MONDAY, 12 SEPTEMBER 2011 19:45 NEWSROOM
* Wakaleta tena balaa za Tarime na Arusha
KATIKA mjadala na vimbwanga vya siasa vilivyo katika chati, watu wanasema ‘mambo yote yako Igunga." Ni harakati za kumsaka mrithi wa Rostam Aziz, aliyekuwa mbunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM na baadaye akajiuzulu.
CCM imeshapiga kambi ya uhakika huko, ikiwania kukirejesha kiti hicho katika imani kwamba ‘kiti ni chetu.' Ilitarajiwa kwamba siasa na kampeni zingenoga sana Igunga, sera za kukosoana majukwaani ndio zingetawala, lakini kwa siasa za Chadema huko Igunga, imedihirisha si utaratibu wao. Wamekuwa mstari wa mbele kutoa maneno mengi, kashfa na propaganda nyingi.
Wamekuwa wakitafuta ushindi kupitia propaganda za majukwaa ya kisiasa. Kama alivyonena Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, kwamba ‘hivi karubuni, siku zote mbwa anayebweka sana, huwa haumi,' hivyo hilo limekuwa haliumizi kichwa CCM ambayo imeenda katika matendo zaidi.
Ushuhuda wa ‘matendo zaidi' ya CCM dhidi ya ‘wabwekaji' ni umati uliofurika katika Uwanja wa Sokoine, kumsikiliza Mwenyekiti mstaafu Mzeee Benjamin Mkapa, alipozindua kampeni za mgombea wake Dk. Peter Kafumu, msomi wa madini mwenye shahada nne na stashahada mbili za uzamili mbili.
Si kwamba hayo yameanzia huko, bali killa wanakopita mambo ni hayo hayo. Siasa za chama hicho ni lazima ziwe na ‘harufu za damu.' Tukumbuke kilichojiri Arusha na Mwanza.
Kampeni zinaporuhusiwa rasmi, ni jambo la kawaida wanasiasa na wafuasi wao wakazunguka sehemu mbalimbali kulingana na ratiba walizopangiwa.
Pia, mazingira ya kampeni hutawaliwa na mengi katika propaganda zake, picha za wagombea kubandikwa katika maeneo ya umma, muziki kupigwa na vibweka vya namna mbalimbali, ili mradi ni matendo yaliyovunja sheria.
Uchaguzi, pia maana yake ni mtu anajitolea kupeperusha bendera ya chama fulani, kuhakikisha anasimamia sera zake kuwaletea maendeleo wananchi husika, huku wananchi wakiendelea kuishi kwa amani na utulivu. Kinyume na hicho, mhusika hafai kugombea nafasi hiyo.
Chadema kwa kuendelea kudhihirisha ni watu wa fujo, makada wao wanaonekana kutumwa na mtandao wa mamlaka ya chama, walimvamia na kumpiga kisha kumwagia tindikali kada wa CCM.
Kisa, ni kwamba alikuwa anabandika picha za mgombea wake, Dk.Kafumu, jambo ambalo ni haki yake ya kisiasa na kisheria, kwani kampeni zilisharuhusiwa.
Simulizi za tukio na namna walivyoathirika wahusika, kilimshitua karibu kila mtu nchini na nje ya nchi, mpenzi wa siasa na asiyependa siasa.
Ni kitendo ambacho daima si ubinadamu hata kidogo. Sijui inajenga picha gani, jumuia ya kimataifa na jamii ya wageni waishio nchini? Watakaa wajiulize, hizi ndizo siasa zetu ?
Mbali na hilo, viongozi wa Chama wanajitosa kutumia dhana ya ajabu, ikiwemo
madai ya ‘nguvu za giza' kitu kinachoshangaza, baadhi yao ni wasomi waliobobea na wana historia ya kutumikia dini, lakini si chochote, wanatumia siasa za ajabu tena zenye utashi wa kudhuru watu.
Hii si mara ya kwanza, kwani kwa mwenendo huo huo haujapita muda mrefu huko mjini Arusha, kwamba mwenendo wa Chadema na falsafa yao ya ‘nguvu ya umma' walisababisha vifo vya watu kadhaa.
Katika harakati hizo, yalitokea mapambano baina ya Polisi na wana-Chadema waliohamasishwa na viongozi wa juu Chama pamoja na mbunge wao wakitumia ‘nguvu ya umma' dhidi ya nguvu halali ya Polisi ikitimza wajibu wa kulinda raia na sheria za nchi.
Ni tukio lililoishia kwa msiba na viongozi wa Chadema kuingia katika lawama za kuwaingiza katika matendo yao kuwashawishi wafuasi wao na hata wakapoteza maisha.
Huko Mwanza, simulizi ni ghasia hizo zinazosababishwa na wafuasi wa Chadema zimeishia katika kujenga hali tete jijini humo na hata jina la chama hicho kuwa baya kwa wakazi wote jijini.
Falsafa ya ‘nguvu za umma' mara zote hutekelezwa kwa matukio ya ghasia na uvunjaji wa sheria za nchi pasipo sababu za msingi. Ni vigumu kutenganisha propaganda za Chadema na matendo ya ghasia.
Pengine kwa kurejea matukio ya kurupukushani za kisiasa katika kampeni ndogo ya uchaguzi wilayani Tunduru, ilishuhudiwa chama hicho kilivyotumia muda mwingi kutunishiana misuli na fujo za kisiasa katika mitaa ya Tunduru dhidi ya Chama cha CUF.
Ngome hiyo ya upinzani ambazo zilitakiwa kuungana mkono dhidi ya CCM, lakini cha ajabu walitunishiana misuli hata kufikia hatua kwamba mara nusuru wafuasi hao wapigane, jambo lililolainisha kampeni za CCM kwa wananchi kujua pumba na mchele.
Kuna wakati bila Kamanda wa Polisi wa Mkoa bila ya kuingilia kati kuwatawanya wafuasi hao wawe katika pande mbili tofauti, basi kungetokea ghasia nzito ambazo haijulikani nini hasa ingekuwa hatima yake.
Hivi karibuni wilayani Tarime, ghasia za Chadema uanaharakati wa haki za wazwa katika migodi nazo ziliishia katika kusababisha vifo hivi karibuni na baadhi ya Wabunge wa chama hicho sasa wanakabiliwa na mikono ya sheria.
Sura kama hiyo ya ghasia, ndio ilijitokeza katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ambapo mazingira ya shari yalitawala wakiamini kifo hicho kina mkono wa viongozi wa juu wa chama.
Kwa ujumla, Chadema muda mwingi imekuwa ikijitapa kwamba wanapambana wakidai haki na demokrasia. Kwa bahati mbaya wadau hao wa demokrasia ndio wamekuwa wavunjaji wakubwa wa demokrasia na haki za binadamu.
Iwapo matendo yao nio hayo, Chadema wanasaka nini katika viti vya uchaguzi, kwa wao kuna na matendo yaliyofanana na matakwa ya demokrasia kitaifa na kimataifa.
Sifa kubwa ya chama cha siasa ni ‘kukubalika'. Kwa hayo yanayojitokeza na kudhulumu haki za binadamu ndio kukubalika?