SoC02 Tunahitaji kujenga taasisi huru na imara ili kuyafikia maendeleo endelevu

SoC02 Tunahitaji kujenga taasisi huru na imara ili kuyafikia maendeleo endelevu

Stories of Change - 2022 Competition

Stephen Ngalya Chelu

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2017
Posts
8,252
Reaction score
18,335
UTANGULIZI
Taasisi ni vyombo vinavyoanzishwa kisheria na serikali na kupewa mamlaka ya kusimamia au kutekeleza majukumu maalum ili kuisaidia serikali katika utendaji. Ili maendeleo yawe na manufaa kwa wananchi, yanapaswa kuwa endelevu kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo misingi imara ya kiuchumi, kijamii na kulinda mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ili kuyafikia maendeleo endelevu, taasisi zina jukumu la kupanga, kutekeleza, kusimamia mipango na kutoa huduma mbalimbali za jamii. Hata hivyo, Tanzania tumekuwa tukishuhudia mapungufu makubwa sana katika katika utendaji wa taasisi zetu kutokana na taasisi hizi kutokuwa huru na imara.

Hivyo basi, ni wazi kuwa ujenzi wa taasisi huru na imara ni jambo la muhimu sana ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana. Lakini kabla ya kujadili ni jinsi gani tunaweza kuzifanya taasisi zetu ziwe huru na imara, kwanza tuone ni madhara gani yanayoikumba nchi kutokana na kutokuwepo kwa taasisi huru na zenye nguvu kimamlaka.


MABADILIKO YA MARA KWA MARA YA SERA NA VIPAUMBELE
Tanzania imekuwa ikipitia mabadiliko ya mara kwa mara ya sera na vipaumbele hali inayotokana na taasisi kukosa nguvu kutunga sera na kusimamia utekelezwaji wake, hivyo kusubiri kauli na misimamo kutoka kwa viongozi wa juu wa serikali. Hali hii imekuwa ikifanya taifa kukosa mwelekeo wa kudumu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kwa mfano, wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na Hayati John Magufuli, serikali ilichukua uamuzi wa kuhamasisha zaidi matumizi ya njia za asili katika kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 huku ikionyeshwa kutokuunga mkono matumizi ya chanjo zilizoidhinishwa na shirika la afya duniani (WHO), na mamlaka zinazosimamia masuala ya afya hapa nchini ziliunga mkono msimamo huo.

_117381410_4d6cae7c-62e8-439f-a607-e45d1661603d.jpg.jpeg

Mtambo wa kujifukiza, Muhimbili (Picha kutoka tovuti ya BBC)

Baada ya kifo cha Rais Magufuli na Mh. Samia Suluhu kuchukua nafasi hiyo, msimamo wa serikali juu ya namna ya kushughulika na ugonjwa wa UVIKO-19 ulibadilika na chanjo zikaletwa huku mamlaka zile zile zilizonyesha kutokuunga mkono ujio wa chanjo hapo mwanzo, zilisimama kidete kuhamasisha wananchi kuchanja. Hii ni picha ya wazi kuwa taasisi zetu bado hazina nguvu ya kuamua kwa uhuru katika mambo yaliyo chini yake.


VITENDO VYA RUSHWA NA UBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA
Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya mwaka wa fedha 2020/2021 imeonyesha kuwa kuna upotevu mkubwa wa fedha za umma katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma. Kwa mfano, ripoti hiyo ilieleza kuwa fedha za Mfuko wa dhamana kwa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati, Sh bilioni 7 zilizopelekwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo hazikutumika kwa malengo ya kutoa dhamana kwa wahusika, zilitumika kwa matumizi ya kibiashara ya kibenki.

Vitendo kama hivyo vya ubadhirifu vimekuwa vikiripotiwa kila mwaka katika ripoti hiyo lakini bado kumekuwa hakuna hatua stahiki zinazochukuliwa ili kudhibiti vitendo hivyo visitokee tena na pia kuwawajibisha waliohusika. Haya ni matokeo ya kukosekana mifumo imara ya kitaasisi kusimamia sheria na tatatibu katika kuratibu na kudhibiti matumizi ya fedha za umma na kuwawajibisha wanaohusika hali inayosababisha vitendo hivi kuendelea kutokea na kukwamisha juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.


MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA NA KUZOROTA KWA UWAJIBIKAJI
Taasisi zinapokuwa butu hutengeneza mwanya kwa viongozi na watumishi wa serikali kutokuwajibika ama kutumia madaraka yao vibaya wakiwa hawana hofu ya kushughulikiwa kisheria kutokana na makosa yao. Pia, sheria zinazowapa kinga ya kutokushitakiwa baadhi ya viongozi wa juu wa serkali huwafanya viongozi hawa kuwa na mkono mrefu kuliko sheria hali inayohatarisha uhuru wa maamuzi katika taasisi na mamlaka mbalimbali.


KUZOROTA KWA HAKI NA DEMOKRASIA
Yameshuhudiwa matukio mengi yenye kuashiria uvunjifu misingi ya haki na demokrasia, lakini mamlaka zinazohusika zimekuwa zikishindwa kushughulikia matukio hayo katika namna ya kuridhisha. Matukio kama kesi za kughushi, kujeruhiwa, kuuawa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa watu ambao wamekuwa wakitumia haki yao kujieleza na kutoa maoni, yamekuwa yakiacha maswali mengi kutokana na mamlaka zinazohusika kushindwa kuyatafutia ufumbuzi. Hali hii imekuwa ikiendelea kujenga mpasuko katika taifa hivyo kutishia juhudi za kujenga utangamano wa kitaifa kueleka maendeleo endelevu.

_107830268_8178abf9-8c1b-4ea1-aed0-6ad388bd33b9.jpg.jpeg

Azory Gwanda (Picha kutoka tovuti ya BBC)


Hivyo basi, ili tuweze kujenga taasisi huru na imara yafuatayo yanapaswa kufanyika.


KUWA NA DIRA YA MAENDELEO YA MUDA MREFU
Hii ndiyo ramani ya wapi hasa sisi kama taifa tunataka kuelekea. Dira hii haipaswi kuwepo kwenye makaratasi tu, bali kunapaswa kuwepo na mipango inayotekelezeka katika kuyafikia malengo yanayotarajiwa. Katika msingi huu, itamlazimu kila kiongozi na mfanyakazi wa umma, bila kujali mitazamo yake binafsi, ketekeleza mipango na mikakati kuelekea dira ya maendeleo ya taifa na si vinginevyo.


KUJENGA MISINGI IMARA YA KISHERIA
Utawala unaozipa taasisi uhuru na nguvu unategemea zaidi uimara wa misingi ya sheria. Hivyo basi, ili kuzifanya ziwe na nguvu na uhuru, unahitajika mfumo mzuri wa kisheria ambao utatoa uwanja mzuri wa taasisi kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi. Misingi hii ya kisheria inapaswa kujengwa kwa utaratibu ufuatao;

Kwanza, kuwa na katiba ambayo itapunguza mamlaka na majukumu ya viongozi wa juu wa serikali na kuyatawanya kwa taasisi zingine. Hii itasaidia kupunguza viongozi kuingilia maamuzi ya taasisi. Hatua hii itasaidia kuongeza uhuru na ufanisi katika utendaji wa kazi.

Pili, kuwaondolea kinga ya kutokushitakiwa viongozi wote wenye kinga hiyo. Hii itazifanya mamlaka za kisheria kuwa na nafasi ya kuwawajibisha wanapovunja sheria. Hii itawafanya viongozi hao kuwa wawajibikaji na kuheshimu sheria na taratibu katika kipindi chote cha kutumikia nafasi zao.


KUHESHIMU MISINGI YA UTAWALA WA SHERIA.
Kama ambavyo imeelezwa hapo kabla kuwa utawala unaoweka mamlaka kwa taasisi ni utawala unaoheshimu sheria. Hivyo viongozi na taasisi zinapaswa kuheshimu na kufuata mipaka yake katika utekelezaji wa majukumu. Hatua hii itafanya viongozi au taasisi kutokuingilia utendaji ama maamuzi ya taasisi nyingine kinyume na sheria.


KUWAJENGEA WANANCHI UELEWA MPANA KUHUSU HAKI ZAO
Wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusi haki zao kisheria. Hii itawafanya wananchi waweze kuihoji serikali na taasisi zake pale ambapo wataona kuwa zinaenda kinyume na utaratibu wa kisheria.


HITIMISHO
Uwepo wa taasisi huru na imara unajenga uhakika kwa taifa kupanga na kuiona kesho. Kwa hiyo napenda kutoa wito kwa viongozi, taasisi na wananchi kwa ujumla kuongeza juhudi za kufanya mabadiliko katika mfumo wa kiutawala ili tupate kuwa na taasisi huru na zenye nguvu ili kuongeza kasi ya taifa letu katika kuyafikia amendeleo endelevu.​
 
Upvote 2
Kwani kwenye sheria ya sasa wananchi hawaruhusiwi kuhoji kuhusu serikali ?
Uhuru kisheria upo, lakini utekelezwaji wa sheria ndipo ttizo lilipo. Ndiyo maana iznahitajika taasisi huru na imara ambazo pamoja na mengine, zisimamie misingi ya sheria kwa haki bila kuingiliwa.
 
Uhuru kisheria upo, lakini utekelezwaji wa sheria ndipo ttizo lilipo. Ndiyo maana iznahitajika taasisi huru na imara ambazo pamoja na mengine, zisimamie misingi ya sheria kwa haki bila kuingiliwa.
Kwani taasisi zitasimamia haki kwa misingi ya sheria hipi sihii wanayotumia serikali ya sasa ? Kwaiyo concept yako ipo upande gani kwenye katiba au kuongezwe kwa mamlaka ya NNE kwa sababu sasa hivi zipo tatu na kuwepo na taasisi nyengine ni uharibifu wa kodi za wananchi bora hizo kodi zipelekwe kwenye vituo vya yatima.
 
Kwani taasisi zitasimamia haki kwa misingi ya sheria hipi sihii wanayotumia serikali ya sasa ? Kwaiyo concept yako ipo upande gani kwenye katiba au kuongezwe kwa mamlaka ya NNE kwa sababu sasa hivi zipo tatu na kuwepo na taasisi nyengine ni uharibifu wa kodi za wananchi bora hizo kodi zipelekwe kwenye vituo vya yatima.
Ninachokieleza hapo si kuongezeka kwa mhimili mwingine bali ni uwepo wa halisi mgawanyo wa mamlaka ili mihimili hiyo mitatu iweze kufanya kazi bila mhimili mmoja kuuingilia kimaamuzi mhimili mwingine.
 
Kwani taasisi zitasimamia haki kwa misingi ya sheria hipi sihii wanayotumia serikali ya sasa ? kuwepo na taasisi nyengine ni uharibifu wa kodi za wananchi bora hizo kodi zipelekwe kwenye vituo vya yatima.
Kwa katiba hii tunayo tumia au nyengine maana naona ume base kwenye mgawanyo ambao bado utakuja kuwa kwenye mstari ule ule tu kama uliopo ?
 
Kwa katiba hii tunayo tumia au nyengine maana naona ume base kwenye mgawanyo ambao bado utakuja kuwa kwenye mstari ule ule tu kama uliopo ?
Msingi wa kujenga taasisi imara unaanzia kwenye katiba ambayo mdiyo sheria mama.
 
Back
Top Bottom