Mkuu Kichuguu,
Heshima mbele sana mkuu, hapo ni Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe "Baba Zole Zole", au kwa jina maarufu "Soloist Natiionally", kama sikosei akiwa safarini Songea na bendi yake mpya ya Super Volcano, baada tu ya kutoka katika bendi yake ya zamani maarufu sana ya Morogoro Jazz, yaani Wana-Sululu Saka Saka na Likembe Mahoka,
Baada ya hiyo ziara ya Songea, alirudi mjini Dar ambako nilimuona akishiriki katika mashindano ya Muziki ya kutafuta nafasi ya kuliwakilisha taifa letu katika Maonyesho Ya Mtu Mweusi, yaliyofanyika Mjini Lagos in the 70s, nakumbuka ingawa nilikuwa mdogo lakini nilihudhuria sana mashindano hayo yaliyokuwa yakifanyika katika Uwanja Wa Mnazi Mmoja, saaa za jioni baada ya kutoka Shuleni. Bendi ya Afro 70 na Patric Balisidya, ndiyo iliyoshinda na kupewa nafasi hiyo ya kwenda Lagos, ambayo ndio hasa iliyokuwa safari yao ya mwisho katika ulimwengu wa muziki.
Marehemu Mbaraka Mwinshehe, na Mpiga Ngoma RIP Morris Nyunyusa, hawa walikuwa ndio wawakilishi wakubwa wa taifa letu, kwenye maonyesho mbali mbali ya sanaa ya kimataifa na walilitangaza sana jina la taifa letu huko, hasa mwaka 1970 walipokwenda kutuwakilisha kwenye maonyesho ya Expo Japan, Mungu awaweke mahali pema huko mbele ya haki,
mara ya mwisho nilimuona Marehemu Mbaraka Mwinshehe, akipiga muziki wa dansi katika ukumbi wa muziki wa Planters, kwenye kona ya njia panda ya Uwanja wa Ndege wananchi wengi tulimiminika kumuona huyu shujaa, lakini alipiga nyimbo tatu tu na umeme ukazimika, ikawa ndio basi tumeliwa kiingilio mwezi uliofuatia Mbaraka alisafiri kwenda nchini Kenya, kurekodi santuri mpya na kutafuta vyombo vipya vya bendi yake, akiwa nchini Kenya alianzia Nairobi, baadaye akiwa safarini kwenda kupiga muziki mjini Mombasa, ndio mauti yakamkuta katika ajali mbaya sana ya gari, ambapo alipoteza damu nyingi sana, kuna uvumi ambao ulienea baadaye kuwa kukosekana kwake kuwa na hela za kutosha ndiko kulikosababisha kushindwa kutibiwa katika Hospitali kubwa ya Private kule Nchini Kenya, ambako inadaiwa angeweza kuponyeshwa iwapo angepewa msaada haraka kama angekuwa na hela zinazotakiwa, lakini siuamini sana huu uvumi,
Lakini anyway, huyu alikuwa mmoja wa mashujaa wetu, ambaye aliweza kulitumia gitaa lake kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia, bada ya kufariki kwake mdogo wake Ibrahim Mwinshehe na mpiga rythm wake, Charles Kasembe, walijaribu kuendeleza libeneke, lakini hawakufika mbali ilikuwa ni vigumu kuvaa viatu vya marehemu ambaye pekee tu ndiye aliyekuwa nyota wa ile bendi,
Mpigaji wake mwingine kwa jina la Lazaro Bonzo, yeye alihamia Nairobi na kuunda bendi ya Orch. Lombe Lombe, lakini nayo pia haikudumu sana, Moro Jazz nao pia hawakufika mbali, na to this day Morogoro hakuna tena bendi ya kutisha kama enzi hizo, ule wimbo wa Mbaraka wa kuisifia timu yetu ya taifa ya mpira wa miguu, mpaka leo unapigwa sana kwenye radio Germany, akiwasifia kina Elias Michael, Mweri, Mohamed Chuma, Zimbwe, Chitete, Shiwa, Maulidi "Mexico" Dilunga, Kitwana Manara, Adama Sabu, Gibbons Sembuli, Abdulrahamani Juma, Mohamed Salim, Omar Mahadhi, Zakaria Kinanda, Mohamed Ngulungu na kocha wao alikuwa akiitwa Paul West Gwivaha, damn! hizo zilikuwa ni enzi ndugu zangu yaani za Gossage Cup.
Ahsante Mkuu Kichuguu, kwa hizo picha za huyu shujaaa, Mungu amuweke mahali pema.