Wapenzi na mashabiki wa Simba watalaumu kila mtu kwa matokeo mabovu kwenye msimu huu wa ligi japo walikuwa na mafanikio kwenye shirikisho Afrika. Kosa lilianzia kwenye usajili wa msimu uliopita kusajili zaidi vijana wa kiume badala ya kusajili wanaume kamili. Sakho, Banda, Mhilu Mwanuke ni vijana "promising" ambao watakuja kuwa na msaada mkubwa sana kwa Simba miaka miwili/mitatu ijayo. Mfano mzuri Yanga ilisajili msimu uliopita wanaume kama Mayele, Aucho, Bangala na wengineo ndio maana wamekuwa na matokeo mazuri. Mzimu ulikokuwa unamtafuna Azam kwa kung'ang'ania vijana ndio huo unamtafuna Simba sasa hivi. Mfano mdogo tu hao wakina Sakho na Banda wakisukumwa tu kidogo chini wala hawaamki hata kama wana nafasi ya kuamka na kufunga lakini mwenzao Kibu akisukumwa mpaka aende chini ni kazi na akiamka anaamka na mpira wake safari inaendelea kuelekea goli la mpinzani labda tu asikie filimbi ya mwamuzi.
Na iwapo viongozi hawatakuwa makini katika kipindi hiki muhimu cha usajili basi mwakani vilio ndio vitakuwa mara mbili zaidi. Ushauri wangu wa bure kwa viongozi wa Simba wazingatie vigezo vifuatavyo:-
1. Wasajili wachezaji wenye "work rate" kubwa uwanjani kama ilivyokuwa kwa Luis na Dilunga. Yaani hawa utawakuta wapo golini kwa adui
wanashambulia mara ghafla unawaona pembeni kwenye goli lao wamefanya "tackling" kuokoa wakiwasaidia mabeki wao wa pembeni.
2. Wasajili wachezaji ambao hawatembei uwanjani baada ya kunyang'anywa mpira au kupoteza mpira kizembe. Wachezaji kama Bwalya na
Sakho wana vipaji vya hali ya juu lakini vipaji hivyo vinawasaidia wao tu kupata sifa na havina msaada kwa timu kabisa. Mbaya zaidi
wanakaa na mpira muda mrefu miguuni mwao halafu wakinyangánywa na adui wanatembea na kuwaachia wenzao kazi ya kuutafuta
mpira.
3. Wasajili viungo na washambuliaji wenye kasi ambao wataichangamsha timu uwanjani. Sio siri Simba sasa hivi ipo "slow " sana.
Inatengeneza mashambulizi yake taratibu sana kutokea nyuma kiasi wakati timu inapoamua kwenda kushambulia unakuta timu pinzani
zimesha jipanga kuzuia. Hili la kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma halina shida iwapo tu utakuwa na wachezaji wenye "quality" ya
Chama na Luisi kwani wao wawili tu wanaweza kugongeana mpira kuanzia nyuma mpaka golini kwa adui.
4. Wasajili wachezaji wenye maumbo makubwa hii itawasidia pale wanapokutana na timu zinacheza mpira wa nguvu.
5. Mwisho kabisa wasajili wachezaji wapambanaji muda wote wawapo uwanjani kwa dakika zote tisini. Aina ya wachezaji wapambanaji ni
kama Kapombe, Inonga, Kibu na Lwanga (japo huyu amekuwa na changamoto ya majeraha).
Ni mtizamo tu.