha, Abdalah Bori, Kitwana Suleiman, David Mwakalebela, Rajabu Risasi, Rashidi Abdalah, Ibrahim Magongo, George Masatu, Nico Bambaga, Beya Simba na wengineo wa Pamba, yakipambwa vilivyo na Chilambo.

Chilambo, alikuwa na uwezo wa kumpatia picha kamili ya mchezaji kiumbo, kiuchezaji, kitabia, kitu ambacho ni watangazaji wachache wamejaliwa katika kutimiza wajibu na kazi zao.

Usiulize kuhusu kaka yangu, Ahmed Jongo, ambaye alikuwa ndiye kaka wa wachezaji wa timu ya Maji Maji ya Songea waliopata umaarufu mkubwa wakati alipokuwa akitangaza kule Radio Tanzania-Ruvuma.

Beki mstaarabu, Samli Ayubu, Celestine ‘Sikinde’ Mbunga, Octavian Mrope, Dadi Athumani, Madaraka Suleimani, Ibrahim Mbuzi, Abdalah Waswa, Abdalah Chuma, Ahmed Kampira, Maulid Toffi, wote hawa walikuwa Maji Maji, ambao walipaishwa vilivyo na Jongo.

Hizi hazikuwa sifa za kusukwa tu, bali ilikuwa ni sifa halisi za wachezaji hao zilizokuwa zikielezwa na watangazaji hawa hata kuwapatia taswira halisi ya wachezaji bila kuwaona kwa macho.

Naye rafiki yetu Charles Hilary, licha ya kuwapa sifa wachezaji wengi wa nchi hii hususan wa Simba na Yanga, lakini chachu ya maendeleo ya timu iliyokuwa ngeni katika Ligi ya mwaka 1986 ya Tukuyu Stars hata kutwaa ubingwa, kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na kupambwa na Hilary.

Nikiwa mmoja katika kikosi kile, Hilary alikuwa akitupamba kwa sifa tulizostahili licha ya ugeni wetu katika Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu), kwani kwetu ilitosha kututia moyo sisi wachezaji.

Tulichokuwa tukifanya wachezaji, ni kurekodi mchezo mzima kwenye ‘kaseti’ na baada ya mechi, tulikwenda kuusikiliza na kuwa burudani kwetu, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kujituma zaidi katika mechi zinazofuata.

Nakumbuka mechi yetu ya nne katika ligi hiyo ya 1986, Charles Hilary ndiye alikuwa mtangazaji dhidi ya Yanga, mechi ambayo ilipigwa Uwanja wa Uhuru, ambako alitusifia tangu tulipoingia uwanjani kuanzia maumbo yetu, hata kutia madoido kuwa, pengine hatukuwa Watanzania, bali kutoka Nigeria, kwani tulikuwa warefu na miili mikubwa tukipambwa na weusi tii.

Hiyo ilitosha kutujenga kisaikolojia kwani tulijiona maumbo yetu yanatosha kuwafunga Yanga, hivyo hakuna sababu ya kupoteza mechi ile, kweli tulifanikiwa kuwafunga mabao 2-1.

Baada ya mechi hiyo, Hilary alisikika akisema, kwa Tukuyu kuifunga Yanga, hakuna timu ambayo ingeifunga Tukuyu katika msimu ule wa 1986, kwa sababu tulikuwa na kila kitu.

Kwa kweli maneno yake hayo yalitupa hamasa kubwa mno muulize Godwin Aswile, Mbwana Makata, Karabi Mrisho, Kelvin Haule, Yusuph Kamba, Aston Pardon, Danford Ngessy, Peter Mwakibibi, John Alex, Daniel Chundu, Ally Kimwaga na wengine tuliokuwa Tukuyu Stars tulivyopambwa kutokana na kujituma kwetu uwanjani na Charles Hilary.

Siyo hao niliowataja katika makala hii, bali walikuwepo wengine wengi ambao utangazaji wa kina Chilambo, Hilary, Jongo na wengineo mahiri kwa wakati huo, ulichangia kuchochea ari kwa wachezaji na timu kwa ujumla.

Binafsi, nawaombea heri kwani mchango wao ulikuwa chachu ya mafanikio ya wachezaji wengi wa zamani waliotangulia mbelea ya haki na wengineo ambao bado tunapumua.

Ndiyo maana ninasema kwa dhati kabisa, mimi ni miongoni mwa wachezaji wa zamani ambao nilinufaika kwa kiasi kikubwa kwa upande wa soka kutokana na hamasa ya watangazaji hawa. Mwenyezi Mungu awazidishie heri!

Mwandishi wa Makala hii ni mchezaji wa zamani wa soka aliyewahi kuwika na timu kadha wa kadha kama Tukuyu Stars, Simba, Yanga na Taifa Stars
 
Back
Top Bottom