Ndugu yangu,
Siku zote kwenye jambo lolote hukusanyika watu wenye malengo tofauti tofauti. Ndio ulimwengu ulivyo. Hata hivyo hatuachi kuzungumzia au kuangazia maswala muhimu kwa visingizio kuwa kuna watu wana ajenda zao.
Tukianza kuhoji dhamira ya kila mmoja bila kutazama upana na uhalisia wa jambo na jinsi linavyoathiri jamii, hatutafika popote. Je hakuna wasichana wanaodhurika na kutofahamu au kuwa na uwezo wa hedhi salama? Jibu, ni kuwa wapo.
Tukisema hedhi ni jambo limekuwa kwa muda mrefu, tunasahau maswala mengi yamekuwa kwa muda mrefu ila leo hii bado tunakabiliana nayo. Maswala ya uzazi salama, ni mfano mmoja tu. Leo hii tunazungumzia kujenga hospitali, kwenda kliniki wazazi wote, elimu ya afya ya mtoto na mzazi, nk. Kwanini tusibaki na utaratibu wa zamani kwa kuwa uzazi umekuwepo tangu zamani?
Mijadala au kazi zinazolenga kweli kumhakikishia msichana na mwanamke hedhi salama siyo udhalilishaji. Hasa, udhalilishaji ni kmuacha msichana au mwanamke ateseke kwa sababu tu, jamii inaonea haya jambo la kiasili, yaliyotokana na uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
Mila na desturi hubadilika kwa jinsi maisha yanavyobadilika. Kwa mfano, zamani hatukuwa na kwenda shule, hivyo kujisitiri kuliendana na shughuli za kipindi hicho. Leo hii umwambie mtoto wa kike asiende shule kwa sababu ajisitiri nyumbani?
Tusiepuke mijadala ya mbadala salama na mbinu bora katika mapito yetu kama binadamu. Muhimu ni kuheshimiana, kuthaminiana na kupunguza madhara hasi kwa binadamu mwenzako na mazingira yako.