[Source Tanzania Daima]
Mshtuko mpya Tarime
na Kulwa Karedia, Tarime
ZIKIWA zimesalia siku sita kabla ya kupiga kura Oktoba 12 mwaka huu, hali ya wasiwasi na mshtuko imewakumba mamia ya wapiga kura kutokana na baadhi yao kutokuwamo kwenye orodha ya watu wanaotakiwa kupiga kura siku ya uchaguzi.
Hali hiyo imetokea siku moja tu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa orodha ya majina ya watakaopiga kura katika jimbo hilo Jumapili ijayo.
Wananchi hao walieleza mshtuko huo jana mjini hapa baada ya kutembelea vituo mbalimbali kulikobandikwa majina yao na baadhi yao kubaini kuwa majina yao hayamo kwenye orodha hiyo, licha ya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Mmoja wa wananchi hao, Mwenge Ally, mwenye shahada namba 44622111, alisema baada ya kufika kwenye kituo chake alichojiandikishia cha Tarime C, jina lake halikuwapo, hali ambayo inamfanya kukosa haki yake ya kupiga kura.
Nimeshangazwa na hali hii, nimekuja hapa kuangalia jina langu lakini halipo... sasa sijui hatima yake nini, shahada yangu hii hapa jamani, inawezekana huu ni mpango uliofanywa na tume ili nikose haki yangu ya msingi, alisema Ally.
Mbali ya Ally, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji katika eneo hilo, Kengula Tagaya, alisema katika kituo B, zaidi ya majina 62 hayamo kwenye orodha hiyo na huenda wasipige kura siku hiyo.
Ni kweli kumetokea matatizo makubwa hapa, hawa wananchi walijiandikisha mimi mwenye nikiwepo, sasa nashangaa kuona majina hayapo... lakini kibaya zaidi ni pale baadhi ya majina yanayotolewa yanaonyesha eti wengine wamehama, jambo ambalo si kweli, alisema Tagaya.
Katika kituo hicho, zaidi ya wananchi 41 majina yao hayakurudi kwa sababu mbalimbali, zikiwemo wengine kuhama makazi au kujiandikisha zaidi ya mara mbili.
Mbali ya kituo hicho, katika kituo cha Tarime mjini, zaidi ya majina 60 yamerudi bila ya kuwa na namba, hivyo kukosa haki yao ya kupiga kura siku hiyo.
Naye Samweli Lazaro Chacha, kwa upande wake alisema amesikitishwa na kitendo cha NEC kurudisha jina likiwa limewekwa kwenye orodha ya wakazi waliohama eneo hilo.
Nashangaa sana kuona tume inarudisha jina langu na kusema eti mimi nimehama. Huu ni ujanja unaofanywa ili tusichague chama tunachokipenda, huu ni mchezo mchafu ambao tume imezoea kuufanya kila uchaguzi unapokaribia, alisema Chacha.
Akijibu malalamiko hayo, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi, alisema tume yake imepokea malalamiko hayo na hatua zinachukuliwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya siku ya uchaguzi.
Suala hili nimelisikia, napenda kukuhakikishieni kwamba tunafanya marekebisho ya haraka ili wote ambao majina yao hayapo, yaingizwe kwenye orodha ya wapiga kura, alisema Kagenzi.
Kagenzi alisema moja ya tatizo la wakazi wa Tarime, wamekuwa wakichanganya majina wakati wa kujiandikisha, jambo ambalo husababisha majina yao kubadilika wakati wa kuandikwa kwenye kompyuta, alisema Kagenzi.
Alisema kwa wananchi wa maeneo ya vijijini, wanapaswa kupeleka malalamiko yao haraka kwa viongozi walioteuliwa na tume kusimamia uchaguzi huo katika maeneo yao ili kufanyiwa marekebisho.
Mkurugenzi huyo alisema, jumla ya wapiga kura 146,510 wamejiandikisha katika uchaguzi huo na vituo 407, vinaratajiwa kutumika siku ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Kagenzi amesema hayuko tayari kupindisha matokeo, hata akilazimishwa kufanya hivyo kwa mtutu wa bunduki.
Msimamizi huyo alilazimika kutoa kauli hiyo, kukanusha uvumi kwamba kuna shinikizo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba lazima amtangaze mgombea wa chama hicho, Christopher Kangoye, kuwa mshindi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa jana, Kagenzi aliwataka wana Tarime kupuuza maneno hayo kuwa hajapewa shinikizo lolote la kutangaza wagombea ubunge na udiwani na wala hana mamlaka kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Nawaomba sana wana Tarime na watu wengine kuachana na uvumi huu, kwani mimi sina mamlaka ya kutangaza mshindi kwa shinikizo, ninachoweza kusema ni kwamba nitafuata sheria zote za uchaguzi, alisema Kagenzi.
Alisema hatakubali kuyumbishwa kwa kafuata matakwa ya watu fulani ambao wanataka kushinda kiti hicho kwa nguvu.
Siku zote nimekuwa mtu mwenye msimamo katika kazi yangu... nazingatia sheria za uchaguzi, sijapokea barua kutoka chama chochote, ikiwemo CCM, naviheshimu vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huu, alisema Kagenzi.
Alisema baadhi ya madai yanayotolewa ni kwamba CCM isiposhinda katika uchaguzi huo, atahamishwa kituo cha kazi, lakini alisisitiza kuwa sheria za uchaguzi haziruhusu kitu kama hicho hata siku moja.
Kagenzi alisema msimamizi wa uchaguzi atamtangaza mshindi yule tu atayekuwa amepata kura nyingi baada ya kuhesabiwa na kukubalika kwa pande zote mbili.
Kumekuwa na tabia ya watu kutoa lugha ambazo hazifai, tena nasikia ni viongozi wakubwa kabisa katika vyama vyao, napenda kutumia nafasi hii kusema hakuna kitu kama hicho, alisema Kagenzi.
Kuhusu malalamiko yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa ameshinikizwa na CCM kutangaza majina ya mawakala mapema ili wajulikane na kununuliwa na chama hicho, msimamizi huyo alikataa kuhusika na suala hilo.
Alisema leo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mawakala wote wa vyama lakini hakuna chama kiichotekeleza agizo lake.
Mimi niliwaandikia barua tangu Septemba 24, wanipe majina na hii ni kwa mujibu wa taratibu, lakini vyama vyote havijaleta na hii ilitokana na kuongezwa vituo vya kupigia kura kutoka 369 hadi 406, alisema Kagenzi.
Katika uchaguzi huo mdogo, jumla ya wapiga kura 146,510 wanatarajiwa kupiga kura, na upinzani mkubwa upo kati ya CCM na Chadema.
Katika hatua nyingine, CCM, inadaiwa kufanya mikutano ya siri nyumbani kwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, (NEC), Christopher Gachuma na kupitisha maazimio ambayo wanaamini yatakisaidia chama hicho kushinda uchaguzi huo.
Habari za kuaminika zilizopatikana jana kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho waliohudhuria mkutano huo, ambao ulifanyika katika Kijiji cha Komaswa, walisema moja ya mkakati uliopangwa ni kuhakikisha CCM inaibuka na ushindi kwa namna yoyote ile.
Ni kweli kikao hiki kilifanyika nyumbani kwa Gachuma na kupanga mikakati mizito ya kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi huo kwa namna yoyote ile... lakini hii imetokana na hali halisi ya upinzani uliopo, kilisema chanzo hicho.
Moja ya azimio linalodaiwa kupendekezwa kwenye kikao hicho ambacho kilifanyika siku za Alhamisi na Ijumaa iliyopita na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu, akiwemo Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Pius Msekwa, ni kuhakikisha kila mpiga kura na viongozi wa serikali za mitaa wanapewa pesa siku moja kabla ya uchaguzi.
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa vikao hivyo kwa kauli moja vilikubaliana kwamba mawakala watakaopitishwa na chama na kupangwa vituoni, kila mmoja atakabidhiwa kitita cha sh 300,000.
Mbinu hiyo inadaiwa kuwa sehemu ya mkakati wa kutaka kulikomboa jimbo hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na marehemu Chacha Wangwe (Chadema), aliyefariki dunia kwa ajali ya gari mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa CCM, Makamba, alipopigiwa simu na gazeti hili ili kutaka kupata ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kwa kusema: Sasa ndugu yangu mimi nikusaidie nini, sina cha kukwambia, alisema na kukata simu.
Hivi sasa hali ya ulinzi imezidi kuimarishwa kukabiliana na vurugu, ambapo juzi gari linalotumika kumwaga maji ya pilipili, yanayowasha mwilini, limewasili, tayari kukabiliana na vurugu zinazoweza kutokea siku hiyo.
Hivi sasa gari hilo ambalo limewahi kutumika kwenye uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar kukabiliana na vurugu, limeegeshwa kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tarime, huku likiwa chini ya uangalizi wa askari na waandishi wa habari wamezuiliwa kulipiga picha.