Yaani nimesoma majibu ya watu kwenye huu uzi, nimesikitika sana, ila pia ninamshukuru mleta mada (every dark cloud has a silver lining).
Jambo la HEDHI SALAMA ni JAMBO LA KIJAMII!! Naomba tutambue hili. Tuanze na haya machache:
1. Linagusa afya ya wasichana na wanawake: sababu moja wapo ya ongezeko la ugumba, saratani ya kizazi na magonjwa ya uzazi, ni pamoja na kutokuwa na usalama wa hedhi. Taarifa potofu na ukosefu wa taulo salama umeumiza wengi. Hasa kwa vizazi vya sasa, ufahamu hafifu wa chakula kinavyoathiri hedhi, matumizi yasiyo sahihi ya dawa, taulo zisizo salama na vitu vingine, vinazidi kuwaumiza na kuwaathiri vibaya wasichana. Kuna tatizo la maumivu makala wakati wa hedhi (dysmenorrhea) umeongezeka sana na unaathiri ufanisi wa binti au mwanamke katika kazi zake za kila siku, na pia huweza kuashiria magonjwa ya uzazi.
2. Linagusa uchumi: Kila mwezi karibia kila binti au mwanamke aliyevunja ungo, lazima agharamike kupata taulo za kike au hata dawa za maumivu. Hii siyo gharama ya hiari, hasa ukihitaji usalama. Je tunajua linayoathiri uchumi wa kina mama? Pakiti ya taulo za kike ni kati ya Tsh 1,200 mpaka Tsh4,000 na zinakaa kati ya 8 hadi 10. Kila mzunguko (kutegemeana na wingi wa damu) mwanamke hutakiwa kutumia si chini ya taulo 3 kwa siku, ile awe salama. Angalao sasa kuna taulo re-usable au re-usable cups, japo siyo nyingi na siyo wote wanaweza kutumia.
3. Linagusa miundo mbinu ya maeneo ya umma: Lazima kuzingatia miundo mbinu - hasa vyoo na mabafu - katika maeneo ya umma mbayo yatakidhi mwanamke kujisafisha na kupunguza uwezekano wa athari za kiafya. Hili ni muhimu hasa mashuleni, katika hospitali, ofisi za umma, katika masoko, nk.
4. Linagusa elimu na maarifa: Elimu na maarifa kwa umma kuhusu hedhi salama ni muhimu kwa kuwa hili ni swala linalogusa sekta mbalimbali, zenye wanawake na wanaume. Elimu na maarifa sahihi hupunguza athari siyo tu kwa wanawake bali hata wanaume.
Kusema unaona kinyaa kuzungumzia maswala ya hedhi salama ni ubinafsi. Hakuna aliyechagua kuzaliwa mwanamke wala mwanaume, hivyo tuheshimu baiolojia ya kila mmoja na kuthamini tunayopitia kama binadamu.