SIKU moja baada ya uzinduzi wa kampeni za CCM, juzi kutikisa mjini hapa, baadhi ya makada wa vyama vya upinzani wamekiri kwamba ni vigumu upinzani kushinda kiti hicho cha ubunge. Kampeni hizo zilizozinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, zimeibua hisia za wananchi, kutokana na mambo mbalimbali yaliyowagusa. Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa makada wa CHADEMA alisema kuwa walidhani uzinduzi wa CCM ungedoda, lakini imekuwa kinyume cha matarajio yao. Alisema idadi ya watu waliohudhuria katika mkutano huo, uliwavunja nguvu za kuendelea kufanya kampeni, kwani imeonyesha dhahiri jimbo hilo bado ni mali ya CCM. "Sikufichi, pamoja na kwamba mimi naichukia CCM, lakini kwenye hili la uzinduzi halina ubishi, jamaa bado wanakubalika na kweli hapa upinzani tunasindikiza tu, kwani wale watu sio mchezo," alieleza.
Alieleza kwamba pamoja na kwamba uzinduzi uliofanywa na CHADEMA Septemba 8, ulikuwa na watu, lakini ule wa CCM ulifunika mara tatu zaidi, jambo linaloonekana dhahiri kwamba upinzani una kazi ngumu. "Tutajitahidi kuendelea kufanya kampeni, lakini mpaka sasa kama hatutumii hisia za uchama, lazima ukiri kwamba jimbo hili ni la CCM, na ni ndoto kwenda upinzani," alisisitiza. Akijibu swali juu ya kwa nini, hawakuiunga mkono CUF kutokana na mgombea wake kuwa na mtaji mkubwa kisiasa, alisema hakuna msimamo wa pamoja juu ya vyama vya upinzani, ndiyo maana kila chama kimeamua kusimamisha mgombea wake. "Kweli mgombea wa CUF ana mtaji mkubwa kuliko wa kwetu (CHADEMA), na kama tungeungana ni wazi tungewaangusha CCM, lakini bado vyama vya upinzani hatujawa na sauti moja," alikiri.
Source: Gazeti la Uhuru, Jumatatu, Septemba 12, 2011
Katika hali ambayo inadhihirisha kukata tamaa kwa upinzani, juzi akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alikiri kwamba sio rahisi kuiondoa CCM madarakani, kupitia siasa za mapambio zinazofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani.
Mtatiro alikiri kwamba CCM bado ni chama imara, kina nguvu na miundombinu mingi ya ushindi, hivyo bila kutafuta mwafaka wa pamoja wa upinzani haitakuwa na maana.
"Wenzetu CHADEMA mwaka jana hawakusimamisha mgombea na sisi mgombea wetu alipata kura 11,000 tulidhani wangetuunga mkono, badala yake wamekuja kugawa kura Igunga," alieleza.
Baadhi ya wananchi walisema kwamba uzinduzi uliofanywa na CCM na kueleza sera zake, kumewafanya wananchi kuendelea kuwa na matumaini na chama hicho.
"Unajua wapinzani ni watu wa ajabu sana, kila kitu kwao tatizo, hawajui hata historia ya jimbo hili, lilikuwa mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora, lakini leo ni wa kwanza, lakini wanasema hakuna kitu kilichofanyika," alieleza Juma Herman.
Herman alisema kwamba wananchi wamekuwa wakitaka kusikia sera za vyama, lakini wanachukizwa na sera za kutukana viongozi wa kitaifa na kupakana tope, kitu ambacho hakiwasaidii wananchi.
"Hivi mtu akisema huyu mbaya, mwananchi anajua ubaya wake nini... ni bora wakaeleza sera na namna ya kuwasaidia wananchi, lakini wao matusi na maandamano, ambayo hayana faida kwetu," alieleza.
Alisema CCM itaendelea kuongoza jimbo hilo na kushika dola kutokana na mikakati yake imara ya kuwaondolea wananchi umasikini na kuwahimiza katika kufanya kazi kuliko kuandamana.
Katika uzinduzi wa kampeni hizo, Mkapa aliwataka wananchi kuwapuuza CHADEMA kutokana na kukosa sera nzuri za kuendeleza nchi zaidi ya kuandamana bila kutoa sera mbadala.
Katika hatua nyingine, baadhi ya vijana wamelaani kitendo kilichofanywa na wafuasi wa CHADEMA cha kummwagia tindikali kijana mwenzao.
Jacob Maduhu (25) alisema kwamba kitendo hicho kimewasikitisha vijana na imekuwa matusi kwao kutokana na chama hicho kujitangaza kwamba ni mkombozi wa vijana.
"Hivi mkombozi wa vijana anaweza kuwaua vijana, hapana hiki ni chama cha mauaji, huwezi kumuharibia maisha kijana unayetaka kumkomboa kwa kumwagia tindikali," alisema Mahudu.
Naye Salma Hamisi alisema kwamba amekuwa haelewi maana ya nguvu ya umma inayohubiriwa na chama hicho, kumbe maana yake ni kuangamiza umma kwa tindikali.
"Kila siku utasikia nguvu ya umma, hawaelezi sera zao, wao ni fujo na maandamano na kuwapiga wanaopingana nao, hizi ni siasa za wapi, maana waasisi wa taifa walitujengea siasa nzuri, sasa hizi za kumwagiana tindikali si zitatumaliza?" aliuliza.