Nimemsikiliza Balozi Jestas Nyamanga akitolea ufafanuzi wa kile alichokiita upotoshaji kuhusu mjadala unaoendelea katika bunge la Ulaya kuhusu Tanzania.
Anadai kilichoketi ni kamati sio bunge zima. Na kwenye kamati waliozungumza ni wabunge watano tu. Hivyo anahitimisha kuwa maoni ya wabunge watano hayawezi kuhesabiwa kuwa ya bunge zima.
Kitu ambacho Balozi hajataka kusema ni kwamba mjadala wa kuhusu Tanzania ni lazima uanzie kamati. Ukitoka kwenye kamati ndipo utaenda kwenye bunge zima. Kwahiyo balozi kusema ni kamati tu imejadili, ni kama anataka kusema mjadala utaishia hapohapo kwenye kamati. Si kweli.
Taarifa ya kamati itapelekwa bungeni ili kuwa na mjadala wa bunge zima. Hata Tanzania tunafanya hivyo. Skendo zote kubwa za Richmond, EPA, Escrow etc mjadala wake ulianzia kwenye kamati na baada ya kamati ndipo bunge zima likajadili. Kwahiyo Balozi angejipa muda ili mjadala utakapohamia kwenye bunge zima asikose cha kuwaambia watu.
Balozi anadai hata kwenye kamati walioongea ni wajumbe watano tu. Na anataka kuitumia idadi hiyo kupuuza maoni ya kamati. Hii si sahihi. Kwanza kitendo cha Mwenyekiti wa kamati hiyo David McAllister kuongea, huo ndio msimamo wa kamati, hata wengine wasipoongea.
Nimkumbushe Balozi kwamba wakati wa skendo ya Richmond, Kamati teule ilikua na wajumbe 11, lakini walioongea public ni watatu tu ambao ni Stella Manyanya, Lucas Selelii na Mwenyekiti wao Harrison Mwakyembe. Je yale mapendekezo yalipuuzwa kwa sababu waliongea wajumbe watatu?
Jambo la muhimu kujiuliza ni je, tuhuma dhidi ya Tanzania ni za kweli au uzushi? Kamati imesema Uchaguzi ulivurugwa. Vyombo vya dola vilitumika kukandamiza upinzani na kukipendelea chama tawala. Baadhi ya watu waliuawa na wengine kuwekwa jela. Je tuhuma hizo ni kweli au uzushi? Hizi ndio hoja za McAllister na kamati yake. Kwahiyo Balozi ajibu hizo hoja sio kusema walioongea kwenye kamati walikua watano tu. 🤣
Halafu Balozi amekwepa kusema ukweli kwamba ni Kamati hiyohiyo iliyotaka maelezo ndani ya saa 48 kwanini Tanzania ilipokea zaidi ya TZS Bilioni 75 za kupambana na athari za corona. Kwanini Balozi hakuishauri serikali igome kutoa maelezo kwa sababu wanaotaka maelezo ni wajumbe watano tu wa kamati? Paradox.!
Wakati akijaribu kujieleza Balozi amejikuta akijikanusha mwenyewe. Amesema Tanzania hatupewi €626M kutoka EU. Halafu hapohapo akasema pesa hizo hazijazuiwa, tumekuwa tukipewa na tutaendelea kupewa kwa sababu zinasaidia miradi ya maendeleo. Sasa kama amekanusha kuwa hatupewi pesa na EU hizo zinazotusaidia kwenye miradi ya maendeleo ni za EU ipi? Liars must have a good memory.
Halafu tuache hii tabia ya kuamini kwamba kila taarifa anayoitoa kiongozi ni ya kweli. Mnakumbuka SACP Zombe alipoua wale wafanyabiashara na kusema ni majambazi, nchi nzima ilimuamini. Kama sio Kikwete kuingilia kati na kuunda kamati, tungeendelea kuamini waliouawa ni majambazi.
Mmesahau kuwa ndege yetu ilipozuiwa Afrika kusini, Bwana Kabudi alijitokeza na kukanusha vikali. Akasema ndege haijazuiwa na wanaoeneza taarifa hiyo ni waongo na wazushi? What happened later?
Tusubiri kamati ya mambo ya nje ya EU imalize vikao vyake ipeleke mapendekezo kwenye bunge zima. Lakini tuache kuhusisha nchi yetu tukufu na "uhuni" wa viongozi wachache. Tanzania yetu ni kubwa kuliko viongozi. Hawa viongozi watapita lakini Tanzania itadumu. Kiongozi akiamua kufanya uhuni, tunapaswa tumlaumu yeye, si kulaumu wanaotaka kutuwekea vikwazo kwa sababu ya uhuni wa viongozi wetu.
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema "Mpumbavu hutizama alipoangukia na kulaumu bali mwerevu huchunguza alipojikwaa na kujisahihisha" Tuangalie tumejikwaa wapi. Kuwatukana mabeberu ni kutizama tulipoangukia. Tuangalie kilichofanya hao mabeberu wakatugeukia ghafla. Mimba haifichwi kwa kuvaa nguo kubwa.!