Wakati Jeshi la Polisi likiwa limejipanga vilivyo katika kukabiliana na vurugu zozote katika kipindi hiki ambacho jimbo la Tarime linajiandaa na uchaguzi mdogo wa kumsaka mbunge wao, watu 15 wenye silaha nzito-nzito zikiwemo za bunduki aina ya SMG na AK-47 wamemwaga risasi kibao jimboni humo na kuwaua watu wawili huku mtu mmoja akijeruhiwa vibaya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Steven Uyuya, tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana katika kijiji cha Magoto, kilichopo katika kata ya Nyakina, tarafa ya Inchage wilayani Tarime.
Kaimu Kamanda huyo amesema watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, na waliingia nchini wakitokea Kenya.
Akasema baada ya kuvamia kijiji hicho, waliwamwagia watu risasi kadhaa kabla ya kupora ng\'ombe 36 na mbuzi sita, kisha kutimkia walikotoka ambako ni nchini Kenya.
Kaimu Kamanda wa Polisi aliyekuwa akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu, amesema tukio hilo lilitokea mishale ya saa 5:30 usiku.
Akasema watu hao walipora ng`ombe wanane wa Bw. Mchama wa Igolu, sita wa Mwita Gombolu na 22 na mbuzi sita wa Menganyi Waikoge.
Akasema katika tukio hilo, majambazi hayo yalimjeruhi kwa risasi katika goti lake la kulia na kumkata panga mguu wa kushoto Bw. Mchama.
Aidha, kutokana na tukio hilo, wananchi waliovamiwa maeneo yao walipiga kelele za kuomba msaada ambapo wananchi kadhaa walijitokeza na kuanza kufuatilia ng`ombe hao.
Amesema wananchi hao wakiwa wamefuatana na polisi kutoka katika kituo kidogo cha Nyamongo, waliwafuatilia ng`ombe hao hadi eneo la Igina Itambe, lililopo wilaya ya Kurya huko Kenya na walipofika katika kijiji hicho, wakashambuliwa na risasi.
Amesema katika tukio hilo watu wawili walipigwa risasi ambao ni Chacha Wambura, 47, mkazi wa kijiji cha Kobori, aliyepigwa risasi ya kifuani na kufa papo hapo na Joseph Chacha, 40, mkazi wa Kisangura aliyepigwa risasi tumboni na kisha kukatwa katwa mapanga miguu yote miwili.
Kaimu Kamanda Uyuya amesema Joseph alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kihanje iliyopo Kenya na baadaye miili ya marehemu wote ilirejeshwa nchini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kutokana na gharama kubwa za uchunguzi nchini Kenya.
Amesema miili hiyo imekwishafanyiwa uchunguzi na imekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya maziko.
Hata hivyo amesema ng'ombe 25 na mbuzi sita walifanikiwa kuokolewa na wanakijiji hao toka mikononi mwa majambazi hayo.
Akizungumzia kuhusu kampeni zinazoendelea mjini humo, amesema hali kwa sasa ni shwari na kampeni zinaendelea katika hali ya utulivu na hakujaripotiwa tukio lolote la uvunjifu wa amani.