Sioni haja ya kumshambulia mtu badala ya hoja. Hivyo basi, tujiulize kama muungano kuvunjika ni jambo linalowezekana au la. Kama linawezekana, tunajiandaaje kisaikolojia? Kuna haja ya kujiandaa?
Binafsi, naamini mjadala wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar unazidi kuwa kwenye vinywa vya wengi hasa kwa sababu kimantiki umepoteza uhalali wa kikatiba pale wazanzibari walipoweka dhahiri kuwa wao kama "Taifa" wana nchi yao inayohitaji kutambuliwa kwa ukamili wake. Ile katiba yao isiyo na mvuto sana kwa wabara wengi (na hata wachache) imevunja sura ya muungano.
Haimaanishi kuwa muungano ulikuwa katika hali nzuri sana kabla ya kutungwa na kupitishwa kwa katiba mpya ya Wazanzibari, la hasha, bali tunazozitambua kama kero za muungano pamoja na manung'uniko mengine toka pande zote mbili na hasa kwa upande wa Zanzibar, pamoja na mapungufu mengi katika katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na pia ukichanganya na udhaifu wa serikali katika kusimamia katiba ndio vimechochea kutufikisha tulipo leo katika mijadala ya Kikatiba na uwepo/uhalali wa muungano.
Tukiweka uzalendo mbele badala ya kuwa watumwa wa siasa zetu za kinafiki zilizohodhi mchakato mzima wa kuujadili muungano, na kwa uzalendo wetu tukaitupilia mbali hii saikolojia ya kutafakari na kutafakariwa kama kondoo katika zizi linalolindwa na fisi, naamini yanaweza yakapatikana majibu mazuri zaidi ya maswali mengi muhimu.
Siamini kama sisi wananchi wa Tanzania hatuwezi kufikia hatua na kusema hapana, imetosha, tujitazame upya. Waliopo kwenye vyombo vya maamuzi wanapokiuka matakwa na kushindwa kufikia matarajio yetu, hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kuwa watu wa "kujiandaa kisaikolojia"? Tuendelee tu na ukondoo wetu au tujitambue kuwa sisi ndio wenye nchi?
Kwako msomaji, Zitto na mleta mada, naomba tutafakari na sote tuchukue hatua.
Ahsanteni.