Pre GE2025 Tukumbushane baadhi ya Matukio ambayo hufanywa na Wanasiasa Majimboni kuelekea Uchaguzi ili kuombea kura

Pre GE2025 Tukumbushane baadhi ya Matukio ambayo hufanywa na Wanasiasa Majimboni kuelekea Uchaguzi ili kuombea kura

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

Waufukweni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2024
Posts
2,060
Reaction score
5,648
Kuna msemo wa Waswahili wanakwambia bora Ukosee njia lakini usikosee Kuoa ila binafsi naona hakuna kosa kubwa katika hii dunia kama kukosea katika kuchagua kiongozi bora ambaye atakuja kutatua changamoto katika Jamii.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa, kumekuwa na mwelekeo wa baadhi ya wanasiasa kujitokeza kama wahudumu wa jamii. Mara nyingi, wanaonekana wakifanya ziara katika vijiji mbalimbali ndani ya majimbo yao, wakijishughulisha na miradi ya maendeleo kama vile kujenga shule, vituo vya afya, na miradi ya maji. Lengo kubwa la mwelekeo huu ni kuteka hisia za wapiga kura ili kupata uungwaji mkono katika uchaguzi.

Pia, Soma: Mbunge agalagala kwenye mchanga akimuombea Kura Rais Samia
Hata hivyo, ni muhimu kwa wapiga kura kuchambua kwa makini nia halisi ya wanasiasa hawa. Ingawa ni vyema kuona viongozi wakijitolea kusaidia jamii, ni lazima kutafakari kama misaada hiyo ni ya dhati au ni njia ya kisasa ya kupigia debe. Mara nyingi, miradi hii huonekana kuwa na nguvu zaidi wakati wa kampeni, na inahitaji kuangaliwa kwa jicho la pili.

Kila mmojawapo anapaswa kuangalia rekodi za viongozi na mipango yao ya baadae, badala ya kuzingatia tu matendo ya muda mfupi. Je, wanasiasa hawa wana mipango endelevu ya kusaidia jamii hata baada ya uchaguzi? Ni lazima wapiga kura wafanye maamuzi yanayoangazia si tu matendo ya sasa, bali pia ufanisi wa viongozi hao katika kutatua changamoto za jamii kwa muda mrefu.

Pia, Soma: Wanasiasa na mbinu ya kuweka TV kwenye mikusanyiko ili kuhadaa wapiga kura

Tujimbushane baadhi ya mambo ambayo hufanywa na baadhi ya Wabunge kwenye Majimbo yao kama sehemu ya kuwashawishi au Kuwahadaha Wananchi ambao ndio wapiga kura na kisha wakipata Ubunge wanatokomea mpaka msimu wa Uchaguzi unapokaribia:

1: Kuanzisha Ligi za Soka - Wanasiasa huanzisha ligi za soka zinazobeba majina yao, ikiwemo kuandaa mashindano ya michezo. Hii inawasaidia kujenga picha ya mtu anayejali.

2: Kutembelea Nyumba za Ibada - Huenda kwenye makanisa na misikiti ili kujenga uhusiano mzuri na waumini, wakijitambulisha kama watu wanaomuogopa Mungu na wana nia njema.

3: Kutoa Misaada kwa Wahitaji - Wakati wa kampeni, wanatoa msaada wa chakula, mavazi, na hata fedha kwa jamii zenye uhitaji.

4: Kushiriki Shughuli za Kijamii - Wanasiasa au Watia nia hujihusisha na shughuli kama usafi wa mazingira, sherehe za kijamii, au miradi ya maendeleo. Hii inawapa fursa ya kujionyesha kama viongozi wa jamii.

5: Kujichanganya na Wananchi - Wanajitahidi kuonekana kwenye biashara zao (mfano kunywa chai migahawani, sokoni), wakichangia na kushiriki katika shughuli za kila siku za wananchi.

6: Kuanzisha Miradi ya Maendeleo - Wakati wa kampeni, huanzisha miradi kama visima, shule, au barabara, ingawa mara nyingi miradi hii inaweza kuwa na nia ya kisiasa zaidi kuliko ya kweli.
 
Back
Top Bottom