Simon Mhina
Katika kile kinachoonyesha kuwa mambo magumu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa Busanda, viongozi wakuu wa chama hicho wanadaiwa kuondoka kwenye kampeni za uchaguzi huo na kumuacha mgombea wao akiwa mkiwa.
Viongozi hao ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa wameondoka Busanda tangu kampeni za Chama hicho zilipozinduliwa.
Wachunguzi wa mambo ya siasa, wamesema kutoweka kwa Msekwa na Makamba kuna lengo la kunawa mikono, na kukwepa lawama iwapo mgombea wao atashindwa.
Akizungumza na gazeti hili, Msekwa alikiri kujiweka pembeni mwa kampeni hizo. Ndio nilikuwepo kwenye ufunguzi nimeondoka, lakini sio kwa kuogopa zomeazomea kama mlivyoandika,alisema.
Alipoulizwa kisa cha kukacha kampeni na kumuacha mgombea ukiwa, Msekwa alisema hizo ndizo sera zake na utaratibu ambao ameuanzisha ndani ya CCM.
Msekwa alisema CCM ilikuwa na utaratibu mbaya wa kuwamwaga vigogo wa Chama hicho kwenye chaguzi ndogo na kuacha kushughulikia kazi nyingine.
Utaratibu wangu ambao nimeupendekeza ni kwamba kila kiongozi awajibike katika eneo lake, kila mtu na lwake, siwezi kuacha ofisi ya Chama chenye mtandao nchi nzima na kushughulikia kajimbo kamoja ka Busanda,alisema Msekwa.
Alisema mambo ya kumwaga vigogo wa Chama, yanatakiwa yafanywe na wapinzani kwavile hawana mtandao wa kutosha.
Mimi Nimefungua kampeni inatosha, mengine yafanywe na mgombea pamoja na viongozi wa CCM ngazi ya Jimbo,alisema.
Kwa upande wake Makamba alisema yeye amejikita zaidi katika Uchaguzi mdogo
.. visiwani Zanzibar.
Mimi nipo Zanzibar kazi yangu ipo huku mambo ya Buchosa, mimi simo wala usiniulize,alisema kwa njia ya simu.
Habari toka kwenye vikao vya CCM mjini Busanda, zinasema siku ambayo vigogo wa Chama hicho walizomewa, Msekwa na Makamba waliitisha kikao cha ndani kujadili hali hiyo.
Habari hizo zinasema katika kikao hicho Makamba alifoka akidai kuwa mara baada ya kushindwa uchaguzi mdogo wa Tarime, kuna watu walipendekeza atimuliwe.
Kufuatia madai hayo, habari hizo zinasema Msekwa naye aliamua kujiweka pembeni kwa sababu hizo hizo.
Hata hivyo, kiongozi ambaye anaonekana kupigana kufa na kupona ni Makamu mstaafu wa CCM, John Malecela (Tingatinga), ambaye hata hivyo kwa kile kinalichoelezwa kuwa amegeuka Bajaji hapa Busanda, hataki kuhutubia mikutano sehemu za mijini.
Mimi sijaondoka naendelea na kampeni, ila nimeweka kambi yangu Nyarugusu na ninahutubia mikutano minne kwa siku, alisema alipozungumza na gazeti hili.
Kinachozidisha ugumu wa kampeni za CCM ni kutokana na vigogo wakiwemo Mawaziri kushindwa kuelezea sera zenye lengo la kutatua matatizo sugu ya jimbo hilo, ambayo ni umeme, maji, elimu, afya na miundombinu.
Mathalani, katika mkutano uliofanyika eneo la Katoro Centre, wananchi wengi wakiwemo wapinzani waliofurika, baada ya kusikia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, atahutubia wakiwa na matarajio kwamba angezungumzia kero ya umeme. Jimbo hilo halina umeme.
Hata hivyo Waziri Ngeleja alijikita zaidi katika kuwapiga vijembe viongozi wa Chadema.
Katika vijembe hivyo, Ngeleja alikuwa akitumia miziki ya bongo fleva ya wanamuziki akina Profesa J. badala ya Ilani ya CCM .
Vilevile alishindwa kuwashawishi wananchi hao kumkubali, baada ya kutumia takwimu za mafanikio ya Wizara yake nchi nzima, bila kufafanua kwamba katika jimbo hilo kuna mafanikio gani na wanatarajia kufanya nini.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara, George Mkuchika, ameonekana kukosa uvumilivu, kiasi cha kuamua kutukana kwa ishara.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4:03 asubuhi, alipokuwa anapita kwenye eneo ambalo kuna kambi ya Chadema.
Mkuchika akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruser lenye namba za usajili T995 AGK alizomewa na wafuasi wa Chadema, kisha kwa hasira akafungua kioo cha gari, akawaonyesha ishara kwa vidole vitatu vikimaanisha aina ya tusi.
Juzi wakati akitokea mjini Geita Mkuchika alilazimika kuficha uso kwa kuvaa kilemba, ili kuepuka zomeazomea.
Vilevile Katika mikutano ya CCM makada hao akiwemo Hiza Tambwe na Salum Msabaha, wanatumia muda mwingi kukejeli familia za viongozi wa Chadema, badala ya kuelezea kitu ambacho watawafanyia wananchi wa Busanda.
Mathalani mmoja wa wapiga debe hao, Shaibu Akwilombe, alitumia muda wote aliopewa kumnadi mgombea wao kuzungumzia madai kuwa mke wa mwenyekiti wa Chadema ni mtoto wa muasisi wa chama hicho.
Hata hivyo, makada hao kila walipotoa kejili hizo, walikuwa wanazomewa.
Kada ambaye alitarajiwa kukiokoa chama hicho ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, lakini kutokana na hali kuwa ngumu, matarajio yamekuwa hafifu.
Kwa ujumla vigogo walioletwa na CCM kuongeza nguvu, wameshindwa kukiletea afya chama hicho kwenye kampeni. Hata hivyo, katika hali inayoonyesha mtafaruku ndani ya kambi ya CCM, Mkuchika alisema sio kweli kwamba CCM imemuita Kilango aokoe jahazi.
Alisema Kilango alipelekwa Busanda na Umoja wa Wanawake (UWT) kwa lengo la kumsaidia mwanamke mwenzao hakuitwa na CCM.
Uchaguzi wa Busanda unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.
NIPASHE