BARUA TOKA MWANA-CCM BUSANDA
"HII NI KURA YA MAONI"
Salaam!
Nikiwa ni mwanachama mwaminifu wa Chama cha Mapinduzi ninaamini uchaguzi uliopo mbele yetu ni uchaguzi ambao ni sawa kabisa na kura ya maoni juu ya mwelekeo wa jimbo letu na hasa hali ya uongozi katika jimbo hili. Ni kura inayohusu hasa kuridhika na uongozi uliowahi kuwepo kwa muda mrefu na ambao unataka kuendelea kuwepo. Hii ni kura ya maoni yetu kuhusu wapi tunataka Busanda iende na ifike chini ya Mbunge ajaye. Uchaguzi uliopo mbele yetu basi ni uchaguzi unaozidi mtu, watu, chama au mwelekeo wa kisiasa. Ni uchaguzi unaotuhusu sisi na watoto wetu na wajukuu zetu. Ni uchaguzi ambao kwa mapenzi ya Mungu umetokea wakati huu na ni wajibu wetu kutambua maana yake.
Ninaamini uchaguzi huu mdogo unahusu kuridhika kuliko kitu kingine chochote. Je tumeridhika na hali iliyopo Busanda? Kama jibu ni "ndiyo" basi kura yetu siyo ngumu kwani ni lazima tumchague mgombea wa CCM. Kama kwa kiasi chochote kile hatujaridhika basi ni lazima tuamue kufanya kitu tofauti, kupiga kura inayoonesha kuwa kweli hatujaridhika, kura inayopiga kelele kuwa "haturidhishwi".
Kura za ndani za Chama cha Mapinduzi wakati huu wa kampeni zinaonesha ni jinsi gani hatujaridhika na hali iliyopo. Kuanzia Kamena, Nyamalimbe, hadi Bukoli wananchi wanaonesha kutokuridhishwa na hali iliyopo. Sehemu hizo zote chama chetu kimekutana na hali ya wasiwasi, ahadi zilizotolewa kwa wananchi hazijatimizwa na ahadi mpya zinatolewa; vijana wanajihisi chama na serikali haiwajali na hivyo wanajiona kutengwa na nafasi ya mafanikio.
Ukienda Nyarugusu ndiyo kabisa. Wakati makampuni makubwa yanaendelea kunufaika na utajiri wa madini unaotuzunguka wananchi wetu bado wanahangaika na uchimbaji duni na mazingira duni kabisa. Matatizo ya umeme ni matatizo ya nchi nzima na kiongozi anapoahidi kuleta umeme kwa ghafla huku kwetu ni kututania kwani hata Dar-es-Salaam kwenyewe hawana umeme jiji zima.
Hapa Katoro ndiyo usiseme kabisa. Matatizo ya hapa ni matatizo ya maeneo mengi yanayotuzunguka. Kunyanyaswa na polisi kwa kubambikiwa kesi, kunyanyaswa na watoza kodi wa TRA, taarifa za mapato na matumizi hazisomwi kama inavyotakiwa kwenye vijiji vingi na kiukweli viongozi waliopo ni kama wamesinzia. Sasa hali hii kwa kiasi ndiyo ilivyo kwenye jimbo zima na Chama chetu ndiyo kiongozi. Ni jinsi gani basi tutakiamsha chama kile tunachokipenda? Tutaweza vipi kutuma ujumbe kuwa "tumechoka na haturidhishwi"? Je, viongozi wa serikali kule Dar-es-Saalam watatambua vipi kuwa na sisi tupo na tunahitaji kusikilizwa? Ipo njia moja tu.
Tusimchague mgombea wa CCM kwani tukifanya hivyo tutakuwa tumeonesha kuridhishwa na hali iliyopo. Tukimchagua mgombea huyo (japo ni kada mzuri wa chama) tutakuwa tunasema kuwa hali yetu ni "nzuri" na hatuhitaji mabadiliko. Kuwa mambo yaendelea vile yalivyo na kwa hakika hivyo ndivyo itakavyokuwa. Ombi langu ni tufanye uamuzi wa makusudi wa kutuma ujumbe kuwa tunamchagua mgombea wa Chadema, Bw. Magesa si kwa sababu tunampenda zaidi bali tunataka kutuma ujumbe wenye pande mbili.
Kwa CCM, tunakiambia chama chetu kuwa una mwaka mmoja na nusu hivi kuonesha kuwa unatujali na kuwa sisi nasi ni muhimu kwako. Kwamba, kama ahadi ulizozitoa zina ukweli basi wazitekeleze na tuone zinaanza kutekelezwa ili watakapokuja kwenye kampeni mwakani watukumbushe kuwa ahadi zao hazikuwa za kuombea kura tu. Nje ya hapo, tutawachagua wapinzani tena na kuwapa jimbo kwa kipindi kamili cha miaka mitano.
Kwa Chadema, tunawaambia kuwa wako kwenye kipindi cha majaribio. Mwaka mmoja na nusu unaokuja tunataka kuona kama viongozi wake watakuja tena kuzungumza na sisi, tutaona Mbunge wetu mpya anafanya nini Bungeni, na zaidi tutampima kama anastahili kupewa kipindi kamili.
Hivyo, uamuzi ni wa kwetu. Kwamba, katika kura hii tunataka mlio wake usikike Tanzania nzima kuwa Busanda wameamua kutuma ujumbe kwa CCM kuwa hakuna jimbo rahisi tena, na hakuna uhodhi wa jimbo. Kama kweli CCM wanalitaka hili jimbo basi waje mwakani na ushahidi wa nini wameshaanza kufanya hata wakati hawana jimbo siyo wakati wa kampeni tu.
Kwa Chadema, watambue kuwa kuwa ushindi tutakaowapa Jumapili hii wajue ni zawadi na jaribio. Ni zawadi kwa jitihada waliyoifanya ya kutetea raslimali za utajiri wa nchi yetu kwa mwaka huu uliopita na ni jaribio kwa sababu na wao kama CCM hawana hati miliki ya jimbo letu. Hivyo, wasichukulie kirahisi ushindi huo kama vile wamestahili.
Tusiogope, tusione aibu, wala tusitishwe na mtu yeyote. Kura ni siri na hakuna mtu yeyote anayejua kura imepigwa vipi. Hata hivyo ili kuweza kuleta mabadiliko ya kweli hapa Busanda, hatuna budi kupiga kura ya kuona kweli tunataka mabadiliko hayo. Ninaamini kutoichagua CCM kwa wakati huu ni ujumbe tosha kabisa kuwa mabadiliko yanatoka kwa wananchi. Mungu katupe nafasi ya kupata uongozi mpya, tusifanye makosa tusije baadaye kuanza kuishi kwa kujuta na kusema "laiti tungemchague yule". Tutumie haki yetu kwa ujasiri, tulete mabadiliko ya kweli!
Na Chadema wakiboronga na baada ya mwaka huu mmoja tunaowapa, CCM bado ina watu wengi tu wazuri na tutawarudisha 2010.
Emmanuel Mashibya, Katoro, Jimbo la Busanda