Heshima kwenu wakuu wangu
Kama kawaida leo nakuja tena katika jukwaa muhimu kwangu hapa JF.
Hakika kuna mambo mengi sana yanayochangia mpaka mtu kuwa na mali nyingi ama utajiri. Ukiachilia mbali matajiri waliorithi mali, waliopata utajiri kwa bahati kama michezo ya bahati nasibu na wale waliojikusanyia mali kutokana na vipaji vyao kama Sanaa na soka, matajiri wote waliobaki ambao walikuwa masikini na wakawa matajiri wana sifa kubwa ya UBAHILI.
Lakini bila kujali umepata vipi utajiri wako, kama hutakuwa mbahili, hakika utafilisika, hakika hutadumu na mali zako, hakika ipo siku watu watakucheka na kusema umefulia. Kiufupi, matajiri wote unawaona duniani ambao wamedumu kwa muda mrefu ni mabahili. Ni vyema pia ujue kwamba ubahili wa mtu kama Warren Buffet hauwezi ukafanana na ubahili kama wa yule Mkinga wa Kariakoo, wote ni ubahili ila tofauti ni mmoja anafanya ubahili kulingana na matrilioni alionayo na mwingine anafanya ubahili kulingana na mamilioni alionayo.
Naomba pia ieleweke kwamba, ninaposema tajiri natambua kwamba unatofautiana ngazi. Kuna wanaomiliki duka moja kubwa la jumla wakati anaanza maisha alianza kuuza duka la kaka yake, kisha kiosk baadae akamiliki duka kubwa namuita tajiri. Kuna yule ambaye ana estate labda Chicago naye namuita tajiri. Ana hisa timu ya Barcelona, naye ni tajiri.
Nikiri kwamba hii mada imekuja kichwani baada ya mara kwa mara watu, waume kwa wake kupenda kuniita bahili. Ki ukweli huwa nafarijika sana, sababu kwangu bahili ni kinyume cha mfujaji, kwangu bahili ni mtu anayetumia rasilimali zake kwa uangalifu, kwa akili ama mtu anayetumia mali yake baada ya kushirikisha ubongo kuamua na si moyo. Kwangu ubahili ni hatua moja muhimu kwenda kwenye utajiri. Pia ni hatua muhimu sana, kubaki na utajiri.
Ubahili ni kuishi maisha chini ya kipato chako, na si kuishi maisha sawa na kipato chako, au zaidi ya kipato chako. Ubahili ni ku save. Sijawahi kuona mtu aliyeanzia chini kwa kipato na baadae akawa tajiri halafu akose sifa ya ubahili.
Mark Zuckerberg mmiliki wa Facebook, huvaa t-shirt na jinsi, vazi la bei raisi kazini na katika sehemu kubwa ya maisha yake. Amancio Ortega (ana mali zenye thamani ya $ 66 Billions) huwa anakwenda mgahawani kula na wafanyakazi wake chakula cha kawaida sana. Charlie Ergen (anamiliki $14 bilioni) huwa anabeba chakula kutoka nyumbani kila siku kwenda nacho ofisini kwake (kwenye kampuni yake). Warren Buffet kila siku hutengewa na mke wake kati ya $2 na $3 kwa ajili ya chai.
Hii ni kweli hata kwa Tanzania au Africa, tunawafahamu watu wengi waliofuja mali na sasa hivi wamebaki masikini na kituko kwenye jamii zetu hususani wale waliorithi ama kupata mali kwa ghafla. Nawakubali Wachaga wengi, wapare wengi sababu hii silaha huwafikisha mbali sana kimaisha.
Ubahili sio sifa mbaya. Lakini usiwe mbahili kula, ukawa mfujaji kwa mademu, usiwe mbahili kuitunza familia yako, ukawa mfujaji kwenye mitungi. Ishi maisha ya kawaida, kipato unachopata wekeza.
HATA UWE UNAINGIZA HELA NYINGI KIASI GANI, UKIWA MTU WA KUFUJA MALI UTAKUFA MASIKINI. NA HATA UWE UNAINGIZA PESA NDOGO KIASI GANI, UKIWA BAHILI NA KUWEKEZA UTAKUWA TAJIRI ENDAPO MUNGU ATAKUPA UZIMA.