Mimi nilichojifunza ni kuwa serikali ya sasa imeanza kubadilika kwenye nyanja ya mawasiliano kwa umma hasa namna ya kukabiliana na tuhuma na uzushi wa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa jinsi ambavyo serikali/Ikulu imekabiliana na uzushi uliofanyika kwa muda wa siku tatu kuhusu afya ya Rais Magufuli imeonyesha mabadiliko makubwa sana!
Nakumbuka wakati Rais Magufuli anaingia madarakani alikuwa anapenda kujibu kwa maneno kila tuhuma na uzushi uliohusu yeye au serikali yake bila kujua kwa kufanya hivyo alikuwa anawapa umaarufu wale ambao walikuwa wanatoa uzushi au tuhuma.
Kujibu kila uzushi na tuhuma kwa maneno ndio kulimpa umaarufu Mwana Mama aitwaye Mange Kimambi ambaye alijikuta akipata wafuasi zaidi ya milioni 1.2 kutoka laki 300000.
Kanuni moja ya kukabiliana na uzushi ni kuupuuza na kama ukiona bado unaendelea basi unachofanya ni kuonyesha ukweli kwa vitendo katika muda mwafaka kwa sababu uzushi ukiachwa kwa muda mrefu uendelee kuwepo huanza kuaminisha jamii.
Uzushi kuhusu afya ya Rais Magufuli imejibiwa kwa muda mwafaka lakini kikubwa zaidi njia iliyotumika katika kujibu imeondoa imani (credibility) yote ya yule aliyeuanzisha na kuushupalia lakini vile vile waliouamini wameonekana ni wajinga au wapumbavu.
Kitu kingine nilichojifunza baada ya kuona baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kama Zitto Kabwe, Dkt Vicent Mashinji na Godbless Lema wakiamini uzushi kuhusu afya ya Rais Magufuli ni kuwa viongozi wa vyama vya upinzani hawajui linaloendelea Ikulu. Kwa maana nyingine, siri za Ikulu kwa sasa hazitoki kwa urahisi. Fikiria viongozi wa vyama vikuu vya upinzani hawajui hata alipo Rais wa nchi achilia mbali afya yake!
Mwisho kabisa nimejifunza kuwa inatakiwa kwanza kuchukua muda kabla ya kuamini kile ambacho kimeandikwa kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ukweli hukawia kufika.
Nimalizie kwa kuandika, Nimeamini Uongo hupanda kwa lifti. Ukweli hupanda kwa ngazi ili kumfikia mlengwa!