Katika hoja yako hii. Je, unakubaliana na Mh. Tundu Lissu anaposema Mwl. Nyerere alizoea kuishi kwa uongo na udanganyifu.
Tunaweza kucheza na maneno kwa mitindo kadhaa. Binafsi, sifurahishwi na uwasilishaji hoja wa Lissu; una jazba isiyo na ulazima. Bila shaka hiyo ndiyo hulka yake ambayo si rahisi kutibika katika umri aliofikia. LAKINI ana hoja nzito ambayo ni muhimu kwa yeyote yule anayetaka kuwa mshiriki mzuri wa jukwaa hili. Kwanza, katika masuala ya siasa na uongozi hapa duniani mantiki hairuhusu mtu "kuabudiwa" kama wengine wanavyotaka kuwafanya Nyerere, Sokoine, Mandela, n.k. Ukiisha ingiza "ibada ya binadamu" basi umeshakufuru
misingi ya mantiki na hata ya Mwenyenzi Mungu (ambaye pekee anastahili kuabudiwa - kwa imani zetu wengine). NA huwezi kuwa na michango ya maana katika jukwaa hili kama unataka kuabudu binadamu.
Pili, mahsusi kwa Mwalimu Nyerere, tukubaliane kuwa alikuwa mkuu (
a great person) ambaye aliyekuwa na picha rasmi (vision) ya nchi yake aliyoitaka yeye kwa malengo mazuri kabisa (hata kama picha hiyo ilikuwa na kasoro). Sio kama wengi waliomfuatia waliokuwa wakiangalia zaidi maslahi mafupi hususan ya mifuko yao na familia na marafiki zao. Ili kutimiza picha aliyokuwa nayo akawa mtu wa mikakati. Ukishakuwa mtu wa mikakati basi tukubaliane
si nyakati zote utakuwa mkweli na muwazi. Wakati mwingine mikakati huhusisha ulaghai (kwa nia njema) ili malengo yake hatimaye yafikiwe. Manake lengo la mikakati ni "kuwaweka watu sawa" waendane na mipango yako - ama iwe mizuri ama iwe mibaya. Cha maana katika mikakati ni uzuri wa lengo lako la mwisho.
Wengi tunachomheshimu Nyerere ni kuwa mikakati yake haikuwa ya kujenga taifa la kujinufaisha yeye na familia yake binafsi. Hakuwa na tamaa nzito za kibinadamu za mali na mengineyo. Malengo yake bila shaka yalikuwa mazuri kwa wote na kwa taifa zima. Tatizo kubwa la dhahiri ni kuwa na
ubinafsi wa fikra uliokithiri; hakuwa tayari sana kukubali mawazo mbadala ya wengine. Ushahidi wa kukosa subira na mawazo mbadala ni mwingi kuanzia kwenye mitafaruku na akina Kambona, Kassanga Tumbo, Jumbe, Mtei, n.k. Wakati mwingine alikuwa sahihi hasa kwa wale waliokuwa na mipango ya kujikweza kwa elimu na nafasi zao lakini ushahidi unaonyesha pia aliishia kujenga uongozi wa kujikomba sana (
bootlickers).
Kwamba aliendesha masuala ya muungano
kimkakati sana halina ubishi. Aidha hatuwezi kusema kuwa alikuwa na nia mbaya katika muungano huu. Hakuna ushahidi wa "nia mbaya". Tatizo kubwa ni kuwa alitwisha uongozi wa pande zote maudhui yake pekee na kutosimamia taratibu kamilifu na za wazi katika mchakato mzima wa muungano. Ni kama vile kwake yeye hoja likuwa ni "muungano kwa gharama yoyote ile". Ni dhahiri basi kuwa mahangaiko tunayopata leo (kuanzia wakati wa Jumbe) kuhusu muungano ni matokeo (
consequences) za mapungufu ya "mikakati" ya Mwalimu katika mchakato aliousimamia. Ukitaka kuwa mkorofi (usiye na mikakati kabisa) kama Lissu unaweza kumpa vigezo vya
"uongo na udanganyifu". Lakini ukiwa mtu mstaarabu huwezi kutumia lugha hiyo kwa Mwalimu; utamchukulia kama mtu aliyekuwa na mikakati dhaifu (upungufu wa kibinadamu!).