Ubalozi wa China nchini Tanzania, umeipatia serikali msaada wa vifaa kinga kwa ajili ya kuendelea kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 (Corona).
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akipokea msaada huo jana jijini Dar es Salaam, alisema utaenda kwa watumishi wa afya kote nchini ambao serikali imewapa kipaumbele cha kwanza ili kuwakinga na maambukizi ya Covid-19.
“Kwa niaba ya serikali tunaishukuru sana Serikali ya China kwa mchango huu na niendelee kuwathibitishia wale wote mnaoisaidia Serikali ya Tanzania, msaada huu tutaupeleka kwa watumishi wa afya, kipaumbele ni kuwakinga watumishi wa afya wasipate maambukizi,”alisema Ummy.
Ummy alisema msaada huo uliotolewa na ubalozi wa China nchini Tanzania ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliothibitika kuwa na ugonjwa wa corona, barakoa (mask) 100,000 pamoja na vipima joto vya mkono (thermal scanner) 150.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, alisema nchi yake na Tanzania ni marafiki kwa muda mrefu na ugonjwa huo ulipoikumba nchi yao kwa mara ya kwanza, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono dhidi ya mapambano hivyo na wenyewe wamejitoa kuisaidia kukabiliana nao.
Wang Ke alisema Serikali ya China kwa sasa imechukua hatua na kujitoa rasmi kuwa nchi itakayoisaidia Tanzania katika misaada ya dharura ya vifaa kinga kukabiliana na ugonjwa wa corona.
Katika mwendelezo wa kuisadia vifaa kinga Serikali, kwa mara nyingine tena inatarajia kupokea msaada wa vifaa tiba vya kusaidia wagonjwa kupumua (Ventilator) 500 kutoka kwa mfanyabiashara raia wa China Jack Ma.
Hadi sasa jumla ya wagonjwa waliogundulika kuwa na virusi vya corona nchini ni 24, akiwamo mmoja aliyepoteza maisha, watano wamepona na wengine 18 wanaendelea kupatiwa matibabu katika vituo maalumu vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.